Addie Alipata Jibu Akiwa Amechelewa
Lakini Si Kuchelewa Mno
Hii ni hadithi juu ya jitihada ya kutafuta haki ya kijamii kwa miaka 87, iliyofanywa na mwanamke mweusi. Yeye aketi juu ya gogo akivua samaki kando ya bwawa. Ngozi yake ni laini, akili yake ni timamu, na ni mwenye adhama. Ni mwenye nguvu, mwenye ujuzi, lakini machoni pake waweza kuona hekima na ucheshi, na unyenyekevu wenye kupendeza. Yeye ni stadi katika kusimulia hadithi. Urithi wake wa Kiafrika ni dhahiri, ukichangamana na kumbukumbu za Marekani Kusini. Sikiliza anaposimulia maisha yake.
“NYANYA yangu alizaliwa katika meli ya watumwa iliyokuwa ikielekea Georgia, kutoka Afrika. Yeye alikuwa dhaifu sana hivi kwamba, hakuna mtu aliyetazamia kwamba angeishi. Kwa hiyo mamake alipouzwa, yeye alienda na mtoto wake mgonjwa. Hiyo ilikuwa mwaka 1844 hivi. Mtoto huyo aliitwa Rachel.
“Dewitt Clinton alilima shamba la pamba la amu wake. Kwa Dewitt, Rachel alimzaa babangu aliyeitwa Isaiah Clinton, aliyezaliwa Juni 1866. Walimwita Ike. Akiwa mvulana, mara nyingi alikuwa akiendesha farasi mmoja na Dewitt na alifunzwa mambo yote kuhusu ukulima wa shamba. Miaka michache baadaye, Dewitt alimwambia Ike hivi: ‘Wakati umefika ujitafutie riziki.’ Kisha akatoa mshipi wenye vibeti vyenye pesa kutoka kiunoni mwake na kumpa Ike.
“Baada ya hayo babangu alienda kumfanyia kazi Bw. Skinner, akawa mwangalizi wa shamba la Skinner, na kumwoa Ellen Howard. Nilizaliwa mnamo Juni 28, 1892, katika Mkoa wa Burke karibu Waynesboro, Georgia. Maisha yangu yalikuwa mazuri ajabu. Nilikuwa na hamu kubwa ya kutoka nje kila siku na kufurahia siku. Mama angenizuia hadi alipofunga nguo yangu upande wa nyuma, na ningemsikia akisema hivi kila siku: ‘Mfunge nguo na uache aende zake.’ Ningepanda juu ya sehemu yenye panda ya plau ili niwe karibu na babangu.
“Siku moja wakati wa dhoruba ya kiangazi, umeme ulimpiga Bw. Skinner na farasi wake kondeni. Wote wawili waliuawa. Bi. Skinner alikuwa mwanamke wa Marekani Kaskazini na alichukiwa na watu wote katika Mkoa wa Burke kwa sababu ya yale aliyofanya Jenerali Sherman alipochoma Atlanta. Kwa hiyo weupe walimchukia Bi. Skinner zaidi ya vile walivyowachukia weusi! Bi. Skinner alilipiza kisasi juu yao. Kwa chuki, mume wake alipokufa, yeye alimuuzia babangu aliyekuwa mtu mweusi, shamba lake. Wazia mtu mweusi akimiliki shamba kabla ya mwanzo wa karne hii katika Georgia!”
Bw. Neely na Duka la Jumla
“Baba alipohitaji kitu chochote, yeye alienda kwa Bw. Neely, aliyekuwa na duka la jumla. Wao walikuwa na kila kitu. Je! wahitaji daktari, nenda kwenye duka la jumla. Wahitaji jeneza, nenda kwenye duka la jumla. Hulipi chochote; bei yacho iongeze tu katika orodha ya gharama hadi wakati wa mavuno ya pamba. Neely alipata kujua kwamba baba alikuwa na pesa katika benki, kwa hiyo akatuletea kila kitu, bidhaa ambazo hatukuhitaji—sanduku lenye barafu, mashine ya kushonea, bunduki, baisikeli, punda wawili. ‘Hatukihitaji!’ baba alikuwa akisema. Jibu la Neely lilikuwa: ‘Ni zawadi. Bei yake nitaiongeza katika orodha yako ya gharama.’
“Siku moja Neely alifika kwenye shamba letu akiwa na gari kubwa jeusi aina ya Studebaker. Baba akasema: ‘Bw. Neely, hatulihitaji! Hakuna mtu anayejua kuliendesha au kulitunza, na kila mtu analiogopa!’ Neely alipuuza hayo. ‘Lichukue, Ike. Bei yake nitaiongeza kwenye orodha ya gharama zako na nimtume mmoja wa wafanyakazi wangu amfunze mmoja wa wafanyakazi wako jinsi ya kuliendesha.’ Hatukufaidika nalo. Siku moja nilimwomba baba aache niende na mmoja wa wafanyakazi ili kulitia petroli. Baba akasema: ‘Usiliguse; nakujua wewe!’ Mara tu tulipotowekea mbali, nikasema: ‘Acha nijaribu kulipeleka. Baba ajua kwamba nitaliendesha.’ Gari likatifua vumbi, nikiligeuza kushoto kisha kulia katika vichaka na miti. Liliacha njia na kuingia katika hori moja.
“Nilikuwa nikimuuliza baba kwa nini hakukataa bidhaa hizo, naye angejibu hivi: ‘Hilo lingekuwa kosa kubwa, matukano. Isitoshe, KKK [Ku Klux Klan] hawawaonei weusi walio rafiki za Bw. Neely.’ Kwa hiyo tuligharimia bidhaa hizo zote ambazo hatukuhitaji. Na nikafikiri juu ya yale ambayo baba alisema sikuzote: ‘Usinunue kile usichohitaji, au karibuni utahitaji kile usichoweza kununua.’ Nilimchukia Bw. Neely!
“Kila mtu alipokuwa akisherehekea mwanzo wa karne mpya, Januari 1, 1900, mamangu alikufa alipokuwa akizaa mtoto wake wa nne. Nilikuwa mwenye miaka minane tu wakati huo, lakini kando ya kaburi nilimwambia babangu kwamba ningemtunza yeye.
“Nyanyangu alitutunza sisi watoto. Yeye aliitwa Mary. Alikuwa mtu wa kidini sana, na mwenye kumbukumbu zuri sana, lakini hangeweza kusoma wala kuandika. Mara nyingi ningekuwa jikoni nikimuuliza-uliza maswali, ‘Mbona watu weupe hawashughuliki na watu weusi, ilihali wao husema kila mtu ni sawa machoni pa Mungu? Tutakapoenda mbinguni, je, watu wote weupe watakuwa huko pia? Je! Bw. Neely atakuwa huko?’ Mary angejibu: ‘Sijui. Sisi sote tutafurahia.’ Sikuwa na hakika sana juu ya hilo.
“‘Nyanya, tutafanya nini mbinguni?’ ‘Ah, tutatembea kwenye barabara za dhahabu! Tutakuwa na mabawa na kuruka kutoka mti mmoja hadi mwingine!’ Nikafikiri: ‘Ni afadhali kuenda nje kucheza.’ Hata sikutaka kwenda mbinguni, lakini pia sikutaka kwenda helo. ‘Nyanya, tutakula nini mbinguni?’ Yeye akajibu: ‘Ah, tutakunywa maziwa na asali!’ Nikapaaza sauti: ‘Lakini sipendi maziwa, na sipendi asali! Nyanya, nitakufa njaa! Nitakufa njaa mbinguni!’”
Naanza Kwenda Shule
“Baba alitaka nielimike. Katika 1909 alinipeleka kwenye Taasisi ya Tuskegee katika Alabama. Booker T. Washington ndiye aliyetoa uongozi wa kielimu na kiadili shuleni. Wanafunzi walimwita yeye Baba. Yeye alisafiri mbali akikusanya pesa kwa ajili ya shule hiyo, nyingi zazo kutoka kwa weupe. Alipokuwa shuleni, alitupa sisi ujumbe huu: ‘Elimika. Pata kazi, na kuweka akiba pesa zako. Halafu nunua shamba. Na kamwe nisikutembelee na kupata hujakata nyasi, hujapaka nyumba yako rangi, au madirisha yamevunjika huku nguo kuukuu zikiziba mashimo kuzuia baridi. Ujione kwa fahari. Saidia watu wako. Wasaidie wajiinue kiuchumi. Waweza kuwa kielelezo.’
“Kwa kweli wao walihitaji ‘kuinuliwa.’ Wao ni watu wema—wenye sifa nyingi nzuri. Kuna mambo fulani ya kale ambayo weupe wapaswa kukumbuka juu ya Weusi. Weusi hawakupewa fursa ya kujifunza. Kufundisha Mweusi kulikuwa kinyume cha kanuni za utumwa. Sisi pekee ndio watu tuliokuja nchini humu kinyume cha mapenzi yetu. Wengine walitamani kuja huku. Sisi hatukutamani. Walitufunga kwa minyororo na kutuleta huku. Walitufanyisha kazi kwa miaka 300 bila malipo. Tulifanyia weupe kazi kwa miaka 300, nao hawakutupa chakula cha kutosha wala viatu. Walitufanyisha kazi tangu asubuhi hadi usiku, wakatupiga viboko tulipobadili nia kidogo tu. Na walipotuachilia huru, wao bado hawakutupa fursa ya kujifunza. Weupe walitaka tufanye kazi shambani na pia watoto wetu wafanye kazi na kwenda shule miezi mitatu kwa mwaka.
“Na wajua ilikuwa shule ya aina gani? Ilikuwa kikanisa kidogo kwani hakukuwa na shule ya Weusi. Kilikuwa na mabenchi. Tulienda shule katika miezi yenye joto zaidi mwakani, yaani Juni, Julai, na Agosti. Hakukuwa vizuia-wadudu vya madirishani. Watoto waliketi sakafuni. Mwalimu mmoja alifunza wanafunzi 103, na wadudu wengi walikuwa wakiingia ndani. Waweza kumfunza nini mtoto kwa miezi mitatu? Katika likizo moja ya wakati wa kiangazi kutoka Tuskegee, nilifunza watoto 108, wa umri mbalimbali.
“Nilihitimu katika 1913 nikawa muuguzi. Katika 1914, niliolewa na Samuel Montgomery. Baadaye alienda kwenye Vita ya Ulimwengu 1, na nilikuwa mjamzito nikiwa na mtoto wangu wa pekee. Muda mfupi baada ya Samuel kurudi, yeye alikufa. Nikiwa na mwanangu mchanga, nilisafiri kwa garimoshi kumtembelea dadangu katika Illinois, nikitumaini kupata kazi ya uuguzi huko. Watu wote Weusi walielekezwa kwenye garimoshi nyuma tu ya behewa la makaa-mawe. Lilikuwa lenye joto, madirisha yalikuwa wazi, na tulifunikwa kwa masizi na kaa moshi. Siku ya pili chakula chetu kilikuwa kimekwisha pamoja na maziwa ya mtoto. Nilijaribu kuingia katika behewa lenye mkahawa lakini nikazuiwa na mfanyakazi mweusi. ‘Huwezi kuingia humu.’ ‘Je! wao waweza kuniuzia tu maziwa ya mtoto wangu?’ Jibu lilikuwa la. Ukosefu wa haki wa kwanza ulioamsha hasira yangu ulikuwa wa Bw. Neely. Huu ulikuwa wa pili.
“Katika 1925, niliolewa na John Few, mfanyakazi wa garimoshi. Yeye aliishi katika St. Paul, Minnesota, kwa hiyo nikahamia huko. Hilo lanileta kwenye ukosefu wa haki wa tatu ulioamsha hasira yangu juu ya suala la haki ya kijamii. Katika St. Paul, nilikuwa kaskazini ya mbali, lakini chuki ya kirangi ilikuwa nyingi zaidi ya Marekani Kusini. Hospitali ya mkoa haikukubali kunisajili kuwa muuguzi. Wao walisema kwamba hawajawahi kusikia juu ya muuguzi mweusi. Katika Tuskegee tulikuwa tumezoezwa vizuri, na mgonjwa ndiye aliyeshughulikiwa kwanza, lakini katika St. Paul, rangi ya ngozi ndiyo iliyoamua kama atashughulikiwa au la. Kwa hiyo niliuza nyumba ndogo niliyokuwa ningali nayo katika Waynesboro na kutumia pesa hizo kutoa malipo ya kwanza ya shamba na jengo. Nilianzisha gereji, nikawaajiri mafundi wanne, na upesi nikawa na biashara nzuri.”
Naanzisha Chama cha NAACP
“Ilikuwa l925 hivi nilipoanzisha chama cha NAACP [Chama cha Kitaifa cha Maendeleo ya Weusi] na nikajishugulisha sana nacho. Je! Booker T. Washington hakuwa amesema: ‘Saidia watu wako. Wasaidie wajiinue kiuchumi’? Jambo la kwanza nililofanya ni kwenda kwa gavana wa jimbo hilo nikiwa na orodha ndefu ya wapiga-kura weusi waliomiliki nyumba na kulipa kodi. Yeye alisikiliza, na kumpatia kazi muuguzi mweusi katika hospitali ileile ya mkoa iliyokuwa imekataa kuniajiri. Hata hivyo, wauguzi weupe walimtenda vibaya sana—hata kumwagia yunifomu yake yote mkojo—hivi kwamba alienda California na kuwa daktari.
“Kwa habari ya biashara yangu ya gereji, hiyo ilikuwa nzuri sana hadi siku moja katika 1929. Nilikuwa ndipo tu nimeweka akiba ya dola 2,000 katika benki, na nilipokuwa nikitembea, watu wakaanza kupaaza sauti kwamba benki zilikuwa zimefilisika. Nilikuwa nimebakisha malipo mara mbili kwa ajili ya gereji yangu. Niliipoteza yote. Niligawana na mafundi wangu pesa zozote nilizookoa.
“Hakuna mtu aliyekuwa na pesa. Nilinunua nyumba yangu ya kwanza kwa kuuza bima yangu ya maisha kwa dola 300. Nilinunua nyumba hiyo kwa dola 300. Niliuza maua, kuku, na mayai; nikawapa watu mahali pa kulala; na kutumia pesa za ziada kununua viwanja vitupu kwa dola 10 kila kimoja. Sikuona njaa kamwe wala sikupata misaada. Tuliyala mayai. Tukala kuku. Tukasaga mifupa ya kuku ili kulisha nguruwe wangu.
“Baadaye, nikawa rafiki ya Eleanor Roosevelt na rafiki wa karibu sana wa Hubert Humphrey. Bw. Humphrey alinisaidia kununua jengo kubwa la makao katika mji wa weupe katika St. Paul. Ajenti wa kuuza mali alihofia uhai wake, kwa hiyo akataka nimwahidi kwamba singetumia jengo hilo kwa miezi 12.”
Wakati wa Badiliko Kubwa Maishani Mwangu
“Jambo lisilo la kawaida ambalo sikusahau kamwe lilitukia katika 1958. Wanaume wawili weupe na mmoja mweusi walinijia wakitafuta mahali pa kulala kwa usiku mmoja. Nilifikiri huo ulikuwa mtego ili niingie matatani kwa kuvunja sheria, kwa hiyo nikawahoji kwa saa kadhaa. Maelezo yao yalikuwa kwamba wao walikuwa Mashahidi wa Yehova waliokuwa wakisafiri kupitia mashambani hadi kwenye mkusanyiko katika New York. Walinionyesha yale ambayo Biblia ilisema juu ya kusudi la Mungu kwa ajili ya dunia-paradiso ambapo hakutakuwa na chuki ya kirangi. Walisema juu ya udugu wa kibinadamu. Nikafikiri, ‘Je! labda wao wana jambo ambalo nimekuwa nikitafuta miaka hii yote?’ Wao walionekana kuwa vile walivyodai kuwa—ndugu. Hawakutaka kulala katika mahali tofauti.
“Halafu miaka kadhaa baadaye, nilimtembelea mmoja wa wapangaji wangu niliyejua alikuwa akifa. Aliitwa Minnie. Nilipomuuliza cha kumfanyia, yeye alisema: ‘Tafadhali nisomee kitabu kile kidogo cha buluu.’ Hicho kilikuwa kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele, kilichogawanywa na Mashahidi wa Yehova. Kwa hiyo kwenye kila ziara nilisoma mambo mengi zaidi na zaidi katika kile kitabu kidogo cha buluu. Siku moja Minnie alikufa, na nilipoenda kwenye nyumba yake, mwanamke mweupe aitwaye Daisy Gerken alikuwako. Alikuwa karibu ni kipofu. Aliniambia kwamba alikuwa akijifunza na Minnie kwa kutumia kile kitabu kidogo cha buluu. Daisy aliniuliza kama kulikuwa na kitu chochote humo nyumbani ambacho ningependa kuchukua. Nikasema: ‘Biblia na kitabu chake kidogo cha buluu tu.’
“Nilijua kwamba nikifuatia mambo yaliyo katika kitabu kile cha buluu, ningelazimika kuacha kazi yangu yote niliyofanyia watu weusi. Nisingeweza kueleza juu ya mambo yote niliyokuwa nikifanya niliyohisi kuwa yafaa. Nilipanga ushirika wa wafanyakazi wa garimoshi. Nikapigana katika kesi za mahakamani na kupata haki kwa ajili ya wengine. Nilipanga maandamano nyakati nyingine katika sehemu mbalimbali za mji wakati uleule. Ilinibidi kuhakikisha kwamba watu wangu hawavunji sheria, na walipofanya hivyo, ilinibidi niwatoe gerezani. Nilikuwa mshiriki wa vyama kumi lakini vile tu vilivyofanya kazi ya kijamii.
“Kwa hiyo nilifikiri kwamba nisingehangaikia maisha ya baada ya kifo. Watu wangu walikuwa wakiteseka sasa! Nilikuwa na wafanyakazi wengi katika NAACP, kutia na sekritari mweupe. Kutoka 1937 hadi 1959, nilitumikia nikiwa katibu-msimamizi wa NAACP katika St. Paul na kuanzia 1959 hadi 1962 nikiwa msimamizi wacho. Nilipanga majimbo manne yakawa shirika na kutumikia huko mpaka hatimaye NAACP ikawa na mkutano wacho wa kitaifa katika St. Paul. Kulikuwa na vita vingi muda huo wote, kila moja ikiwa ya maana. Kabla ya kustaafu nikiwa na miaka 70 katika 1962, nilimtembelea Rais John F. Kennedy. Kwa kusikitisha, wakati huo nilijihusisha sana katika kutafuta haki kwa njia yangu hivi kwamba nisingeweza kutwaa nafasi ya kujifunza juu ya njia ya Mungu.”
Hatimaye Nagundua Njia Pekee ya Kupata Haki ya Kijamii
“Daisy Gerken, nami, sikuzote tuliendelea kuwasiliana kwa simu, naye alikuja kuniona kila mwaka. Muda usio mrefu baada ya mimi kwenda Tucson, Arizona, uandikishaji wangu wa zawadi wa Mnara wa Mlinzi ulikwisha. Niliugua goti langu, kwa hiyo Adele Semonian, mmoja wa Mashahidi wa Yehova alipozuru, kwa tukio zuri nilikuwa nyumbani. Tulianza kujifunza Biblia pamoja. Hatimaye, nikapata kuelewa wazi maana halisi juu ya kweli. Nikang’amua singeweza kusuluhisha matatizo yote ya watu wangu na ‘kuwainua kiuchumi.’ Tatizo lilikuwa kubwa kuliko Bw. Neely. Kubwa kuliko Marekani Kusini. Kubwa kuliko Marekani. Kwa kweli, kubwa kuliko ulimwengu huu.
“Ni suala la ulimwenguni pote. Ni nani aliye na haki ya kutawala ulimwengu? Je! ni mwanadamu? Je! ni Shetani aliye adui wa Mungu? Au ni haki ya Muumba? Ni haki yake bila shaka! Mara tu suala hilo litakapotatuliwa, basi dalili za ukosefu wa haki za kijamii ambazo nilikuwa nimekuwa nikipigania maishani mwangu mwote zitatoweka. Na hata iwe nilikuwa nimetimiza nini, tungali twazeeka na kufa, iwe sisi ni weusi au weupe. Mungu atafanya dunia kuwa paradiso yenye haki ya kijamii kwa wote. Nilisisimuka nikiwa na taraja la kuishi milele na kutunza mimea na wanyama na kumpenda jirani yangu kama mimi mwenyewe—hivyo ikitimiza kusudi la awali la Mungu katika kuumba mwanamume na mwanamke hapa duniani. (Zaburi 37:9-11, 29; Isaya 45:18) Nilichachawa sana kujifunza kwamba haingenibidi kwenda mbinguni kuishi kwa kunywa maziwa na asali au sivyo nife njaa!
“Nina masikitiko fulani, hasa kwamba nilitumia sehemu kubwa ya maisha yangu nikitafuta haki ya kijamii kutoka kwa chanzo kisichofaa. Ningelipenda kumpa Mungu nishati za ujana wangu. Kwa kweli, nilifikiri nilikuwa nikifanya hivyo kwa kusaidia watu wengine. Ningali nawasaidia, lakini safari hii ni kwa kuelekeza watu kwenye tumaini la Ufalme wa Mungu chini ya Kristo Yesu, jina pekee lililopewa chini ya mbingu ambalo kwalo twaweza kuokolewa. (Mathayo 12:21; 24:14; Ufunuo 21:3-5) Baba yangu alikuwa akisema huku akinionyesha ngumi yake: ‘Ukifumba mkono wako sana hivi, basi hakuna kitu kitakachoingia wala kutoka.’ Nataka kufumbua mkono wangu ili niwape wengine msaada.
“Nilibatizwa nikawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova nikiwa na umri wa miaka 87. Siwezi kulegeza mwendo sasa kwa sababu wakati wangu ni mfupi. Ningali mwenye bidii lakini si kama hapo awali. Nimekosa labda mikutano miwili tu ya kutaniko katika miaka miwili iliyopita. Yanibidi nijifunze yote niwezayo ili niweze kufunza familia yangu kwa kadiri niwezayo watakapofufuliwa. Kwa msaada wa Adele, mimi hutumia kati ya saa 20 na 30 kwa mwezi katika utumishi wa shambani.
“Sasa, mambo hayo ambayo nimesema ni mambo makuu maishani mwangu. Nisingeweza kukueleza kila kitu, au sivyo tungeketi hapa juu ya gogo hili kwa majuma mengi hali tukipiga gumzo tu.”
Ghafula! nyoka mkubwa aishie majini akanyiririka kutoka nje na kupanda juu ya gogo, naye Addie akapaaza sauti: “Nyoka huyu ametoka wapi?” Akashika ghafula ufito wake wa kuvulia samaki na kamba ya samaki aliokuwa amevua na kuondoka hapo mara hiyo. Hoji hilo likakwisha.—Kama ilivyosimuliwa na Addie Clinton Few kwa ripota wa “Amkeni!” Muda mfupi baada ya hoji hili, Addie alikufa akiwa na umri wa miaka 97.