Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 4/1 kur. 4-6
  • Amani Kuna Uwezekano Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Amani Kuna Uwezekano Gani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Amani Kupitia Dini na Sheria
  • Jitihada Zaidi za Kuleta Amani
  • Kani Iliyofichika Yenye Kuzuia Amani
  • Amani ya Kweli—Kutoka Chanzo Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Jinsi Ambavyo Amani Yaweza Kupatikana Duniani
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Acha “Amani Ya Mungu” Ilinde Moyo Wako
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Nani Ataongoza Ainabinadamu Kwenye Amani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 4/1 kur. 4-6

Amani Kuna Uwezekano Gani?

KUJAPOKUWA na vichwa vikubwa vya habari za magazetini, kama wengi wetu tung’amuavyo, ukweli ni kwamba ainabinadamu ingali mbali na amani halisi. Kuondolewa kwa majeshi ya kigeni katika Afghanistan hakukuleta amani kwenye bara hilo. Na kungali kuna ugomvi wa aina moja au nyingine katika Ufilipino, Sudan, Israel, Ailandi Kaskazini, Lebanoni, na Sri Lanka, kutaja chache tu.

Kwa kuwa walio wengi zaidi kati ya watu walio na akili timamu hupendelea zaidi amani, kwa nini amani huponyoka sana? Kwa karne nyingi wanasiasa wamejaribu kuleta amani kwa njia nyingi, lakini sikuzote jitihada zao zimekosa mafanikio. Kwa nini? Acheni tutazame vielelezo vichache tuone.

Amani Kupitia Dini na Sheria

Watu fulani wana maoni ya kwamba Milki ya Kiroma ilifanya jaribio lenye mafanikio kufanyiza amani. Chini yayo, mchanganyiko wa sheria imara, usimamizi wenye kupindikana, majeshi yenye kuogopesha sana, na barabara zilizoundwa vizuri, kwa karne nyingi ulidumisha uthabiti wa kimataifa ujulikanao kuwa Pax Romana (Amani ya Kiroma) katika maeneo makubwa ya Esia Magharibi, Afrika, na Ulaya. Ingawa hivyo, mwishowe Milki ya Kiroma ilijiachilia ikashindwa na ufisadi wa kindani na mavamio ya kutoka nje, na ile Amani ya Kiroma ikaangamia.

Hicho ni kielezi cha ukweli mmoja wa kuhuzunisha juu ya jitihada za kibinadamu. Baada ya hizo kuwa na mwanzo wenye tumaini, kwa kawaida huzorota. Mungu mwenyewe alisema: “Mbetuko wa moyo wa mwanadamu ni mbaya kuanzia ujana wake na kuendelea,” na kwa kawaida mbetuko mbaya huu ndio hushinda hatimaye. (Mwanzo 8:21, NW) Tena, nabii Yeremia alisema hivi: “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” (Yeremia 17:9) Wanadamu hawatabiriki. Madhumuni mema ya mtu mmoja huenda yakapinduliwa na wivu au tamaa za makuu ya ubinafsi ya wengine. Au huenda mtawala mwenye kanuni za juu akawa mfisadi yeye mwenyewe. Kwa sababu ya hilo, wanadamu wawezeje kuleta amani?

Katika karne ya tatu K.W.K., jitihada nzuri ajabu ya kufanyiza amani iliripotiwa kutoka nusukontinenti ya India. Huko, mtawala mwenye nguvu jina lake Asoka alijifanyizia milki kubwa kupitia vita na umwagaji damu. Halafu, kulingana na maandishi, aliongolewa akafuata kanuni za Dini ya Buddha. Kwa kukataa vita katakata, alisimamisha majengo ya ukumbusho kuzunguka milki zikiwa na semi za kusaidia raia zake waishi maisha bora. Na yaonekana milki yake ilikuwa yenye amani na ufanisi.

Je! njia ya Asoka ndiyo ya amani? Kwa kusikitisha, siyo. Maliki huyo alipokufa, amani yake ilikufa naye, na milki yake ikabomokabomoka. Hicho ni kielezi cha kwamba hata jitihada za mtawala mwenye madhumuni mazuri na uwezo huvurugika hatimaye kwa sababu ya yeye kulazimika kufa. Mwandikaji wa Mhubiri alitaja tatizo hili alipoandika hivi: “Nami nikaichukia kazi yangu yote [ambayo] . . . sina budi kumwachia yeye atakayenifuata. Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili.”—Mhubiri 2:18, 19.

Ndiyo, hali ya kufa kwa mwanadamu ni kipingamizi kisichoshindika chenye kuzuia kuleta kwake amani inayodumu. Kwa uhakika shauri la mtunga zaburi ni la hekima katika habari hii: “Msiwatumainie wakuu, wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, siku hiyo mawazo yake yapotea.”—Zaburi 146:3, 4.

Jitihada Zaidi za Kuleta Amani

Jitihada nyingine za kibinadamu zatoa vilevile kielezi cha sababu ambayo hufanya mwanadamu ashindwe katika jaribio lake la kuleta amani. Kwa kielelezo, katika karne ya kumi, harakati moja yenye kuitwa Amani ya Mungu ilianzishwa Ulaya. Ikiwa imekusudiwa ilinde mali ya kanisa, ilisitawi ikawa mwafaka usio na uchokozi ambao kufikia katikati ya karne ya 12 ulikuwa umeenea kwenye sehemu kubwa ya Ulaya.

Wazo jingine huitwa “usawaziko wa uwezo.” Kwa kufuata sera (mwongozo) huu, jumuiya ya mataifa—kama Ulaya—huvunja moyo kufanya vita kwa kudumisha ugawanyaji wa mamlaka iliyosawazika kwa kadiri fulani miongoni mwa madola. Taifa fulani imarifu likitisha lililo dhaifu, taifa jingine imarifu hujiunga kwa muda na lililo dhaifu ili kuvunja moyo lile lililotaka uchokozi. Sera hii iliongoza mahusiano ya Ulaya kuanzia mwisho wa Vita vya Kinapoleoni hadi kufoka kwa vita ya ulimwengu ya kwanza katika 1914.

Baada ya vita hiyo, Ushirika wa Mataifa ulianzishwa kuwa baraza ambamo mataifa yangeweza kufanya maongeo ya kutatua tofauti zayo badala ya kuzipigania. Ushirika ulikoma kufanya kazi wakati vita ya ulimwengu ya pili ilipofoka, lakini baada ya vita, roho yao ilifufuka katika Umoja wa Mataifa, ambao ungali upo.

Hata hivyo, jitihada zote hizi zilishindwa kuleta amani halisi au inayodumu. Ingawa ile harakati ya Amani ya Mungu ilikuwako katika Ulaya, Wanaulaya walipigana na Waislamu katika Krusedi zenye kiu ya damu. Na ingawa wanasiasa walikuwa wakijaribu kuhifadhi amani katika Ulaya kwa kusawazisha mamlaka, wao walikuwa wakifanya vita na kujenga milki katika mabara yaliyo nje ya Ulaya. Ushirika wa Mataifa haukuweza kuzuia vita ya ulimwengu ya pili, na Umoja wa Mataifa haukuzuia machinjo katika Kampuchea wala mapambano katika mahali kama vile Korea, Naijeria, Vietnam, na Zaire.

Ndiyo, kufikia sasa jitihada bora zaidi za wanasiasa kufanyiza amani zimekosa mafanikio. Watawala hawajui kamwe jinsi ya kufanyiza amani inayodumu, kwa kuzuiwa na hali ya kufa na makosa yao wenyewe na ya wengine ya kibinadamu. Lakini, hata kama haingekuwa hivyo bado wanasiasa hawangeweza kuleta amani. Kwa nini? Kwa sababu ya kipingamizi kingine ambacho kwa kweli hakishindiki kwa urahisi.

Kani Iliyofichika Yenye Kuzuia Amani

Biblia hunena juu ya kipingamizi hicho isemapo hivi: “Ulimwengu wote mzima unalaa unalala katika uwezo wa yule mwovu.” (1 Yohana 5:19, NW) Mwovu huyo ni Shetani Ibilisi kiumbe roho wa kumzidi binadamu ambaye ni mwenye nguvu kuliko sisi. Kutoka mwanzo, Shetani amehusika katika uasi, kusema uwongo, na kuua. (Mwanzo 3:1-6; Yohana 8:44) Ingawa umefichika, uvutano wake wenye nguvu juu ya mambo ya ulimwengu huthibitishwa na waelezaji wengine waliovuviwa. Paulo alimwita “mungu wa mfumo huu wa mambo,” “mtawala wa mamlaka ya hewa.” (2 Wakorintho 4:4; Waefeso 2:2, NW) Zaidi ya mara moja Yesu alimwita “mtawala wa ulimwengu huu.”—Yohana 12:31; 14:30; 16:11, NW.

Kwa kuwa ulimwengu unalala katika mamlaka ya Shetani, hakuna uwezekano wowote kwamba wanasiasa wa kibinadamu wataleta amani inayodumu. Je! hiyo yamaanisha kwamba amani haitakuja kamwe? Je! mtu yeyote aweza kuongoza ainabinadamu kwenye amani?

[Blabu katika ukurasa wa 5]

Hata kama mtawala ni mwenye hekima na mwenye kufuata kanuni za juu kama nini, hatimaye yeye hufa na mara nyingi wengine wasio hodari sana na wasiofuata sana kanuni huchukua nafasi yake

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Kipingamizi kimoja kikubwa zaidi chenye kuzuia amani ni Shetani Ibilisi

[Picha Credit Line katika ukurasa wa 5]

Foto ya U.S. National Archives

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki