Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 1/22 kur. 23-27
  • “Niwapo Dhaifu, Ndipo Niwapo Mwenye Nguvu”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Niwapo Dhaifu, Ndipo Niwapo Mwenye Nguvu”
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutambua Uhitaji Wetu wa Kiroho
  • Kutoa Ushahidi Kupitia Simu
  • Paradiso ya Kidunia Kupitia Nguvu za Yehova
  • Kumkaribia Mungu Kulinisaidia Niwezane na Hali
    Amkeni!—1993
  • Sababu kwa Nini Watu wa Namna Zote Wanakuwa Mashahidi wa Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Je! Ilifaa Nijitahidi Kushinda Watu Wote?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Si Mwamba Wala Kisiwa Tena
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 1/22 kur. 23-27

“Niwapo Dhaifu, Ndipo Niwapo Mwenye Nguvu”

NILILELEWA katika mji mdogo ulioko sehemu ya kusini ya San Francisco, California, uitwao Petaluma. Mama yangu alikuwa mtu wa kidini kwa kadiri fulani, lakini baba yangu hakuwa na maoni mazuri kuhusu dini. Sikuzote niliamini katika muumba—sikujua tu alikuwa nani.

Nilipokuwa nikikua, nilikuwa mtoto mwenye furaha. Jinsi nikumbukavyo kwa furaha namna nilivyofurahia siku hizo zenye uhuru! Sikujua kamwe kwamba kulikuwa na mambo yaliyokuwa yakiendelea mwilini mwangu ambayo yangeniondolea uhuru wangu mwingi. Ilikuwa katika 1960, mwaka wangu wa mwisho wa shule ya sekondari, kwamba nakumbuka nikizungumza na rafiki yangu bora kuhusu maumivu niliyokuwa nayo katika vidole vyangu kadhaa.

Muda si muda miguu yangu ikaanza kuniuma sana hivi kwamba mama yangu akanipeleka hospitali katika San Francisco, ambapo nilikaa kwa siku sita hivi. Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 18, na matokeo ya upimaji yalifunua kwamba nilikuwa na baridi yabisi. Nilianza kupokea sindano za gold sodium thiosulfate, kisha prednisone, na kisha aina nyingine ya cortisone. Kwa ujumla, nilitumia dawa hizo kwa muda wa miaka 18, na katika kila kisa ziliondoa maumivu kwa miaka michache lakini kisha zikawa bila matokeo hatua kwa hatua, nikawa nikiendelea kutumia nyingine. Maumivu hayo ya daima hayakuweza kupuuzwa, nikawa nikitafuta sana aina tofauti ya msaada wa kitiba. Nimepata matibabu ya badala ambayo yamesaidia kwa kadiri fulani. Nashukuru kwamba sipatwi na maumivu mengi kama niliyokuwa nikipata wakati maradhi haya yalipokuwa katika hatua kali zaidi mwilini mwangu.

Siku moja katika 1975, mwana wangu alipata kiaksidenti kitabu cha rekodi ambacho mama yangu alikuwa akiweka rekodi zangu nilipokuwa mtoto mchanga. Nilipata kwamba nilipokuwa na umri wa miezi sita, daktari alikuwa ameanza kunitibu kwa matibabu ya eksirei kwa ajili ya tezikago iliyokuwa kubwa kupita kiasi. Naamini kwamba matibabu hayo ya mnururisho niliyofanyiwa nilipokuwa kitoto huenda yakawa ndiyo sababu niko katika hali hii leo. Ikiwa ndivyo, hilo lilikuwa kosa baya kama nini!

Niliolewa katika 1962. Katika 1968, wakati wa hatua za mapema za maradhi hayo, mume wangu, Lynn, nami tulifanya kazi pamoja katika duka letu la kuokea mikate. Tulikuwa tukiamka saa 10:00 hivi alfajiri, kisha mume wangu alikuwa akikanda unga na nyakati fulani akilala kidogo juu ya magunia ya unga huku mkate ukiwa ndani ya jiko la kuokea. Tulikuwa tukiikata-kata mikate na kuipakia, kisha Lynn alikuwa akiipeleka kuiuza. Katika pindi moja mwuza-bima fulani alipitia dukani petu na kutuambia kuhusu Ufalme wa Mungu ulioahidiwa. Tulipenda tulichosikia, lakini tulikuwa na shughuli nyingi mno. Wale waliotaka kupelekewa mikate waliongezeka, nasi tukawa na mzigo zaidi wa kazi ya kimwili. Kwa furaha yetu, duka jingine la kuokea mikate lilinunua letu! Lynn akaenda kuwafanyia kazi, nami nikaenda kufanya kazi katika duka la urembeshaji. Hata hivyo, baridi yabisi ilipozidi, niliweza kufanya kazi siku tatu tu kwa juma na hatimaye nililazimika kuacha kabisa.

Katika kipindi hicho, mmoja wa Mashahidi wa Yehova alikuwa akipitia nyumbani kwetu kwa ukawaida na kunitolea magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Sikuzote nilikuwa nikimpa mchango na kuchukua magazeti hayo, nikifikiri kwamba nilikuwa namfanyia fadhili. Baada ya yeye kuondoka, nilikuwa nikiyaweka kwenye rafu bila kuyafunua kwa siku chache, kisha mmoja wetu sikuzote alikuwa akiyatupa. Hilo lilikuwa jambo baya sana, kwa kuwa sasa twathamini thamani yayo ya kiroho. Hata hivyo, wakati huo, hatukuona mambo ya kidini kuwa ya muhimu sana.

Kutambua Uhitaji Wetu wa Kiroho

Jioni moja mume wangu nami tulikuwa tukizungumza jinsi lazima kulikuwa na kusudi zaidi katika uhai zaidi ya kula na kulala na kufanya kazi kwa bidii sana. Tulianza kutafuta hali ya kiroho ambayo haikuwapo katika maisha zetu. Tulielekeza uangalifu wetu kwenye kanisa dogo lililokuwa kule chini barabarani, lakini hatukupata kuinuliwa kiroho tulikokuwa tukikutazamia. Washiriki wa kanisa walizungumza sana kuhusu matatizo ya kwao.

Shahidi aliyeleta magazeti hayo alikuwa akija kwa mwaka mmoja hivi, lakini zoea langu halikubadilika hadi hatimaye niliposoma toleo la Amkeni! la Oktoba 8, 1968 (la Kiingereza), lililokuwa na kichwa “Je, Ni Kuchelewa Mno Kuliko Unavyofikiri?” Nilipenda nilichosoma, na kwa furaha, kilimwathiri mume wangu kwa njia hiyo hiyo. Tulianza kujifunza na kufyonza kweli haraka sana. Tulikubali kwa hamu mambo yote mazuri ajabu tuliyokuwa tukijifunza. Katika 1969 tulibatizwa.

Kadiri wakati ulivyosonga, ilikuwa vigumu kwangu kusimama na kuketi na vigumu hata zaidi kutembea. Ilinibidi nilazimishe magoti yangu kujikunja ili niingie au kutoka garini. Nilikuwa nimejifunza kuishi kulingana na mapungukio na maumivu ambayo yalinifanya nilie wakati mwingi. Kwa hiyo nilikuwa nikijipaka kijuu-juu virembeshi vyangu nasi tulielekea mikutanoni au katika utumishi wa shambani. Nilitembea mlango hadi mlango kwa muda mrefu kadiri nilivyoweza. Nilijaribu kwenda katika utumishi wa shambani mara moja au mbili kila juma, hadi ukavu na maumivu katika magoti yangu na miguu yaliponizuia. Mara nyingi nilihofu kuhusu kuanguka na kutoweza kuinuka. Husaidia sana ninapoongea na Yehova. Nyakati fulani namlilia nikiwa na machozi mengi.

Hata hivyo, kugeukia machozi hakukua rahisi sikuzote. Mtu aliye na baridi yabisi aweza pia kupatwa na ukavu wa macho. Wakati fulani nimepatwa na ukavu mbaya sana hivi kwamba ilikuwa vigumu kusoma. Hilo lilipotukia, nilisikiliza kanda za Biblia. Mara nyingi nilitembea nikiwa nimefunga macho kwa sababu kusogeza kope kulikwaruza macho yangu. Hata afadhali ningekuwa kipofu. Nyakati fulani, nililazimika kuweka machozi bandia katika macho yangu baada ya kila dakika tano. Vibaya hata zaidi, nilikuwa nikilazimika kuweka dawa katika macho yangu na kuyafunga kwa bendeji kwa siku tano au sita hadi yapate nafuu. Kubaki mwenye shukrani si rahisi wakati mtu anang’ang’ana na ugonjwa wa muda mrefu ambao hauwezi kutarajiwa kurekebishwa katika mfumo huu.

Katika 1978, nililazimika kutumia kiti chenye magurudumu. Haikuwa rahisi kufanya uamuzi huo. Niliahirisha kutumia kiti chenye magurudumu kwa muda mrefu kadiri nilivyoweza, lakini sikuwa na chaguo jingine tena. Nilikuwa nikijua kwamba siku hiyo itafika, lakini tumaini langu lilikuwa kwamba ulimwengu mpya wa Mungu ungekuja kwanza. Lynn alinunua kiti kirefu kilicho na sehemu ya chini pana iliyo na magurudumu matano. Kwacho, niliweza kujisukuma huku na huku nyumbani.

Nilifadhaika nilipojaribu kufikia kitu fulani, kwa kuwa sikuweza kunyoosha mkono wangu mbali vya kutosha na kushika sawasawa na vidole vyangu vilivyokunjamana. Kwa hiyo, nilikuwa nikitumia kijiti changu cha “kushikia.” Kwacho, naweza kuchukua kitu kutoka sakafuni, kufungua kabati na kutoa chombo, au kupata kitu kutoka katika friji. Kadiri ninavyokuza stadi mpya na kijiti changu cha “kushikia,” naweza kushughulikia kazi ndogo-ndogo za nyumbani. Naweza kupika, kuosha na kukausha vyombo, kupiga pasi na kukunja nguo, na kusafisha sakafu. Nahisi fahari uwezo wangu unapoboreka, na nina furaha kwamba bado naweza kuchangia mahitaji fulani ya nyumbani. Hata hivyo, nilichokuwa nikiweza kufanya kwa dakika chache sasa hunichukua saa kadhaa.

Kutoa Ushahidi Kupitia Simu

Ilichukua muda fulani, lakini hatimaye nikapata moyo mkuu wa kujaribu kutoa ushahidi kupitia simu. Sikufikiri ningeweza kufanya hilo, lakini sasa nafurahia sana na nimekuwa na mafanikio. Kwa mshangao wangu, kufanya hivyo ni sawa na kwenda mlango hadi mlango, katika maana ya kwamba naweza kuzungumza na watu kuhusu Yehova na makusudi yake.

Moja ya toaji ninazotumia huanza hivi: “Halo, huyo ni Bw.——? Mimi ni Bi. Maass. Naongea na watu kifupi tu, na ikiwa una dakika chache, naweza kusema nawe? (Itikio la kawaida ni: “Ni kuhusu nini?”) Inatisha sana kuona mambo yanayotendeka leo ulimwenguni, sivyo? (Naruhusu maelezo.) Ningependa kushiriki nawe wazo hili la Kibiblia ambalo hutupatia tumaini hakika kwa wakati ujao.” Kisha nasoma Sala ya Bwana na ikiwezekana 2 Petro 3:13. Nimepatia akina dada wenzangu Wakristo au Lynn ziara za kurudia wazifuatilie kwa niaba yangu.

Kwa muda wa miaka ambayo imepita, nimekuwa na mazungumzo mazuri na nimeweza kupeleka broshua, magazeti, na vitabu kwa wale walioonyesha upendezi. Wengine wameanza kujifunza Biblia kupitia simu. Bibi mmoja niliyeongea naye alisema kwamba kujifunza peke yake tu kungetosha. Lakini baada ya mazungumzo kadhaa, alikubali kuja nyumbani kwetu kwa ajili ya funzo la Biblia, kwa kuwa nilimwambia kuhusu hali zangu.

Wakati mwingine nilipokuwa nikipiga simu, mashine ya kujibia simu ilitoa namba mpya. Ingawa sikuzote mimi hupiga simu eneo la kwetu tu na namba hii ilikuwa ya nje, nilihisi nikichochewa kujaribu namba hiyo kwa vyovyote. Baada ya kuongea nami kwa muda fulani, bibi aliyejibu simu alisema kwamba yeye na mume wake walitaka kuwasiliana na watu ambao ni Wakristo kweli. Kwa hiyo Lynn nami tulikwenda nyumbani kwao, umbali wa saa nzima hivi, ili kujifunza pamoja nao.

Bado napata shangwe na furaha katika kuongea na wengine kuhusu Yehova na ahadi yake ya mbingu mpya na dunia mpya, ambapo uadilifu utakaa. Hivi majuzi, mwanamke mmoja ambaye nimekuwa nikiongea naye kwa miezi kadhaa aliniambia: “Wakati wowote nizungumzapo nawe, natambua kwamba natwaa ujuzi zaidi.” Najua kwamba ujuzi ninaoshiriki na wengine huongoza kwenye uhai na hunitokezea shangwe hata ingawa nina sura ya nje iliyolemaa. Nyakati fulani naweza kufanya mengi katika utumishi kuliko nyakati nyingine, lakini natamani ningeweza kufanya mengi zaidi, mengi zaidi kila wakati! Najua kwamba Yehova ajua hali za kila mtu na kwamba yeye huthamini kile tuwezacho kufanya, hata kionekane kuwa kidogo namna gani. Mara nyingi nimekuwa nikiwazia Mithali 27:11: “Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu, ili nipate kumjibu anilaumuye,” na nataka kuwa miongoni mwa wale ambao humthibitisha Shetani kuwa mwongo.

Kuwa mikutanoni hutia moyo sikuzote, hata ingawa ni vigumu kwangu kufika huko. Yehova ametoa maandalizi mazuri ajabu ili tulishwe vizuri kiroho ambayo nataka kuyatumia kikamili. Tuna furaha kama nini kwamba watoto wetu wawili wameifanya kweli kuwa mali yao wenyewe! Binti yetu, Terri, ameolewa na ndugu mzuri, na wana watoto wanne ambao nawapenda sana. Jinsi inavyochangamsha mioyo yetu kuona kwamba wajukuu wetu wanampenda Yehova pia! Mwana wetu, James, na mke wake, Tuesday, wamefanya chaguo la kumtumikia Yehova katika Betheli ya Brooklyn, Makao Makuu ya Mashahidi wa Yehova, katika New York.

Paradiso ya Kidunia Kupitia Nguvu za Yehova

Mimi hujaribu kuweka akilini ahadi nzuri ajabu ya Yehova ya dunia iliyo paradiso. Hata sasa, kuna viumbe vyake vingi vya kufurahia. Mimi hufurahia machweo yenye kuvutia. Hufurahia unamna-namna wa maua na manukato yayo. Napenda waridi! Siwezi kutoka nje ya nyumba mara nyingi sana, lakini niwezapo, mimi hufurahia sana kuhisi jua lenye ujoto. Mimi hufunga macho yangu na kuona mandhari maridadi milimani, nikiwa na familia yangu tukifurahia uwanda wa nyasi uliojaa maua ya mwituni. Nawazia kwamba kuna kijito chenye kububujika na matikiti mengi matamu yenye maji mengi kwa ajili ya kila mtu! Ninapoweza, mimi huchora picha za mambo ambayo hunisaidia kuwazia Paradiso ya kidunia iliyoahidiwa ambayo itakuja. Ninapochora, mimi hujiwazia nikiwa huko. Najua Yehova aweza kufanya ziwe halisi picha za akilini ambazo nazipenda sana wakati huu.

Mimi hupenda kukumbuka andiko lililo kwenye Yakobo 1:12. Hilo husema: “Mwenye furaha ni mtu afulizaye kuvumilia jaribu, kwa sababu akiisha kukubaliwa atapokea taji la uhai, ambalo Yehova aliahidi wale waendeleao kumpenda.” Paulo alilinganisha ugonjwa aliokuwa nao na ‘malaika wa Shetani, aliyekuwa akifuliza kumpiga kofi.’ Yeye alisali kwamba Yehova amwondolee ulemavu huo lakini akaambiwa kwamba nguvu za Mungu zilikuwa zikifanywa kamilifu katika udhaifu wake. Kwa hiyo mafanikio ya Paulo japo udhaifu wake yalikuwa uthibitisho wa nguvu za Mungu juu yake. Paulo alisema: “Niwapo dhaifu, ndipo niwapo mwenye nguvu.” (2 Wakorintho 12:7-10) Nahisi kwamba machache niwezayo kufanya sasa japo mapungukio yangu ni kupitia tu nguvu za Mungu juu yangu.

Yohana alirekodi simulizi ambalo hunitia moyo sana. Ni kuhusu mwanamume aliyezuiliwa na ugonjwa katika machela kwa miaka 38. Yeye pamoja na wagonjwa wengine, walikuwa wakilala wakiwa na tumaini kando ya kidimbwi cha maji, wakitamani sana kujiburudisha ndani yacho. Yeye hakuweza kuyafikia maji hayo, ambayo alifikiri yangeweza kumponya. Siku moja Yesu alimwona na kumwuliza: “Je, wataka kuwa timamu katika afya?” Jinsi ningejibu kwa machozi ya shangwe! “Yesu akamwambia: ‘Inuka chukua kitanda chako, utembee.’” (Yohana 5:2-9) Kuna wengi wetu ambao wanangoja kwa hamu kusikia mwito kama huo!—Kama ilivyosimuliwa na Lurreta Maass.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Nilifikiri kuhusu mtoto aliyependa watu, naye huyu hapa, akivuka uwanda wa nyasi kwa furaha

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nilipokuwa mchangamfu, niliwaza kuhusu mvulana mwenye kujasiria akiwa juu ya milonjo, mbwa wake akiwa chini yake

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kukusanya nambari za simu kwa ajili ya utumishi wa shambani

Kupiga simu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki