Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 10/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Rehema za Papa
  • Maradhi Yasiyo na Dalili za Kawaida
  • Abiria wa Ndege Wenye Fujo
  • Gharama za Maziko Zinazoongezeka
  • Visukuku Vilivyo Hatarini
  • Je, Ni Tiba ya Meno Isiyo na Maumivu?
  • Mabaki ya Nyuklia
  • Kutoa Ishara za Mwili ili Kupata Neno Linalofaa
  • Misiba Inayotokea Kazini
  • Ugonjwa Unaoenea wa Kansa ya Mdomo
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Kuchoma Maiti?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Wanatafuna Kuelekea Taabu
    Amkeni!—1996
  • Ugonjwa wa Mifupa Unaoshambulia Kimyakimya
    Amkeni!—2010
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 10/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Rehema za Papa

Katika kusherehekea milenia, Papa John Paul wa Pili ameutangaza mwaka wa 2000 kuwa Mwaka Mtakatifu na ameahidi kuwarehemu wale watakaoenda kuhiji Roma, laripoti gazeti L’Osservatore Romano. Rehema ni njia moja ambayo Wakatoliki huondolewa adhabu kwa ajili ya dhambi. Gazeti la Vatikani lasema: “Kazi yoyote njema inayofanywa kwa msaada wa Mungu yastahili kuthawabishwa.” Hata hivyo, gazeti hilo hilo lasema kwamba zoea hilo lazusha maswali mengi yenye kupendeza, kama vile, “Ikiwa wema wa Mungu wa kusamehe huonyeshwa watu wote, kuna uhitaji gani wa Kanisa kutoa rehema?” na “Ikiwa Kanisa laweza kutoa rehema [kamili], kwa nini anajishughulisha na rehema ya kadiri?”

Maradhi Yasiyo na Dalili za Kawaida

Ugonjwa wa mifupa ni maradhi yasiyo na dalili za kawaida ambayo “yanatisha zaidi ya Wamarekani milioni 28 na Wakanada takriban milioni 1.4,” laripoti gazeti Toronto Star. Maradhi hayo huwapata wanaume na wanawake, wachanga kwa wakubwa, na “hutukia wakati chembe za mifupa zilizozeeka zaidi zinapoharibika haraka zaidi kabla ya mahali pake kuchukuliwa na mifupa mipya.” Wale walio na maradhi hayo huenda wasione dalili zozote zake mpaka wanapovunjika mfupa. Wataalamu wanaamini idadi inayoongezeka ya matineja na wanariadha wa vyuo wanaojinyima chakula kupita kiasi “wanadhoofisha mifupa ambayo wanahitaji kuijenga kwa ajili ya wakati watakapokuwa watu wazima. Vijana wanaojinyima chakula mara nyingi hukosa kula chakula kinachohitajiwa ili kujenga viunzi vyao.” Kulingana na ripoti hiyo, “mtu hufikia takriban asilimia 90 ya uzito wa mifupa anapokuwa na umri wa miaka 18; watu wazima hufikia kilele hicho wanapokuwa na umri wa miaka 30.” Ripoti hiyo yapendekeza kwamba ili kuongeza uzito wa mifupa, kila mtu apaswa ‘kupata kalisi ya kutosha na vitamini D, kufanya mazoezi kwa ukawaida, na kuepuka kuvuta sigareti na kunywa vileo kupita kiasi.’

Abiria wa Ndege Wenye Fujo

“Hasira kali ndani ya ndege”—tabia isiyodhibitiwa ya abiria wa ndege—“imeongezeka kwa asilimia 400 katika miaka mitano iliyopita,” lasema gazeti Business Traveler International. Ni nini kinachosababisha ongezeko hilo kubwa? Sababu kuu ni mkazo. Kucheleweshwa au kuahirishwa kwa safari za ndege, msongamano, na hofu ya kusafiri kwa ndege, mambo hayo yote husababisha hangaiko, ambalo laweza kuongoza kwenye hasira kali. “Mashirika ya ndege husifu usafiri wa angani kuwa wa haraka na usio na matatizo yoyote, lakini sivyo ilivyo,” asema Stuart Howard, wa shirika la International Transport Workers’ Federation. Mwakilishi mmoja wa shirika kuu la ndege aamini kwamba kuanzishwa kwa safari za ndege ambapo uvutaji sigareti hauruhusiwi ni kisababishi kikuu cha hasira kali ndani ya ndege. Kulingana na ripoti hiyo, “wavutaji sigareti waliofadhaika walichangia zaidi ya nusu [ya] visa vya tabia zenye fujo za abiria” kwenye shirika moja la ndege mnamo mwaka wa 1997. Kisababishi kingine ni matumizi ya kileo, ambacho matokeo yake huongezeka, ndege inapopaa juu. Ripoti hiyo yapendekeza nini iwapo abiria mwenzako aanza kupiga kelele? “Usiite wafanyakazi wa ndege. Badala yake, ondoka kitini mwako na kutahadharisha wafanyakazi hao juu ya tatizo hilo kwa njia ya busara.” Pia inapendekeza: “Jiepushe na kuudhiwa kunakoweza kutokea kwa kusoma vitabu vyenye habari sahili au kusikiliza muziki unaotuliza” kwenye stirio ya kubebeka.

Gharama za Maziko Zinazoongezeka

Idadi kubwa ya watu wanageukia zoea la kuchoma maiti ili kupunguza gharama za maziko. Kulingana na shirika la National Funeral Directors Association, wastani wa gharama ya kawaida ya maziko huko Marekani ulikuwa dola 4,600 za Marekani mnamo mwaka wa 1996. Kinyume cha hilo, “kuchoma maiti kunagharimu kati ya dola 500 na 2,000 za Marekani,” lasema gazeti Chicago Sun-Times, “ikitegemea aina ya chombo kinachoteuliwa kuchomea maiti na chombo kirefu cha udongo cha kutilia majivu ya maiti.” Pia kuchoma maiti hakuhitaji ploti ya kaburi na alama ya kaburi, inayoweza kuongeza gharama ya maziko ya kawaida kwa asilimia 40. Gazeti hilo lilisema kwamba huko Marekani mnamo mwaka wa 1997, njia ya kuchoma maiti ilitumiwa katika asilimia 23.6 ya vifo vyote, na tarakimu hiyo inatarajiwa kufikia asilimia 42 katika miaka kumi ijayo.

Visukuku Vilivyo Hatarini

Maeneo yenye visukuku ambayo yamedumu kwa milenia nyingi yanatishwa na wizi, uharibifu wa vitu kimakusudi, na watalii wenye bidii inayopita kiasi, laripoti New Scientist. “Wanajiolojia fulani wangependa kuhamisha visukuku vyenye thamani zaidi kwenye majumba ya ukumbusho au kupiga marufuku wageni katika maeneo hayo,” lasema gazeti hilo. Hata hivyo, wengine wanatoa hoja kwamba umma una haki ya kuona visukuku hivyo vikiwa katika mazingira yao ya asili. Katika jitihada ya kusuluhisha tatizo hilo, shirika la International Palaeontological Association limeanza kuandaa orodha ya maeneo yaliyo hatarini ulimwenguni. Lakini kufikia sasa, ni maeneo yapatayo 50 tu ambayo yameorodheshwa.

Je, Ni Tiba ya Meno Isiyo na Maumivu?

Wagonjwa wengi wenye matatizo ya meno watafurahi sana watakapoona keekee ya daktari wa meno imeacha kutumiwa. Kulingana na FDA Consumer, huenda kwa kiwango fulani jambo hilo likawezekana hivi karibuni. Hivi karibuni, Shirika la Marekani la Usimamizi wa Chakula na Dawa liliidhinisha matumizi ya erbi: leza ya YAG kwa ajili ya upasuaji wa meno. Badala ya kung’oa jino lililooza kwa kutumia keekee ndogo mno, sasa madaktari wa meno wanaweza kutumia leza kuling’oa, kimsingi kwa kufusha tishu ya jino lililooza, lasema gazeti hilo. Leza ina manufaa kadhaa zaidi ya keekee za kawaida. Kwa upande mmoja, kwa kawaida matibabu ya leza hayana maumivu. Hivyo, wagonjwa wengi hawatahitaji tena dawa ya nusukaputi au sindano ya nusukaputi. Pili, kwa kuwa daktari wa meno hahitaji kusubiri kinywa chako kigande, matibabu yaweza kuanza mara moja. Kwa kuongezea, hakuna mitikiso inayoudhi ya keekee inayozunguka kwa kasi. Hata hivyo, hitilafu moja ya maana ni kwamba leza haiwezi kutumiwa kwenye meno ambayo tayari yana vijazo.

Mabaki ya Nyuklia

Tangu miaka ya 1960, zaidi ya tani za meta 200,000 za mabaki ya nyuklia zimetupwa na viwanda vinavyotengeneza nyuklia ulimwenguni, laripoti gazeti New Scientist. Na kila mwaka tani nyingine 10,000 huongezewa kwenye rundo hilo. Mabaki hayo ya kufisha huenda wapi? “Mengi yake huhifadhiwa kwenye maeneo ya viwanda vya nyuklia,” lasema gazeti hilo. Hata hivyo, maeneo hayo yalikusudiwa yawe na mabaki ya nururishi kwa miongo michache tu. Kwa hiyo ifikapo pindi fulani, mabaki ya nyuklia yatahitaji kuhamishwa hadi kwenye maeneo ambapo yatadumu kwa muda mrefu. Lakini tatizo ni kwamba hakuna nchi ambayo imefaulu kuanzisha hifadhi ya chini ya ardhi kwa ajili ya vifusi vyake vya nururishi. Tokeo ni kwamba “viwanda vinavyotengeneza nyuklia vimenaswa katika mtego ambao viliutega vyenyewe,” lasema New Scientist.

Kutoa Ishara za Mwili ili Kupata Neno Linalofaa

“Utafiti mpya waonyesha kwamba mara nyingi ishara za mwili husaidia wasemaji wapate maneno yaliyo katika kumbukumbu lao,” laripoti gazeti Newsweek. Ingawa mara nyingi ishara za mwili zinazofafanua mambo hutumiwa ili kuonyesha ukubwa au umbo la kitu fulani, ishara nyingine za mwili kama zile “zinazoandamana na sentensi,” huwa na kusudi tofauti. Robert Krauss, profesa wa saikolojia kwenye Chuo Kikuu cha Colombia, asema kwamba aina hii ya ishara za mwili “husaidia watu wapate maneno yaliyo magumu kukumbuka kutoka kwenye kumbukumbu lao” kwa kufungua ile anayoiita “kumbukumbu la msamiati.” Watafiti wanalinganisha kumbukumbu hilo na badiliko la ujumbe ambalo hutukia wakati harufu fulani, ladha, au sauti inapohusianishwa na tukio fulani. Kwa mfano, kama vile harufu ya marashi fulani huenda ikakufanya uwazie juu ya nyanya yako, kuonyesha ishara za mwili kwaweza kutokeza “fursa” inayofanana na hiyo kwa neno fulani, kulingana na mwanasayansi anayehusika na mfumo wa neva Brian Butterworth.

Misiba Inayotokea Kazini

Ulimwenguni pote, watu 3,000 hufa kila siku katika aksidenti zinazohusishwa na kazi, laripoti gazeti la Kifaransa la kila siku Le Monde. Kulingana na shirika la International Labour Bureau, wafanyakazi wapatao milioni 250 hujeruhiwa kila mwaka, kukiwa na vifo vinavyozidi milioni moja. “Idadi ya vifo vinavyohusishwa na kazi ni kubwa zaidi kuliko wastani wa idadi ya vifo kwa mwaka vinavyosababishwa na aksidenti (990,000), mapambano ya kijeshi (502,000), jeuri nyingineyo (563,000), na UKIMWI (312,000),” lasema gazeti hilo.

Ugonjwa Unaoenea wa Kansa ya Mdomo

Katika jiji la Delhi, India, visa vya kansa ya mdomo ni mara nne zaidi ya huko Los Angeles, California, laripoti gazeti The Indian Express. Kwa sasa, asilimia 18.1 ya visa vipya vyote vya kansa miongoni mwa wanaume wa jiji la Delhi ni vya kansa ya mdomo—zaidi ya visa asilimia 10 vilivyotukia mwaka wa 1995. Visababishi vikuu vya kansa ya mdomo ni kutafuna tumbaku, bidi (sigareti za India), na pan masala (mchanganyiko wa tumbaku, kokwa zilizosagwa za tambuu, na vitu vinginevyo), ambavyo husokotwa ndani ya jani na kutafunwa. Gazeti hilo lilitaja ongezeko la watoto wa shule wanaotumia pan masala bila kuishuku kuwa jambo linaloshtua. Mtaalamu mmoja alionya kwamba nchi nzima ya India inaelekea kukumbwa na “ugonjwa unaoenea wa kansa ya mdomo.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki