Kanisa Lililogawanyika ni Baya Kadiri Gani?
“KAMA ilivyo na familia kubwa ambayo imeshtuliwa, inayoishi katika nyumba nzee iliyo mbovu na ambayo ukuta wayo wa mbele umetoka tu kuanguka kwa ghafula, inaonekana kama kuna ubishi mkali unaoendelea katika karibu kila chumba—huku kikundi cha watoto wa Yesu cha wapiga-tari, kikipigia kelele wagoni wa jinsia-moja wenye fahari wanaovalia suti nyeusi za hariri wa Kanisa Anglikana linalofuata desturi za Kikatoliki.”—The Sunday Times, London, Aprili 11, 1993.
Familia hii ni Kanisa la Uingereza. Ubishi huo ni juu ya suala la kutawaza wanawake kuwa makasisi. Ufafanuzi huo wa waziwazi wa mgawanyiko wafafanua vilevile hali iliyoko katika Jumuiya ya Wakristo yote. Huku maaskofu wa Kanisa Orthodoksi na papa wakishutumu uamuzi wa kuruhusu wanawake kuwa makasisi, ripoti moja yamalizia kwamba matokeo ya ujumla ni kwamba “ile ndoto ya kuungana tena na Jumuiya ya Wakristo yote imedidimia kuliko wakati mwingine wowote.”
Kanisa Limegawanyikaje?
Tusomapo Mathayo 7:21, Yesu Kristo alisema kwamba wengi wangedai kuwa na imani kwake akiwa Bwana na bado washindwe ‘kufanya mapenzi ya Baba yake.’ Gazeti Maclean’s laonelea hivi: “Wasomaji wa Mathayo wanaotafuta wokovu wanaweza kusamehewa kwa kutojua hasa mapenzi ya Mungu ni nini, wakati Wakristo, na makanisa yao, wanapotofautiana sana juu ya suala hilo.” Baada ya mahoji yaliyofanywa miongoni mwa Wakanada, mkataa ulifikiwa kwamba kuna “tofauti kubwa sana za itikadi na za matendo miongoni mwa Wakristo Wakanada—kwa hakika kuna tofauti nyingi zaidi miongoni mwa washiriki wa dhehebu lolote lile kuliko zile tofauti zilizoko kati ya madhehebu yenyewe.”
Kulingana na uchunguzi walo, asilimia 91 ya Wakatoliki wakubali matumizi ya vidhibiti-uzazi hata ingawa kanisa lao lashutumu jambo hilo; asilimia 78 waonelea kwamba wanawake wapaswa kukubaliwa kuwa makasisi; na asilimia 41 wakubali utoaji-mimba “katika hali fulani.” Migawanyiko kati ya madhehebu tofauti-tofauti juu ya “masuala mengi ya kitheolojia,” gazeti Maclean’s lasema, “yakazia ile migawanyiko inayofanya makanisa mashuhuri yavunjike.”
Viwango Maradufu
Kuna viwango maradufu na vilevile viwango vinavyopingana juu ya maadili. Watu fulani wadai kushikamana na kanuni za Biblia, lakini wengine huzidharau. Kwa kielelezo, je, sherehe ya “ndoa” iliyofanywa kwa ajili ya wanawake wawili waliokuwa Wagoni wa jinsia-moja katika Metropolitan Church of Toronto, ilipatana na mapenzi ya Mungu? Ni wazi kwamba washiriki walifikiri hivyo. “Twataka kusherehekea upendo wetu hadharani na vilevile mbele ya Mungu,” wao wakasema.
Mwandikaji mmoja wa gazeti aliuliza ilikuwaje kwamba “askofu-mkuu mmoja wa Katoliki ambaye alikuwa amepelekewa malalamishi mengi, alihamisha makasisi waliokuwa wakifanya ngono na wavulana wa altare kwa [kanisa jingine lenye] wavulana wengine zaidi.” Kasisi Andrew Greeley adokeza kwamba makasisi wapatao 2,000 hadi 4,000 huenda wamewatenda vibaya kingono wavulana wadogo wapatao 100,000, mara nyingi bila hatua yoyote kuchukuliwa.
Kanisa lililogawanyika hutokeza watu waliogawanyika. Katika nchi za Balkan, “Wakristo” wa Serbia na Kroatia wahisi kwamba Kristo yupo pamoja nao katika vita yao “ya haki.” Wengi wao huvaa mifano ya msalaba wakiwa vitani; inaripotiwa kwamba mmoja wao “nyakati zote aliweka mfano wa msalaba kinywani mwake vita ilipochacha zaidi.”
“Kusiwe na Migawanyiko Miongoni Mwenu”
Ni kweli kwamba Biblia huacha mambo fulani yaamuliwe na dhamiri, lakini jambo hilo halipasi kutokeza mgawanyiko. Mtume Paulo alisema waziwazi hivi: “Nyote mseme [na kutenda] kwa upatano, na . . . kusiwe na migawanyiko miongoni mwenu.”—1 Wakorintho 1:10 New World Translation; Waefeso 4:15, 16.
Kuchunguza “Ukristo” kwa unyoofu miaka yapata elfu mbili baada ya mtume Paulo kuandika maneno hayo kwazusha maswali fulani mazito sana. Ni kwa nini “Wakristo” wamegawanyika hivyo? Je! kanisa lililogawanyika hivyo laweza kudumu? Je! Jumuiya ya Wakristo itapata kuungana wakati wowote? Makala ifuatayo itazungumzia maswali hayo.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Maandamano ya makasisi wakipinga utaoji-mimba
[Hisani]
Jalada na juu: Eleftherios/Sipa Press