Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 1/22 kur. 22-23
  • Kitenge Chenye Matumizi Mengi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kitenge Chenye Matumizi Mengi
  • Amkeni!—1998
  • Habari Zinazolingana
  • Aliazimia Aishi Kulingana na Viwango vya Adili za Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • “Sijawahi Kamwe Kuhisi Upendo Kama Huu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Mwishowe Mbegu Ilichipuka
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Kutatua Matatizo ya Vijana
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 1/22 kur. 22-23

Kitenge Chenye Matumizi Mengi

NA MLETA-HABARRI WA AMKENI! KATIKA NAMIBIA

KITENGE—wajua ni nini? Ikiwa waweza kupata wakati fulani, twende katika safari ndogo kwenye kijiji cha Kiafrika tuone kitenge chenye matumizi mengi kazini na mchezoni.

Kijiji tunachozuru ni Rundu, Namibia. Kwanza tunasimama sokoni kwenye shughuli nyingi. Wanawake wenye nyuso zenye uchangamfu wanajadiliana juu ya bei, wananunua, wanauza, au wanasimama tu kuzungumza. Lakini angalia kwa ukaribu zaidi, na utaona kwamba karibu wote wamevaa namna ya mavazi ya pekee, skati ya kuzungushia kiunoni ijulikanayo kama kitenge.

Hicho kitenge kilichotengenezwa kwa pamba kina urefu wa meta mbili na upana wa meta moja na nusu na chafurahisha kwa unamna-namna wa rangi na michoro isiyo na mwisho. Baadhi yake vimepambwa kwa picha za wanyama, na vingine, kwa watu au sura za nchi.

Kisha, twawatembelea wanakijiji fulani katika nyumba zao nadhifu za matope na nyasi. Wanawake hao wana shughuli nyingi katika kazi zao za kila siku—wakiondoa mchanga mbele ya nyumba yao au wakitayarisha moto kwa ajili ya chakula cha familia zao. Wengine wamevaa kitenge tu, wakati huu kikiwa kimevutwa juu na kufungwa juu ya kifua kama vazi la gauni. Wanawake hao wavaapo—labda blauzi na skati—watafunga kitenge viunoni ili kuzuia skati yao isipate uchafu watembeapo katika barabara za kijijini zenye vumbi.

Je, umemwona mwanamke yule mchanga mwenye kuvutia? Amefunga kitenge—meta zote mbili kufanyiza kilemba maridadi. Na ona jinsi anavyombeba mtoto wake. Amefunga kitenge kingine kupitia bega lake kama mshipi. Mtoto wake ni mwenye furaha akiwa amebebwa hivi kwenye mgongo wa Mama. Akianza kulia, anavuta tu mshipi huo mbele yake, na kumnyonyesha au kumtuliza aendeleapo kutembea.

Huenda pia umemwona akifunga pesa zake kwenye ncha ya skati yake ya kuzungushia—kibeti chenye kufikika kwa urahisi. Anapomaliza kununua, anafungua kitenge chake cha ziada, anaweka mboga ndani, anakifunga kwa ustadi mboga zikiwa ndani, na anauweka mfuko wake wa vyakula kichwani na kuupeleka nyumbani.

Aingiapo nyumbani kwake, utaona matumizi mengine ya kidesturi ya kitambaa hiki chenye matumizi mengi. Mbele ya kila mlango kwaning’inia kitenge chenye rangi nyangavu. Kama uwezavyo kuona, hakuna kuta za ndani. Kamba ndefu imefungwa kutoka mwisho mmoja hadi mwingine wa kao hilo, na vitenge vinne vimeangikwa juu yake, vikigawanya chumba cha mapumziko na chumba cha kulala.

Mkaribishaji wetu anaweka mboga zake chini na anatambua kwamba hana kuni. Kabla hajaenda msituni kutafuta kitita cha kuni, anahakikisha kuwa ana kitenge cha ziada. Baada ya kukusanya kuni, anatumia kitenge kimoja kuzifunga kuni zote pamoja. Kisha anachukua kitenge kingine na kukisokota kwa nguvu kufanyiza mviringo mnene, ambacho anakiweka kichwani. Hiki hutumika kama mto mzuri awekapo tita lake kubwa la kuni kichwani na kulipeleka nyumbani.

Mara tu chakula cha rafiki yetu kianzapo kuchemka, anaamua kuwa ana wakati wa kuwatembelea jirani zake. Huku akizungumza na kutoa ishara, anakiweka kitenge chake chini kama blanketi na kumweka mtoto wake juu yake. Mtoto anamchekea mama yake kwa furaha anapompa kijiti cha kuchezea.

Punde si punde, rafiki yetu anaondoka kwenda kuangalia chakula. Lakini kuna mawingu, na mara moja mvua yaanza kunyesha. Bila kujali, anamchukua mtoto wake mkononi na kwa hekima anajifunika kichwani kwa kitenge hicho. Akiwa na mwavuli ukiwa umewafunika, anaelekea nyumbani kukiangalia chakula.

Skati, vazi, kibeti, mfuko wa kuwekea mboga, mto, blanketi, mwavuli, kibebea-mtoto, kilemba—matumizi ya kitenge yaelekea kuwa yasiyo na mwisho na ni ushuhuda wa ubunifu wa watu hawa wa Afrika.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kitenge kina matumizi mengi: kama kitu cha kufungia kuni, mshipi wa kumshikilia mtoto, kilemba maridadi, blanketi yenye rangi nyingi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki