Waliodhulumiwa Kingono na Mapadri Wakiwa Watoto Wateta Waziwazi
“WAKATI wa mwongo uliopita, mapadri wapatao 400 wa Roma Katoliki wameripotiwa kwa wasimamizi wa kanisa na wa serikali kwa ajili ya kudhulumu watoto kingono,” kulingana na U.S.News & World Report. Hivi karibuni, mkutano wa kitaifa wa waokokaji wa dhuluma hiyo ulifanywa karibu na Chicago, Illinois. Wengi walisema waziwazi jinsi walivyodhulumiwa na mapadri wanaovutiwa na watoto kingono.
Lakini gazeti NCR (National Catholic Reporter) lasema kwamba wasemaji walitoa kichwa kingine mara kwa mara muda wote wa kongamano hilo: “Dhuluma ya kwanza ni ya kingono; ya pili iliyo chungu zaidi, ni ya kiakili.” Dhuluma hiyo ya pili hutukia wakati kanisa linapokataa kusikiliza wadhulumiwa, linapokataa kuchukua mashtaka yao kwa uzito, na linapochukua hatua ili tu kulinda mapadri wadhalimu. “Kwa kufaa au kwa kutofaa,” NCR laripoti, “walionyesha kwamba makasisi Wakatoliki kuwa wamo katika kikundi kisichofaa na kilichokosa njia chenye mwelekeo wa kudumisha vyeo na mamlaka kuliko katika kutumikia mahitaji ya wanakanisa.” Wasemaji kadhaa walifanya milinganisho yenye kutisha na yale Mapinduzi Makubwa ya Kidini, yaliyogawanya kanisa kabisa katika karne ya 16.
Kulingana na Richard Sipe, aliyekuwa padri akabadili na kuwa daktari wa akili na stadi wa dhuluma ya kingono na mapadri Wakatoliki, kukana huko kwa kanisa kunafunua “kuhusika kwayo binafsi katika tatizo hilo kwa kina, kwa kujuta, na kwa kujua.” Yeye aliongeza: “Kanisa linajua na limejua kwa muda mrefu mambo mengi kuhusu utendaji wa kingono wa mapadri walo. Limepuuza, likaachilia, likaficha na likadanganya kuhusu mweneo wa utendaji wa kingono wa mapadri walo.”
Basi haishangazi kwamba, waokokaji wengi wa dhuluma hiyo wanashtaki kanisa mahakamani. NCR linamnukuu wakili mmoja aliye mtaalamu wa kesi kama hizo akisema kwamba kuna kesi za mapadri wenye kudhulumu watoto kingono katika kila moja ya dayosisi 188 za kanisa katika United States. Yeye asema kwamba kesi za nje ya mahakama zinalipiwa kiasi kikubwa cha dola kufikia 300,000 za U.S. kila moja. U.S.News & World Report lasema kwamba kesi kama hizo tayari zimegharimu kanisa dola 400,000,000, kiasi ambacho chaweza kufikia dola bilioni 1 kufikia mwaka 2000. Na Vyombo vya Habari vya Kanada viliripoti hivi karibuni kwamba waokokaji 2,000 waliodhulumiwa kingono wakiwa watoto katika makao 22 ya mayatima na wenye akili punguani yanayosimamiwa na kanisa katika Quebec wanashtaki mapadri sita wa kidini walipe dola bilioni 1.4 kwa hasara.
Hata hivyo, kwa kushangaza, wakili wa U.S. aliyetangulia kutajwa, anayewakilisha watu 150 waliodhulumiwa na mapadri katika majimbo 23, asema kwamba hajapata kamwe kuwa na mteja aliyekuwa na hamu ya kwenda mahakamani. Kila mmoja wao alijaribu kwanza kupata haki “katika uchungaji wa kanisa lenyewe.” NCR lafanya mkataa: “Inaonekana kwamba waokokaji huenda mahakamani, si ikiwa hatua ya kwanza, bali ikiwa hatua ya mwisho baada ya mengineyo yote kushindwa.”