‘Aibu Yetu Iko Wazi kwa Ulimwengu Mzima’
THE New York Times la Julai 20, 1990, lilikuwa na kichwa kikuu: “Askofu wa Kanada Ajiuzulu Katika Kashfa ya Kingono ya Maaskofu.” Habari yenyewe ilikuwa nini? Ilikuwa ni kisa kingine tena cha makasisi wakishtakiwa kuwatenda vibaya wavulana kingono. Wakati huu kashfa hiyo ilitukia katika mkoa wa Newfoundland, Kanada, na makasisi hao walikuwa Wakatoliki. Ni nini kilichoifanya iwe tofauti?
Times liliripoti: “Askofu Mkuu wa Newfoundland amejiuzulu baada ya mashtaka kwamba viongozi wa Kanisa Katoliki la Roma hawakujali au hawakushughulikia vyema kashfa ya miaka mitatu ya mapadre wa Katoliki ya Roma na wengine iliyohusu madai ya kutendwa vibaya kingono kwa wavulana wa altari, vijana yatima na wengine.” Akishtakiwa kwanza kwa utovu wa adabu katika 1979, padri mmoja alihesabiwa kifungo cha miaka minne gerezani hivi karibuni baada ya kupatikana na hatia ya mashtaka 36!
Kwa kawaida visa hivi hufichwa, na hakuna tendo lo lote la maana la kutia nidhamu ambalo huchukuliwa. Labda padri huhamishwa kwenye parishi nyingine au kazi nyingine ambapo upotovu wa nidhamu huelekea kuanza tena. Katika kisa hiki, askofu mkuu huyo alilazimika kujiuzulu baada ya kusema: “Sisi ni kanisa lenye dhambi. Tuko uchi. Hasira yetu, maumivu yetu, uchungu wetu, aibu yetu iko wazi kwa ulimwengu mzima.”—Linganisha Ufunuo 17:15-18.
Kamati ya uchunguzi ilionyesha kwamba mashtaka yalikuwa yamefanywa kwa muda wa zaidi ya miaka 15, lakini polisi na maofisa wa serikali “hawakutenda kwa njia ya kukata maneno dhidi ya wenye hatia.” Na lililo baya hata zaidi, viongozi wa kanisa hawakutenda kwa njia ya kukata maneno. Walishtakiwa kuwa walishughulika zaidi na mapadri wenye kukosa kuliko wale wenye kutendwa vibaya. Walakini, Biblia ya Kikatoliki inasema nini kuhusu matendo ya kukosa adili kama hayo?
Kuhusu wale waliotenda matendo ya upotovu, New American Bible, St. Joseph Edition, inasema: “Mungu aliwakabidhi katika tamaa yao kwa mazoea machafu; walijihusisha katika mahusiano ya kushusha miili yao,. . .nao wanaume wakaiacha ngono ya asili na wanawake na wakawakiana tamaa. Wanaume wakatenda matendo ya aibu na wanaume. . .Wao wajua amri ya Mungu ya haki kwamba wote wafanyao mambo kama hayo wastahili kifo; walakini hawayafanyi tu bali wayakubali kwa wengine.”—Warumi 1:24-32.
Biblia ya Katoliki inasema kutatukia nini kwa wowote kama hao wasiotubu? “Hamng’amui kwamba wasio watakatifu hawatauridhi ufalme wa Mungu? Msijidanganye wenyewe: hakuna waasherati,. . .hakuna wapotovu wa ngono. . . watauridhi ufalme wa Mungu.” Na bado, kwa watu mmoja mmoja kama hao, kuna nidhamu yenye msingi wa Kibiblia: kutenga na ushirika wa kundi la Kikristo, kama ambavyo Paulo alivyosema: “Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na watu wasio na adili. . . , msishirikiane na mtu yeyote anayeitwa ‘ndugu’ ikiwa ni mkosefu wa adili. . . Ni wazi kwamba msile kamwe na mtu kama huyo. . . . ‘Mwondosheni mtu mwovu miongoni mwenu.’”—1 Wakorintho 5:9-13; 6:9, 10, NAB.