Haki za Wagonjwa Zaheshimiwa
‘Siwezi kufanya upasuaji huu bila damu. Ikiwa wataka kupasuliwa ni lazima ukubali njia yangu ya matibabu. Au sivyo, utafute daktari mwingine.’
MANENO hayo ya daktari hayakutikisa imani ya Cheng Sae Joo, mmoja wa Mashahidi wa Yehova aishiye Thailand. Akiwa amepimwa na kupatikana kuwa ana meningioma, aina ya uvimbe wa ubongo, Cheng alihitaji sana kupasuliwa. Lakini aliazimia kutii ile amri ya Biblia: “Mjiepushe . . . na damu.”—Matendo 15:28, 29.
Cheng alienda kwenye hospitali mbili nyingine, akipendelea kutibiwa katika nchi yake mwenyewe ikiwezekana. Kwa kumhuzunisha, madaktari huko nako walikataa kufanya upasuaji bila damu. Hatimaye, Cheng alijulishwa na Huduma za Habari za Kihospitali katika Thailand kwa Taasisi ya Neva ya Chuo cha Kitiba cha Wanawake cha Tokyo. Hospitali hiyo ilikuwa tayari imetibu zaidi ya wagonjwa 200 wenye uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia miali gamma, mojawapo njia za karibuni zaidi katika matibabu ya kutumia miali.
Mipango ilifanywa ili Cheng akae na Mashahidi wa Japani waliokuwa wakiishi karibu na hiyo hospitali. Kikundi fulani kilimlaki kwenye uwanja wa ndege, kutia ndani Mashahidi wa Yehova wawili wanaojua lugha ya Kithailand pamoja na mwakilishi wa Huduma za Habari za Kihospitali. Baada ya karibu juma zima la kuchunguzwa, Cheng alilazwa kwenye hospitali hiyo ambapo alitibiwa kwa njia ya miali gamma. Matibabu hayo yalichukua karibu muda wa saa moja tu. Cheng aliondoka hospitali siku iliyofuata, na kurudi Thailand siku iliyofuata tena.
“Sikudhania kamwe kuwa msaada mkubwa kama huo ungeweza kutolewa kupitia mpango huu,” akasema Cheng. “Nilivutiwa sana na upendo ambao ulionyeshwa pamoja na ushirikiano kati ya wengi waliohusika.”
Likiripoti habari hii, gazeti la Japani Mainichi Shimbun lilitoa maelezo haya: “Kufikia sasa, sababu za kidini za kukataa damu zimetajwa. Hata hivyo, kutia damu mishipani kuna madhara mengi kama vile UKIMWI, hatari ya kuambukizwa magonjwa ya virusi kama vile Mchochota wa Ini C, na mizio. Kwa sababu hiyo kuna wagonjwa wasiotaka kutiwa damu mishipani bila kujali itikadi zao za kidini.”
Gazeti hilo liliendelea kueleza: “Wagonjwa wengi waliokataa kutiwa damu mishipani wamelazimika kuenda hospitali nyingine, lakini kuna uhitaji wa kufanya mabadiliko upande wa taasisi za kitiba kuelekea kuheshimu uchaguzi wa mgonjwa. Kibali cha matibabu (mgonjwa kupokea maelezo kamili juu ya mambo yanayohusika na kisha kukubali utibabu) chahitajiwa, na visa vya kutia damu mishipani vyahusika pia. Lazima itambuliwe kwamba hili si suala linalohusisha dini fulani tu.”
Kama Cheng Sae Joo, wengi wanaopendelea kutibiwa bila kutiwa damu mishipani lazima wahamie hospitali nyingine. Hata hivyo, wanathamini sana jitihada za madaktari walio tayari kuheshimu haki za wagonjwa wao.
Huduma za Habari za Kihospitali zilianzishwa na Mashahidi wa Yehova katika matawi ya Watch Tower Society ili kutafuta ushirikiano wa madaktari wanaoheshimu itikadi zao. Ulimwenguni kote, Huduma za Habari za Kihospitali hutafuta kushirikiana pamoja na hospitali mbalimbali, madaktari, wafanyikazi wa afya, wanasheria, na mahakimu.