“Kuzagaa kwa Amani”?
“KUZAGAA KWA AMANI.” “Lo, Ulimwengu Wenye Amani Kama Nini.” “Amani Inabubujika Kila Mahali.” Hivi vilikuwa baadhi ya vichwa vikuu katika magazeti ambavyo vimegutusha wasomaji mwaka mmoja au miwili hivi iliyopita. Kote ulimwenguni, badiliko la kuacha kuwako habari za majonzi na maangamizi na kuwako za matazamio mema liligutusha. Kulikuwa kukitukia nini?
Kwa kustaajabisha, juzijuzi mapambano kadhaa makubwa yalimalizika yote au yakapunguzwa uzito katika muda wa miezi michache tu. Katika Afrika, amani ‘ilifoka’ katika Angola. Katika Esia ya Kati, Urusi iliondoa majeshi yayo katika Afghanistan. Katika Amerika ya Kati, kupigana kulitulia kati ya serikali ya Nikaragua na waasi wa Contra. Katika Esia ya Kusini-mashariki, Wavietnam waliafikiana kuondoka Kampuchea. “Kuzagaa kwa amani” (kuenea pote) hata kulifika Mashariki ya Kati wakati ile vita yenye kiu ya damu kati ya Irani na Iraki ilipokoma mwishowe.
Labda yenye kustahiki kuangaliwa zaidi ni hali mpya iliyo kati ya zile serikali mbili zenye nguvu ulimwenguni. Baada ya miaka 40 ya vita baridi, ilikuwa vigumu kuamini zile ishara za mapatano, maneno ya juu ya masilahi ya pamoja, na hatua zilizo thabiti za kuelekea amani kati ya Urusi na United States. Tena, kulingana na The Economist, sasa Ulaya imekuwa ndiyo yenye kipindi kirefu zaidi kisichokuwa na vita katika historia yote iliyorekodiwa. Kwa kweli, amani yatangazwa katika habari.
Hiyo yamaanisha nini? Je! wanasiasa wako katika ukingo wa kuleta “amani kwa wakati wetu”? Miaka 51 iliyopita, maneno hayo yalitamkwa na waziri mkuu Mwingereza Neville Chamberlain. Kumbe yakawa kinyume kikatili kabisa wakati vita ya ulimwengu ya pili ilipofoka muda mfupi baadaye. Je! baada ya muda wote huo yatatimia sasa hatimaye?