Sanduku la Swali
◼ Tunapaswa kuzingatia nini ikiwa tunataka baadhi ya mali au mali zetu zote zimilikiwe na tengenezo la Yehova tunapokufa?
Wanadamu wanapokufa, hawana mamlaka tena juu ya mali zao. (Mhu. 9:5, 6) Kwa hiyo, wengi huandika hati ya kisheria mapema ambayo hueleza mambo ambayo wangetaka yafuatwe kuhusu jinsi ya kugawa mali zao. (2 Fal. 20:1) Kwa ujumla, hati hiyo ya kisheria huonyesha pia mtu atakaye tekeleza mambo yaliyoandikwa. Katika nchi nyingi, serikali huamua jinsi ya kugawa mali za mtu aliyekufa ikiwa hakuandaa hati ya kisheria. Hivyo, iwapo tungependa mali zetu zitumiwe kwa njia hususa, kama vile tengenezo la Yehova limiliki baadhi ya mali hizo au mali zote, ni muhimu tuandae hati ya kisheria ambayo itaonyesha jambo hilo na tuchague kwa makini mtu atakayetekeleza mambo yaliyoandikwa katika hati hiyo.
Mtu atakayetekeleza maagizo yaliyo katika hati hiyo ya kisheria ana wajibu mzito. Ikitegemea kiwango cha mali au pesa, kukusanya na kugawa mali hizo kunaweza kuhusisha mambo mengi na wakati mwingi. Kwa kuongezea, mara nyingi mamlaka za serikali huwa na miongozo ambayo ni lazima ifuatwe. Si kila mtu ambaye ni mshiriki wa kutaniko anaweza kutekeleza maagizo yaliyo katika hati hiyo ya kisheria kwa njia nzuri. Mtu ambaye tutamchagua anapaswa kuwa mwenye uwezo, mwaminifu, na aliye tayari kufuata maagizo yetu.—Ona makala “Hekima na Manufaa za Kupanga Urithi na Mali,” katika Amkeni! ya Desemba 8, 1998.
Iwapo Utaombwa Kuwa Mtu Atakayetekeleza Mambo Yaliyoandikwa Kwenye Hati ya Kisheria: Ikiwa mtu fulani atakuomba umtimizie jukumu hilo la kisheria baada ya kifo chake, kwanza hesabu gharama na usali ili kuona kama kweli utaweza kutimiza wajibu huo. (Luka 14:28-32) Baada ya kifo cha mtu huyo, utahitaji kuwafahamisha wote watakaopokea urithi au mali hizo. Mara tu upatapo mamlaka ya kufanya hivyo, wajibu wako utakuwa kugawa mali hizo kulingana na sheria na kufuata kabisa maagizo katika hati hiyo. Mtu mwenye jukumu la kutekeleza maagizo yaliyoandikwa katika hati hiyo anapaswa kujua kwamba iwe mali ni nyingi au chache, hapaswi kupuuza maagizo hayo. Zawadi zozote zinazotolewa kwa shirika la kisheria linalotumiwa na Mashahidi wa Yehova ni michango iliyowekwa wakfu ambayo ni mali ya tengenezo la Yehova.—Luka 16:10; 21:1-4.