Kuutazama Ulimwengu
Pigo la Maradhi ya Kuambukizwa
Thuluthi moja ya vifo milioni 52 vilivyotokea mwaka uliopita ilisababishwa na maradhi ya kuambukizwa, lasema Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Wengi kati ya wanaokadiriwa kuwa milioni 17 waliokufa walikuwa watoto wachanga. Kulingana na The World Health Report 1996, iliyotolewa na WHO, angalau maradhi mapya 30 ya kuambukizwa yametambulishwa katika miaka 20 ambayo imepita, kutia ndani virusi vya Ebola pamoja na UKIMWI. Ingawa maradhi makubwa kama vile kifua kikuu, kipindupindu, na malaria yaweza kukingwa au kutibiwa kwa gharama ya chini, hayo yanarudi nayo yamezidi kukinza dawa. Ripoti hiyo yasema kwamba sababu ni “matumizi yasiyodhibitiwa na yasiyofaa ya dawa za viuavijasumu,” pamoja na mambo mengine, kama vile usafiri wa kimataifa na ukuzi wa idadi ya watu katika maeneo ya kitropiki yenye kujaa mbu.
Ungamo Katika Maduka ya Kuuza Vitabu
Shirika la Katoliki la Italia limeamua kuweka sehemu za ungamo katika maduka yao mengi ya kuuza vitabu vya kidini, kila sehemu ikiwa na kasisi asikilizaye ungamo. Jaribio hilo lilianza katika Milan. Kila Jumatano katika duka la kuuza vitabu jijini, kasisi alikuwapo kwa ajili ya “wote wanaotaka kumwona kasisi—lakini si kanisani—ili kuomba shauri la kiroho, au hata kuungama,” akasema meneja wa duka hilo. Aliongezea: “Matokeo ya kwanza yalikuwa bora zaidi kuliko matarajio yetu makubwa zaidi.” Kwa nini kufanya hivyo? “Ili kuongeza ungamo la sakramenti,” laeleza gazeti la habari la Italia La Repubblica.
Hakuna Chochote Kinachotupwa
Baada ya nyama za kilo 270 hivi kuondolewa, ni nini hufanywa na sehemu za ng’ombe zinazobaki? Baadhi ya viungo vya ndani, kama vile thiroidi, kongosho, mapafu, wengu, tezi adrenali, vifuko vya mayai, tezi pituitari, na nyongo kutoka ini na kibofu cha nyongo, hutumiwa kutengeneza dawa. Kolajeni huziduliwa kutoka mifupa, kwato, na ngozi ili itumiwe katika viongeza-unyevu na mafuta ya kupaka. Ufupa mwororo na shahamu hutumiwa katika vitu kama vile butyl stearate, PEG-150 distearate, na glycol stearate ambazo hutumiwa katika mapambo mengi na bidhaa za nywele. Sabuni nyingi hutengenezwa kwa shahamu. Na mifupa na kwato husagwa ili kutengeneza jelatini ambazo hutumiwa katika mamia ya vyakula, kama vile aisikrimu, peremende fulani, na bidhaa nyinginezo “zisizo na mafuta.” Sehemu nyinginezo pia hutumiwa katika bidhaa tofauti-tofauti kama vile kalamu za rangi, viberiti, nta ya sakafuni, linoliamu, kizuia-mgando wa barafu, saruji, viua-magugu, selofeni, karatasi ya picha, bidhaa za michezo, upambaji wa vitu, na mavazi. Bei ya juu zaidi ambayo hulipiwa vijiwe vya nyongo—dola 600 (za Marekani) kwa ratili moja! Wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Mbali huvinunua ili vitumiwe katika dawa za nguvu za uzazi.
Msiba wa Kuzaa
Karibu wanawake 585,000 hufa kila mwaka wakiwa waja wazito au wakizaa, wasema uchunguzi mmoja wa kina uliofanywa na UNICEF (Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa). Kulingana na hiyo ripoti The Progress of Nations 1996, mingi ya misiba ya kuzaa yaweza kuzuiwa. Inasema: “Mara nyingi, hivi si vifo vya wagonjwa, wala vya wazee sana, wala vya wachanga mno, bali ni vya wanawake wenye afya walio kwenye upeo wa maisha yao.” Wanawake wapatao 75,000 hufa kila mwaka kwa sababu ya utoaji-mimba usiofaulu; na 40,000 kutokana na kukwama kwa mtoto wakati wa kuzaa; na 100,000 kutokana na kusumishwa kwa damu; na 75,000 kutokana na madhara ya ubongo na figo yatokezwayo na eclampsia (mapindo na msongo wa juu wa damu mwishoni-mwishoni mwa uja-uzito); na zaidi ya 140,000 kutokana na kuvuja damu. Ukosefu wa utunzi wa wakunga katika nchi nyingi husemwa kuwa kisababishi kikuu. Maofisa wa UNICEF wasema habari zaonyesha kwamba wastani wa mwanamke 1 kati ya wanawake 35 katika Asia ya Kusini na 1 kati ya 13 katika Afrika iliyo kusini ya Sahara hufa kutokana na mambo yanayohusika na uja-uzito na kuzaa, kwa kulinganisha na 1 kati ya 7,300 Kanada, na 1 kati ya 3,300 Marekani, na 1 kati ya 3,200 Ulaya. Hizo tarakimu ni za juu kwa karibu asilimia 20 kuliko kadirio la awali la vifo vipatavyo 500,000 kila mwaka.
Visa vya UKIMWI Vingali Vinaongezeka
“Vile virusi ambavyo husababisha UKIMWI huendelea kuenea katika sehemu kubwa-kubwa za ulimwengu, hasa katika Asia na kusini mwa Afrika, na idadi ya watu wenye ugonjwa wa UKIMWI pia imeongezeka haraka sana,” laripoti The New York Times. Habari zilizokusanywa na Programu ya Pamoja ya Umoja wa Mataifa juu ya H.I.V.-UKIMWI zaonyesha kwamba katika 1995 watu wapatao milioni 1.3 walikuwa wagonjwa kwa dalili za UKIMWI, ongezeko la asilimia 25 kuliko mwaka uliopita. Sasa inakadiriwa kwamba watu wazima milioni 21 ulimwenguni pote wameambukizwa HIV, na kwamba karibu asilimia 42 kati yao ni wanawake. Na watu wengine 7,500 zaidi huambukizwa kila siku. Mamilioni kadhaa ya watoto pia yasemekana wameambukizwa. Huchukua karibu miaka kumi tangu wakati wa ambukizo mpaka ugonjwa wenyewe uonekane kwa uzito. Ripoti ya UM yakadiria kwamba watu 980,000 walikufa kutokana na maradhi yanayohusika na UKIMWI katika 1995 na kwamba idadi hiyo itaruka hadi 1,120,000 katika 1996. Hivi majuzi virusi hivyo vimeenea sana kusini mwa Afrika na India, na vinatarajiwa kuenea kwa njia hiyo katika China na Vietnam. Kiwango cha ambukizo katika baadhi ya mataifa ya Afrika tayari ni juu kufikia asilimia 16 hadi 18. Ni jambo la kutia wasiwasi kwamba idadi ya wanawake vijana wanaoambukizwa inaongezeka haraka sana ulimwenguni pote. Thuluthi moja ya watoto wanaozaliwa na wanawake hawa pia watakuwa na virusi hivyo.
Tahadhari na Mwendo wa Kasi!
Kuendesha gari kwa kasi mno huua Waingereza 1,000 kila mwaka na kujeruhi 77,000, laripoti The Daily Telegraph la London. Hata kudumisha kiwango cha mwendo unaotakikana kwaweza kuwa si salama katika hali fulani. Zaidi ya asilimia 10 ya aksidenti zinazotokea katika barabara za mwendo wa kasi husababishwa na kuendesha gari karibu mno na gari lililoko mbele. Kanuni ya Barabara ya Uingereza yapendekeza kwamba uache nafasi ya sekunde mbili kati yako na gari lililoko mbele, lakini hilo lapaswa kurudufishwa unapoendesha gari katika barabara yenye maji-maji au yenye kuteleza au wakati huwezi kuona mbali. Kufuata gari jingine kwa ukaribu si salama na pia huchosha na kusababisha mikazo. Mara nyingi madereva hulalamika kwamba wanapoacha nafasi ifaayo, gari jingine huja na kuingia katika nafasi hiyo. Lakini, itikio salama la pekee ni kupunguza mwendo wako na kuacha nafasi hiyo iwe kubwa tena. Kushika breki kwa ghafula kwaweza kusababisha aksidenti, hivyo tahadhari na hatari zozote ziwezazo kutokea. Kuwa na breki za kufungua magurudumu hakupunguzi umbali wa kusimamisha gari. Paul Ripley ambaye ni mfunzi wa kuendesha magari asema hivi: “Mwendo salama wakati wowote ule mara nyingi ni kidogo sana kuliko vile madereva wengi wang’amuavyo.”
Madaktari-Wapasuaji, Tahadharini na Mnachosema
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Erasmus katika Uholanzi wamepata kwamba wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wanaweza “kusikia,” hata kama wamepewa dawa ya kawaida ya nusukaputi. Baada ya upasuaji, wagonjwa 240 walipewa silabi ya kwanza ya neno ambalo lilikuwa limetajwa wakati walipokuwa wakifanyiwa upasuaji nao waliulizwa walikamilishe kwa kusema neno la kwanza lililokuja akilini mwao. Hata muda wa saa 24 baadaye, wagonjwa wengi waliweza kukumbuka maneno ambayo yalikuwa yametajwa mara moja tu. Hilo ladokeza, watafiti wasema, kwamba wagonjwa waliopewa dawa ya nusukaputi waweza “kusikiliza” wanapofanyiwa upasuaji nao waweza kuhisi vibaya juu ya maneno hasi au yenye kutukana. Hiyo Research Reports From the Netherlands, iliyotolewa na Shirika la Uholanzi la Utafiti wa Kisayansi ilikata kauli hivi: “Basi wafanyakazi wa kitiba watahitaji kutahadhari juu ya maongeo yao wakati wa kufanya upasuaji.”
“Maradhi ya Kichaa cha Ng’ombe”
◼ Kutokea kwa “maradhi ya kichaa cha ng’ombe” katika Uingereza kumefanya jambo moja ambalo limekuwapo kwa muda mrefu katika ufugaji wa wanyama litokezee. Wanyama wamegeuzwa kutoka hali yao ya asili ya kula majani hadi kuwa walaji wa nyama kwa kulishwa sehemu za wanyama wengine. Damu iliyokaushwa, mifupa iliyopondwa, na nyama, au vyakula vilivyotengenezwa, ambavyo vinatia ndani matumbo, uti wa mgongo, bongo, na viungo vingine vya ndani, kama vile kongosho, koo, na figo zilizosagwa-sagwa hutumiwa kwa kawaida ili kuhifadhi, kuongeza mapato, na kuharakisha ukuzi wa mnyama. Kufikia wakati ndama wa kawaida anapotimia umri wa miezi sita, amelishwa kwa karibu kilo 12 za chakula kilichotengenezwa kwa masazo ya wanyama wengine, asema Dakt. Harash Narang, mmoja wa wataalamu ambao walikuwa wa kwanza kutoa onyo kuhusu maradhi hayo. “Nilishangaa,” akasema, akirejezea ziara yake kwa kichinjio. “Sisi hasa tulikuwa tunarejesha ng’ombe kwa ng’ombe. Kwangu mimi, hiyo ni hali ya wanyama kula wanyama wa aina yao.”
◼ Kwa jambo lisilo zito, mkulima mmoja wa Uingereza wa ng’ombe wa maziwa amepata njia ya kutumia ng’ombe wazee ambao hawezi kuwauza kwa faida kwa sababu ya ogofyo la “maradhi ya kichaa cha ng’ombe.” Kama ilivyoripotiwa katika gazeti Newsweek, yeye huwatumia kubeba mabango. Yeye huweka matangazo ya biashara juu ya ng’ombe wake wanapolisha kando ya barabara kuu yenye shughuli nyingi naye hupata karibu dola 40 kwa kila ng’ombe kila juma. “Ni lazima tutafute njia mpya za mapato,” mkulima huyo akasema. “Inaonekana ni njia nzuri kwa hawa ng’ombe kulipia gharama za kuwatunza.”