“Udanganyifu Mbaya Zaidi wa Kisayansi”
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
Yule mtu wa Piltdown, aliyegunduliwa 1912, alikuwa “udanganyifu mbaya zaidi wa kisayansi katika karne hii,” lasema The Times la London. Ilifunuliwa hivyo katika 1953 baada ya majaribio ya kisayansi kuthibitisha kwamba badala ya kuwa kile kiungo kilichokosekana katika ile iitwayo eti nasaba ya mageuzi ya mwanadamu wa kisasa, fuvu lilikuwa la mtu wa kisasa na utaya wa chini ulikuwa wa nyani mkubwa aina ya orangutangu. Ni nani aliyeeneza udanganyifu huo wenye ujanja?
Kwa miaka mingi Charles Dawson, aliyekuwa wakili na mwanajiolojia asiye mtaalamu, ambaye alipata mabaki hayo alishukiwa. Wengine walioshukiwa pia walikuwa Sir Arthur Keith, mwanamageuzi wa dhati ambaye pia alikuwa msimamizi wa Royal College of Surgeons; mtungaji wa vitabu Mwingereza Sir Arthur Conan Doyle; na kasisi Mfaransa Pierre Teilhard de Chardin. Lakini, uthibitisho kamili ulikosekana na hatimaye Dawson ndiye alionekana kuwa mwenye makosa.
Sasa, mkosaji mwenyewe ametajwa. Yeye ni Martin A. C. Hinton, aliyekuwa msimamizi wa zuolojia kwenye London’s Natural History Museum, ambaye alikufa mnamo 1961. Miaka tisa iliyopita kasha la kitambaa kigumu la Hinton lilipatikana katika jumba hilo la makumbusho. Ndani mlikuwa na meno ya tembo, vipande vya mabaki ya kiboko, na mifupa mingine, ambayo imechunguzwa kwa uangalifu sana. Yote ilikuwa na chuma na manganizi kwa kiwango kilekile kilichopatikana katika mifupa ya Piltdown. Lakini jambo kuu likawa kugunduliwa kwa kromiamu katika meno, ambayo pia ilitumiwa katika kuzitia hizo madini.
Akitokeza mambo hayo, Profesa Brian Gardiner, wa King’s College, London, alisema: “Hinton alijulikana kuwa mtu mwenye mzaha wenye kudhuru. . . . Nia [yake] inaonyeshwa katika baadhi ya barua zake.” Gardiner akafikia mkataa: “Nina hakika kabisa kwamba ni yeye.” Uthibitisho wadokeza kwamba Hinton alitaka kulipiza kisasi dhidi ya Arthur Smith Woodward, aliyekuwa mkubwa wake, ambaye hakutambua mambo ambayo yeye Hinton alitimiza wala hakumpa fedha alizofikiri amestahili kupokea. Woodward alidanganywa akadanganyika, na kufikia alipokufa miaka mitano kabla ya kufunuliwa kwa huo udanganyifu, yeye alikuwa amesadiki kwamba yule mtu wa Piltdown alikuwa wa kweli. Swali linalobaki bila jawabu ni, Kwa nini Hinton hakukiri kwamba huo ni udanganyifu mara tu baada ya Woodward kukubali hadharani kuwa jambo hilo lilikuwa kweli? Yaonekana kwamba kwa sababu mtu wa Piltdown alikubaliwa upesi kuwa wa kweli miongoni mwa wanasayansi, Hinton alihisi kwamba hakuwa na namna ila kuubana uwongo huo.
Watu mashuhuri kama hao wakikubali fuvu la mtu wa Piltdown, hata umma nao ukadanganyika. Majumba ya makumbusho ulimwenguni kote yalionyesha sana nakala na picha za fuvu hilo, huku vitabu na majarida yakieneza kwa haraka habari hizo. Madhara ya mzaha wa Hinton ni makubwa sana. Maneno haya ya Biblia yafaa kama nini: “Kama mjinga arushaye vijiti vya moto, mishale, na kifo, ndivyo alivyo mtu adanganyaye mwingine na kusema ‘wajua, nilikuwa nacheza tu!’”—Mithali 26:18, 19, Byington.
[Mchoro katika ukurasa wa 31]
Maeneo meusi ni vipande vya fuvu la kibinadamu
Eneo lote lililo kwenye nuru limefanyizwa kwa plasta
Maeneo meusi ni vipande vya utaya na meno ya orangutangu