Maoni ya Biblia
Sababu kwa Nini Krismasi Si ya Wakristo
‘KRISMASI ni haramu! Yeyote aisherehekeaye au hata kukaa nyumbani bila kwenda kazini Siku ya Krismasi atahukumiwa adhabu!’
Hata liweze kuonekana kuwa jambo la ajabu jinsi gani, kwa hakika jambo hilo lilikuwa sheria huko nyuma katika karne ya 17. Wapuriti walipiga marufuku sherehe hiyo Uingereza. Ni nini lililosababisha msimamo huo imara hivyo dhidi ya Krismasi? Na kwa nini leo kuna mamilioni ambao huhisi kuwa Krismasi si ya Wakristo?
Krismasi Ilitoka Wapi Hasa?
Huenda ukashangaa kujua kwamba Krismasi haikuanzishwa na Yesu Kristo na wala yeye wala wanafunzi wake wa karne ya kwanza hawakuisherehekea. Kwa kweli, hakuna rekodi yoyote ya sherehe ya Krismasi hadi miaka 300 baada ya Kristo kufa.
Watu wengi walioishi wakati huo waliabudu jua, kwa maana walihisi uhitaji wao mkubwa wa kulitegemea kwa mzunguko walo wa kila mwaka. Sherehe zenye madoido ziliandamana na ibada ya jua katika Ulaya, Misri, na Uajemi. Jambo kuu la sherehe hizo lilikuwa ni return of light (kurudi kwa nuru). Kwa kuwa jua lilikuwa linaonekana likiwa dhaifu wakati wa kipupwe, liliombwa lirudi kutoka ‘kutangatanga mbali.’ Sherehe zilitia ndani kufurahia, kufanya karamu, kucheza dansi, kupamba nyumba kwa taa na madoido, na kupeana zawadi. Je! unayafahamu mambo hayo?
Waabudu jua waliamini kwamba mbao isiyochomwa ya gogo kubwa la sherehe ambalo huchomwa siku ya Krismasi ilikuwa na nguvu za kimizungu, kwamba mioto ingepatia mungu-jua nguvu na kumrudisha kwenye uhai, kwamba nyumba zilizopambwa kwa mimea ya kijani kibichi zingeogopesha mashetani, kwamba mti holi ungeabudiwa kuwa ahadi ya kurudi kwa jua, na kwamba matawi ya mti dhiki (mistletoe) yangeleta bahati nzuri yakivaliwa kama hirizi. Vitu hivyo vina uhusiano na sherehe gani leo?
Desemba ulikuwa mwezi mkuu wa sherehe katika Roma ya kipagani zamani kabla Krismasi haijaanzishwa huko. Sikukuu ya saturnalia ya juma nzima (iliyowekwa wakfu kwa ajili ya Saturn, mungu wa ukulima) na ile Dies Natalis Solis Invicti (Siku ya kuzaliwa ya Jua Lisiloshindwa) ilifanyika wakati huo. Pia Desemba 25 ilijulikana kuwa siku ya kuzaliwa ya Mithrasi, mungu wa Uajemi wa nuru.
Ni Kuwafanya Wapagani Wawe Wakristo?
Katika jitihada za kubadilisha wapagani hao, kulikuwa na kuchanganywa kusiko kwa kimaandiko kwa itikadi za Kikristo na za kipagani, na hivyo kanisa likachagua tarehe ya Krismasi ambayo ililingana na sherehe ya maana zaidi ya kipagani. Na vipi juu ya desturi za Krismasi? Encyclopedia of Religion and Ethics yakubali kuwa karibu sherehe zote za desturi za Krismasi “si desturi halisi za Kikristo, bali desturi za kilimwengu ambazo zimeingizwa ndani au kukubaliwa na Kanisa.” Inahisiwa kwamba labda kuzipa desturi hizi mtazamo wa Kikristo ungefanya wale waliokuwa wakizishiriki wawe Wakristo.
Hata hivyo, badala ya kuongoa Upagani uwe wa Kikristo, desturi hizo zilifanya Ukristo uwe wa kipagani. Katika kipindi cha miaka ya 1600, Wapuriti walisumbuka juu ya asili ya kipagani iliyo wazi ya Krismasi hivi kwamba sikukuu hiyo ilikuwa haramu katika Uingereza na baadhi ya nchi koloni za Amerika. Adhabu zilitolewa kwa ajili ya kusherehekea Krismasi au tu kukaa nyumbani bila kwenda kazini Siku ya Krismasi. Katika New England (U.S.), haikuwa hadi 1856 ndipo Krismasi ilitambuliwa kisheria.
Lakini kuna jambo moja kuhusu Krismasi ambalo ni la maana sana kuliko vile kanisa, wapagani, au Wapuriti walivyoliona wakati wa zamani. Jambo la maana la msingi kwa Wakristo wa kweli ni . . .
Yesu Kristo Huionaje Krismasi?
Kama sherehe ingefanywa kwa heshima yako, je! kibali chako kwa asili yake hakingekuwa cha maana? Kwa hivyo, twafanya vema kuuliza: Je! Biblia inaonyesha jinsi Yesu huyaona mapokeo yaliyojaa upagani?
Yesu aliwalaumu viongozi wa kidini waliokana ibada safi ili kupata waongofu. Yeye aliwaambia viongozi hao hivi: “Mna [safiri] katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja awe mwongofu, halafu mnamfanya awe wa uharibifu mara mbili kuliko ninyi wenyewe.”—Mathayo 23:15, Phillips.
Wongofu haukutimizwa kwa kuchanganya itikadi za kipagani na za Kikristo. Paulo, mtume wa Yesu, aliwaandikia Wakristo walioishi Korintho hivi: “Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana [Yehova, NW] na meza ya mashetani.” (1 Wakorintho 10:21) Na katika waraka wake wa pili kwao, Paulo aliongezea: “Msifungamanishwe na wasioamini na kujaribu kufanya kazi pamoja nao. . . . Kwaweza kuwa na upatani jinsi gani kati ya Kristo na Ibilisi?”—2 Wakorintho 6:14, 15, Phillips.
Ikiwa mama anayedhamiria angemwona mtoto wake akiokota peremende kwenye mtaro wenye maji machafu, angesisitiza aitupe mara moja. Lile wazo la kuila—hata kuishika—lamchukiza. Ingawa Krismasi ni tamu kwa wengi, imetolewa mahali penye kuchukiza. Kukirihi kwa Yesu kwalingana na kule kwa nabii Isaya, ambaye aliwasihi waabudu wa kweli wa siku zake hivi: “Nendeni zenu, nendeni zenu, tokeni huko, msiguse kitu kichafu.”—Isaya 52:11.
Kwa hivyo, Wakristo wa kweli leo hawasherehekei Krismasi. Ingawa msimamo wao huenda ukaonekana kuwa wa ajabu kwa wengine, wanayaona mapokeo kama Yesu alivyoyaona. Alipoulizwa: “Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee?” alijibu: “Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?” Na akaongezea: “Mkalitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu.”—Mathayo 15:2, 3, 6.
Wakristo wa kweli leo wanaonyesha umoja pamoja na Yesu kwa kuwa katika “dini iliyo safi na isiyo na taka,” isiyochafuliwa na mapokeo ya kipagani ya wanadamu.—Yakobo 1:27.
[Blabu katika ukurasa wa 13]
“Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?”—Mathayo 15:3