Je! Maskini Waweza Kuwa Wafuataji Haki?
Amelia alikuwa na umri wa siku 29 tu wakati nyanya yake alipomleta kwa daktari. Mama ya Amelia hangeweza kufunga safari hiyo, kwa maana alikuwa mgonjwa nyumbani akiwa pamoja na watoto wengine wanne.
Baba alikuwa mahali pengine akitafuta kazi. Daktari alichunguza huyo mtoto mchanga.
Kulikuwako ishara za kukosa vyakula vyenye kuufaa mwili, jambo ambalo halikosi kuwa la kawaida katika Afrika Magharibi.
Lakini tatizo kuu lilikuwa utendaji usiofaa wa chembe za mwili. Kifua kidogo sana cha Amelia kilitunga usaha wa ambukizo.
Daktari alipokuwa akimpa nyanya maagizo ya dawa za kutumia, nyanya aliuliza: “Dawa hii itagharimu kiasi gani?”
“Dola nne hadi tano,” mwanamume huyo akajibu.
Nyanya aliugua. Hata hakuwa na dola mbili za kulipa bei ya kumwona daktari. “Tupate wapi pesa nyingi hivyo!” yeye akapaaza sauti.
“Ni lazima uzipate mahali fulani,” daktari akasisitiza. “Waombe rafiki zako na watu wa ukoo. Usipotibu ambukizo hili, litaenea hadi kwenye mkondo wa damu, na mtoto atakufa.”
Kwa njia fulani familia ya Amelia ilipata pesa hizo, na huyo mtoto mchanga akaishi kuingia mwezi wake wa pili. Hata hivyo, mamilioni katika mabara yanayositawi kuzunguka ulimwengu hawawezi kukopa pesa kutoka kwa marafiki na watu wa ukoo. Na matazamio ya nafuu ya kiuchumi si maangavu.
The State of the World’s Children Report 1989 ya UNICEF (Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa) yajulisha rasmi hivi: “Baada ya miongo ya maendeleo ya kiuchumi yenye kuendelea bila kubadilika, maeneo makubwa ya ulimwengu yanarudi nyuma katika umaskini.” Katika Afrika na Amerika ya Kilatini, mapato ya wastani yalishuka kwa asilimia 10 hadi 25 katika miaka ya 1980. Na wakati wa miaka michache iliyopita, katika 37 ya mataifa ya ulimwengu yaliyo maskini sana, gharama za afya zimepungua kwa asilimia 50.
Hii yamaanisha nini kwa mamilioni wanaoishi katika umaskini? Kwa wengi, yamaanisha hawawezi kununua chakula au dawa zinazohitajiwa. Kwa hiyo, watoto wao, wenzi wa ndoa, au wazazi huenda wakalazimika kufa bure tu, isipokuwa wakigeukia kupata pesa kwa njia ile moja tu ionekanayo kuwa wazi kwao—kwa kuiba! Ndiyo, umaskini waweza kumaanisha kung’ang’ana na matatizo ya kiadili yenye kubana vikali sana pande zote: kuiba au kufa? kusema uwongo au kufa njaa? kuhonga au kukosa mahitaji ya maisha?
Katika Afrika Magharibi kuna usemi huu: “Hapo umfungapo ng’ombe, atakula nyasi papo.” Ndiyo kusema, watu watatumia kwa faida hali yoyote iwaruhusuyo kujitajirisha. Mara nyingi mno, wenye mamlaka katika mabara mengi kotekote duniani hutumia vyeo vyao kutoza hongo kwa nguvu, kutumia vibaya pesa zilizowekwa amana, au kuiba. ‘Jisaidie maadamu waweza,’ ndivyo wao husababu mambo. ‘Huenda usiwe na nafasi ya kufanya hivyo baadaye.’ Shida ya kiuchumi ya mataifa yanayositawi izidipo kuwa mbaya, huenda mafukara wakaunga mkono wazo la kwamba ufuataji haki hauwezi kuwa ndio mwongozo bora kwa maskini.
Biblia husema: “Usiibe.” (Kutoka 20:15) Lakini ikiwa kwa kweli maskini hawawezi kuwa wafuataji haki, je! kunakuwa na shaka juu ya uhalali wa maadili ya Biblia? Je! sheria za Mungu hazitumiki kwa njia yenye mafaa, hazijali mahitaji halisi ya watu? Maono ya maelfu ya Wakristo wa kweli katika mabara yanayositawi yatoa jibu la kutazamisha kwa maswali haya.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Hapo umfungapo ng’ombe, atakula nyasi papo”
[Picha katika ukurasa wa 4]
Maskini ni miongoni mwa wale wajitaabishao katika mabara yanayositawi