Je! Wewe Uko Tayari Kukabili Hali Ngumu ya Kitiba Yenye Kujaribu Imani?
Weka habari hii mahali ambapo unaweza kuipata ikihitajiwa
1 Hakuna mtu yeyote anayefikiria sana uwezekano wa kuwa hospitalini leo au kesho. Hata hivyo, ‘wakati na tukio lisilotazamiwa hutupata sisi sote.’ (Mhu. 9:11, NW) Hata kama wewe hukubali utibabu wa hospitalini kuwa namna unayopendelea ya utunzaji wa afya, wewe utafanya nini ujihami mwenyewe usitiwe damu mishipani usiyotaka aksidenti ikitokea na ikuache bila fahamu nawe unakimbizwa hospitalini? Ndiyo, aksidenti au hali ya ghafula ya afya yenye kuzorota yaweza kukuleta bila kutazamiwa katika hali ya kukabiliana uso kwa uso na jaribu la imani yako.
2 Ukijipata hospitalini kwa sababu yoyote, utafanya nini ili udumishe ukamilifu wako ikiwa mtu fulani huko akuambia kwamba utakufa usipotiwa damu mishipani? Je! utakubali dai hilo kuwa lawakilisha kikweli hali yako? Je! wewe unasadikishwa kwamba hutaki damu? Je! wewe uko tayari kukabili jaribu hili la imani yako na ‘ujiepushe na damu’?—Mdo. 15:28, 29.
3 Kukinza kwa mafanikio kutiwa damu mishipani kusikotakiwa, kunakochafua kiroho kwaanza kwa kuwa na usadikisho imara. Usadikisho huo lazima utegemee uelewevu ulio wazi wa yale yanayosemwa na Biblia juu ya damu. La sivyo, kwa sababu ya hisia-moyo za pindi hiyo, waweza kwa urahisi kuogopeshwa na mtu fulani anayedai kwamba ajua mengi zaidi kuliko wewe juu ya hali hiyo. Je! wewe ungeweza kuongozwa vibaya ufikiri kwamba huenda madaktari wakajua zaidi juu ya damu kuliko anavyojua Mungu? Hakika, katika hali hizo utataka ‘kuazimia kwa imara kufanya linalofaa’ machoni pa Yehova, hata waseme nini wale walio binadamu tu. (Kum. 12:23-25) Lakini je! ni lazima ukabili tatizo hilo ukiwa peke yako tu?—Mhu. 4:9-12.
UTUMISHI WA HABARI ZA HOSPITALI NA HALMASHAURI ZA KUPATANISHA NA HOSPITALI
4 Ili kusaidia wale wanaotaka msaada wanapokabiliwa na tatizo la kutiwa damu mishipani, Sosaiti imeanzisha Utumishi wa Habari za Hospitali katika Brooklyn na katika maeneo mengine imeanzisha Halmashauri za Kupatanisha na Hospitali. Washiriki wa Halmashauri hizi ni wazee waliozoezwa kipekee kwa ajili ya kazi hii.
5 Utumishi wa Habari za Hospitali una uwezo wa kufanya utafiti katika majarida ya kitiba zaidi ya 3,600 ulimwenguni pote ili kupata habari juu ya upatikanaji na mafanikio ya namna nyingi za upasuaji na utibabu usiotumia damu. Kisha unazigawia Halmashauri za Kupatanisha na Hospitali, vitovu vya utunzaji wa afya, na baadhi ya madaktari habari hizo juu ya maendeleo haya ya kitiba. (Nyakati fulani Utumishi wa Habari za Hospitali hupeleka makala za kitiba zinazoonyesha jambo linaloweza kufanywa bila kutumia damu na umefanikiwa kumaliza pambano lililokuwa likiendelea hospitalini.) Huendelea kujulisha halmashauri juu ya maamuzi yenye kupendelea ambayo yatasaidia mahakimu wafikirie kesi zetu kwa muono-ndani ulioongezewa maarifa. Pia huweka maandishi kuhusu madaktari wapasuaji wenye ushirikiano ili halmashauri ziwe na faili zenye habari za karibuni zaidi wazitumie yanapozuka matatizo ya kutiwa damu mishipani.
6 Utumishi wa Habari za Hospitali husimamia pia mazoezi na kazi ya Halmashauri za Kupatanisha na Hospitali. Katika maeneo walimo, Halmashauri za Kupatanisha na Hospitali huwatolea kwa ukawaida wafanyakazi wa hospitali habari zenye kuarifu ili kufanyia maendeleo mahusiano pamoja nao. Pia wanawahoji wafanyakazi hao ili kupata madaktari zaidi ambao watatutibu bila kutumia damu. Ingawa kwa wakati huu sisi hatuna Halmashauri za Kupatanisha na Hospitali katika eneo lililo chini ya tawi letu mwingi wa utumishi, utunzaji, na hangaikio na kupendezwa kwa halmashauri kama hizo hushughulikiwa na baraza za wazee wa kundi lenu. Wazee hao wako tayari kukusaidia, lakini kuna hatua muhimu sana ambazo lazima utangulie kuzichukua ili kuweka msingi waweze kufanya hivyo kwa njia yenye mafanikio zaidi.
HATUA MUHIMU SANA ZA KIMBELE —JE! WEWE UMEKWISHA KUZICHUKUA?
7 Kwanza, hakikisha kwamba wote katika familia wana hati ya kitiba ya mwelekezo ikiwa imejazwa kikamili—imeandikwa tarehe, imetiwa sahihi, na kutiwa sahihi na mashahidi. Baadhi ya akina ndugu waliowasili hospitalini wakiwa na hati isiyo na tarehe na/au isiyotiwa sahihi na mashahidi, uhalali wayo ulitiliwa shaka. Na je! watoto wetu wote wasiobatizwa wana hati zao za utambulisho zikiwa zimejazwa? Ikiwa sivyo, katika hali ya dharura inayohusu mtoto wako, wafanyakazi wa hospitali watajuaje msimamo wako kuhusu damu na yule watakayemwita?
8 Kisha hakikisha kwamba wote wanakuwa na hati zao NYAKATI ZOTE. Hakikisha jambo hilo pamoja na watoto wako kabla ya kwenda shule kila siku, ndiyo, hata kabla ya kwenda kwenye uwanja wa michezo au maeneo ya kufanyiwa tafrija. Sisi sote twapaswa kuhakikisha kwamba tuna hati hizi kazini, tunapokuwa likizoni, au kwenye mkusanyiko wa Kikristo. Usikose kuwa nazo kamwe!
9 Fikiria jambo ambalo lingekupata ukiwasili katika chumba cha visa vya dharura hospitalini ukiwa katika hali yenye hatari, ukiwa umepoteza fahamu na/au ukiwa huwezi kujisemea. Ikiwa huna hati yako, na hakuna mtu wa ukoo wako au mzee katika hospitali wa kusema kwa niaba yako, na shauri linakatwa kwamba ‘wahitaji damu,’ yaelekea utatiwa damu mishipani. Kwa kusikitisha, jambo hilo limewapata wengine. Lakini tunapokuwa na hati yetu, inasema kwa niaba yetu, ikieleza mapenzi yetu.
10 Hiyo ndiyo sababu hati ya kitiba ni bora kuliko bangili au mkufu wa kitiba. Hivyo vya pili havielezi sababu yetu yenye msingi wa Biblia ya msimamo wetu na havina sahihi inayothibitisha jambo lililotaarifiwa. Uamuzi wa mahakama ya Kanada ilisema hivi kuhusu hati ya dada mmoja: “[Mgonjwa huyu] amechagua kwa njia pekee inayowezekana kujulisha madaktari na wengine wenye kuandaa utunzaji wa kitiba, ikiwa anapoteza fahamu zake au kwa vyovyote awe hawezi kuwasilisha mapenzi yake, kwamba yeye hakubali kutiwa damu mishipani.” Kwa hiyo usikose kamwe kuwa nayo!
11 Kwa kuwa mwelekezo wetu wa kitiba umekusudiwa sana-sana kushughulikia hali za dharura, basi katika upasuaji wa kujichagulia ungekuwa mwenye hekima kuandika mwelekezo wa kimbele wako binafsi, ulio kamili zaidi (ukitegemea mwelekezo wetu wa kitiba) ili uweze kutia ndani mambo hususa, kama vile namna ya upasuaji na ikiwezekana majina ya madaktari na hospitali. Katika nchi nyingi hii ni haki aliyo nayo kila mtu ya kuhakikisha kwamba anapata utibabu wa uchaguzi wake. Hata ingawa wewe na daktari wako hamtazamii matatizo magumu, fafanua kwamba mwelekezo huu wapaswa kufuatwa ikitokea hali isiyotazamiwa.—Mit. 22:3.
12 Hatua ya pili muhimu ni kuongea na wafanyakazi wa kitiba ambao utalazimika kushughulika nao katika ama utibabu wa kujichagulia au wa dharura. Hasa wapaswa kuongea na nani?
ONGEA NA WAFANYAKAZI WA TIBA
13 KIKOA CHA TIBA: Huu ni wakati ambapo kuhofu binadamu hakupasi kushinda. (Mit. 29:25) Ukionekana kutokuwa na hakika, mtu fulani huenda akakata shauri wewe si mnyofu. Upasuaji unapohitajiwa, wa kujichagulia au wa dharura, wewe au mshiriki wa familia aliye wa karibu zaidi lazima aulize kiongozi wa kikoa cha upasuaji akiwa ameazimia kabisa maswali yenye kuuliza mambo hususa. Swali moja muhimu ni, Je! kikoa hicho kitaheshimu mapenzi ya mgonjwa na katika hali zote kimtibu bila damu? Bila uhakikishio huo hungekuwa na himaya kamili.
14 Taarifu waziwazi na kwa usadikisho wenye kuheshimika mapenzi yako ni nini. Elewesha waziwazi kwamba wewe unataka utibabu mwingine wa tatizo lako badala ya damu. Kwa utulivu na kwa usadikisho zungumza mwelekezo wako binafsi wa kitiba wa kimbele na pia fomu ya hospitali inayoiondolea kupasishwa daraka. Ikiwa hospitali haina fomu hiyo waweza kutumia ikiwa kama mwongozo, ile fomu iliyo kwenye ukurasa 29, fungu la 2 wa kijitabu Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu. Ikiwa daktari mpasuaji hana nia ya kufanya kazi kupatana na mapenzi yako uliza msimamizi wa hospitali, hasa katika shirika au kifaa cha watu binafsi, akutafutie daktari mwingine. Katika maeneo mengi hiyo ni sehemu ya kazi yake.
15 MTAALAMU WA DAWA NUSUKAPUKI: Kati ya wote walio katika kikoa cha tiba ambaye utataka kuongea naye kabla ya upasuaji, LAZIMA USIKOSE KUONGEA NA DAKTARI HUYU. Akiwa amepewa daraka la kukuweka hai wakati madaktari wapasuaji wanapopasua, mtaalamu wa dawa nusukaputi ndiye hufanya maamuzi kuhusu mambo kama vile utumizi wa damu. Hivyo wewe huna himaya kamili kwa kuongea na daktari mpasuaji tu. Kwa sababu hiyo, lazima uongee na umsadikishe mtaalamu wa dawa nusukaputi kwa habari ya msimamo wako, ili kuamua kama utastahiwa au la.—Linganisha Luka 18:3-5.
16 Yaonekana, zoea la kawaida ni mtaalamu wa dawa nusukaputi kutembelea mgonjwa kifupi usiku ukiwa umeendelea kidogo kabla ya upasuaji—inakuwa ni kuchelewa mno ikiwa yeye apinga msimamo wako juu ya damu. Ukiwa pamoja na daktari wako wa kibinafsi, sisitiza kwamba daktari mpasuaji atangulie kuchagua mtaalamu wa dawa nusukaputi mwenye ushirikiano ambaye ungeweza kuongea naye mapema vya kutosha kabla ya upasuaji wa kujichagulia. Ndipo kutakuwa na wakati wa kutafuta mwingine ikiwa yule wa kwanza hana nia ya kufuata mapenzi yako. Hasa katika mashirika ya kibinafsi hakika una haki ya kuridhika na mtaalamu wa dawa nusukaputi kwa ajili ya upasuaji wako.
17 Kwa hao wote, ni lazima uwaeleweshe msimamo wako usiojadilika: HAKUNA KUTUMIA DAMU. Omba utibabu mwingine badala ya damu kwa ugonjwa wako. Watajie matibabu mengine badala ya damu yanayojulikana kwa hali yako. Ikiwa kikoa cha tiba chahisi kwamba hayo hayafai kwa ugonjwa wako, waulize wafanye utafiti kuhusu uwezekano mwingine katika fasihi ya kitiba. Labda waweza kuwapa habari fulani wakitaka kwa usaidizi wa wazee. Wewe au wazee mwaweza sikuzote kuwasiliana na ofisi ya tawi inapowezekana.
KUTUMIA HAKI ZAKO
18 Chunguza kwa uangalifu ile fomu ya kuondolea hospitali kupasishwa daraka na ile fomu ya idhini ambayo hospitali hukuomba utie sahihi wakati wa kulazwa hospitalini. Nyakati nyingine mara wakiisha kutaarifu kwamba watastahi mapenzi yako, fungu linalofuata litajulisha wazi kwamba mwenye kutia sahihi anakubali kwamba hospitali yaweza kutumia utibabu “wenye kuokoa uhai” wanapokabiliwa na matatizo. Hiyo ingeweza kutia ndani damu. Wewe una haki ya kubadili taarifa zozote kama hizo ili damu isitiwemo au waweza kuzifuta kabisa. Wauguzi huenda wakakwambia kwamba huwezi kufanya hivyo, lakini unaweza! Waeleweshe kwamba fomu kama hizo ni mkataba uliofanya nao na huwezi kutia sahihi mkataba ambao hukubaliani nao. Yeyote akijaribu kukulazimisha utie sahihi dhidi ya mapenzi yako, mwambie ungetaka kusema na msimamizi na/au akiwamo mwakilishi wa wagonjwa wa kitovu hicho cha utunzaji wa afya. Je! waweza kufanya mambo kama hayo? Ndiyo, waweza kwa kuwa una haki fulani kama mgonjwa.
19 Haki moja kama hiyo yaitwa idhini baada ya kuarifiwa, ambayo humaanisha kwamba hakuna utibabu wa aina yoyote unaoweza kutumiwa bila ruhusa yako. Hata unaweza kukataa utibabu wote ukitaka. Kwa kawaida, idhini yako ya kupata utibabu hufuata uelewesho ulio wazi wa yale kikoa cha tiba kinachokusudia kufanya, kutia na hatari zote zile. Halafu, lazima wakwambie matibabu mengine yaliyo badala ya damu yanayopatikana. Ndipo, ukiisha kuarifiwa, wachagua utibabu unaotaka.
20 Ili uhakikishe unatoa idhini ya kitu gani, ni LAZIMA uulize maswali mazuri juu ya chochote ambacho huelewi, hasa wakati maneno makubwa au semi za kitiba zinapotumiwa na wafanyakazi wa hospitali. Kwa kielelezo, ikiwa daktari asema kwamba angependa kutumia “plazima,” ungeweza kuamua bila kujua kwamba anarejezea ‘vitanua kiasi cha damu vya plazima,’ lakini sivyo. Kabla ya kukubali, uliza hivi: “Je! hiyo ni sehemu ya damu?” Kuhusu utaratibu wowote wake wakufuatwa, uliza: “Je! utibabu huo unahusu utumizi wa vitu vyovyote vilivyofanyizwa kwa damu?” Akieleza kidude fulani ambacho angetaka kutumia, muulize: “Je! damu yangu inawekwa mahali wakati wowote katika pindi ya kutumia kidude hicho?”
21 Lakini ufanye nini ikiwa umefanya yote yaliyo juu na bado hakuna ushirikiano au hata kunakuwa na ukinzani fulani kwa msimamo wako? Usisite kuomba msaada. Wengine wamengojea mpaka inapokuwa ni kuchelewa mno kupata msaada na kuhatarisha maisha yao yenyewe.
MSAADA WENYE THAMANI WAKATI WA UHITAJI
22 Angalia njia zifuatazo za kupata msaada unaohitajiwa: (1) Mara tu wewe au mmoja wa wapendwa wako anapokabili upasuaji wa kujichagulia au wa dharura ambapo kunakuwa na pambano kwa sababu hospitali inataka kutumia damu; au (2) ikiwa hali yako ya kitiba au ya mmoja wa wapendwa wako inazorota kwa njia yenye hatari; au (3) ikiwa kwa habari ya mtoto (au mtu mzima), daktari, mwuguzi, au msimamizi asema watatumia damu:
23 WASILIANA NA WAZEE WA KUNDI LENU ikiwa hujafanya hivyo. (Kweli kweli, kwa sababu ya msimamo wetu kuhusu damu, ni mwendo wa hekima kujulisha wazee wetu wakati wowote inapokuwa lazima twende kwenye kifaa chochote cha utunzaji wa afya.) Wazee watakusaidia kuamua hatua utakayochukua baada ya hapo.—Isa. 32:1, 2.
24 Wazee waweza kukusaidia uwasiliane na madaktari wenye ushirikiano katika eneo lenu ambao wana nia ya kukusaidia. Ikiwa hakuna wanaopatikana kwenu, wazee waweza kuchunguza maeneo ya karibu. Na hilo lisipofanikiwa wanaweza kuwasiliana na ofisi ya tawi inapowezekana.
25 Pia wazee wana nia ya kukusaidia wewe au mtu wa ukoo wako aongee na daktari au msimamizi, lakini lazima uombe msaada huo. Bila shaka, ndugu hawa hawawezi kukufanyia maamuzi, lakini mara nyingi wanaweza kukusaidia katika kufikiria maoni ya Sosaiti juu ya mambo ya kukuweka chonjo uone machaguzi yako kitiba na kisheria.
26 Ikiwa kikoa cha tiba kingali hakielekei kushirikiana nawe, ongea na msimamizi wa hospitali uone kama kuna wengine miongoni mwa wafanyakazi watakaostahi mapenzi yako. Ikiwa hilo haliwezekani basi huenda ukataka kutafuta utibabu mahali pengine. Kumbuka umaana wa kujaribu kupata huduma ya kitiba unayohitaji kabla hali yako haijazorota na kuwa hatari. Usikawie mno!
27 Ingawa hatuwezi kumwambia yeyote apate bima ya afya, au atumie madaktari na mashirika ya kibinafsi, ni lazima sisi tukujulishe kwamba wafanyakazi wa vifaa vya afya vya watu binafsi kwa kawaida huwa wenye ushirikiano zaidi inapohusu kustahi msimamo wetu usiojadilika.
MASWALI YA KUJIHADHARI NAYO YANAYOKUSUDIWA KUKUNASA UKUBALI JAMBO HATARI KWAKO
28 Yakupasa kujua kwamba kuna baadhi ya maswali ambayo madaktari na wengine huuliza ambayo si nyakati zote yanapoulizwa kwa kusudio jema. Moja linaloulizwa mara nyingi sana na madaktari na wengine ni:
• “Je! ingekuwa afadhali kwako kufa (au kuacha mtoto wako afe) kuliko kukubali ‘kutiwa damu mishipani kunakookoa uhai’?”
29 Ukisema ndiyo, hiyo ingekuwa kweli katika maana ya kidini. Lakini mara nyingi swali hilo linaeleweka kimakosa na nyakati nyingine hata hutokeza maamuzi mabaya. Lazima ukumbuke kwamba wewe humo katika huduma katika hali hii. Badala ya hivyo, wewe unaongea juu ya utibabu unaohitajiwa. Kwa sababu hiyo, lazima ujipatanishe na wasikilizaji wako, kitiba au kisheria.—Zab. 39:1; Kol. 4:5, 6.
30 Kwa daktari, hakimu, au msimamizi wa hospitali, “ndiyo” yaweza kumaanisha wataka kuwa mfia-imani au wataka kudhabihu mtoto wako kwa ajili ya imani yako. Kuwaambia juu ya imani yako imara katika ufufuo katika hali hii kwa kawaida hakutasaidia. Watakubandika jina mfuata dini bila akili, asiyeweza kufanya maamuzi ya kiakili wakati uhai umo hatarini. Katika habari ya mtoto, watakuona kuwa mzazi asiyejali ambaye hukataa ule unaoitwa eti utibabu “wenye kuokoa uhai.”
31 Lakina wewe HUUKATAI utibabu wenyewe. Unatofautiana tu na daktari kwa habari ya ni AINA GANI ya utibabu. Msimamo huu mara nyingi utabadili maoni yote kwao na kwako. Licha ya hilo ni jambo lenye kupotoa maana kwa upande wao kufanya ionekane kama kwamba damu ni salamu na ndiyo utibabu PEKEE “wenye kuokoa uhai.” Hivyo lazima uwaeleweshe jambo hilo wazi sana. Waweza kufanyaje hivyo? Waweza kujibu hivi:
• “Mimi sitaki (mtoto wangu) kufa. Kama ningalitaka (mtoto wangu) kufa, ningalikaa nyumbani. Lakini nilikuja hapa kupata utibabu ili (mtoto wangu) kuishi. Ninalotaka mimi ni utibabu mwingine wa ugonjwa (wa mtoto) wangu badala ya damu. Kuna matibabu mengine yanayopatikana.”
32 Maswali mengine kadhaa yanayoulizwa na daktari na wengine ni:
• “Itakuwaje kwako ikiwa unatiwa damu mishipani kwa nguvu? Je! utaonwa kuwa na daraka?”
• “Je! kukubali au kutiwa damu mishipani kwa nguvu kutasababisha uondolewe katika dini yako au unyimwe uhai wa milele? Utaonwaje na kundi lako?”
33 Dada mmoja alimjibu hakimu kwamba kwa habari kama hiyo hangeonwa kuwa na daraka kwa yale aliyoamua. Ingawa ni kweli kwa namna moja ya maoni, hakimu huyo aliliona kumaanisha kwamba kwa kuwa dada hangeonwa kuwa na daraka, basi yeye angejitwalia daraka kwa niaba yake. Aliamuru atiwe damu.
34 Lazima uelewe kwamba katika kuuliza maswali haya, wengine wanatafuta njia ya kuondolea mbali katao lako la kukubali damu. Usiwape njia hiyo bila kukusudia! Hivyo tungeepukaje huko kueleweka vibaya? Ungeweza kujibu hivi:
• “Ikiwa damu ingetiwa ndani yangu kwa nguvu kwa njia yoyote, ingekuwa sawa kwangu na kulalwa kinguvu. Ningepatwa na matokeo mabaya ya kihisia-moyo na ya kiroho katika maisha yangu yote kwa shambulio hilo nisikotaka. Ningekinza kwa nguvu zangu zote uhalifu kama huo juu ya mwili wangu bila idhini yangu.”
35 Wazo lenye nguvu, na lililoonyeshwa wazi lazima litolewe kwamba damu iliyotiwa mishipani kwa nguvu katika mwili wetu ni uhalifu wenye kuchukiza uliofanywa dhidi ya miili yetu. Si jambo la vivi hivi. Kwa hiyo simama imara. Elewesha wazi wewe wataka utibabu mwingine badala ya damu.
WEWE UTAFANYA NINI ILI UWE TAYARI?
36 Tumepitia mambo fulani ambayo wewe wahitaji kufanya ili ujihami mwenyewe na familia yako na kutiwa damu mishipani kusikotakwa. (Baadaye, twatumaini kuandaa habari zaidi juu ya kushughulikia matatizo yanayozuka wakati vitoto vichanga na watoto wanapotishwa kutiwa damu mishipani.) Pia tumeona yale ambayo Sosaiti imefanya kwa upendo ili kuandaa msaada wakati wa uhitaji. Yakupasa kufanya nini na habari hii ili uhakikishe kwamba uko tayari kukabiliana na hali ngumu ya kitiba yenye kujaribu imani?
Kwanza: Iweni na mazungumzo ya familia mfanye mazoezi mambo haya na kujitahidi kujua yale mtakayosema na kufanya, hasa katika hali ya dharura.
Kisha: Hakikisheni kwamba mna hati zote mnazohitaji.
Halafu: Lifanyeni kuwa jambo la sala nzito kwa Yehova ili kuwategemeza katika uamuzi wenu imara ‘kuendelea kujiepusha na damu.’ Kutii sheria yake juu ya damu hutuhakikishia kibali chake cha uhai usio na mwisho.—Mdo. 15:29; Mit. 27:11, 12.