Ubora wa Kuwapa Watoto Elimu ya Mapema Wakiwa Nyumbani
● Gazeti “Science News” linasema kwamba uchunguzi uliofanywa muda mrefu umehakikisha kwamba kuna ubora mwingi wa kuwapa watoto elimu wanapokuwa nyumbani. Ilionekana kwamba akili na ujuzi wa watoto uliongezeka sana wakati wazazi walipoanza kuwapa elimu kabla ya kwenda shuleni na hata baada ya hapo. Ilionekana pia kwamba, hata watoto walipoelimishwa nyumbani kwa vipindi vifupi vifupi, walipata akili na ujuzi zaidi walipokwenda shuleni.
Kati ya watoto waliosaidiwa nyumbani na wazazi wao, kiasi cha mtoto mmoja tu kwa mia ndicho kilichohitaji kusaidiwa sana shuleni katika darasa la tano. Lakini karibu 30 kwa mia kati ya watoto ambao hawakufundishwa nyumbani walihitaji kusaidiwa sana walipofika darasa hilo.
Biblia inakazia sana wazazi wawape watoto wao elimu. Watu wa Mungu wa kale walipewa amri hii: “Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto . . . wapate kusikia na kujifunza.” (Kum. 31:12) Elimu hiyo ‘ya mtaa mzima’ iliungwa mkono nyumbani, kwa maana wazazi waliambiwa yafuatayo kuhusu sheria na kanuni za Mungu: “Nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.” (Rum. 6:7) Hivyo, “tangu utoto” Timotheo aliyajua Maandiko Matakatifu.—2 Tim. 3:15.
Hiyo ndiyo sababu Mashahidi wa Yehova wanatia watoto wao wenye umri wa namna zote katika shughuli zao za elimu ya Biblia. Elimu hiyo inahusu kuwasaidia kusoma pia, na kwa kawaida wanawasaidia kabla hawajaingia shuleni.