Louis Pasteur—Kilichofunuliwa na Kazi Yake
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UFARANSA
JE, UHAI waweza kutokea wenyewe kutoka chanzo kisicho na uhai? Katika karne ya 19, wanasayansi fulani walifikiri hivyo. Walihisi kwamba uhai unaweza kujitokeza wenyewe kutoka mata isiyo na uhai, bila mwingilio wa muumba.
Lakini kwenye jioni ya masika katika Aprili 1864, wasikilizaji waliokuwapo katika jumba la mkutano kwenye Chuo Kikuu cha Sorbonne katika Paris walisikia jambo tofauti. Katika utoaji wenye umahiri mbele ya tume ya wanasayansi, Louis Pasteur kwa mafanikio alithibitisha kuwa kosa ile nadharia ya kwamba uhai ulijitokeza kutoka kwenye kitu kisicho na uhai.
Utoaji huu na uvumbuzi mwingine wa baadaye ulimfanya awe “mmoja wa wanasayansi wakuu zaidi ulimwenguni,” kama inavyosema The World Book Encyclopedia. Lakini kwa nini mtu huyo aliacha athari kama hiyo kwa wale wa wakati wake, naye alikuja kujulikanaje ulimwenguni kote? Sisi hunufaikaje wakati huu na baadhi ya uvumbuzi wake?
Utafiti wa Mapema
Louis Pasteur alizaliwa katika 1822 katika mji mdogo wa Dôle, mashariki mwa Ufaransa. Baba yake, mtengenezaji wa ngozi ili zisioze, alimtakia mwana wake makuu. Licha ya kuwa na mwelekeo wa sanaa, na vilevile kipawa halisi cha usanii, Louis alikubali kuchukua masomo ya sayansi. Alipata digrii ya cheo bora katika sayansi alipokuwa na umri wa miaka 25.
Utafiti wake wa mapema ulihusu asidi tatariki, msombo upatikanao katika machujo yaliyoachwa katika mapipa ya divai. Matokeo ya utafiti huo yalitumiwa na watafiti wengine miaka michache baadaye kuweka msingi wa kemia kikaboni ya kisasa. Kisha Pasteur akaendelea kuchunguza vitenzi vya uchachishaji.
Kabla ya utafiti wa Pasteur, kuwapo kwa vitenzi vya uchachishaji kama vile hamira kulijulikana. Lakini vilifikiriwa kuwa tokeo la uchachukaji. Hata hivyo, Pasteur alithibitisha kwamba vitenzi hivi vya uchachushaji havikuwa tokeo la uchachukaji, bali ndivyo vilivyosababisha uchachukaji. Alionyesha kwamba kila aina ya kitenzi ilisababisha namna tofauti ya uchachukaji. Ripoti aliyochapisha juu ya hili katika 1857 leo inaonwa kuwa “cheti cha kuzaliwa cha mikrobiolojia.”
Kuanzia hapo na kuendelea, kazi na uvumbuzi wake ulisonga mbele. Kwa sababu ya sifa yake, watengenezaji wa siki katika Orléans walimwendea ili atatue matatizo yao mengi magumu. Pasteur alithibitisha kwamba kitenzi kinachohusika katika kugeuza divai kuwa siki ndicho kile kiitwacho sasa kijiumbe, ambacho kilikuwa kwenye sehemu ya juu ya kiowevu. Mwishoni mwa utafiti wake, alitoa mbele ya watengenezaji wa siki na waadhamu wa mji huo lile somo lake lijulikanalo sana “Somo juu ya Siki ya Divai.”
Upasteurishaji (Uuaji wa Vijiumbe)
Utafiti wa Pasteur wa uchachukaji ulimwezesha kufikia mkataa kwamba mengi ya matatizo ya usibishaji katika kiwanda cha vyakula yalisababishwa na vijiumbe-maradhi. Vijiumbe-maradhi vilikuwa hewani au katika viwekeo visivyooshwa ifaavyo. Pasteur alidokeza kwamba kuharibika kwa bidhaa za chakula kunakosababishwa na bakteria kungeweza kuzuiwa kwa kuboresha usafi na kuharibika kwa viowevu kungeweza kuzuiwa kwa kudumisha halijoto ya kati ya digrii 50 na 60 Selsiasi kwa dakika chache. Njia hii ilitumiwa kwanza kwenye divai ili kuzuia uchachukaji usiotakikana. Vijiumbe-maradhi vikuu viliuawa bila kusababisha badiliko katika ladha au harufu ya divai.
Utaratibu huu, upasteurishaji, uliotokana na Pasteur, ulirekebisha biashara ya chakula. Siku hizi ufundi huu hautumiwi tena kwa divai bali bado wafaa kwa bidhaa kadhaa kama vile maziwa na maji ya matunda. Hata hivyo, njia nyinginezo, kama vile uhasishaji kwa halijoto ya juu zaidi, waweza pia kutumiwa.
Biashara nyingine kubwa iliyonufaika kutokana na utafiti wa Pasteur ilikuwa ni ile ya kutengeneza pombe. Katika wakati huo, Wafaransa walikuwa na matatizo mengi ya utokezaji na ushindani wenye nguvu wa Wajerumani. Pasteur akashughulikia matatizo hayo na kutoa mashauri mengi kwa watengenezaji hao wa pombe. Yeye alidokeza kwamba wakazie uangalifu usafi wa togwa ya mtengenezaji pombe na vilevile usafi wa ujumla wa hewa ya eneo hilo. Mafanikio yalitokea bila kukawia, naye akapata haki nyingi za ubuni baada ya hapo.
Uhai Hutoka Katika Uhai
Tangu nyakati za kale, dhana nyingi za ajabu zilikuwa zimetokezwa ili kueleza kutokea kwa wadudu, mabuu, au viumbe vinginevyo vipatikanavyo katika mata yenye kuoza. Kwa mfano, katika karne ya 17, mwanakemia Mbelgiji alidai kwamba alikuwa amefanya panya atokee kwa kuweka blausi chafu katika mtungi wenye ngano!
Katika wakati wa Pasteur mjadala miongoni mwa wanasayansi ulikuwa umepamba moto. Ulikuwa mwito wa ushindani kwelikweli kukabili watetezi wa nadharia ya kwamba uhai ulijitokeza wenyewe kutoka kitu kisicho na uhai. Lakini kwa sababu ya kile alichokuwa amejifunza katika utafiti wake wa uchachukaji, Pasteur alikuwa na uhakika. Kwa hiyo alifanya majaribio yaliyonuiwa kukomesha kabisa-kabisa wazo la kwamba uhai ulijitokeza wenyewe.
Jaribio lake akitumia chupa zenye shingo nyembamba ni mojapo majaribio yake yajulikanayo sana. Kirutubisho cha kiowevu kilichoachwa nje katika chupa isiyofunikwa huingia viini haraka. Hata hivyo, kiwekwapo katika chupa ambayo huishia kwa shingo nyembamba, kirutubisho hichohicho cha kiowevu hubaki bila kuingia viini. Kwa nini iwe hivyo?
Maelezo ya Pasteur yalikuwa sahili: Zinapopitia kwenye shingo nyembamba, bakteria zilizo hewani zinaachwa kwenye uso wa glasi, hivi kwamba hewa haina viini inapofika kwenye kiowevu. Viini ambavyo hutokea katika chupa isiyofunikwa havijitokezi vyenyewe kutokana na kirutubisho cha kiowevu bali husafirishwa hewani.
Ili kuonyesha kwamba hewa ni kisafirishaji kikuu cha vijiumbe-maradhi, Pasteur alikwenda hadi Mer de Glace, barafuto katika milima ya Alps ya Ufaransa. Kwenye kimo cha futi 6,000, yeye alifunua chupa zake zilizofunikwa na kuacha hewa iingie. Kati ya chupa 20, ni moja tu iliyoingiwa na viini. Kisha akaenda kwenye sehemu ya chini ya Milima ya Jura na kurudia jaribio lilo hilo. Hapa, kwa kuwa kimo kilikuwa chini sana, chupa nane ziliingiwa na viini. Hivyo akathibitisha kwamba kwa sababu ya hewa safi zaidi kwenye vimo vya juu zaidi, hakukuwa na hatari nyingi ya kuingiwa na viini.
Kupitia kwa majaribio kama hayo Pasteur alionyesha kwa njia ya kusadikisha kwamba uhai hutokana na uhai uliokuwapo tu. Huo haujitokezi kinafsia, yaani, wenyewe.
Pigano Dhidi ya Maradhi Yenye Kuambukiza
Kwa kuwa uchachukaji huhitaji kuwapo kwa vijiumbe-maradhi, Pasteur alisababu kwamba ndivyo ilivyopasa kuwa kuhusu maradhi yenye kuambukiza. Uchunguzi wake wa maradhi ya kiwavinondo, tatizo kubwa la kiuchumi kwa watokezaji wa hariri katika kusini ya Ufaransa, ulithibitisha kwamba kusababu kwake kulikuwa sahihi. Mnamo miaka michache, aligundua kisababishi cha maradhi mawili na kudokeza njia zenye uangalifu za kuchagua viwavinondo wenye afya. Jambo ambalo lingezuia maradhi yenye kuenea.
Alipokuwa akichunguza kipindupindu cha kuku, Pasteur aligundua kwamba ukuzi wa kiini kilichokuwa na miezi michache tu hakikufanya kuku wawe wagonjwa bali kiliwakinga na ugonjwa. Likiwa tokeo, aligundua kwamba angeweza kuwachanja kwa namna iliyodhoofishwa ya kiini hicho.
Pasteur hakuwa wa kwanza kutumia chanjo. Mwingereza Edward Jenner alikuwa ameitumia kabla yake. Lakini Pasteur ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia kitenzi cha maradhi chenyewe katika namna iliyodhoofishwa badala ya kutumia kijiumbe-maradhi kingine kinachohusiana. Yeye pia alifanikiwa kupata chanjo dhidi ya kimeta, maradhi yenye kuambukiza ya wanyama wenye damu moto, kama vile ng’ombe na kondoo.
Kufuatia hili, aliendelea kufanya pigano lake la mwisho na lijulikanalo sana, dhidi ya kichaa cha mbwa. Ingawa hakutambua, kwa kukabili kichaa cha mbwa, Pasteur alikuwa akishughulika na uwanja ulio tofauti sana na ule wa bakteria. Sasa alikuwa akishughulika na virusi, ambavyo hangeweza kuviona kwa hadubini.
Mnamo Julai 6, 1885, mama fulani alimpeleka mvulana wake mwenye umri wa miaka tisa kwenye maabara ya Pasteur. Mtoto huyo alikuwa ametoka tu kuumwa na mbwa mwenye kichaa. Licha ya sihi za mama huyo, Pasteur alisita kumsaidia mvulana huyo. Hakuwa daktari na alikuwa hatarini mwa kushtakiwa kutibu kinyume cha sheria. Isitoshe, hakuwa amejaribu njia zake kwa mwanadamu. Hata hivyo, alimwomba aliyekuwa akifanya kazi pamoja naye, Dakt. Grancher, amchanje mvulana huyo. Alifanya hivyo, kukiwa na mafanikio. Kati ya watu 350 waliotibiwa kwa muda usiozidi mwaka mmoja, ni mmoja tu—aliyeletwa kuchelewa—ambaye hakunusurika.
Kwa wakati huohuo, Pasteur alikuwa akitoa uangalifu kwa usafi wa hospitali. Homa ya ambukizo la kondo ilikuwa ikisababisha vifo vya wanawake wengi sana kila mwaka kwenye hospitali ya uzaaji ya Paris. Pasteur alidokeza ufundi wa aseptia na kuzingatia sana usafi, hasa wa mikono. Uchunguzi wa baadaye uliofanywa na daktari mpasuaji Mwingereza Joseph Lister na wengine ulithibitisha usahihi wa mikataa ya Pasteur.
Kazi Yenye Thamani
Pasteur alikufa katika 1895. Lakini kazi yake ilikuwa na thamani, nasi twanufaika na sehemu zayo hata leo. Hiyo ndiyo sababu ameitwa “mfadhili wa wanadamu wote.” Jina lake bado lahusianishwa na chanjo na taratibu ambazo yeye hutambuliwa kuwa ndiye aliyezianzisha.
L’Institut Pasteur, taasisi iliyoanzishwa katika Paris wakati Pasteur alipokuwa angali hai ili kutibu kichaa cha mbwa, leo ni kitovu kinachoheshimiwa sana cha uchunguzi wa maradhi yenye kuambukiza. Inajulikana hasa kwa kazi yayo ya chanjo na dawa—na hata zaidi tangu 1983 wakati kikundi cha wanasayansi wayo, wakiongozwa na Profesa Luc Montagnier, walipotambulisha kwa mara ya kwanza kirusi cha UKIMWI.
Mjadala wa uhai kujitokeza wenyewe, ambao Pasteur alihusika nao na ambao aliibuka akiwa mshindi, haukuwa ulaghai wa kisayansi tu. Ulikuwa zaidi ya hoja yenye kupendeza ya kuzungumziwa miongoni mwa wanasayansi wachache tu au watu wenye akili. Ulikuwa na umaana mkubwa zaidi—ulihusisha uthibitisho uliohusu kuwapo kwa Mungu.
François Dagognet, mwanafalsafa Mfaransa aliyeshughulika hasa na sayansi, ataja kwamba “wapinzani [wa Pasteur], wenye kuamini nadharia kwamba hakuna uhai usioonekana na vilevile waatheisti, waliamini kwamba wangeweza kuthibitisha kwamba kiumbe chenye chembe moja kingeweza kutokea katika molekuli yenye kuoza. Hili liliwaruhusu kukataa kuwapo kwa Mungu. Hata hivyo, kulingana na Pasteur, hakukuwa na uwezekano wa uhai kutoka katika kifo.”
Hadi leo hii uthibitisho wote kutoka majaribio, historia, biolojia, uchimbuzi wa vitu vya kale, na anthropolojia huendelea kuonyesha kile alichodhihirisha Pasteur—kwamba uhai waweza kuja tu kutoka uhai uliokuwapo, si kutoka kitu kisicho na uhai. Na uthibitisho huo pia huonyesha waziwazi kwamba uhai hutokezana “kulingana na aina yake,” kama usimulizi wa Biblia katika Mwanzo usemavyo. Wazao sikuzote huwa wa “jinsi,” au aina ileile na wazazi.—Mwanzo 1:11, 12, 20-25.
Hivyo, kwa kujua au kwa kutojua, kupitia kazi yake Louis Pasteur aliandaa uthibitisho na ushahidi wenye nguvu dhidi ya nadharia ya mageuzi na uhitaji kamili wa kuwa na muumba ili uhai uwepo duniani. Kazi yake ilionyesha kile alichokubali mtunga-zaburi mnyenyekevu: “Jueni kwamba BWANA ndiye Mungu. Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake.—Zaburi 100:3.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kifaa kilicho juu kilitumiwa kuua viini katika divai, kikiua vijiumbe-maradhi visivyotakikana; kinaonyeshwa wazi katika mchoro ulio chini
[Picha katika ukurasa wa 26]
Majaribio ya Pasteur yalithibitisha nadharia ya uhai kujitokeza wenyewe kuwa si ya kweli
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Picha zote kurasa 24-26: © Institut Pasteur