Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita
Sehemu 14: 622 W.K. na Kuendelea—Kunyenyekea Penzi la Mungu
“Kati ya wajumbe hawa Sisi tumekweza baadhi yao juu ya wengine.” Al-Baqarah (sūrah 2), mstari wa 253, kutoka kwenye Qur’āna
WATU wenye kuamini kuna Mungu mweza yote, aliye mwenye upendo hutambua hekima ya kunyenyekea penzi lake. Wao huthamini mwongozo ambao amewaandalia kupitia wajumbe waliopewa amana ya maarifa ya kimungu. Baadhi ya wajumbe hawa hutambuliwa na zaidi ya moja ya dini zile kubwa za ulimwengu. Kwa kielelezo, watu zaidi ya milioni 800 wenye kufuata Uislamu wana maoni ya kwamba Adamu, Noa, Abrahamu, Musa, Daudi, na Yesu ambao ni watu waliokuwa Wayahudi-Wakristo, ni manabii wakubwa wa Mungu. Lakini wao huamini kwamba kuna nabii wa saba ambaye amekwezwa juu ya wajumbe wengine wote—nabii Muḥammad.
Jina Islamu limejaa maana, kwa kuwa huonyesha kunyenyekea au kusalimu amri—katika maana hii ni kwa njia ya kufuata sheria na penzi la Allah. Mtu mwenye kufuata njia hii ya kunyenyekea au kusalimu amri hutajwa kuwa “Mwislamu,” neno hilo likiwa ni kitenzi-kivumishi cha kuonyesha mwenye kutenda mambo ya uislamu. Yule ambaye Waislamu wapaswa kumnyenyekea ni Allah. Lionwapo kuwa jina la kibinafsi, Allah huwa ni ufupisho wa Al-Ilah, hayo yakiwa ni maneno ya Kiarabu yanayomaanisha “Yule Mungu.” Jina hilo laonekana katika Qur’ān mara 2,700 hivi.
Nabii wa Maana Zaidi Katika Uislamu
Muḥammad bin Abdullah (mwana wa Abdullah), aliye mwanzishi wa Uislamu, alizaliwa katika Meka, Saudi Arabia, karibu mwaka 570 W.K. Yeye hakuridhishwa na imani na desturi za ibada ya kufuata miungu mingi katika eneo la kwao. Yaonekana hata hakuhisi akipendelea kufuata Dini ya Kiyahudi wala Ukristo. H. M. Baagil, mtungaji Mwislamu, aeleza zaidi hivi: “Kwa sababu Ukristo ulikuwa umepotoka kwa kuyaacha sana mafundisho ya awali ya Yesu, ndipo Allah akamtuma Muhammad, Nabii Wake wa mwisho ili awe sehemu ya mpango Wake wa hapo awali, awe mhuishaji wa kurekebisha mabadiliko yote haya.”
Muḥammad aliingiza mtindo wa mapendezi ya Kiarabu katika desturi na kawaida za ibada. Jiji la Meka na maabadi yalo matakatifu, Kaaba, likawa badala ya jiji la Yerusalemu na hekalu lalo. Ijumaa ikawa siku ya sala ya ushirika badala ya Jumamosi ya Wayahudi na Jumapili ya Wakristo. Na badala ya Musa ama Yesu, sasa Muḥammad akaja kuonwa na Waislamu kuwa nabii wa maana zaidi wa Mungu.
Akiwa na miaka karibu 40, Muḥammad alijulisha wazi kwamba alikuwa ameitwa awe mjumbe wa Mungu. Kwanza alishiriki imani zake pamoja na watu wa ukoo na marafiki, na pole kwa pole akasitawisha kikundi cha wafuasi. Mwanzo halisi wa muda wa Kiislamu ulikuwa katika 622 W.K., wakati yeye alipohama Meka kwenda Medina, na tukio hilo likaitwa hijrah, neno la Kiarabu la kusema “mhamo.” Hivyo, tarehe za Kiislamu hutajwa kuwa A.H. (Anno Hegirae, mwaka wa ule mkimbio).
Muḥammad alijaribu kufanya Wayahudi katika Medina wakubali kufuata dini yake mpya na daraka lake akiwa nabii. Lakini alishindwa kuwavuta kwa usadikisho. Walimpinga na wakamtungia hila pamoja na adui zake katika Meka na Medina pia. Baada ya muda vikundi vile vikubwa-vikubwa vya Wayahudi viliondoshwa, na mbari moja, ile ya Qurayẓah, ikaharibiwa na kuwaua wanaume wayo na kuwatia utumwani wanawake na watoto.
Mwishowe, jiji la Meka lilitekwa kwa amani katika 8 A.H. (630 W.K.), na pia sehemu kubwa ya Peninsula ya Kiarabu. Miongo michache baada ya kifo cha Muḥammad, mabishano kuhusu mapokezano ya cheo yalileta magombano ya wenyewe kwa wenyewe hata yakafanya jumuiya iwe na maoni ya kuelekea kukubaliana na vikundi na mawazo yasiyo ya Kiislamu.
Si Dini Tu
Uislamu ni njia ya maisha yenye kuhusisha ndani mambo yote, yenye ujumla wa Serikali, sheria zayo, vyama vyayo vya kijamii, na utamaduni wayo, na kwa hiyo si dini tu. Ndiyo sababu kitabu Early Islam chasema kwamba kwa miaka zaidi ya 600, “Uislamu ulikuwa ndiyo dini yenye matakwa yaliyo magumu zaidi, jeshi la kisiasa lililo thabiti zaidi na utamaduni ulio muhimu zaidi katika ulimwengu.”
Kwa kweli, katika muda wa karne moja baada ya kifo cha Muḥammad, milki ya Kiarabu, ambayo kwenye kilele chayo ilikuwa kubwa kuliko Milki ya Kiroma, ilienea kutoka India kuvuka Afrika Kaskazini mpaka Hispania, ikasaidia kupeleka mavumbuzi yaliyotajirisha utamaduni wa Magharibi. Ilifanya michango mikubwa ajabu katika nyanja za sheria, hisabati, elimu ya nyota, historia, fasihi, jiografia, falsafa, ustadi wa kujenga, tiba, muziki, na elimu za mahusiano ya kijamii.
Kama Kimwondo Chenye Kumalizika Upesi
“Ushinde wa maeneo ya Kiarabu ulisababishwa moja kwa moja na mahubiri ya Muhammad,” yasema The Collins Atlas of World History. Bila shaka, mambo mengine pia yalichangia mpanuko wa Kiislamu. Kwa kielelezo, mahitilafiano ya kidini kati ya Wakristo wa Byzantium na Wazoroasta wa Uajemi yaliwapofusha wasing’amue kwamba Waarabu walikuwa wakiwasogelea.
Kujitahidi kutumia dini ili kushikamanisha milki iliyotapakaa sana halikuwa jambo jipya. Lakini “Waislamu walisadiki kwamba katika Korani wao ndio waliokuwa na taarifa ya ukweli iliyo neno la mwisho lisiloweza kupingwa,” aeleza mtungaji Desmond Stewart. Wakatosheka kwamba wako sawa kabisa, “wakiamini kwamba mambo yote yenye ustahiki wa kujulikana yalikuwa tayari yajulikana, na kwamba mawazo ya watu wasio Waislamu hayakuwa ya maana.” Mabadiliko “yalikinzwa kwa ushupavu.”
Kwa hiyo, kufikia karne ya 11, milki ilikuwa tayari ikizorota. Stewart aifananisha na “kimwondo chenye kupita mbio katikati ya anga la usiku [ambacho] . . . baada ya muda mfupi kilimalizika nguvu.” Hivyo, dini hii, iliyofanyiza hisia ya udugu na ikatoa njia iliyorahisishwa ya mkaribio wa kibinafsi kwa Mungu, kwa kweli ilichangia kuiangusha milki ile ile ambayo ilikuwa imeisaidia kuifanyiza hapo kwanza. Ilianguka ghafula sawasawa na vile ilivyoinuka haraka. Milki hiyo ikawa imekufa, lakini dini yayo ikaendelea kuishi.b
Unyenyekeo wa kweli watia ndani kutii Mungu, sheria zake, na wawakilishi wake. Muḥammad alifaulu kuungamanisha makabila ya Kiarabu katika Arabia, akaanzisha jumuiya ya Kiislamu (Ummah) yenye kutegemea yeye na Qurʹān. Hiyo ilikuwa hali ya kidini ambamo unyenyekeo ulisaidia kuwafanya wawe ndugu walio chini ya kiongozi mmoja. Uislamu uliruhusu kutumia upanga katika kupigana na maadui wa makabila ya Kiarabu. Upanga huu ulisaidia kupanua milki yao na dini yao. Muḥammad alipokufa, tofauti zenye jeuri zilitokea. Kwanza zilikuwa za kisiasa, zikitokana na suala la kuchagua Khalifah mmoja, kiongozi. Zilisukuma wengi kutumia panga zao waue ndugu zao. Kuchanganya dini na serikali kulitumika kuigawanya jumuiya. “Unyenyekeo” haungeweza kuungamanisha watu hao chini ya kiongozi mmoja.
Pokeo lasema kwamba Muḥammad mwenyewe alitangulia kuona mafarakano 72 ya wazushi wa dini ya Kiislamu yakifanyika. Lakini leo wenye mamlaka fulani hunena juu ya mamia kadhaa.
Migawanyiko miwili iliyo mikubwa ni Washia na Wasunni. Hata hivyo, kila mmoja una migawanyiko mingi sana midogo-midogo. Kati ya kila Waislamu 100, karibu 83 ni Wasunni na karibu 15 ni Washia. Wale wengine ni wa vikundi vya mafarakano mbalimbali yenye kutofautiana sana kuanzia Wadruze, Waislamu Weusi, na Waabanga wa Indonesia, ambao huchanganya Uislamu na Dini ya Kibuddha, Dini ya Kihindu, na dini za huko.
Sehemu moja ya wachache walio Washia ni imani yao ya kwamba dini na Qur’ān ina maana zilizofichika ambazo hukusudiwa kueleweka na wahusika peke yao. Lakini kule kujitenga kwa Washia kulitokana hasa na suala la mapokezano ya cheo. Washia (neno linalomaanisha “wafuasi wa chama cha ‛Alī”) hushikilia fundisho liitwalo uhalali, wakidai kwamba haki ya utawala ni ya ‛Alī, aliye binamu na mwana-mkwe wa Muḥammad, na ya wazao wa ‛Alī.
‛Alī na wazao wake walikuwa maimamu, viongozi wenye mamlaka kamili ya kiroho. Kuna ukosefu wa makubaliano kuhusu hesabu ya maimamu waliokuwako, lakini kikundi kikubwa zaidi cha Washia, ambacho huitwa Washia wa Thenashara, huamini wamekuwako 12. Katika 878 W.K. imamu wa 12 akawa “mwenye kufichika,” yaani, alitoweka baada ya kuahidi kwamba angerudi wakati wa mwisho wa ulimwengu ili asimamishe imara serikali yenye haki ya Kiislamu.
Kila mwaka Waislamu Washia hufanya ukumbusho wa kufia imani kwa Ḥusayn, mjukuu wa Muḥammad. Mtungaji Rahman aeleza hivi: “Kwa kuzoezwa kusherehekea tukio hili tangu utoto wake, yaelekea Mwislamu wa Shī‘ī atakua akiwa na hisia ya kina kirefu kuhusu tanzia na ukosefu wa haki ambao utamfanya aone ni sawa kabisa kufia imani.”
Je! Ni Shuhuda za Kukosa Muungamano?
The Columbia History of the World chaeleza kwamba, “kuanzishwa kwa falsafa na mantiki ya Kigiriki katika karne ya tisa” kulitokeza falsafa tofauti kabisa ya Kiislamu iliyoleta mabadiliko ya muda mrefu juu ya fikira na mawazo ya kidini ya Uislamu. . . . Kadiri wakati ulivyopita Uislamu wenyewe, ukiwa dini na njia ya maisha, ulipatwa na mabadiliko makubwa yenye kuathiri muungamano wao.”
Kwa kielelezo, Usufii, ambalo ni neno la Magharibi la kusema mafumbo ya dini ya Kiislamu, ulitokea wazi katika karne ya nane na ya tisa na ukasitawi haraka kuwa harakati kubwa sana ya kidini. Kufikia karne ya 12, jamii za Wasufii, au vikundi vya udugu, vilienea kwa mapana. Makao ya watawa Wasufii yalianza kwa umaarufu mwingi hata yakakaribia kuwa ya maana kuliko musikiti. Mazoea yaliyo katika Usufii yahusisha ndani tendo la kutia akili usingizini kwa kutumia mbinu za kukaza fikira kwenye jambo moja au kwa kucheza dansi za kibumbuwazi, kutamka-tamka maneno fulani ya pekee, kuamini miujiza, na kuwaabudu watakatifu waliokufa.
Wasufii waliridhiana msimamo wao na desturi na imani za mahali. Waturuki walidumisha mazoea yao ya kishamani, Waafrika wakadumisha waganga wao wa kienyeji, Wahindi wakadumisha watakatifu wao na miungu yao ya kipindi cha Dini ya Kihindu na ya kipindi kilichotangulia, nao Waindonesia—kama vile ielezwavyo na The New Encyclopædia Britannica—wakadumisha “maoni [waliyokuwa nayo] kabla ya kutokea kwa Uislāmu lakini kwa juujuu wakawa wanafuata mazoea ya Kiislāmu.”
Usitawi wa farakano maarufu la kidini lililotokea majuzi ni ile dini ya Baha’i iliyositawi kutokana na Uislamu wa Kishia katika Iran katikati ya karne ya 19. Jingine ni farakano la Kisunni ambalo huitwa Aḥmadīyah, lililositawi katika India mwishoni mwa karne ya 19, wakati ambapo Mirza Ghulam Ahmad, aliyepiga mbiu ya kujitambulisha binafsi kuwa ni nabii, alidai kuwa yeye ni udhihirisho wa Muḥammad, kwamba yeye ni Yesu aliyerudi, na kwamba ni umbo lililozaliwa upya la Krishna Mhindu. Alifundisha kwamba baada ya Yesu kuponyoka kifo kule Golgotha, alikimbilia India, akabaki huko akiwa mtendaji mpaka alipokufa akiwa na umri wa miaka 120.
Katika vichapo vyake vya maelezo kuhusu Qur’ān, mtungaji Mwislamu S. Abul A‛la Maududi asema hivi: “Wakati wa kufunuliwa kwa Al-Baqarah [ile sūrah iliyonukuliwa kwenye kichwa cha makala hii], wanafiki wa namna zote walikuwa wameanza kutokea.” Walikuwa ni kutia ndani na “‘Waislamu,’ munāfiqīn (wanafiki) . . . ambao katika akili walisadiki Uislamu ni kweli lakini hawakuwa na ushujaa wa kiadili wenye kutosha kuwafanya waache mapokeo yao ya zamani.”
Kwa hiyo tangu pale pale mwanzoni, ushuhuda waonyesha kwamba wafuasi wengi hawakumnyenyekea Allah kwa njia ambayo Muḥammad alikusudia. Lakini wengine walimnyenyekea.
[Maelezo ya Chini]
a “Qur’ān” (neno ambalo lamaanisha “kukariri”) ndiyo njia ya kuendeleza neno hilo ambayo hupendelewa na waandikaji Waislamu na ambayo tutaitumia hapa badala ya ile namna ya Magharibi ya kuliendeleza kwa kuliandika “Koran.”
b Yale maoni ya kawaida kwamba Uislamu ni dini ya Waarabu peke yao si sahihi. Wengi wa Waislamu wa leo ni watu wasio Waarabu. Indonesia, ambayo ndiyo nchi yenye Waislamu wengi zaidi, ina wafuasi milioni 150.
[Sanduku katika ukurasa wa 29]
Ili Kukusaidia Uelewe Uislamu Vizuri Zaidi
Zile Nguzo Tano za Uislamu zataka kwamba Waislamu wafanye ungamo la peupe angalau mara moja kuhusu imani ijulikanayo kuwa Shahādah—“Hakuna mungu ila Mungu; Muḥammad ndiye nabii wa Mungu”; waseme sala zao mara tano kwa siku; walipe zakati, ambayo ni kodi ya lazima, ambayo sasa kwa kawaida hukusanywa kwa watu wenye kujitolea; wafunge kuanzia kucha kwa jua hadi kuchwa kwa jua katika mwezi wa tisa, Ramadani; na ikiwa wana uwezo wa kifedha, wafanye haji (hija) ya kwenda Meka angalau mara moja.
“Jihadi” (“vita takatifu” au “mng’ang’ano mtakatifu”) huonwa kuwa nguzo ya sita na lile farakano la dini ya Khariji lakini haionwi hivyo na Waislamu kwa ujumla. The New Encyclopædia Britannica yasema kwamba kusudi layo “si kuongoa watu mmoja mmoja waje kwenye Uislāmu bali ni kupata mamlaka ya kisiasa ya kudhibiti kwa ujumla mambo ya jamii za watu ili kuyaendesha kupatana na kanuni za Uislāmu.” Qur’ān huruhusu “vita takatifu” ya jinsi hiyo, ikisema hivi: “Usiue mwanadamu yeyote ambaye Allah amekukataza kumuua, isipokuwa kwa kusudi la haki.”—Sūrah 17:33.
Vyanzo vikubwa vya fundisho na sheria ya Kiislamu ni Qur’ān, iliyoandikwa kwa kipindi cha karibu robo karne; sunnah (mapokeo); ijmā‘ (makubaliano ya jumuiya); na qiyās (fikira ya mtu binafsi). Fungu la sheria za Kiislamu, ile Sharī‘ah, ambalo hushughulika na ujumla wa maisha ya Waislamu ya kidini, ya kisiasa, ya kijamii, ya kinyumbani na ya kifaragha, lilipangwa kwa utaratibu wakati wa karne ya nane na ya tisa W.K.
Meka, Medina, na Yerusalemu ndizo sehemu tatu zilizo takatifu zaidi za Uislamu, na cheo cha utakatifu wazo ni kulingana na mpangilio huo: Meka ikiwa hivyo kwa sababu ina mahali patakatifu pa Kaaba, ambapo pokeo lasema palijengwa na Abrahamu; Medina pakiwa ndipo penye musikiti wa Muḥammad; na Yerusalemu ikiwa hivyo kwa sababu pokeo lasema hapo ndipo Muḥammad alipokuwa wakati wa kupaa kwake mbinguni.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 30]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Milki ya Kiislamu kama ilivyoonekana wakati wa kilele chayo