Je! Hofu Ni Mbaya Sikuzote?
INAWEZA kuangamiza furaha na kuharibu tumaini. Imesemwa kuwa sumu ya kiakili, mharabu wa uwezo wa kusababu, na inasemekana kuwa yenye kuharibu zaidi ya ugonjwa wa mwili ulio mbaya zaidi. Ndiyo, hofu ni hisia yenye nguvu nyingi. Hata hivyo, je! ni mbaya sikuzote?
Wazia kwamba unaendesha gari lako katika barabara usiyozoea. Barabara hiyo inapanda milimani na kuanza kupinda na kugeuka. Usiku waanza kuingia, na pamoja nao waja ukungu mwembamba wa theluji. Gari lako lateleza kidogo, nawe wang’amua kwamba umefika kwenye mwinuko ambapo barabara inakuwa yenye barafu.
Sasa lazima ukae chonjo sana. Upitapo kwa uangalifu kila kizingo chenye barafu, unafikiria jinsi ilivyo rahisi kushindwa kuendesha gari juu ya barabara yenye kuteleza na kutumbukia ndani ya bonde lililo chini. Zaidi ya hilo, wewe hujui hata kidogo ni hatari nyingine gani zinazokungoja katika lile giza. Mawazo kama hayo yajapo akilini mwako, kinywa chako chakauka na moyo wako wapigapiga kwa mwendo ulioongezeka. Uko macho kabisa. Hata uwe ulikuwa ukifikiria nini kabla ya hapo, sasa akili zako zimechukuliwa kabisa na shughuli ngumu uliyo nayo: kudumisha gari barabarani na kuepuka aksidenti.
Hatimaye, barabara yashuka kwenye mwinuko ulio chini zaidi. Kuna taa za barabara za mji, na hakuna barafu tena. Polepole, ule mkazo waondoka mwilini mwako. Unatulia na kupumua kwa kufarijika. Kumbe hiyo yote ilikuwa hofu ya bure tu!
Lakini je! yote ilikuwa ya bure tu? Sivyo kabisa. Wasiwasi wa kadiri chini ya hali kama hizo ni tendo-mwitikio la kikawaida. Hutufanya tukae chonjo, tujihadhari. Hofu inayofaa yaweza kutusaidia tusifanye jambo lolote bila kufikiri, tujiumize. Ndiyo, hofu si mharabu wa uwezo wa kusababu wala si sumu ya kiakili sikuzote. Chini ya hali fulani, inaweza hata kuwa yenye kunufaisha.
Biblia husema juu ya hofu nayo huvuta uangalifu wetu kwenye aina mbili hasa. Aina moja ya hofu ni sumu ya kiakili kweli kweli. Lakini zaidi ya ile nyingine kuwa ya kawaida na yenye kufaa, inahitajiwa kabisa pia kwa ajili ya wokovu wetu. Ni zipi hizo aina mbili za hofu? Nasi twaweza kujifunzaje kusitawisha moja huku tukiepuka ile nyingine? Hili litazungumzwa katika makala inayofuata.