‘Nilipanda Juu kwa Mabawa Kama Tai’
Kama ilivyosimuliwa na Ingeborg Berg
MIMI nilizaliwa zaidi ya miaka mia moja iliyopita, mnamo Juni 5, 1889, karibu na Buruji ya Fredensborg, juu kidogo tu ya kaskazini mwa Copenhagen. Wakati jamaa ya kifalme ya Denmark ilipokuwa na wageni, kutia na wafalme na wamaliki kutoka nchi za Ulaya, mabibi wa kutoka makao ya matajiri katika Fredensborg walialikwa kusaidia kutayarisha chakula na kukipakua. Nikiwa msichana mdogo, nilipelekwa huko mara nyingi na kuruhusiwa kucheza na kukimbia-kimbia katika buruji hiyo.
Kumbukumbu yangu iliyo dhahiri zaidi ni kuhusu Czar Nicholas 2 wa Urusi na jamaa yake. Nje ya chumba chake cha kulala alisimama mlinzi wake, kozaki (askari) mwenye upanga uliofutwa. Kozaki walipenda sana watoto, na mmoja wao wakati mmoja alijaribu kunikumbatia. Kwa kuogopeshwa sana, hasa na ndevu zake kubwa, nilikimbia kwa kupita katika safu ndefu za buruji.
Katika pindi moja Czar Nicholas 2, Maliki Wilhelm 2 wa Ujeremani, na mwana wa Malkia Victoria, ambaye baadaye akawa Mfalme Edward 7 wa Uingereza, walizuru mfalme Mdenmark Christian 9. Walipokuwa wakitembea-tembea katika barabara za Fredensborg, wakiongea kwa fadhili na watu, Czar Nicholas alinipapasa kichwani nilipopinda magoti kumwinamia. Ulikuwa wakati wenye amani, na vichwa vya mataifa hawakuhofia usalama wao kama wafanyavyo leo.
Amani Yaondolewa
Katika 1912 nilianza kazi nikiwa mwuguzi katika Jutland Kusini, nikitumikia watu wenye kuunga mkono Wadenmark kwenye mpaka ulio upande wa Ujeremani. Jutland Kusini ilikuwa imekuwa chini ya utawala wa Kijeremani tangu vita katika 1864 kati ya Denmark na Prussia. Nilisaidia akina mama wenye vitoto vilivyozaliwa karibuni na nikajuana sana na nyingi za jamaa changa hizo.
Katika 1914 niliolewa na mlinda-mpaka Mdenmark na nikaja kuishi kwenye mpaka ulio upande wa Denmark. Muda si muda vita ikafoka. Baadaye iliitwa ile Vita Kubwa na, hatimaye, Vita ya Ulimwengu 1. Asubuhi moja, seng’enge ilikunjuliwa ikaenezwa kandokando ya mpaka, ikizuia mwendo wa uhuru kuivuka. Amani na usalama tulivyokuwa tumepata mpaka wakati huo vikawa vimekwisha.
Ogofyo na matokeo ya upumbavu wa vita yalitukaribia sana tulipopata habari kwamba baba wachanga katika jamaa zote nilizokuwa nimezuru nikiwa mwuguzi walikuwa wakiitwa wakaingie utumishi wa kijeshi. Na wote isipokuwa mmoja waliuawa kwenye Kikosi-mbele cha Magharibi kule Marne! Ilikuwa vibaya sana kufikiri juu ya wajane wachanga hao, wakiteseka kwa kupoteza waume zao na watoto wadogo wakipoteza baba zao. Wanawake wachanga hawa wangewezaje kutunza mashamba yao? “Mungu yuko wapi?” nikauliza.
Wakati wa vita, hali mpakani ilikuwa ya wasiwasi mara nyingi huku wakimbizi wakijaribu kuuvuka. Mimi niligawiwa kupekuapekua wanawake waliotuhumiwa kuwa wafanya magendo. Kwa kawaida, chakula ndicho walibeba, na mara nyingi nilikiachilia na kuwaacha waende zao. Vita iliisha katika 1918, na katika 1920 Jutland Kusini ikaunganishwa upya na Denmark.
Kupata Imani Katika Mungu
Ingawa imani yangu katika Mungu ilikuwa imedhoofika kwa sababu ya matendo yote ya kukosa haki niliyoyaona, nilikuwa nikitafuta maana fulani ya maisha. Mume wangu Alfred na mimi tulihudhuria kanisa kwa ukawaida, lakini maswali yetu hayakujibiwa.
Katika 1923 tulihamia kijiji kidogo cha uvuaji samaki kwenye Kilangobahari cha Flensburg, na Alfred akaanza kazi akiwa mvua samaki. Muda si muda tukajuana na jamaa moja waliokuwa Wabaptisti. Ingawa sisi tulikuwa Walutheri, siku moja tulikubali mwaliko wao kuja kwenye hotuba ya Biblia katika Ferry Inn katika Egernsund. Kabla ya kwenda, nilipiga magoti nikasali hivi: “Ikiwa kuna Mungu, tafadhali sikiliza sala yangu!”
Hotuba ilikuwa juu ya mwanamke kwenye kisiwa cha Sikari, na ilinipa tamaa ya kusoma Biblia. Tokeo ni kwamba, mimi nikawa kama mtu mpya! Nilimwandikia mama yangu hivi: “Sikuzote wewe ulisema kwamba napaswa kuongolewa nije kwa Mungu. Nafikiri kwamba hilo limetukia sasa; nimekuwa nikiogopa kukuambia kwa kuhofu shangwe ambayo mimi nimepata itatoweka. Lakini ingalipo!”
Muda fulani baadaye, katika 1927, katika chumba cha juu ya nyumba yetu nilipata kijitabu chenye kichwa Freedom for the Peoples. Kilivuta fikira zangu, na fikira zangu zikanaswa sana katika yaliyomo hivi kwamba nilisahau ni saa ngapi na niko wapi. Watoto walipokuja nyumbani kutoka shuleni na kutaka kula ndipo nikajilazimisha kuacha kukisoma.
Alfred alipokuja nyumbani jioni hiyo, nilimwambia kwa idili nyingi mambo niliyokuwa nimesoma. Nilimwambia kwamba ikiwa yaliyosemwa na kijitabu hicho ni kweli, basi kanisa halikuwa nyumba ya Mungu, na yatupasa kujiuzulu na kuliacha mara hiyo. Alfred aliwaza kwamba kufanya hivyo kungekuwa haraka isiyofaa, na akasema hivyo. Lakini tuliafikiana kuandika barua kwenye ofisi ya tawi ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi katika Copenhagen na kuomba fasihi zaidi.
Kwa kujibu ombi letu, mwangalizi mwenye kusafiri, Christian Remer, alitumwa kuja kutuzuru. Tulimpa chumba cha watoto na tukaweka vitanda vyao katika chumba cha juu ya nyumba. Asubuhi na alasiri, Ndugu Romer alienda nje kuhubiri mlango kwa mlango, na kila jioni akajifunza nasi. Alikaa siku nne, nasi tukawa na wakati mzuri kweli kweli. Alipoondoka, nilimwuliza tena Alfred juu ya kujiuzulu kanisani. Wakati huu aliafikiana nami kwa idili.
Kwa hiyo Alfred akamwendea mhudumu akiwa na maandishi ya kujiuzulu kwetu. Mhudumu alifikiri kwamba Alfred alikuwa amekuja kwa sababu kulikuwako kitoto kingine cha kubatizwa. Hata hivyo, alipoelewa kwa nini Alfred amekuja, hakusadiki. “Kanisa lina ubaya gani?” akataka kujua. Alfred alitaja mafundisho ya Utatu, kutokufa kwa nafsi, na mateso ya milele. “Biblia haifundishi mambo hayo,” Alfred akasema. Mhudumu alipojibu kizembe kwamba yeye hangenena kamwe juu ya mambo haya kwa watu wenye uwezo wa kufikiria mambo wao wenyewe, Alfred alisema hivi kwa uthabiti: “Sisi twataka kutoka kanisani!”
Uvuvi na Ubatizo wa Ghafula
Mkusanyiko ungefanywa katika Copenhagen, lakini pesa zetu zilikuwa chache na hazingeweza kugharimia safari ile. Mimi nilisali kwa Mungu atuonyeshe njia ya kufika huko kwa kuwa tulitaka kubatizwa. Muda mfupi kabla ya mkusanyiko, Alfred alisafiri katika kilangobahari kuvua samaki. Alivua wengi sana hata mashua ikajaa, nasi tukawa twaweza kulipia safari yetu. Wavuvi wa pale walistaajabu, kwa kuwa ni samaki wachache waliovuliwa katika kilangobahari mwaka huo. Kwa uhakika, zaidi ya miaka 50 baadaye, wavuvi wa hapo wangali waliongea juu ya “ule muujiza.” Sisi tuliuita ule uvuvi samaki wa Petro. Kwa hiyo siku ya Agosti 28, tulibatizwa.
Ubatizo huo ulikuwa tofauti na mabatizo ya leo. Nyuma ya pazia kilikuwako kidimbwi cha ubatizo. Pazia lilipofunguliwa, Ndugu Christian Jensen huyo tayari kuufanya uzamisho. Alikuwa amevalia koti-mkia, akiwa amesimama katikati ya kidimbwi huku maji yakiwa yamemfika kiunoni. Sisi wabatizwa tulivalia kanzu ndefu nyeupe. Kwanza wanaume ndio waliobatizwa halafu wanawake.
Wakati wa mkusanyiko katika Copenhagen tulikaa na wazazi wangu. Nilipokuja nyumbani jioni hiyo, baba yangu aliuliza tulikuwa wapi.
“Tulikuwa kwenye mkutano mmoja,” nikasema.
“Kulitukia nini huko?”
“Tulibatizwa,” nikajibu.
“Eti mlibatizwa?” akanguruma. “Kwani ubatizo uliopewa ukiwa mtoto haukufaa?”
“Sivyo, Baba,” nikajibu. Halafu akanizaba kofi kali kwenye sikio, akipiga kelele hivi: “Mimi nitakubatiza wewe!”
Nilikuwa na umri wa miaka 39 tena mama wa watoto watano wakati wa hilo kofi la sikio la mwisho kupata kutoka kwa baba yangu, ambaye japo alifanya hivyo alikuwa mzuri na mfadhili sana. Hakutaja tena kamwe kituko hicho. Uzuri ni kwamba, Alfred alikuwa bado hajaja nyumbani, na ni baada ya miaka mingi kwamba nilimwambia lililokuwa limetukia.
Wakati wa Kupepeta
Tulipofika nyumbani, nilizuru mtu fulani ambaye nilikuwa na maoni ya kwamba alikuwa ni dada nikamsimulia kwa shauku juu ya ule mkusanyiko na ubatizo wetu. Aliketi kimya sana halafu akasema: “Maskini, maskini Dada Berg. Usiamini tena mambo haya. Siku moja ndugu mmoja kutoka Flensburg alikuja, naye atatueleza ukweli.”
Niliduwaa. Nikaendesha baiskeli kwa shida nyingi ili nifike nyumbani. Kengele ya kanisa la hapo karibu ilikuwa ikilia sana, na kwa kila mlio wayo ilikuwa kana kwamba mimi nasikia “kifo, kifo” katika masikio yangu. Kwa ndani nikalilia Yehova kuomba msaada, na maneno ya Zaburi 32:8, 9 yakaja kwenye akili yangu: “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; nitakushauri, jicho langu likikutazama. Msiwe kama farasi wala nyumbu, walio hawana akili. Kwa matandiko ya lijamu na hatamu sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia.”
Nilipowasili nyumbani, nilichukua Biblia yangu nikasoma Sala ya Bwana. Nikapata upya uhakikishio. Ule mfano wa maneno juu ya lulu ya thamani kubwa ulikuja kwenye akili yangu. (Mathayo 13:45, 46) Ufalme ulikuwa kama lulu hiyo. Mimi nilitaka kutoa vyote nilivyokuwa navyo ili niupate Ufalme. Mawazo hayo yalinifariji. Na kulikuwako mibaraka mingine.
Katika 1930 gazeti The Golden Age (sasa Amkeni!) lilianza kuchapishwa katika Kidenmark chini ya jina The New World (Ulimwengu Mpya). Na mwaka uliofuata, sisi Wanafunzi wa Biblia tulifurahi sana kupokea jina la Mashahidi wa Yehova. Wakati huo tulikuwa wachache tu katika eneo letu, na mara kwa mara mikutano ilifanywa katika nyumba yetu. Kwa kuwa barabara ya tulipoishi iliitwa Ngazi, tuliitwa Kundi la Ngazi.
Kuvumilia Mitihani Zaidi
Katika 1934 nilifanyiwa upasuaji mkubwa na tokeo likawa kwamba, nilipooza. Nikawa kitandani kwa miaka miwili na nusu, na watabibu walitabiri kwamba ningekaa katika kiti-magurudumu muda wote uliobaki wa maisha yangu. Ulikuwa wakati mgumu sana kwangu, lakini jamaa yangu ilikuwa msaada mzuri ajabu.
Alfred alininunulia Biblia yenye chapa kubwa, na mwana wetu mchanga zaidi akawa kinara cha kuiegemeza ili niweze kulala kitandani na kuisoma. Lakini pia nilitaka kuhubiri, kwa hiyo Alfred akaweka kando ya barabara bango lenye kutangaza magazeti mapya. Wale waliopendezwa waliingia kuniona, nami nikaongea nao. Tokeo la bango hilo ni kwamba watu katika jimbo hilo waliita jamaa yetu Ulimwengu Mpya.
Waangalizi wenye kusafiri walikuwa chonjo kunizuru. Hivyo nikapata kujuana vizuri na ndugu hawa wakomavu wenye ujuzi, wakanitia moyo sana. Pia, nilitumia wakati huo kujifunza Biblia, na maarifa hayo yakanitegemeza. Nilihisi kana kwamba ‘nilipanda juu kwa mabawa kama tai.’—Isaya 40:31, ZSB.
Katika 1935, wakati utambulisho wa “mkutano mkubwa” ulipofahamika wazi, ndugu na dada walio wengi katika eneo letu, kutia na mwana na binti wetu wakubwa zaidi, waliacha kushiriki mkate na divai kwenye Ukumbusho. Hata hivyo, wachache wetu hatukutia shaka kamwe juu ya wito wetu wa kimbingu. Hata hivyo, tulifurahi pia juu ya uelewevu wetu mpya wa kusudi tukufu la Yehova kuhusu mkutano mkubwa na thawabu yao ya uhai wa milele duniani.—Ufunuo 7:9; Zaburi 37:29.
Nilipata nafuu kidogo kidogo, tofauti na vile madaktari walivyokuwa wametazamia, nami nikaweza tena kuwa na ushiriki kamili katika kazi muhimu ya kuhubiri na kufundisha.
Vita ya Ulimwengu 2 na Baadaye
Ng’ambo ya kilangobahari tungeweza kuona Ujeremani, nasi tukaanza kuhisi uvutano wa Unazi. Baadhi ya jirani zetu wakawa Wanazi, nao wakatutisha hivi: “Ngojeni mpaka Hitler aje. Ndipo nyie mtajikuta katika kambi ya mateso au katika kisiwa cha ukiwa!”
Tukahisi ni vema zaidi tuhame. Watu fulani wenye urafiki walitusaidia kupata nyumba ya ghorofani katika Sonderborg, mji mkubwa zaidi usio mbali sana. Vita ya Ulimwengu 2 ilianza katika Septemba 1939; sisi tulihama katika Machi 1940; na siku ya Aprili 9, vikosi vya Kijeremani viliitwaa Denmark. Hata hivyo, ajabu ni kwamba Ujeremani haikujishughulisha na Mashahidi wa Yehova.
Ndoto ya Hitler ya kushinda ilipoangamia hatimaye, nilifanya mafunzo ya Biblia na Wajeremani wengi waliozinduka walioishi katika Sonderborg. Lo, ilikuwa shangwe iliyoje si kuona tu wengi wa wanafunzi hawa wa Biblia wakiweka wakfu maisha zao kwa Yehova bali pia walio wengi kati ya watoto na wajukuu wangu wakiwa watendaji katika utumishi wa Kikristo!
Mume wangu alikufa katika 1962, mjukuu mmoja katika 1981, na binti yangu mkubwa zaidi akafa katika 1984. Kufuliza kuwa mtendaji katika utumishi wa Yehova ndiko kumenisaidia kupita katika nyakati hizi za majonzi.
Imekuwa vizuri ajabu kuona maendeleo ya kazi ya Ufalme katika Denmark kutoka wakati ambapo mimi nilianzia katika 1928. Wakati huo tulikuwa na wahubiri karibu 300 tu, lakini sasa kuna zaidi ya 16,000! Mimi nashukuru kwamba nikiwa na umri wa miaka mia moja, ningali naweza kuwa mtendaji katika utumishi. Nimejionea kikweli utimizo wa maneno yaliyo kwenye Isaya 40:31, ZSB: “Lakini wao wanaongojea Bwana [Yehova, NW] watapata nguvu mpya; watapanda juu na mabawa kama tai; watapiga mbio na hawatachoka; watatembea, wala hawatazimia roho.”