Muono-Ndani Juu ya Habari
Madhumuni Yenye Ubinafsi
Upesi baada ya kuja mamlakani katika 1933, kiongozi wa Nazi Adolf Hitler alifanya mapatano ya mkataba na Kanisa Katoliki. Mkataba huu ulimpa Hitler haki ya kuzuia uteuzi wa maaskofu Wajeremani kwa kubadilishana naye mapendeleo fulani ambayo kanisa lilikabidhiwa. Lakini ni nani kati yao angenufaika zaidi? Ensaiklopedia mpya ya Katoliki ya Kifaransa yatoa jibu la moja kwa moja kwa swali hilo.
“Papa Pius II mwenyewe . . . aliona yahitajiwa kabisa kuhakikisha kulinda salama kanisa la Kijeremani kwa njia ya mkataba fulani. Huo ulifanywa kati ya Aprili na Julai 1933. Ingawa hapo kwanza ulipendelea Kanisa Katoliki, kwa kweli mkataba huu ulifanikisha Hitler, kwa maana ulitambua utawala wake. Tena, kwa kuwa Hitler aliuvunja mara nyingi, papa alishtakiwa juu ya kufanya dhamiri za Wakatoliki zisinzie na kuwafanya maaskofu wawe hoi kwa kufanya makubaliano ya kipumbavu.”
Leo, hasa katika Ufaransa na Ujeremani, Kanisa Katoliki huchambuliwa peupe kwa mambo ambayo utawala wa makasisi wao uliridhiana wakati wa utawala wa Nazi. Matatizo haya husitawi wakati viongozi wa kanisa washindwapo kutii maneno na kielelezo cha Yesu Kristo, aliyesema hivi juu ya wafuasi wake wa kweli: “Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi si sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:16, NW) Ni kweli, mambo hayo ya kuridhiana na viongozi wa kanisa yamefanya wapate upendeleo wa wanasiasa, lakini hiyo imefanya nini kwa uhusiano wao na Mungu? Akiandikia Wakristo wenzake, Yakobo mwanafunzi wa Yesu alionya hivi: “Urafiki na ulimwengu ni uadui na Mungu.”—Yakobo 4:4, NW.
Wapatao Hasara Katika Michezo ya Nasibu
Uwezekano wa kushinda mchezo wa nasibu ni karibu mara 1 kwa kila mara milioni 14. Hata hivyo, mamilioni ya watu hucheza kwa ukawaida michezo ya nasibu yenye kudhaminiwa na serikali, laripoti The Globe and Mail, gazeti la Kikanada. Utafiti waonyesha kwamba michezo ya nasibu haina jambo la kuvutia isipokuwa tumaini la kushinda zawadi kubwa, jambo ambalo mara nyingi huchochewa na utangazaji wenye kukaza fikira “juu ya zawadi na hatari za kushindwa kununua tikiti.” Kwa kuwa lengo la mchezo wa nasibu ni kupata faida na kutokeza washindi wachache, wadhamini hufanya matangazo ya kila siku kwa “matumaini ya kuimarisha tabia za kununua kikawaida.“
Je! jambo hilo lina matokeo? Ndiyo! Akiripoti katika gazeti American Health juu ya ongezeko la kucheza kamari miongoni mwa matineja, Dakt. Durand Jacobs aonyesha michezo ya nasibu kuwa utangulizi wa kucheza kamari “kwa sababu [michezo] hiyo ni ya gharama ndogo, hupatikana kwa urahisi na huhimizwa kuwa ni sawa.” Aongezea hivi: “Mchezo wa nasibu ndicho kishawishi ambacho huongoza wabalehe waingilie namna nyingine za mazoea ya kamari.” Mkanada mmoja aliye mtaalamu juu ya habari za uzoevu wa kucheza kamari ataarifu hivi: “Mtu yeyote ambaye angejaribu kukuambia kwamba michezo ya nasibu si kucheza kamari anatenda kipumbavu ama ni mpumbavu. . . . Tunatumia mamia ya mamilioni ya dola kwa michezo ya nasibu kwa matumaini ya kushinda kitu fulani. Huko ni kucheza kamari.”
Michezo ya nasibu huendeleza upendo wa pesa. Dakt. Marvin Steinberg, msimamizi wa Baraza la Connecticut Kuhusu Kamari lliyo Mazoea, aliona kwamba matineja wenye kutatizika kwa kucheza kamari walitumia pesa zao za chakula cha mchana, waliiba pesa, na hata waliiba madukani ili kutegemeza zoea lao la kucheza kamari. Ni ya kweli kabisa maneno ya mtume Paulo: “Shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo . . . [wamejichoma] kwa maumivu mengi.”—1 Timotheo 6:9, 10.