‘Ole, Ole, Jiji Lile Lililo Kuu’
KATI ya majiji yote ulimwenguni ambayo hudai kuwa makubwa, ingeonekana kwamba hakuna yoyote ambayo yangestahili kudai hivyo zaidi ya yale yaonwayo kuwa matakatifu kidini. Lakini maneno “ole, ole” yaonyesha kwamba lile jiji la kidini liitwalo ‘kuu’ kwenye Ufunuo 18:10 kwa wazi halina kibali cha kimungu, kama tutakavyoona baadaye.
Je! Ni Kuvuka Kwenda Kupata Kutokufa?
Majiji matakatifu ya Kihindu katika India huitwa tīrthas, kumaanisha “mivuko” au “vivuko.” Mengi, kama Banaras (ambalo pia huitwa Benares, Kasi, au Varanasi), yako katika kingo za mito. Lakini hayo hueleweka kuwa, si mivuko halisi, bali vivuko vya kiroho ambavyo hudhaniwa huwaruhusu wanadamu kuvuka kwa usalama mito na bahari za maisha ili kwenda kufikia maisha mazuri zaidi ya ile ng’ambo nyingine.[1]
Ensaiklopedia moja husema: “Vārānasi ni moja la majiji ya zamani zaidi yanayoendelea kukaliwa ulimwenguni . . . , kao la kwanza kukaliwa na Waarya katikati ya bonde la Ganges.” Lilikuwa kitovu cha kidini mapema sana kufikia mileani ya pili K.W.K. Ingawa ni jiji la Kihindu, laonekana pia katika maandishi ya kihistoria ya Wabuddha na Waislamu. Katika karne ya sita K.W.K., ambapo Banaras lilikuwa lingali jiji kuu la Ufalme wa Kasi, Buddha alihubiri mahubiri yake ya kwanza hapo karibu. Uislamu ulihusika katika 1194, wakati Waislamu walipotwaa udhibiti wa jiji hilo.
Likiwa kaskazini mwa India kwenye mto Ganges, Banaras ni moja la majiji saba ya Kihindu yaliyo matakatifu zaidi nchini.[3] Mahali fulani pa mfano ndani ya mipaka yalo pamegawiwa kila mungu wa Kihindu na kila mmoja wa wale tīrthas wakubwa. Hivyo, The Encyclopedia of Religion huita jiji hilo “kilimwengu cha jiografia takatifu ya India.” Yaongezea hivi: “Wingi wa nguvu zijazo kutokana na ule mkusanyo wa mfano wa kuwaleta miungu, tīrthas, na wahenga wenye hekima katika mahali pamoja hapa umefanya Banaras pawe ndipo mahali pa kusifika zaidi kwa safari za kuhiji katika India.”[4][5]
Wahindu huona Banaras kuwa ni mahali ambapo mtu akifia hapo huwa ni dalili ya heri na fanaka. Kifungu cha maneno yapendwayo, Kāśyām maranam muktih, humaanisha “Kifo katika Kasi ni ukombozi.” Pokeo husema kwamba yeyote mwenye kufia hapo atafunzwa na Siva mwenyewe, jambo ambalo ni kama kubebwa “kulivuka furiko la samsāra kwenda ‘ufuo wa mbali’ wa kutokufa.”a
Kama mito iliyoko kila mahali, mto Ganges hujipindapinda ukipita kwenye majiji yenye usitawi, ukifyonza maji machafu ya kinyesi na takataka na kemikali kadiri uendavyo. Kwa sasa, Wahindu wenye kujitoa hutupa maiti zikadiriwazo kuwa 10,000 ndani ya mto huo kila siku, kama iamuriwavyo na pokeo la kidini. Wakati huohuo, wasafiri wenye kuhiji, bila kujua juu ya hatari ya wazi kabisa ya magonjwa, hushuka vigazi vya kingo za mto huo kuoga kwa kufuata desturi za kidini.[8] Je! kweli hiyo ndiyo njia inayoenda kwenye kutokufa?
Hilo “Jiji la Milele” Ni la Milele Kadiri Gani?
Mto mwingine, ambao yawezekana hapo kwanza uliitwa Albula kwa kurejezea weupe wa maji yao, hutiririka kupita katika jiji moja la kidini Ulaya, lile “Jiji la Milele” lenye vilima saba (Roma). Kwa kuwa mto huo ulikwisha kupoteza weupe wao, sasa waitwa Tiber. Nalo jiji limekwisha kupanuka zamani likaacha kuwa la vilima saba. Hata hivyo, “ule urithi wa zamani uliobakia Roma,” yasema The New Encyclopædia Britannica, “hauna kifani katika jiji lolote la Magharibi.”[9]
Majumba mengi ya ukumbusho na majengo ya kihistoria yashuhudia urithi huo. Ni ajabu kwamba hata yameweza kubakia, kwa kufikiria zile nyakati nyingi ambazo jiji hilo limeshindwa na kutekwa nyara—mwanzoni mwa karne ya nne K.W.K. na Wagoli na katika Wakati wa Kawaida, na Wavisigothi katika 410, Wavandali katika 455, Wanormani katika 1084, vikosi vya askari wa kigeni katika 1527, jeshi la Napoleon katika 1798, na Wajerumani na Waungani katika Vita ya Ulimwengu 2.[10]
Ingawa jiji la Roma ya awali lenye kuta ni asilimia 4 tu ya eneo la jumla la jiji la ki-siku-hizi, hiyo ndiyo Roma ambayo mamilioni ya watalii humiminika kuona, kwa maana hapo ndipo yalipo mengi ya majengo ya ukumbusho.[11] Uvutio mwingine wa watalii, angalau katika mapema ya 1993, ulikuwa ule wonyesho “Sixtus wa 5 na Roma.” Akiwa papa kuanzia 1585 hadi 1590, Sixtus aliacha sifa ya kudumu sana katika Roma hivi kwamba ameitwa “baba ya mpangilio wa miji ya ki-siku-hizi.” Kikieleza kwa nini yeye aliunda Roma upya, kichapo The European kiliandika hivi: “Kwanza, ni kuandaa msingi imara wa ujenzi kuthibitisha mamlaka ya Vatikani dhidi ya tisho la Uprotestanti. . . . Pili, ni kulifanya jiji la Roma, ambalo kwa njia nyingi bado lilikuwa mji wa mkoa ulio soko la kawaida tu, listahili kuwa makao makuu ya Yerusalemu Jipya.”[12]
Jiji Vatikani, ambacho ni kieneo kidogo cha Roma, hudai kuwa ndilo “hayo makao makuu ya Yerusalemu Jipya.” Katika 1929 serikali ya Ufashisti ya Italia ilitia sahihi Mkataba wa Latera, kwa njia hiyo ikitambua enzi kuu ya Jiji Vatikani. Tangu wakati huo papa ametawala jiji hilo kwa mamlaka ya utekelezaji, utunzi wa sheria, na hukumu iliyo kamili. Vatikani lina mfumo walo lenyewe wa posta na simu na jeshi lalo lenyewe, kutia na Walinzi wa Kiswisi wenye mavazi rasmi, walio na daraka la kumlinda papa. Lakini kile ambacho watalii hutaka kuona hasa ni Basilika ya Mtakatifu Petro, ambalo kwa karne nyingi lilikuwa ndilo kanisa kubwa zaidi katika Jumuiya ya Wakristo. Sifa hiyo ya kuipambanua ilipotea katika 1989 wakati ile basilika iliyo katika Yamoussoukro, Côte d’Ivoire, ilipomalizika.[13]
The New Encyclopædia Britannica husema kwamba “kwa miaka 1,000, mtu kuwa raia wa Roma ilikuwa ni kushika funguo za kuuingia ulimwengu, kuishi katika usalama, fahari, na starehe ya kadiri.”[14] Lakini hayo kwisha! Ufisadi wa kisiasa katika Roma na kuzubaa kwa maendeleo ya kidini katika Jiji Vatikani kwathibitisha kwamba yale yaitwayo matukufu ya jana si ya milele.
Mahali Patakatifu Zaidi Sana pa Uislamu
Karibu Waislamu bilioni moja katika ulimwengu wote huliona jiji la Mecca kuwa “ndio uwanja wa utendaji wa kimungu, wa kimalaika, wa kiunabii, na wa kibinadamu wenye fanaka tangu ile dakika ya mwanzo kabisa ya uumbaji.”b Kulingana na Uislamu hapo ndipo uumbaji ulipoanzia, ndipo Abrahamu alipojenga nyumba ya kwanza ya ibada, na ndipo alipopeleka suria wake Hajiri na mwana wao, Ishmaeli.[15]
Hivi majuzi zaidi, labda karibu 570 W.K., Mecca, Saudi Arabia, ndipo nabii Muḥammad alipozaliwa. Kwanza mafundisho yake hayakuitikiwa sana. Mecca ilikuwa kisehemu chenye maji katika jangwa kwenye njia ya biashara ya misafara kati ya India na Ulaya, na mabepari wao wenye nguvu walihofu kwamba marekebisho yake ya kidini yangeweza kufanya uchumi usisitawi kwa haraka. Kwa kushindwa kupata huko mahali pa kuwa ngome, nabii aligeukia Yathrib, ambalo lilikuja kuitwa Al-Madīnah (Medina), jiji lililoko kilometa zaidi ya 300 kuelekea kaskazini-mashariki. Lakini katika 630 W.K.., alirejea Mecca, akaliteka, na kulifanya kitovu cha kiroho cha Uislamu.[16]
Leo Mecca ni jiji tajiri lenye kujulikana ulimwenguni pote, hata ingawa ni Waislamu tu wawezao kukaa huko.[17] Wakati wa Dhuʼl-Hijja, ule mwezi mtakatifu wa safari ya kuhiji, mamilioni huzuru kutimiza wajibu wao wa kidini wa haji.[18] Wakiwa Mecca wasafiri wenye kuhiji huzuru ule Msikiti Mtakatifu, ambako wao hutembea mara saba kuzunguka kijengo kitakatifu kilicho karibu na sehemu ya kati ya ua wa msikiti usio na paa.
Hicho kijengo kitakatifu ni ile Kaaba, jengo lililo na umbo la mchemrabasawa (kyubu) ambao kwa kawaida hufunikwa kwa pazia kubwa la hariri na lenye lile Jiwe Jeusi takatifu. Jiwe hilo, ambalo Waislamu huamini lilipewa Adamu kwa msamaha wa dhambi alipokwisha kuondoshwa Edeni, hudhaniwa kuwa lilikuwa jeupe wakati huo. Katika pokeo la Kiislamu ile Kaaba ya kwanza iliangamia katika Furiko la Noa, lakini lile Jiwe Jeusi likahifadhiwa na baadaye likapewa Abrahamu na malaika Gabrieli, kisha Abrahamu akaijenga upya Kaaba na kurudisha lile Jiwe Jeusi mahali pafaapo. Ule upande wa Kaaba—ambapo ndipo mahali patakatifu zaidi duniani kulingana na Uislamu—ndiko Waislamu hujielekeza wasalipo mara tano kwa siku.[19]
Malango ishirini na manne huongoza ndani ya ua wa ule Msikiti Mtakatifu, lakini mwingilio wa kimapokeo kwa wasafiri wenye kuhiji ni lile Lango la Amani, lililo kwenye kona ya kaskazini. Na bado, mambo hayawi yenye amani sikuzote wakati wa ile haji. Katika 1987, wapinzani wa Kiislamu walijaribu kutwaa udhibiti wa msikiti. Utaratibu ulirudishwa upesi lakini si kabla ya Waislamu zaidi ya 400 kuuawa na wapatao 650 kujeruhiwa. Ukosefu wa wazi hivyo wa amani katika mahali patakatifu zaidi pa Kiislamu ni jambo la kusikitisha, lakini Waislamu waweza kupata faraja kutokana na fundisho la Kiislamu, ambalo kulingana nalo mtu yeyote afaye akiwa katika haji huingia moja kwa moja mbinguni.[20]
Je! Ni Kumiliki Amani Maradufu?
Yerusalemu, ambalo huonwa na Wayahudi na wenye kudai kuwa Wakristo kwamba ni Jiji Takatifu na kuonwa na Waislamu kuwa ndipo mahali pa tatu kwa utakatifu mwingi zaidi duniani (kwa kufuata Mecca na Medina), humaanisha “Kumiliki Amani Maradufu.” Kuanzia 1070 K.W.K., lilikuwa ndilo jiji kuu la Israeli ya kale, ingawa kwa karibu miaka 900 kabla ya hapo lilikuwako likiitwa jina Salemu. (Mwanzo 14:18) Likiwa ndilo kitovu cha taifa, lilikuwa mahali pafaapo kwa mambo mengi, likiwa limezungukwa na vilima kama kiota kwenye mwinuko wa karibu meta 750 juu ya usawa wa bahari, hiyo ikilifanya wakati huo liwe moja la majiji makuu yaliyoinuka zaidi ulimwenguni.[21]
Katika karne ya nne K.W.K., Yerusalemu lilikuja chini ya udhibiti wa Wagiriki. Kufikia karne ya pili K.W.K., lilizidi kuathiriwa na Milki ya Roma yenye kupanuka. Wakati wa utawala wa Herode Mkuu, Yerusalemu lilisitawi. Sehemu ya ukuta wa ua wa hekalu alilolijenga yaonekana ingali imesimama, sasa ikiitwa Ukuta wa Magharibi (wa Maombolezo). Kwa sababu Wayahudi walijaribu kujiondolea kongwa la Waroma, majeshi ya Roma yalishambulia Yerusalemu katika Aprili 70 W.K. Muda unaopungua miezi mitano baadaye, jiji hilo na hekalu lalo lililala likiwa magofu.[22]
Kulingana na hesabu moja, Yerusalemu limeshindwa mara 37. Katika visa vingi jambo hilo limekuwa na matokeo ya kuliharibu kwa sehemu au kabisa. Lakini Yerusalemu fulani jipya limekuwa likitokea juu ya lile la zamani. Kwa hiyo katika karibu 130 W.K., Mmiliki Hadrian aliagiza jiji jipya lijengwe, moja lililoitwa Aelia Capitolina. Hakuna Myahudi aliyeruhusiwa kuliingia kwa karibu karne mbili. Ndipo, katika nusu ya kwanza ya karne ya saba W.K., Waislamu wakateka jiji hilo na baadaye wakaijenga Kuba ya Mwamba katika au karibu na ule uliokuwa uwanja wa hekalu.[23]
Serikali ya Israeli ya ki-siku-hizi ilianzishwa katika 1948, na katika 1949, Yerusalemu likagawanywa kati ya Israeli na Yordani. Lakini katika 1967, wakati wa ile Vita ya Siku Sita, Waisraeli waliiteka nusu ya mashariki ya jiji hilo. Tangu wakati huo wamefanya jiji hilo kuwa la ki-siku-hizi, huku wakijaribu kulidumishia ukamilifu walo wa kihistoria.[24] Kufikia 1993 idadi ya watu humo ilikuwa zaidi ya nusu milioni.[25]
Kwa kuwa kuna dini kubwa tatu za ulimwengu ambazo huliona Yerusalemu kuwa takatifu, nyakati nyingine misukosuko ya kidini hufoka. “Kati ya mapambano yote yaliyo kati ya Wayahudi na Waarabu, lile linalohusu Yerusalemu ndilo la kutatanisha zaidi na kusumbua sana,” lasema Time. Kwa sasa hakuna ushuhuda mwingi wa ile amani maradufu ambayo jina la Yerusalemu huahidi.
“Majiji Yako Yatakuwa Magofu Yenye Ukiwa”
Jiji litajwalo kwenye Ufunuo 18:10 hufananisha dini zote zinazomchukiza Mungu. ‘Ole, ole, jiji lile lililo kuu, Babeli, jiji lile lililo na nguvu! kwa kuwa katika saa moja hukumu yako imekuja’! Kwa wazi, hiyo yamaanisha kwamba dini inayompinga Yehova Mungu imehukumiwa maangamizi. Yajapokuwa na mahekalu, sherehe, na vyombo vya kidini, majiji ‘makuu’ ya leo ambayo ni dini hayatatoa ulinzi wowote wa kudumu katika siku ya hukumu ya Mungu.
[Maelezo ya Chini]
a “Samsara” hueleweka na Wahindu kumaanisha kuhama kwa nafsi ya milele, isiyoangamia, kutoka maisha mamoja kwenda maisha mengine.
b Islam: Beliefs and Teachings, kilichochapishwa na Shirika la Elimu ya Kiislamu, hudai kwamba “idadi ya karibuni zaidi ya Waislamu ulimwenguni kote ingeweza kuwa ni karibu milioni 1,100.”
[Picha katika ukurasa wa 24]
Ule msikiti mtakatifu wa Mecca na ile Kaaba
[Hisani]
Camerapix
[Picha katika ukurasa wa 25]
Ukuta wa Yerusalemu wa Maombolezo ya Wayahudi na ile Kuba ya Mwamba ya Kiislamu (kushoto)
[Hisani]
Garo Nalbandian