Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Upasuaji wa Macho Nilifurahia kusoma makala yenu “Keratotomia ya Nusu-Kipenyo—Ni Nini?” (Septemba 22, 1994) Nikiwa daktari mpasuaji anayehusika na ustadi wa mchepuko wa jicho, nikiwa nimefanyiwa keratotomia ya nusu-kipenyo kwenye macho yangu mwenyewe na nikiwa nimefanya taratibu zaidi ya 2,000, nilipendezwa sana na ubora na usahihi wa makala yenu. Kwa kusikitisha, habari inayotolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari mara nyingi haiwi sahihi na hupotosha. Nilihisi makala yenu ilifanya kazi nzuri kabisa ya kueleza faida na hasara za keratotomia ya nusu-kipenyo.
R. F. B., Marekani
Kifo Nataka kuwaambia jinsi nilivyothamini zile makala “Vijana Huuliza . . .” “Kwa Nini Baba Alikufa?” (Agosti 22, 1994) na “Nishindeje Huzuni ya Kifo cha Baba?” (Septemba 8, 1994) Hata ingawa bado nina wazazi wangu, majuzi nilishindwa na kifo cha wapendwa wawili waliokufa. Makala hizi ziliniletea faraja kubwa na kunionyesha jinsi ya kukabili msiba huo.
T. H., Ufaransa
Baba yangu alikufa kwenye Jumba la Ufalme baada ya kutoa hotuba. Tangu wakati huo nimekuwa nikishindana na huzuni na hasira. Nilisababu kwamba haikuwa haki kwamba mtu yeyote ambaye alimpenda sana Yehova na kujitoa kwake angepasa kufa kwa ghafula hivyo. Katika kusoma makala hizo, nilihisi kwamba Yehova alikuwa akionyesha ufikirio na kutoa msaada ili kuponya moyo wangu uliovunjika.
S. A., Nigeria
Baba yangu alikufa kwa kansa, na nilikuwa na wakati mgumu zaidi ya wote nikijaribu kukabiliana na hilo. Ilishangaza kuona jinsi makala hii ilivyopatana na hisia zangu mwenyewe kwa wazi mno. Kinachoniumiza ni kwamba baba yangu anakosa kila kitu kinachoendelea katika maisha yangu sasa. Nimeanza tu mradi wangu niliotamani sana wa maisha: kazi-maisha ya mweneza-evanjeli wa wakati wote. Nilitaka sana anione nikifanya hivyo. Kukosa uongozi wake mzuri na hekima ni kugumu nyakati fulani, lakini kujua kwamba kuna wengine wanaojali ni faraja kubwa.
C. T., Marekani
Kuutazama Ulimwengu Nataka kuwapongeza kuhusu namna yenye uangalifu ambayo Amkeni! hutayarishwa. Nathamini hasa ile sehemu “Kuutazama Ulimwengu.” Ingawaje hushughulika na vichwa tofauti-tofauti kwa ufupi, shauri layo lenye msaada, mada zenye kuchochea upendezi, na maoni yamenisaidia kubadili mengi ya mazoea yangu. “Kuutazama Ulimwengu” huandaa usomaji wenye kupendeza.
T. C. C., Brazili
Mbinu ya Heimlich Nimekuwa mfunzi mwenye kustahili wa huduma ya kwanza kwa miaka 11 na ningependa kutoa maelezo kuhusu habari iliyokuwa kwenye “Kuutazama Ulimwengu” juu ya “Kunyongwa na Chakula.” (Agosti 22 1994) Mwataja ile inayoitwa eti mbinu ya Heimlich. Hata hivyo, ni ujuzi wa kawaida kwamba mpigo kwenye msuko waweza kuondoa pumzi. Kwa hiyo mbinu ya Heimlich yaweza kufanya mambo yawe mabaya zaidi katika hali ya huduma ya kwanza.
G. B., Austria
Mamlaka fulani za kitiba za Kiulaya huona mbinu ya Heimlich kuwa hatari na hupendekeza itumiwe kama mbinu ya mwisho. Hata hivyo, madaktari katika Marekani, kwa ujumla huhisi kwamba inapotumiwa ifaavyo, mbinu ya Heimlich inashinda njia nyingine zote za kusaidia wale wenye kunyongwa na chakula. Hatari ya kupata majeraha ya ndani ya mwili hufikiriwa kuwa ndogo ikilinganishwa na hatari ya kunyongwa na chakula hadi kifo. Kwa kielelezo, uchunguzi mmoja wa Marekani ulidai kwamba ni mitokezo minne tu ya utumbo inayohusianishwa na mbinu ya Heimlich ambayo ilikuwa imewekwa kwenye maandishi. Iwe kwamba madaktari wa Ulaya na Marekani watafikia upatano kuhusu jambo hili wakati wowote karibuni labaki kuonekana.—Mhariri.