Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 1/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MISIBA YAKUMBA UNITED STATES
  • ‘UM KUSHIRIKI SEHEMU KUU’
  • WAZAZI “WATUMIAO MAMLAKA KWA KUSABABU” NI BORA ZAIDI
  • TEMBO—SASA NI NAMNA YA KIUMBE ALIYE HATARINI
  • SIMBA WALA-BINADAMU
  • TISHO LA ZIADA
  • KUFANYA MAJANGWA YACHANUE
  • MUSIKITI WA KWANZA KATIKA ROMA
  • Pembe za Tembo—Zina Thamani Gani?
    Amkeni!—1998
  • Ufalme Uliojengwa Juu ya Mchanga, Mafuta, na Dini
    Amkeni!—1992
  • Uhifadhi Dhidi ya Utoweko
    Amkeni!—1996
  • Je! Kuna Nafasi ya Kutosha Mwanadamu na Mnyama?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 1/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

MISIBA YAKUMBA UNITED STATES

Misiba miwili iliharibu majimbo mbali mbali ya United States wakati wa Septemba na Oktoba 1989. Kwanza, Tufani Hugo, yenye pepo za mwendo wa kilometa 216 kwa saa, ilifagia sehemu ya kusini-mashariki ya United States, ikiacha nyuma mlolongo wa uharibifu. Siku ya Oktoba 17, tetemeko la dunia lenye kipimo cha 7.1 katika mizani ya Richter lilishtusha eneo la San Francisco Bay, likiua watu wengi na kusababisha madhara yaliyokadiriwa kuwa maelfu kwa mamilioni ya dola katika sehemu hiyo ya magharibi ya nchi. Kwa usadifiano, wakati wa siku mbili zilizofuata (Oktoba 18, 19), mfululizo wa matetemeko ya dunia, yenye ukubwa wa karibu 6 katika mizani ya Richter, yalitikisa China ya kaskazini. Watu angalau 29 waliuawa.

‘UM KUSHIRIKI SEHEMU KUU’

Wanaubalozi wenye kuhudhuria Kusanyiko Kuu la Umoja wa Mataifa la 44 walitaarifu kwamba masuala matatu yaliyo ya maana zaidi ulimwenguni ambayo yanahitaji sana kutatuliwa ni madeni ya nchi zinazositawi, uchuuzi wa dawa za kulevya, na kulindwa kwa mazingira. Wengi walikubali kwamba ni lazima UM uhusike katika kuyatatua. Msimamizi wa Kusanyiko Kuu alisema kwamba washiriki wote “walikazia uhitaji wa Umoja wa Mataifa kushiriki sehemu kuu ukiwa ndio tumaini la mwisho la ainabinadamu kwa amani na haki.”

WAZAZI “WATUMIAO MAMLAKA KWA KUSABABU” NI BORA ZAIDI

“Wazazi ambao hawatoi adhabu kwa ukali, bali wawekao mipaka imara na kushikamana nayo, wataelekea kwa kadiri kubwa kutokeza watoto wenye kutimiza mengi na wenye kupatana na wengine,” yataarifu U.S.News & World Report. Wazazi hao hutajwa kuwa “watumiao mamlaka kwa kusababu” (“fanya hivyo kwa sababu hii”), kwa kutofautishwa na wale “watumiao mamlaka kimabavu” (“fanya hivyo kwa sababu mimi ndio mzazi”) na “wenye kuendekeza” (“fanya lolote utakalo”), hiyo ikiwa ni mitindo ya kutia nidhamu ambayo ilitokeza watoto wenye tabia zenye kutofautiana sana. Machunguzi hayo, yenye kuhusisha miongo miwili, yalionyesha kwamba wazazi watumiao mamlaka kusababu walikuwa na elekeo zaidi la kuwa na watoto walio thabiti, wenye kuridhika, wenye kujidhibiti, na wenye kujitegemea kwa maamuzi, na wasioelekea sana kujaribu dawa za kulevya. “Wazazi watumiao mamlaka kwa kusababu hawana ubwana-mkubwa,” asema mwanasaikolojia Diana Baumrind wa Chuo Kikuu cha Kalifornia, aliyeendesha machunguzi hayo. “Wao hujali sana kuwajua watoto wao, jinsi wanavyoendelea shuleni na marafiki zao ni nani. Udhibiti wao huwa na kiwango cha juu cha kujikabidhi wajibu wa kumjali mtoto, nao hawaogopi kukabiliana na mtoto.”

TEMBO—SASA NI NAMNA YA KIUMBE ALIYE HATARINI

Mkusanyiko wa Biashara ya Kimataifa ya Namna za Viumbe Walio Hatarini, uliokutana katika Lausanne, Uswisi, Oktoba mwaka juzi, ulimweka tembo wa Kiafrika katika orodha yao ya namna ya viumbe walio hatari. Hatua hiyo yapiga marufuku kufanya biashara ya meno ya tembo. Mkusanyiko huo watumaini kwamba hatua hii itakomesha uwindaji haramu ufanywao na wawindaji wa meno ya tembo. Yakadiriwa kwamba idadi ya tembo wa Kiafrika imepunguzwa kwa nusu katika mwongo uliopita. Katika 1979 kulikuwako tembo milioni 1.3 katika kontinenti hiyo. Sasa kuna 625,000 hivi.

SIMBA WALA-BINADAMU

Mbuga Kruger ya Kitaifa ya Afrika Kusini ni ukanda wa bara ambao hutanuka kwa urefu upatao kilometa 320 kandokando ya mpaka na Msumbiji. Ili kuepuka vita ya wenyewe kwa wenyewe, Wasumbiji wengi wametoroka kupitia mbuga hiyo kwa kujasirisha uhai wao sana, kwa kuwa mbuga hiyo imejaa simba na wanyama wengine hatari. Kwa ujumla, simba huwaepuka wanadamu. Hata hivyo, yafikiriwa kwamba harakati hiyo ya wakimbizi imewaonjesha simba ladha ya mnofu wa kibinadamu, kwa kuwa wao waweza kwa urahisi kuwalemea watu wasioweza kuendelea kusonga mbele na ambao huanguka chini kwa kunyong’onyea. Hivi majuzi, watu watatu katika Afrika Kusini waliuawa na simba, na mawili ya mashambulio haya yalitukia ndani ya Mbuga Kruger ya Kitaifa. Kwa hiyo, watunza mbuga wameagizwa wawatafute na kuwaua simba wote ambao wamekuwa wala-binadamu.

TISHO LA ZIADA

Jambo jingine limeongezwa kwenye tauni ya sasa ya kutumia dawa za kulevya: uharibifu wa misitu ya mvua. “Kwa kusukumwa na dai la Waamerika na Wanaulaya la kutaka kokeni, Waperu wenye kukuza koka wamekata sehemu kubwa za msitu wa mvua wa Amazon na wanatupa mamilioni ya lita zenye kemikali zenye sumu ndani ya nyanda zayo za juu na vyanzo vya maji,” lasema The New York Times. Kulingana na ripoti hiyo, wakuzaji koka “wamevamia mbuga mbili za kitaifa na misitu miwili ya kitaifa, wakakata sehemu kubwa ya msitu wa mawingu yaliyo rahisi kuharibika uitwao ‘tegemezo la nyika’ na kuharibu eneo likadiriwalo kuwa ekari zaidi ya 500,000 za misitu ya kitropiki.” Sasa jani la koka ndilo zao kubwa zaidi linalositawishwa katika Amazon ya Peru. Katika hekaheka yao ya kukuza kokeni, wakulima wameacha mazoea ya ukulima wao wa tangu zamani ambayo yalizuia mmomonyoko wa udongo wa juu.

KUFANYA MAJANGWA YACHANUE

Katika mpango wa kutaka makuu ya kuweza kujitosheleza katika mazao ya chakula, Saudi Arabia inafanya jangwa lichanue. Katika jangwa la Saudi kumetapakaa mamia ya maeneo mviringo yenye ujani-ubichi, kila moja likiwa ni kufikia ekari 200 kwa ukubwa, kwa kunyunyiziwa maji yapigwayo bomba kutoka mbali kule chini. Lakini gharama ya kugeuza jangwa liwe ardhi yenye mazao si rahisi. Tayari serikali imetumia maelfu ya mamilioni ya dola katika mradi huo. “Kukuza ngano katika Saudi Arabia ni ghali kama kukuza matikiti kwenye ncha ya kaskazini,” lasema The Economist. Na hata ingawa pesa zipatikanazo kwa kutokeza petroliamu huenda zikaonekana kuwa haziishi, sivyo ugavi wa maji ulivyo. Sehemu kubwa ya maji yatumiwayo hutoka kwenye miamba-yavu ya kina kirefu ya maji “ya zamani” yaliyokwama humo ambayo hayawezi kujazwa upya. Yakiendelea kutumiwa kwa kadiri ya ongezeko la sasa la watu, yahofiwa kwamba huenda ile miamba-yavu yenye maji ikakauka katika muda wa miaka 10 hadi 20.

MUSIKITI WA KWANZA KATIKA ROMA

Benito Mussolini, mtawala Mfashisti wa Italia katika siku za Vita ya Ulimwengu ya 2, aripotiwa kuwa alikataa kuruhusu musikiti ujengwe katika Roma, akisema kwamba angeruhusu jambo hilo wakati tu kanisa Katoliki la Kiroma lingeruhusiwa kuwa katika Mecca. Nyakati zimebadilika. Si kwamba tu musikiti mmoja unajengwa kama kilometa tano na nusu kaskazini-mashariki mwa Vatikani bali pia wasemwa na wachora ramani zao kuwa ndio mkubwa zaidi katika Ulaya. “Hata ikiwa sio ulio mkubwa zaidi, na kuna shaka juu ya jambo hilo, huo ndio musikiti wa maana zaidi katika Ulaya,” asema Abdul Qayuum Khan, mkurugenzi wa Kitovu cha Utamaduni wa Kiislamu katika Roma. “Uhakika sahili ni kwamba huo pekee ndio ulio katika moyo wa Ukristo, katika Mecca ya Ukatoliki, ungeweza kusema.” Hata hivyo, yasemwa kwamba msimamo rasmi wa Vatikani wapendelea jambo hilo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki