Kuutazama Ulimwengu
Kuombolezea Ukosefu wa Adabu
‘Jeuri, mwenendo wa kibaradhuli, mavazi ya kizembe na yenye kuudhi, kutumia lugha chafu, kudanganya, na kutumia nguvu kikatili kumefanya maisha yawe yasiyotabirika, yasiyo rahisi, na yasiyopendeza,’ laripoti The Times la London. Sehemu iliyoenea sana ya mwenendo wa kibaradhuli katika mabara fulani ni kupuuza kimakusudi sura ya kibinafsi. “Makoti ya ngozi, kanda za kufungwa kichwani za vikosi vya wanamgambo, pua zilizotobolewa, buti za ngozi zilizopambwa kwa njumu na michoro ya kikatili mwilini ni matangazo ya vita,” asema Athena Leoussi, wa Chuo Kikuu cha Reading. Mavazi kama hayo ni ishara ya wazi ya kudharau watu wengine, kulingana na Leoussi. Gazeti The Times lasema ‘kupungua kwa hisani, kujizuia, na utaratibu kwatisha jamii labda hata zaidi kuliko uhalifu.’ Basi, suluhisho ni nini? Ni lazima adabu “zifinyangwe ndani ya muundo wa familia,” lasema gazeti hilo. “Haziwezi kuelezewa tu kwa watoto, bali ni lazima zifunzwe kwa vielelezo.”
Hatari ya Simu Zenye Kuchukulika
Uchunguzi wa hivi majuzi katika Japani umehakikisha kwamba mawimbi ya redio yatokayo katika simu zenye kuchukulika yaweza kusababisha matatizo mazito kwa vifaa vya kitiba vya hospitali. “Katika jaribio moja, mashine ya kudumisha mzunguko wa damu wakati wa upasuaji wa moyo ilisimama wakati simu yenye kuchukulika ilipotumiwa umbali wa sentimeta 45 kutoka ilipokuwa mashine hiyo,” lasema Asahi Evening News. Watafiti walipata pia kwamba kamsa zililia kwenye pampu za kupitishia mishipani viowevu na pampu zinazotoa ugavi wa dawa za kupigana na kansa wakati simu yenye kuchukulika ilipotumiwa futi mbili na nusu hivi kutoka kifaa hicho. Mashine za eksirei na vifaa vya kupima mkazo ziliathiriwa pia. Kwa kutegemea habari hizi Wizara ya Posta na Simu hupendekeza kwamba simu zenye kuchukulika zisiingizwe katika vyumba vya upasuaji na vyumba vya utibabu wa dharura. Kulingana na uchunguzi mmoja, taasisi 25 hivi za kitiba katika Tokyo tayari huwekea mipaka utumizi wa simu zenye kuchukulika, 12 kati yazo zikipiga marufuku kabisa simu zenye kuchukulika.
Watawa Wajifunza Karate
Wakikabiliwa na tisho lenye kuongezeka la jeuri dhidi ya wanawake, kikundi cha watawa kwenye St. Anne’s Provinciate katika Madhavaram, Jimbo la Tamil Nadu, India Kusini, wameanza kupata mazoezi ya karate. Shihan Hussaini, msimamizi wa Chama cha Karate cha All India Isshinryu, asema kwamba watawa wamefanya vyema zaidi kuliko wanawake wengine ambao amewazoeza kwa miaka yake 24 akiwa mfunzi wa karate. ‘Nafikiri ni kwa sababu ya nishati fichu na nidhamu waliyo nayo,’ yeye asema. Kifaa kimoja wanachofundishwa kutumia watawa hao chaitwa sein ko. Kina umbo la kisalaba, na kwa “kutumia kifaa hiki, inawezekana hata kuua mvamizi,” adai Hussaini.
Nuru ya Jua Husafisha Maji
“Wanasayansi wa Kanada wamegundua kwamba nuru ya kawaida ya jua huvunja-vunja misombo ya zebaki iwezayo kudhuru katika maji,” laripoti gazeti The Globe and Mail, la Toronto. Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Manitoba na Taasisi ya Freshwater ya Winnipeg walipata kwamba kuacha maji ya ziwa yaliyochafuliwa kwa methilizebaki yapatwe na jua kwa juma moja tu kulitokeza kupungua kwa kiwango cha methilizebaki kwa asilimia 40 hadi 66. “Hadi kufikia jaribio hili, wanasayansi walikuwa wameamini kwamba vijiumbe-maradhi pekee ndivyo vilivyovunja-vunja methilizebaki katika maji ya ziwa,” lasema Globe. Ripoti hiyo pia hutaja kwamba nuru ya jua yaelekea “kufanya kazi kwa haraka zaidi mara 350 kuliko utaratibu wa vijiumbe-maradhi uliojulikana mbeleni.”
Watoto Walio na Mkazo
Idadi ya watoto walio na vidonda vya tumbo na mchochota wa mfuko wa tumbo imerudufika katika miaka kumi, laripoti gazeti la Brazili O Estado de S. Paulo. Matokeo haya, yanayotegemea uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha São Paulo, hutaja mkazo wa kihisia-moyo kuwa kimoja cha visababishi vikuu. “Misongo ya kijamii huonyeshwa katika mfanyizo wa kihisia-moyo wa mtoto, . . . kufikia kiwango cha kusababisha maradhi,” asema daktari wa maradhi ya tumbo Dorina Barbieri. Gazeti hilo liliendelea kuorodhesha visababishi kadhaa ambavyo huchangia mkazo wa utotoni, kutia ndani mahitilafiano ya familia, aksidenti au vifo katika familia, dhana ya kwamba wanapaswa kufanya kila kitu kwa ukamilifu, ulaji usiosawazika, roho ya mashindano, na kukosa wakati wa kupumzika.
Kubaki Mwenye Ujuzi kwa Muda Mrefu
Je, wataka kudumisha uwezo wako wa kiakili ukiwa mzuri hadi miaka yako ya uzeeni? “Usipuuze elimu yako, baki ukiwa mtendaji kimwili na ulinde mapafu yako,” lasema gazeti American Health. “Kuna mambo tuwezayo kufanya ili kuongeza uwezekano wa kudumisha uwezo wa kiakili,” adai Marilyn Albert, mtaalamu wa saikolojia na mfumo wa neva wa Shule ya Kitiba ya Harvard. Dakt. Albert akisia kwamba elimu “hubadili mfanyizo wa ubongo” kwa njia fulani ili kulinda stadi za kiakili zisipungue wakati wa uzee. Kwa kuongezea, inafikiriwa kwamba utendaji wa kimwili waweza kuboresha mzunguko wa damu kwenye ubongo na kuupatia oksijeni zaidi. Kwa hiyo Albert adokeza: “Tembea kila siku, soma angalau kitabu kimoja kipya kila mwezi, na ikiwa wewe ni mvutaji-sigareti, pumzisha mapafu (na ubongo) wako, kwa kuacha kuvuta.”
Ndui ya Nyati wa Majini Yakumba India
Ndui ya nyati wa majini, isababishwayo na ‘kirusi ambacho kiko katika kikundi kimoja na kirusi cha ndui,’ imetambuliwa katika wilaya ya Beed ya magharibi mwa India, laripoti The Times of India. Ingawa ndui ya nyati si mbaya sana kama ndui, wanasayansi bila shaka wanahangaishwa na mweneo huu. “Kirusi hicho chapasa kuchunguzwa kwa uangalifu,” asema Dakt. Kalyan Banerjee, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Elimu ya Virusi. “Hatuwezi kusema ni mbaya kadiri gani.” Jambo la kuhangaikiwa sana ni uwezekano kwamba ndui hiyo itaenea hadi katika maeneo ya mashambani ambapo vifaa vya kitiba ni vichache. Ndui ya nyati wa majini husababisha kwa wanadamu homa kali, kuvimba kwa mafundo ya limfu, makovu mengi ya ndui mwilini, na udhaifu wa ujumla.
Ilani Nyingine Isiyo ya Kweli
“Utafutaji wa viumbe kutoka anga la nje ulipata maendeleo makubwa sana mwaka jana,” likaripoti gazeti New Scientist. Watafiti wenye kufanya kazi katika Taasisi ya SETI, iliyoko Mountain View, California, “walipokea ishara ambazo ziliandaa uthibitisho usioweza kupingwa wa uhai wenye akili.” Hata hivyo, baada ya uchunguzi zaidi, kikundi hicho kilipata kwamba ishara za mawimbi ya redio “hazikuwa zikija kutoka viumbe kutoka anga la nje lakini kutoka jiko la kuokea la mikrowevu katika chumba cha chini ya walipokuwa.” Hii si mara ya kwanza kwa Taasisi ya SETI kutamauka, lataja New Scientist. Watafiti wanaopekua-pekua anga katika Australia walipata kwamba “ilani nyingi zisizo za kweli zilitoka katika setilaiti.” Msemaji wa Taasisi ya SETI hivi majuzi alikiri kwa American Astronomical Society kwamba ishara zote za mawimbi ya redio yaliyotambuliwa na SETI katika 1995 zilikuwa “zinatoka kwa tekinolojia yetu wenyewe.”
Kipito Kipya cha Maji
Kipito kipya cha maji chenye urefu wa kilometa 3,450 kuelekea kusini kutoka jiji la Brazili la Cáceres hadi Mto Plate wa Argentina kinakusudiwa. Hicho kitaunganisha mto Paraná na mito ya Paraguai. Kipito hicho cha maji, au hidrovia, kitashinda maelfu ya kilometa ya barabara mbovu, kikirahisisha kusafirishwa kwa njegere, pamba, nafaka, mitapo ya chuma, chokaa, manganizi, na shehena nyingineyo hadi kwenye masoko ya nchi za kigeni. Hiyo hidrovia ni mradi wa muungano unaohusisha Argentina, Brazili, Paraguai, Uruguai, na Bolivia iliyozungukwa na bara. Kulingana na The Economist, “wastawishaji huona kipito hiki kuwa Mississippi ya Amerika Kusini, kikisafirisha mizigo kwenda na kutoka eneo la kati lililo muhimu la nusu-bara lililo tayari kusitawi kwa haraka.”
Thamani ya Pai
Pai, kama wengi walivyojifunza shuleni, ni uwiano wa duara la mviringo kwa kipenyo chalo. Watu wengi waweza kupiga hesabu kwa njia ya kuridhisha wakitumia thamani inayokadiriwa ya pai, 3.14159, lakini pai si namba kamili, kwa hiyo thamani ya desimali ya pai haina kikomo. Katika karne ya 18, thamani iliyokuwa sahihi kwa desimali 100 ilipatikana, na katika 1973 wanahisabati wawili Wafaransa walipata desimali milioni moja. Sasa Yasumasa Kanada, wa Chuo Kikuu cha Tokyo cha Japani, amepiga hesabu ya thamani hiyo, kwa kutumia kompyuta, kufikia zaidi ya desimali bilioni sita. Tarakimu hiyo haina utumizi wowote, kwa kuwa “desimali 39 tu zatosha kupiga hesabu ya duara la mviringo unaozunguka ulimwengu wote mzima mnamo nusu-kipenyo cha atomu ya hidrojeni,” lataja The Times la London. Profesa Kanada alisema hufurahia kupiga hesabu ya pai “kwa sababu ipo.” Lakini usijaribu kukariri matokeo yake. Kwa tarakimu moja kwa sekunde, bila kuacha, inaweza kuchukua hadi miaka 200 hivi,” lasema The Times.