Kuutazama Ulimwengu
Fedha za Damu
Katika 1994 watu wa Ujerumani walipigwa butwaa walipojua kwamba watu 2,500 hivi walikuwa wameambukizwa HIV kupitia utiaji-damu mishipani na vifanyizwa vya damu. (Ona Amkeni! la Aprili 22, 1994, ukurasa 28.) Katika mjadala bungeni katika Januari 1995, laripoti Süddeutsche Zeitung, waziri wa afya wa huo muungano aliwaomba majeruhi “msamaha kwa niaba ya serikali” kwa makosa ambayo yalizidisha magumu yao. Katika huo mjadala ilisemwa kwamba hasa biashara ya kutengeneza madawa pamoja na madaktari walikuwa wachangizi wakuu na kwamba shirika la Msalaba Mwekundu la Ujerumani liliharibu sifa yalo kwa kujaribu liwezavyo ili kuwa “mtengeneza madawa kutoka kwa damu.” Mwanamke mmoja ambaye aliambukizwa HIV na mume wake aliyekufa alilalamika hivi: “Angalau watu 70 wasiotungama damu wangeliweza kuwa hai bado ikiwa [biashara ya kutengeneza madawa] wakati huo ingefikiria mengine isipokuwa kutengeneza fedha tu.”
Uhaba wa Mapadri
Wakati mmoja Hispania iliyojulikana kwa kupeleka wamishonari Wakatoliki nchi za nje, sasa yang’ang’ana kutosheleza uhitaji wayo wa mapadri. Gazeti la habari El País la Madrid laripoti kwamba jumla ya idadi ya mapadri katika Hispania yadidimia kwa 150 kila mwaka. Mamlaka za Kanisa zahofu kwamba wanafunzi wa seminari 2,000 walioandikishwa kwa sasa hawatatosheleza uhitaji wa mapadri wachungaji wa wakati ujao. Mwaka jana ni mapadri 216 tu walioagizwa rasmi—wapungua kwa 73 zaidi kuliko 1993—na asilimia 70 ya makasisi wa Hispania wana umri uliopita miaka 50. Kwa upande ule mwingine, hivi majuzi Mashahidi wa Yehova katika Hispania wameona idadi ya mapainia ikiongezeka kwa 300 kila mwaka. Mapainia ni wahudumu wasiolipwa wanaotumia angalau muda wa saa 90 kila mwezi wakihubiri habari njema ya Ufalme.
Hatari Zaidi za Utiaji-Damu Mishipani
Kulingana na The Canberra Times la Australia, shirika la Msalaba Mwekundu limeonya madaktari kwamba damu chafu yaweza kupitisha ambukizo fulani la bakteria yenye kuua na kwamba hadi leo hakujapatikana njia hususa ya kuchungua hicho kiumbe hai. Likirejezea habari fulani katika The Medical Journal of Australia, gazeti la Times lasema kwamba watu wanne katika jimbo la New South Wales walikufa kutokana na damu hii iliyoambukizwa na bakteria kati ya 1980 na 1989. Makala hiyo ya gazeti la habari ilitaarifu zaidi hivi: “Tatizo ni kwamba hiyo bakteria, Yersinia enterocolitica, yaweza kukua kwa haraka katika vifuko vya damu hata wakati damu yakaribia kuganda. Watu ambao wamepata kuwa na maambukizo ya tumboni majuma kadhaa kabla ya kuchanga damu pindi kwa pindi wanaweza kupitisha hicho kiumbe hai, ambacho chaweza kuzaana sana wakati damu inapokuwa ingali akibani ikingojea kutiwa mishipani. Wagonjwa wanaotiwa damu mishipani waweza kupata mshtuko wa ghafula na kifo kutokana na hiyo sumu.”
Watoto Wanene Mno wa Kanada
“Wanalishe wengi, matabibu wa watoto na watafiti” wasema kwamba “wazazi wenye wasiwasi wanalisha watoto wao chakula kisicho na lishe bora, kilichotayarishwa kwa muda mrefu na chenye shahamu nyingi,” laripoti The Globe and Mail. Mara nyingi wazazi wote wanapofanya kazi, maisha huwa yenye shughuli mno, yakiacha wakati mchache sana, kwa familia kula pamoja milo yenye lishe. Matokeo ni nini? Kulingana na makadirio ya wataalamu, “angalau asilimia 20 ya watoto Wakanada ni wanene mno kwa sababu ya mlo wenye shahamu nyingi na kukosa mazoezi,” lasema The Globe. Dakt. Stan Kubow, profesa mshiriki wa shule ya mlo na lishe kwenye Chuo Kikuu cha McGill katika Montreal, asema usawaziko wahitajiwa. Asema wazazi wahitaji “kuhakikisha kuna maziwa, protini, matunda, mboga na utembo katika milo yao [watoto].” Mtafiti mmoja mwenye hangaiko aliuliza hivi: “Ikiwa hujali afya yako, wewe hujali kuhusu nini basi?”
Tahadhari ya Asbesto Yaendelea
Maelfu ya wafanyakazi wa kujenga wa Uingereza watakufa kutokana na kansa isababishwayo na asbesto kwa sababu ya makadirio yenye kasoro ya wakuu wa usalama, laripoti gazeti New Scientist. Miaka iliyopita, katika miaka ya 1960, wataalamu wa tiba walipokuwa wakisema kwamba nyuzi za asbesto zilikuwa hatari kwa afya, serikali ya Uingereza ilianzisha miongozo ya viwanda ili kupunguza ukolevu wa nyuzi hizi katika hewa. Hata hivyo, watafiti sasa wapata kwamba wafanyakazi walio hatarini zaidi ni maseremala, mafundi wa umeme, mafundi wa mifereji, na waweka mabomba ya gesi, wafanyao kazi bila ulinzi kwa vifaa vyenye asbesto. Kwa sababu aina moja ya kansa ya mapafu huchukua miaka 30 kutokeza, kosa hilo limevumbuliwa hivi majuzi tu. Kwa sasa haijulikani ni taratibu zipi za ujenzi ama bidhaa za asbesto zilizo hatari zaidi. Likiwa tokeo, Shirika la Afya na Usalama la Uingereza lahimiza wafanyakazi wa kujenga wawe macho sana ikiwa wanapata chombo chenye asbesto na kuripoti fadhaiko lao kwa waajiri wao, ambao wapaswa kuchunguza kitu hicho na kuandaa ulinzi unaofaa.
Mshindi Ni Nani?
“Katika biashara ya kamari, hakuna cha kupata hasara,” laripoti Veja. Hilo gazeti lasema kwamba Wabrazili hutumia karibu dola bilioni 4 (za Marekani) kila mwaka kwa michezo ya bahati nasibu na zile aina nyingine za kucheza kamari. Hiyo ni zaidi ya mapato ya mwaka ya biashara iliyo kubwa ya kitaifa ya magari! Ile sehemu ya bingo ya kujumuika na wengine huvutia sana. “Katika bingo waweza kuongea na watu usiowajua au unaowafahamu, kula, kunywa, na kushangilia huku ukijaribia bahati yako,” gazeti hilo likaripoti. Lakini mshindi ni nani? “Hakuna aina nyingine ya kucheza kamari iliyopo ambayo ni yenye mapato ya juu kuliko bingo,” akadai mwanahisibati Oswald de Souza. “Mshindi wa duru [ya bingo] hupokea asilimia 45 tu ya fedha zote zilizotumiwa kwenye mchezo wa kamari.”
Matatizo Yazidi Masuluhisho
Licha ya uhakika wa kwamba serikali ya India huandaa fedha kwa programu ya chakula iliyo kubwa kupita zote ulimwenguni, bado kuna watu milioni 250 katika nchi hiyo ambao wanateseka kutokana na aina tofauti-tofauti za utapiamlo. Ripoti ya Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa yaonyesha kwamba licha ya jitihada zinazofanywa, asilimia 43.8 ya watoto katika India wanateseka kutokana na utapiamlo wa kukosa nishati za protini. Kwa kuongezea, milioni 6.6 wamedumaa kidogo na wana tatizo la kutendesha mishipa, milioni 2.2 wamepatwa na kasoro za kimwili na kiakili, na kila mwaka 60,000 wanakuwa vipofu kutokana na ukosefu wa vitamini. Miongoni mwa watoto ambao bado kwenda shuleni asilimia 56 wana upungufu wa madini, na watoto wako miongoni mwa watu milioni 40 walio na ugonjwa wa rovu.
Kununua Chakula cha Mikebe Iliyobonyea
“Wanunuzi wa vyakula madukani, ili kujaribu kuokoa fedha, huenda wakawa wananunua au kuweka mikebe ambayo imepaswa kutupwa kwani yaweza kudhuru afya,” laonya Winnipeg Free Press. “Mingi ya mikebe ya kuwekea chakula iliyobonyea yakubalika, lakini mingine haikubaliki,” akasema Peter Parys wa idara ya afya ya jiji. “Kwa kawaida mikebe huwa salama wakati wa kupakia chakula; madhara huja baadaye.” Orodha fupi ya kile cha kutupa, kulingana na idara ya afya ya jiji, yatia ndani kutu kwenye vizibo, kutu zisizosugulika kwenye sehemu ya juu au pande za mkebe, ama utikiswapo mtikisiko kama wa umajimaji, pamoja na mikebe ambayo imefura ama kuvimba kwa njia yoyote, mikebe yenye kuvuja, na mikebe isiyo na alama au alama iliyopitisha siku. Ripoti ya gazeti la habari yatahadharisha hivi: “Kizibo unapovunjika, mikebe huja kuwa mahali pafaapo pa kuzalishia salmonella na staphylococcus. Kila moja ya hizo bakteria yaweza kusababisha kuhara, kutapika, na msokoto wa tumbo.”
Viwango vya Chini vya Uzaaji
Waume na wake wengi katika Ulaya Mashariki wanaahirisha kuzaa kwa sababu ya hali ya kukosa usalama wa kifedha na kazi. The New York Times lataja kwamba “kukosa usalama kumeongoza si tu kwa upungufu wa haraka wa kiwango cha uzaaji bali pia kushuka kwa viwango vya ndoa na ongezeko la zaidi ya mara kumi la uhasishwaji.” Times laongezea kwamba kulingana na wataalamu wa kukadiria idadi ya watu “upungufu wa haraka hivyo haujapata kamwe kuonekana isipokuwa katika nyakati za vita, tauni ama njaa.” Ili kukomesha mwelekeo huu, serikali za Hungaria, Luxembourg, Poland, Ubelgiji, na Ureno kwa muda zimetoa fedha kwa familia zenye kupata watoto kama kichochezi cha kupata watoto. Hivi karibuni zaidi, serikali ya jimbo la Kijerumani la Brandenburg ilianza kutoa dola 650 kwa kila mtoto aliyezaliwa.
Madhara Yenye Kudumu ya Vita
Majeruhi wa vita katika ile iliyokuwa Yugoslavia watia ndani wengi zaidi ya wale waliouawa ama kulemazwa na risasi ama mabomu. Uchunguzi wa hivi majuzi wafunua kwamba “mamia ya tani za dutu zenye sumu zilizoachiliwa kwenye hayo mazingira na mioto, milipuko na mivujo ya kemikali zitakuwa na madhara mabaya ya kiafya,” lasema The Medical Post. Kemikali hizi na metali zenye sumu zachafua mito na huenda hata zikachafua matungamo ya maji yaliyoko chini ya ardhi. Kulingana na Post, wataalamu waonya kwamba kutakuwa na “ongezeko lenye kutokeza la idadi ya watoto wenye kasoro za kuzaliwa likiwa tokeo la wazazi wao kunywa maji yaliyochafuliwa na dutu zenye sumu.”