Amani Je! Itakuja kwa Kuondoa Silaha?
“NI KOSA kubwa sana kudhani amani itakuja kwa kuondoa silaha,” akasema Winston Churchill miaka mitano kabla ya mataifa kutumbukia ndani ya vita ya ulimwengu ya pili. “Wakati mtakapokuwa na amani hapo ndipo mtaweza kuondoa silaha,” yeye akaongezea.
Lo, hicho chasikika kuwa kinyume sana! Ni nani atajasiria kuondoa silaha kabla hakujahakikishwa kwamba kuna amani? Lakini kwawezaje kuwako amani halisi na huku silaha zimerundikwa sana kwa ajili ya vita? Hiyo ni hali ambayo wanasiasa hawajapata kamwe njia ya kutokea.
Winston Churchill alitoa taarifa yake katika 1934, baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kuondoa Silaha uliofanywa na Ushirika wa Mataifa miaka miwili tu mapema kidogo. Kusudi la mkutano huu, uliokuwa umechukua miaka 12 kuutayarisha, lilikuwa kuzuia Ulaya isifanyize tena silaha. Duniani pote watu walikuwa wangali wakumbuka dhahiri kuchinjwa vibaya sana kwa wapiganaji milioni tisa hivi katika Vita ya Ulimwengu 1, kuongezea mamilioni waliojeruhiwa na hesabu kubwa sana ya raia walioumizwa. Hata hivyo, silaha hazikuondolewa kamwe. Kwa nini?
Jitihada za Kuondoa Silaha
Sera ya kuondoa silaha yaweza kufikilizwa lakini ni mara chache ambapo huwa na matokeo. Kwa kielelezo, chini ya Mkataba wa Versailles wa 1919, Ujeremani iliondoa silaha kwa kufanya “mahakikishiano ya kutosha kwamba silaha za kitaifa zingepunguzwa ziwe za kiasi cha chini kabisa chenye kupatana na usalama wa kinyumbani.” Ilikuwa hivyo kwa kupatana na moja la madokezo ya rais wa United States Woodrow Wilson, ambalo baadaye liliingizwa katika Kifungu cha 8 cha agano la Ushirika wa Mataifa. Lakini Hitler alipoingia mamlakani, muda si muda akapuuza sera hiyo.
Je! Umoja wa Mataifa ulifanikiwa zaidi katika kuanzisha msingi thabiti wa kuondoa silaha baada ya vita ya ulimwengu ya pili? Sivyo, lakini kutofanikiwa kwao hakukusababishwa na ukosefu wa jitihada nyingi. Ingawa hivyo, kuondoa silaha kulikuwa suala la uharaka mkubwa, huku silaha za uharibifu mkubwa zikiwapo. The New Encyclopcedia Britannica yasema kwamba, “ubishi uliokuwako hapo kwanza kwamba mashindano ya kuunda silaha huleta hasara ya kiuchumi na kuongoza kwenye vita isiyoepukika ulibadilishwa kwa hoja ya kwamba kutumia silaha za nyukilia kwa wingi wakati ujao kulitisha kuharibu usitawi wa utamaduni wenyewe.”
Tume ya Kuondoa Silaha yenye kuhusisha mataifa 12 ilianzishwa katika 1952 ili kuzuia shindano la kuunda silaha lililokuwa likiendelea kati ya Mashariki na Magharibi. Tume hiyo haikuwa na mwanzo wenye nguvu, na hatimaye hizo mamlaka kubwa mbili ziliweka mtengano mkubwa kati ya kambi zao zenye kupingana. Miafaka na mikataba mingine mbalimbali imefanyizwa kufikia wakati wa sasa. Hata hivyo, hali ya kutoaminiana haikuruhusu kuondolewa kabisa kwa silaha zote za vita. Kufanya hivyo, yasema The New Encyclopcedia Britannica, ni jambo ambalo “latetewa na wenye kuwazia-wazia jambo lisilowezekana.”
Kuhesabu Gharama
Kama silaha zaondolewa au haziondolewi—ni gharama gani ambazo zahusika? Gharama hazihesabiwi sikuzote kulingana na matumizi ya pesa. Jambo la maana sana kufikiriwa pia ni kazi za kuajiriwa ambazo hupatikana kutokana na biashara za kuunda silaha. Katika mabara mengi pesa za kodi hutumiwa kununua silaha, na kuundwa kwazo huongezea kazi za kuajiriwa. Kwa hiyo kuondoa silaha kungeweza kuongoza kwenye ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Ndiyo sababu nchi zilizo na wajibu mzito wa kupanga matumizi ya pesa za ulinzi hutetemekea wazo la kuondoa silaha kabisa. Kwa maoni yao fikira ya jinsi hiyo ni ndoto mbaya sana ya usiku, licha ya kuwa ndoto ya kuwazia jambo lisilowezekana.
Hata hivyo, hatuwezi kupuuza zile pesa nyingi sana zenye kuhusika katika kuendesha shughuli za vita. Yakadiriwa kwamba asilimia 10 ya thamani ya jumla ya mazao ya ulimwengu inatumiwa kuhusiana na silaha. Hicho ni kiasi gani? Tarakimu halisi hutofautiana kulingana na hali ya infleshoni, lakini fikiria ukila pauni milioni 1 (dola milioni 1.54 za United States) kwa njia hii kila dakikaya siku! Wewe ungechagua kutanguliza mambo gani kwanza kama ungekuwa na kiasi hicho? Je! ungekitumia kwa kusaidia wenye njaa? Kwa matibabu? Kwa hali njema ya watoto? Kurudisha uzuri wa mazingira? Kuna mengi sana ambayo yangeweza kufanywa!
Kwa kielelezo, chukua ile programu ya kwamba “vifaru vya vita vigeuzwe viwe tingatinga” iliyotangazwa majuzi katika Urusi, ambako viwanda fulani vya silaha vinabadilishwa ili vitokeze namna 200 za “vyombo vya hali ya juu ili vitumiwe upande wa biashara ya ukulima.” Kwa nini vyombo hivyo vya ukulima vyahitajiwa sana? Kwa sababu, kulingana na Farming News ya Uingereza, “theluthi moja tu ya matunda na mboga za kimajani ambazo hukuzwa katika mashamba ya serikali ndizo humfikia mnunuzi, huku zile nyingine zikiachwa zioze katika mashamba au ziharibike kwenye vituo vya usafirishaji na maghala.”
Ingawa huenda likawa ni jambo la kusifika sana kutokeza tingatinga badala ya vifaru vya vita, jambo hilo latangazwa sana katika vichwa vikuu vya magazeti kwa sababu ni ajabu isiyo ya kikawaida. Zaidi ya hilo, matokeo yalo ni kidogo katika kupunguza jumla ya silaha ambazo huundwa. Mamia ya mamilioni ya pauni, rubo, na dola zisizohesabika zaendelea kutumiwa kuhusiana na silaha katika ulimwengu ambamo ‘watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu,’ sawa na vile Yesu Kristo alivyotabiri. Woga huo waweza kuondolewaje? Je! jambo hili la kuondoa silaha kabisa litabaki likiwa ndoto tu? Ikiwa sivyo, ni kitu gani chahitajiwa ili kuziondoa kabisa?—Luka 21:26, HNWW.