Kuutazama Ulimwengu
MWAKA MBAYA KWA DINI
Kulingana na ripoti moja iliyo katika Los Angeles Times, watu katika United States wanapoteza staha yao kwa dini iliyopangwa kitengenezo. Uchunguzi mbalimbali uliofanywa 1988 ili kutafuta maoni ya watu ulionyesha kwamba, kwa kulinganishwa na 1986, Waamerika zaidi walikuwa wamepoteza imani yao katika maadili ya makasisi na wakahisi kwamba dini ilikuwa ikipoteza uvutano juu ya jamii ya watu. Ripoti hiyo iliarifu kwamba mzinduko huo ulionekana wazi sana miongoni mwa vikundi vya wachache na Wakristo Waevanjeliko, au “waliozaliwa tena,” ikitaja kwamba visababishi vyaonekana kuwa ni zile kashifa zilizohusu wahubiri wa televisheni kama vile Jimmy Swaggart na Jim Bakker.
HEWA MBAYA
Kulingana na The Star ya Johannesburg, salfa (kiberiti) nyingi zaidi hunyesha kutoka angani juu ya eneo la Afrika Kusini la Transvaal ya mashariki kuliko mahali pengine popote katika ulimwengu wa Magharibi. Anguko hilo la salfa hutoka hasa kwenye vituo vya kufanyiza nguvu za umeme kwa kutumia jenereta zenye kuendeshwa na makaa-mawe, na lingeweza kuongezeka lifikie tani 149 kwa kilometa ya mraba kila mwaka. Hiyo ingekuwa ni hali mbaya mara nane kuliko ile iliyo katika Ujeremani ya Magharibi, ambako tayari anguko la jinsi hiyo limeleta “hasara isiyoondoleka kwenye misitu, mazao na majengo.” Salfa ni kitu kikubwa ambacho huwamo katika mvua ya asidi. Uchunguzi mmoja ulipata kwamba wingi wa asidi ya mvua hiyo iliyo katika Transvaal ya mashariki wakaribia kuwa kama ule ulio katika siki (vinegari). Kwa kuwa vigezo vya kubadilika-badilika kwa hali ya hewa katika Afrika Kusini huelekea kunasa uchafuzi karibu na dunia, watu wengi wahangaika juu ya matisho ya kiafya ambayo yahusika. Wazazi wahofu kuhusu watoto wao. Saturday Star yaarifu kwamba ukungu huo wa moshi unasababisha “moja ya hesabu za juu zaidi za malalamiko yaliyomo ulimwenguni kuhusu masikio, pua na koo.”
KUTENDWA VIBAYA KWA WANYAMA
NA KUTENDWA VIBAYA KWA WATOTO
Uchunguzi mmoja wa hivi majuzi ulionyesha kwamba kutendwa vibaya kwa wanyama katika nyumba fulani huenda kukawa ishara ya kwamba hali ya kutenda watoto vibaya inaendelea chini ya paa iyo hiyo, laripoti gazeti Parents la United States. Kati ya jamaa 57 zenye kusumbuliwa na hali ya kuwatenda watoto vibaya, asilimia 88 zilitenda wanyama vibaya pia. Kwa kawaida mwenye kutenda mnyama vibaya alikuwa mzazi, lakini huenda pia watoto wenye kutendwa vibaya wakafungulia kasirani yao juu ya wanyama. Tengenezo lililoendesha uchunguzi huo lilihimiza wazazi, walimu, na wengine wawachukue watoto kwa uzito wawaelezapo kwamba wanyama hutendwa vibaya katika nyumba zao. Makala hiyo ilidokeza hivi: “Fundisheni watoto kwamba ni kosa kukitenda vibaya kitu cha aina yoyote.”
‘KALIPWA ILI
KUBAKI KIMYA’
Uchunguzi mmoja uliofanywa na Shirika la Kitiba la Australia (AMA) kuhusu magazeti ya wanawake, yenye kutangazwa kwa chapa kwa wastani wa kipindi cha miaka mitano, ulifunua kwamba magazeti yenye matangazo ya sigareti yalionekana kuwa huchunguza kwa uangalifu habari zenye kutangaza wazi madhara ya kuvuta sigareti. Kati ya magazeti yaliyochunguzwa, kulikuwako hesabu mara kumi ya makala zenye kuhusu kupoteza uzito wa mwili na malaji yafaayo kuliko hesabu iliyokuwapo kuhusu kuvuta sigareti. Katibu mkuu wa hilo Shirika la Kitiba la Australia alishtaki magazeti hayo juu ya kupuuza kimakusudi hatari za kuvuta sigareti na akafanya upya wito wa kupiga marufuku utangazaji wa tumbako. “Magazeti hayo yanalipwa ili yabaki kimya nayo yanabaki kimya,” akasema. “Hicho ni kitendo cha aibu kubwa ya kutojali madaraka.”
MASHINE KUBWA YA KUTOBOA ARDHI KWA AJILI YA WARUSI
Mashine kubwa sana ya kutoboa mahandaki imeungamanishwa katika Richmond, Kanada, ili iwe ya mradi wa kutokeza nguvu za umeme kwa kutumia maji katika Urusi, yaripoti The Vancouver Sun. Mashine kubwa hiyo ya kutoboa ina uzito wa tani 660 na urefu wa meta 28. Vikataji vyayo 59 vya kiduara, vilivyofanyizwa kwa mchanganyo wa chuma-cha-pua, vyaweza kukata mwamba mgumu kwa kadiri yenye kufikia sentimeta 10 kwa dakika, vikiwa vimewekwa tayari katika kichwa cha ukataji chenye mduara wa meta 8.5. Zile mota kumi za kuchimba kwa kutumia nguvu za umeme hufanyiza jumla ya nguvu-farasi 2,800. Mashine hiyo itatumiwa kutoboa mahandaki mawili ya kilometa 5.4 kwa ajili ya mradi wa Irganaisk wa kufanyiza nguvu za umeme kutokana na maji, katika Milima ya Caucasus. Mashine sita kama hizo zinachimba mahandaki kwa sasa chini ya Mfereji wa Uingereza.—Ona Amkeni! ya Januari 8, 1990.
UCHAWI KUHUSIANA NA MPIRA WA MIGUU
Klabu cha Michezo cha Bahia, kilichokuwa mshindi wa Kombe la Union katika Brazili mwaka 1988, hutumia “silaha” gani ya siri ili kuwa na uhakikisho kamili wa kushinda? Ni “mafumbo ya kichawi,” laripoti gazeti Veja la Kibrazili. Kabla ya kila mchezo, mkanda-miili aliye pia mganga-vidonda wa timu ile hutayarishia wachezaji maji ya kuogea yaliyotiwa utomvu wa lavenda na mwingine wa kitunguu-saumu. “Nikisahau kutayarisha maji haya ya kuogea, wachezaji huyadai,” yeye akasema. Pia, kabla wachezaji hawajakimbia kwenda nje kwenye uwanja wa kuchezea, yeye huweka kijipande cha kitunguu-saumu katika kila soksi. “Ni kweli kwamba uchawi ule sio huleta ushindi mchezoni,” akiri mkanda-miili huyo. “Lakini una nguvu nyingi za kuathiri hali ya mawazo na pia hutumika kuogopesha wachezaji wapinzani.”
USHAURI WA KUPENDEZA KWA MAMA
Mama mmoja Mkatoliki Mroma alipomwandikia padri Mkatoliki ambaye huhariri safu ya ukawaida katika karatasi-habari Sunday Telegraph akimwomba ushauri, alipokea jibu ambalo labda halikutarajiwa. Barua yake ilieleza huzuni kwa sababu binti yake wa umri mkubwa zaidi aliyeolewa, ajapokuwa amelelewa akiwa Mkatoliki, alikuwa amekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Jibu la kasisi huyo lilikuwa na ushauri fulani wa kupendeza. Kwa sehemu yeye aliandika hivi: “Ni lazima binti huyo awe huru . . . kujitafutia mwenyewe njia ya kufuata maishani. Wewe pata faraja kutokana na uhakika wa kwamba yeye anazoea dini fulani. Ni vizuri zaidi kuwa Shahidi wa Yehova aliye mzoevu kuliko kuwa Mkatoliki asiye mzoevu.”
WENYE KURUDI GEREZANI
Karibu asilimia 63 ya wafungwa wote waliofunguliwa katika magereza ya mikoa katika United States walikamatwa tena kwa uhalifu mzito katika muda wa miaka mitatu, kulingana na ripoti moja ya hivi majuzi ya Idara ya Haki. Wafungwa wa umri mdogo kuliko miaka 25 waliokuwa wamewekwa huru, ambao walikuwa wamekamatwa mara 11 au zaidi, walikuwa ndio wenye kadiri kubwa zaidi ya kuweza kurudia uhalifu—asilimia 94 kati yao walikamatwa tena.
MAHALI AMBAKO BAISKELI HUTAWALA
Katika muda wa mwaka mmoja tu, China ilitokeza baiskeli milioni 41 hivi, laripoti gazeti Asiaweek. Hiyo yamaanisha kwamba baiskeli 3,400 zilitokezwa kwa kila gari lililofanyizwa. Kwa kutofautisha, United States ilifanyiza baiskeli 82 tu kwa kila magari 100 iliyoyatokeza. Na baiskeli hizo “kwa sehemu kubwa zilikuwa ni mashine za kuvutia sana za spidi kumi zilizoundwa ili ziweze kutumiwa na kijana mbalehe kwa muhula mmoja au miwili akiwa aziendesha kweli kweli,” lasema gazeti hilo. Wachina huziona baiskeli kuwa zenye mafaa sana. “Kuendesha baiskeli hutaka theluthi moja ya nishati ambazo hutumiwa kwa kutembea. Motakaa ndogo humaliza nishati zilizo mara 50 za kiasi kile ambacho mtu mwenye kuendesha baiskeli hutumia,” kulingana na Asiaweek.
FURAHA—KWA KUWA MSEJA AU KWA KUFUNGA NDOA?
Wakati uliopita, uchunguzi mbalimbali katika United States umeonyesha kwamba watu waliofunga ndoa, kwa ujumla, waliripoti kuwa wenye kadiri kubwa zaidi za furaha ya kibinafsi kuliko wasiofunga ndoa. Huenda jambo hili likawa linabadilika. Habari za majuzi zaidi zilizokusanywa kutoka machunguzi 13 ya kitaifa yaliyoendeshwa kuanzia 1972 hadi 1986 na Kitovu cha Utafiti wa Maoni ya Kitaifa yalidokeza kwamba kuna upungufu wa furaha yenye kutokana na hali ya kufunga ndoa. Ingawa katika 1972, asilimia 38 ya watu waliofunga ndoa walisema walikuwa “wenye furaha sana” kuhusu maisha zao, katika 1986 tarakimu hizo zilikuwa zimepungua zikawa asilimia 31. Hata hivyo, miongoni mwa wasiofunga ndoa, hesabu ya waliosema ni “wenye furaha sana” ilipanda juu kutoka asilimia 15 katika 1972 ikawa asilimia 27 katika 1986.
MASHINE ZA SODA AMBAZO HUUA
Kutikisa-tikisa mashine ya kuuza soda ili kutoa soda moja si jambo la upumbavu tu bali ni zaidi ya hivyo. Kufanya hivyo kwaweza kuwa hatari sana. Daktari mmoja wa Jeshi la United States aandika katika The Journal of the American Medical Association kwamba yeye alijua habari za vijana 15 wa kiume walioumizwa na mashine zenye kuanguka za soda katika muda ambao wazidi kidogo tu miaka miwili. Watatu kati yao walikufa. Daktari huyo aarifu kwamba maumizo hayo yalitukia kwa sababu mashine hizo za soda huwa nzito kupindukia zikiwa zimejazwa kabisa, hivi kwamba mvuto au mtikiso wa nguvu sana utaibwaga chini mashine hiyo. Mashine hiyo ikitikiswa mbele mno, huenda ikagonga kwa kishindo cha kadiri inayofikia ratili elfu moja kwenye sehemu ya juu ya upande wa mbele wa mashine. Majeruhi waliobaki hai walishangaa sana jinsi mashine hizo zilivyokuwa nzito.