Familia Hatarini!
“NAO wakaishi raha mustarehe.” Siku hizi ndoa chache zaidi na zaidi huwa na mwisho kama huo wa hadithi. Ahadi ya arusi ya kupendana ‘kwa mema na mabaya kwa kadiri waishivyo,’ mara nyingi ni usemi tu. Uwezekano wa kuwa na familia yenye furaha huonekana kuwa mchezo wa kamari ambao hauelekei kufaulu.
Kati ya mwaka wa 1960 na 1990, viwango vya talaka viliongezeka zaidi ya maradufu katika nchi zilizo nyingi za Magharibi ambazo zina viwanda. Katika nchi fulani talaka ziliongezeka mara nne. Kwa mfano, kila mwaka ndoa zipatazo 35,000 hufungwa katika Sweden, na karibu nusu yazo zitavunjika, zikihusisha watoto zaidi ya 45,000. Wenzi wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa hutengana kwa kiwango kikubwa hata zaidi, wakiathiri makumi ya maelfu ya watoto wengi zaidi. Mwelekeo huohuo unadhihirika katika nchi ulimwenguni pote, kama iwezavyo kuonwa katika sanduku kwenye ukurasa wa 5.
Ni kweli kwamba, familia ambazo zimevunjika na kuvunjwa kwa ndoa si mambo mapya katika historia. Sheria za Hammurabi za karne ya 18 K.W.K. zilitia ndani sheria zilizoruhusu talaka katika Babilonia. Hata Sheria ya Kimusa, iliyoanzishwa karne ya 16 K.W.K., iliruhusu talaka katika Israeli. (Kumbukumbu la Torati 24:1) Hata hivyo, vifungo vya familia havijapata kamwe kuwa dhaifu kuliko vilivyo katika karne hii ya 20. Zaidi ya miaka kumi iliyopita, mwandishi fulani wa gazeti la habari aliandika hivi: “Miaka 50 kutoka sasa, huenda hata tusiwe na familia zozote katika maana ya kidesturi. Huenda mahali pa familia hizo pakawa pamechukuliwa na vikundi vya aina tofauti.” Na tangu wakati huo mwelekeo waonekana kuthibitisha wazo lake. Familia imezorota upesi sana hivi kwamba lile swali, “Je itadumu?” lazidi kuhusika.
Kwa sababu gani ni vigumu sana kwa wenzi wengi wa ndoa kushikamana na kudumisha familia yenye muungano? Ni nini siri ya wale ambao wameshikamana kwa kipindi kirefu cha maisha, wakiadhimisha kwa furaha mwaka wa 25 na wa 50 wa ukumbusho wa kila mwaka wa arusi yao? Mwaka wa 1983 ilitukia kuripotiwa kwamba, mwanamume na mwanamke katika iliyokuwa jamhuri ya Sovieti ya Azerbaijan waliadhimisha mwaka wa 100 wa ukumbusho wa kila mwaka wa arusi yao—mume akiwa na umri wa miaka 126 na mke akiwa na umri wa miaka 116.
Tisho Ni Nini?
Katika nchi nyingi baadhi ya misingi ya talaka la kisheria ni uzinzi, ukatili wa kiakili au wa kimwili, kumwacha mwenzi wa ndoa, uraibu wa alkoholi, kutoweza kuzaa, kichaa, kufunga ndoa na mwenzi mwingine ilhali ndoa ya kwanza ingali halali, na uraibu wa dawa za kulevya. Hata hivyo, sababu ya ujumla zaidi ni kwamba mtazamo wa msingi kuelekea maisha ya ndoa na ya familia ya kidesturi umebadilika sana, hasa katika miongo ya juzijuzi. Kustahi mpango wa ndoa ambao kwa muda mrefu ulionwa kuwa mtakatifu kumemomonyoka. Uitwao eti uhuru wa kingono, ukosefu wa adili, mwenendo mlegevu, na mtindo-maisha wenye ubinafsi umetukuzwa na watayarishi wenye pupa wa muziki, sinema, mifululizo ya televisheni ya drama zenye mivutano ya kijamii, na fasihi maarufu. Yote hayo yamekuza utamaduni ambao umechafua akili na mioyo ya vijana na wazee vilevile.
Uchunguzi wa mwaka wa 1996 ulionyesha kwamba asilimia 22 ya Wamarekani husema kwamba mahusiano ya kingono nje ya ndoa yaweza kunufaisha ndoa nyakati nyingine. Toleo la pekee la gazeti la habari lililo kubwa zaidi la Sweden, Aftonbladet, liliwahimiza wanawake wapate talaka kwa kuwa “itaboresha hali.” Wanasaikolojia na wanaanthropolojia wa utamaduni upendwao hata wamekisia kwamba mwanadamu “ameratibiwa” na mageuzi kubadili wenzi kila miaka michache. Yaani, wao wanadokeza kwamba mahusiano ya kingono nje ya ndoa na talaka ni mambo ya asili. Wengine hata hubisha kwamba talaka ya wazazi yaweza kuwafaidi watoto, ikiwatayarisha kukabiliana na talaka lao wenyewe siku fulani!
Vijana wengi hawatamani tena kuishi maisha ya familia ya kidesturi, pamoja na baba, mama, na watoto. “Siwezi kuwazia nikiishi maisha yangu yote na mwenzi yuleyule,” ni mtazamo wa watu walio wengi. “Ndoa ni kama Krismasi, hadithi tu. Mimi siiamini hata kidogo,” akasema mvulana wa Denmark mwenye umri wa miaka 18. “Hisia ni, mbona ujisumbue kuishi na [wanaume] na kuosha soksi zao,” akajulisha wazi Noreen Byrne wa Baraza la Wanawake la Kitaifa katika Ireland. “Wewe wachezee tu . . . Wanawake wengi wanaamua kwamba hawawahitaji wanaume ili waendeleze maisha yao.”
Nyumba za Mzazi Mmoja Zaongezeka
Ulaya kote mtazamo huo umeongoza kwenye kuongezeka upesi kwa mama waseja. Baadhi ya wazazi hao waseja ni matineja wahisio kwamba mimba isiyopangiwa si kosa. Wachache ni wanawake watakao kumlea mtoto wao wakiwa peke yao. Walio wengi ni wanawake waishio pamoja na baba ya mtoto kwa kipindi fulani, bila mipango yoyote ya kufunga ndoa naye. Mwaka uliopita, gazeti Newsweek lilichapisha habari kuu juu ya swali “Je, Ni Kifo cha Ndoa?” Lilitaarifu kwamba asilimia ya watoto wazaliwao nje ya ndoa yaongezeka upesi sana katika Ulaya na kwamba yaonekana hakuna yeyote anayejali. Huenda Sweden ikawa ya kwanza katika orodha, nusu ya watoto wote wakiwa wamezaliwa nje ya ndoa. Katika Denmark na Norway idadi yakaribia nusu ya watoto, na katika Ufaransa na Uingereza, watoto wapatao 1 kati ya 3.
Marekani, familia za wazazi wawili zimepungua sana katika makumi machache ya miaka iliyopita. Ripoti moja yasema hivi: “Mwaka wa 1960, . . . asilimia 9 ya watoto wote waliishi katika nyumba za mzazi mmoja. Kufikia mwaka wa 1990, idadi hiyo iliongezeka kufikia asilimia 25. Leo, asilimia 27.1 ya watoto wote Wamarekani huzaliwa katika nyumba za mzazi mmoja, idadi ambayo yazidi kuongezeka. . . . Tangu mwaka wa 1970, idadi ya familia za mzazi mmoja imeongezeka zaidi ya maradufu. Familia ya kidesturi yatishwa sana leo hivi kwamba yaelekea kutoweka, wasema watafiti fulani.”
Katika nchi ambamo Kanisa Katoliki limepoteza sehemu kubwa ya mamlaka yake ya kiadili, familia za mzazi mmoja zinaongezeka. Nyumba za Kiitalia zipunguazo nusu zafanyizwa na mama, baba, na watoto, napo mahali pa familia ya kidesturi panachukuliwa na wenzi wasio na watoto na nyumba za mzazi mmoja.
Mfumo wa kutoa huduma za jamii bure katika nchi fulani huwatia watu moyo kutooa. Mama waseja ambao hupokea msaada wa umma wangeweza kuupoteza ikiwa wangeoa. Mama waseja katika Denmark hupata riziki zaidi ya kusaidia kutunza watoto, na katika jumuiya fulani, mama wenye umri unaopungua miaka 18 hupata fedha zaidi na hulipiwa kodi yao. Kwa hiyo, fedha zahusishwa. Alf B. Svensson adai kwamba talaka katika Sweden hugharimu walipa-kodi kati ya dola elfu 250 na elfu 375 katika riziki, marupurupu ya nyumba, na msaada wa kijamii.
Makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yaonekana kuwa yafanya machache sana au hayafanyi lolote katika kujaribu kurekebisha mwelekeo huo wenye kuangamiza kabisa miongoni mwa familia. Mapasta na makasisi wengi wanashindana mwereka na matatizo ya familia zao wenyewe, hivyo wakihisi kwamba hawawezi kuwasaidia wengine. Baadhi yao hata waonekana kuwa wanatetea talaka. Gazeti Aftonbladet la Aprili 15, 1996, liliripoti kwamba pasta Steven Allen kutoka Bradford, Uingereza, alitunga sherehe ya pekee ya talaka, ambayo adokeza kwamba yapaswa kuwa ibada halali ya kutaliki katika makanisa yote ya Uingereza. “Ni ibada ya kuponya ili kuwasaidia watu wakubali na kujirekebisha ili wafaane na yaliyowapata. Huwasaidia watambue kwamba Mungu bado awapenda na awafungua watoke katika umizo hilo.”
Kwa hiyo familia yaelekea wapi? Je, kuna tumaini la kudumu kwake? Je, familia mojamoja zaweza kudumisha muungano wake chini ya tisho kubwa hivyo? Tafadhali chunguza makala inayofuata.
[Chati katika ukurasa wa 5]
NDOA ZA KILA MWAKA ZIKILINGANISHWA NA TALAKA KATIKA NCHI FULANI
NCHI MWAKA NDOA TALAKA
Australia 1993 113,255 48,324
Denmark 1993 31,507 12,991
Estonia 1993 7,745 5,757
Jamhuri ya Cheki 1993 66,033 30,227
Japani 1993 792,658 188,297
Kanada 1992 164,573 77,031
Kuba 1992 191,837 63,432
Maldives 1991 4,065 2,659
Marekani 1993 2,334,000 1,187,000
Muungano wa Urusi 1993 1,106,723 663,282
Norway 1993 19,464 10,943
Puerto Riko 1992 34,222 14,227
Sweden 1993 34,005 21,673
Ufaransa 1991 280,175 108,086
Uingereza 1992 356,013 174,717
Ujerumani 1993 442,605 156,425
(Kwa kutegemea kitabu 1994 Demographic Yearbook, Umoja wa Mataifa, New York 1996)