Kuokolewa Wakati wa Maafa
DUKA la orofa tano katika Seoul, Korea, liliporomoka ghafula, likinasa mamia kadhaa ya watu ndani! Wafanyakazi wa kuokoa walifanya kazi ngumu mchana na usiku ili kuokoa uhai wa watu wengi kadiri ilivyowezekana. Kadiri siku zilivyopita, ndivyo uwezekano wa kupata waokokaji zaidi waliozikwa chini ya rundo kubwa la vifusi ulivyozidi kudidimia.
Kulipokuwa hakuna tena tumaini lolote la kupata waokokaji, ndipo jambo la kushangaza lilipotokea. Kilio dhaifu cha huzuni kilisikika kikitoka chini ya hivyo vifusi. Wakiwa na wasiwasi waokoaji walifukua kwa mikono yao mitupu ili kumwokoa mwanamke mwenye umri wa miaka 19 aliyekuwa amezikwa akiwa hai kwa siku 16 zilizoonekana kuwa ndefu. Shimo la lifti iliyoporomoka lilikuwa limefanyiza uvungu uliotoa himaya juu yake na ulikuwa umemkinga na tani nyingi za saruji iliyokuwa ikianguka. Ijapokuwa alikuwa amepoteza maji mengi sana mwilini na amekatwa, alikuwa ameponyoka kifo!
Siku hizi, karibu kila mwezi kuna ripoti za msiba fulani, iwe ni tetemeko la dunia, dhoruba kali, mlipuko wa volkeno, aksidenti, au njaa kuu. Na hadithi za kustaajabisha za kuokoza na za uokokaji huvutia mamilioni ya watu, ambao husikiliza na kusoma habari. Hata hivyo, onyo la afa fulani linalokuja—moja ambalo ni kubwa zaidi kupita jinginelo katika historia ya kibinadamu—kwa ujumla limepuuzwa. (Mathayo 24:21) Biblia hulifafanua tukio hilo linalokuja katika maneno haya: “Tazama, uovu [“afa,” NW] utatokea toka taifa hata taifa, na tufani kuu itainuliwa toka pande za mwisho wa dunia. Na waliouawa na BWANA siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili; hawataliliwa, wala kukusanywa, wala kuzikwa; watakuwa samadi juu ya uso wa nchi.”—Yeremia 25:32, 33.
Maneno yenye kushtusha! Lakini tofauti na misiba na aksidenti za asili, afa hilo halitakuwa uchinjaji usiochagua. Kwa hakika, kuokolewa—kuokolewa kwako—kwawezekana!
Wakati wa Uharaka
Ili kuelewa jambo hili kabisa, lazima mtu aelewe kwa nini afa hili la tufeni pote litatokea. Kwa kweli, hilo ndilo suluhisho halisi pekee kwa matatizo ya mwanadamu. Ni watu wachache tu leo ambao huhisi wakiwa salama salimini. Licha ya jitihada za sayansi, maradhi yenye kuambukiza yanaendelea kuangamiza wakazi wa dunia. Vita vinavyotokana na tofauti za kidini, kikabila, na kisiasa vimeua maelfu ya watu. Njaa kuu huongezea taabu na kuteseka kwa wanaume, wanawake, na watoto wasio na hatia. Hali ya kudhoofika kiadili huharibu hasa ule msingi wa jamii; hata watoto wamepotoshwa wafanye mabaya.
Kwa usahihi usio na kifani, unabii wa Biblia ulioandikwa miaka zaidi ya 1,900 iliyopita hufafanua hali yetu. Wasema hivi: “Ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.”—2 Timotheo 3:1, Union Version; linganisha Mathayo 24:3-22.
Je, laonekana jambo lenye kupatana na kufikiri kuzuri kwamba Mungu mwenye upendo angekuwa asiyejali hali yetu iliyo mbaya? Biblia yasema hivi: “Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; . . . hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu.” (Isaya 45:18) Ndiyo, badala ya kuruhusu sayari hii yenye kupendeza iangamizwe na wakazi wake wote waishe, Mungu ataingilia kati. Swali ni, Atafanyaje hivyo?
Chagua Uhai!
Biblia yajibu hivi kwenye Zaburi 92:7: “Wasio haki wakichipuka kama majani na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele.” Suluhisho la Mungu kwa matatizo ya dunia ni kuondoshwa kwa uovu wenyewe. Kwa kufurahisha, hili halimaanishi kwamba watu wote wahitaji kuondoshwa. Zaburi 37:34 yatuhakikishia hivi: “Wewe umngoje BWANA, uishike njia yake, naye atakutukuza uirithi nchi, wasio haki watakapoharibiwa utawaona.”
Maneno hayo yaonyesha kwamba kuna uwezekano wa kuokolewa katika afa kubwa kupita yote litakalowapata wanadamu. Mungu ametupatia chaguo. Maneno ambayo kwayo Musa aliwahimiza sana Waisraeli walipokuwa wakijitayarisha kuingia Bara Lililoahidiwa yanatumika kwetu katika njia ileile: “Nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima [“uhai,” NW], ili uwe hai, wewe na uzao wako.” (Kumbukumbu la Torati 30:19) Lakini, mtu ‘huchaguaje uhai’ na kuokolewa? Je, wokovu wa kweli wamaanisha nini kwa kweli?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
COVER: Explosion: Copyright © Gene Blevins/Los Angeles Daily News
[Picha kaitika ukurasa wa 3 zimeandaliwa na]
Yunhap News Agency/Sipa Press