Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 1/22 kur. 18-21
  • Hata Pafu la Chuma Halikumzuia Kuhubiri

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Hata Pafu la Chuma Halikumzuia Kuhubiri
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Awa Mmoja wa Mashahidi wa Yehova
  • Upasuaji Mwingi Lakini Bila Damu
  • Waambie Unawapenda
    Masimulizi ya Mashahidi wa Yehova
  • Mwishowe Mbegu Ilichipuka
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • “Sijawahi Kamwe Kuhisi Upendo Kama Huu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • “Nimeshika Imani”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 1/22 kur. 18-21

Hata Pafu la Chuma Halikumzuia Kuhubiri

Nyakati nyingine inataka uhodari ili kuendelea kuishi. Hii ni hadithi ya mmoja aliyekuwa na uhodari kama huo. Jina lake ni Laurel Nisbet.

AKIWA amezaliwa 1912 katika Los Angeles, Laurel alikuwa mwanamke kijana mwenye kujawa na nguvu aliyependa maisha na familia yake. Akiwa na mume na watoto wawili wa kutunza ilikuwa kazi rahisi kwake chini ya hali za kawaida, lakini katika 1948 upendo wake kwa uhai ulitahiniwa karibu kupita vile iwezavyo kueleweka. Aliambukiwa na ile virasi iletayo ugonjwa wa kupooza.

Baada ya kupatwa na dalili kama za homa kwa siku kadhaa, hatimaye alishindwa kujongea. Mume wake alimpeleka kwenye hospitali ya wilaya. Humo alikuwa miongoni mwa wengi waliokuwa wameshikwa na ugonjwa wa kupooza. Hofu zilimjaa wakati hali zenye msongamano zilipomfanya alazimike kulala sakafuni kijiani na kungojea pafu la chuma. Kila mpumuo ulikuwa jitihada kubwa mno. Pafu la chuma lilipopatikana hatimaye, alitulizwa alipowekwa ndani yalo. Sasa angeweza kupumua pumzi hiyo ya uhai yenye thamani aliyokaribia kupoteza!

Mapafu ya chuma (mashine) yalibuniwa kusaidia watu ambao misuli ya kifua chao ilikuwa imepooza. Mwanzoni ilidhaniwa kwamba hiyo ingekuwa hatua ya muda huku misuli ya mgonjwa ikipata nafuu, kumwezesha kupumua yeye mwenyewe. Lakini kwa mshangao wa Laurel na kwa hofu kuu ya ulimwengu, mashine hizo za chuma za kupumulia zikawa makao ya kudumu ya wengi waliopatwa na ugonjwa wa kupooza. Laurel aliendelea kuishi akilala chali kwa miaka 37 akiwa amefungiwa ndani ya pafu la chuma. Anashikilia rekodi ya ulimwengu ya kuwa mgonjwa wa kupooza aliyeishi muda mrefu kupita wote akiwa amefungiwa ndani ya pafu la chuma.

Je! hiyo ndiyo sababu pekee akapata kujulikana sana? Sivyo kabisa. Laurel alikuwa mwanamke kijana katika miaka yake ya 30 alipowekwa ndani ya lile pafu. Alikuwa na watoto wawili wa kulea na mume wa kutunza. Mwanzoni alihuzunika sana sana. Halafu, baada ya siku moja ya kujihurumia, akaamua kufanya vizuri awezavyo katika hali yake. Hatimaye, mumewe akamleta nyumbani, naye akaanza kujenga upya maisha yake. Alijifunza kutunza nyumba yake, kutoka mlemle ndani ya kifua cha chuma.

Sasa, lazima uwazie hiyo ilikuwaje. Kichwa chake tu ndicho kilichotokeza nje ya mashine hiyo ya kupumulia. Ukosi wa plastiki na ufito wa chuma, uliokaza ukosi kwenye mtulinga, vilitumiwa kuweka silinda katika hali ya kutoweza kuingiwa na hewa. Mivukuto chini ya tanki ilibadili msongo wa hewa ndani ya tanki. Mara 15 hivi kwa dakika, mivukuto hiyo, ikitenda kama bomba, iliondoa hewa kutoka tanki. Hilo lilifanya kifua cha mgonjwa kuinuka hewa ilipoingia kupitia pua au kinywa. Mivukuto ilipofinyana na hewa kupulizwa ndani kwa nguvu, msongo ulifanyizwa katika kifua naye mgonjwa alitoa pumzi nje. Hivyo waweza kuona kwa nini ilikuwa lazima ukosi usiweze kuingiza hewa kwa kuwa mabadiliko ya msongo wa hewa yalifanya lile pafu la chuma lifanye kazi kwa mafanikio. Laurel angeweza kujongeza kichwa chake, na basi. Alikuwa amepooza kabisa tokea shingo kuteremka. Alitazama mazingira yake kutoka kwa kioo kilichowekwa juu ya mashine yake ya kupumulia kilichoonyesha kioo kingine kilichowekwa kwenye ukuta uliokuwa ule upande mwingine. Hilo lilimwezesha kuona mlango wake wa mbele na yeyote aliyeukaribia.

Awa Mmoja wa Mashahidi wa Yehova

Siku moja alipata mgeni, Del Kuring, mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Alikuja moja kwa moja ndani ya sebule ya Laurel na kuanza kumfundisha zile kweli nzuri sana za Biblia. Laurel alistahi Neno la Mungu naye alisikiliza kwa akili na moyo uliofunguka. Funzo la Biblia likaanzishwa, ambalo liliongoza kwenye wakfu wake kwa Mungu katika 1965 akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Sasa alikuwa na sababu hata zaidi ya kuishi. Siku moja angeweza kutembea tena duniani na kuonea shangwe Paradiso ambayo Mungu alikusudia ainabinadamu iwe nayo! Alihisi shangwe kama nini, pia, binti yake Kay alipokubali imani yake mpya.

Huenda ukauliza, ‘Namna gani ubatizo wake?’ Eh, hangeweza kubatizwa. Kwa kutoweza kupumua yeye mwenyewe, uzamisho katika maji haungewezekana. Hakuweza kamwe kwenda kwenye Jumba la Ufalme. Hakuweza kamwe kuhudhuria mkusanyiko. Hakuweza kamwe kuona binti yake akibatizwa. Lakini alitimiza mengi katika utumishi wake kwa Yehova kuliko Wakristo wengi wasio na kizuizi.

Waona, Laurel alikuwa mhubiri wa habari njema. Wakati wa miaka 37 ya kizuizi chake aliweza kusaidia watu 17 waje kwenye maarifa sahihi ya kweli ya Biblia. Alifanyaje hivyo? Bila shaka, hangeweza kwenda mlango kwa mlango kama vile Mashahidi wengi walivyo na pendeleo la kufanya. Lakini angeweza kutolea ushahidi wale wengi waliomhudumia. Nilikuwa na pendeleo la kuwa mmoja wao.

Nilikuwa mwanafunzi wa shule ya wauguzi katika 1972 nami nikaanza kumfanyia kazi nikiwa mhudumu wake. Laurel nami tulikuwa na wakati mwishoni mwa zamu yangu ya kazi kuongea na kupata kujuana. Siku moja akasema: “Sasa, ningependa unisomee.” Nilipokubali, aliniagiza nichukue kitabu kidogo cha buluu chenye kichwa Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele. Nilimuuliza nianze wapi, naye akasema tu, “anza na sura 1.” Hivyo funzo la Biblia likaanza, nami pia nikawa Shahidi wa Yehova aliye wakfu.

Mashine ya Laurel ya kumwezesha kupumua ilionekana kupitia dirisha kubwa lililokuwa upande wa mbele wa nyumba yake. Aliishi kwenye barabara yenye shughuli nyingi, hivyo yeyote mjini La Crescenta aliyepitia hapo angeweza kuona mashine hiyo ya kupumulia. Hilo lilitokeza huruma na udadisi mwingi kwa wapitaji, na mara nyingi watu wasiomjua walikuja nyumbani kumsalimu. Sikuzote yeye alifurahia kuonana na watu naye alipata marafiki wengi kwa njia hiyo, na alikuwa akiwatolea ushahidi watu hao. Kutoa ushahidi kwake kwa ujasiri kwa ajili ya Yehova na tumaini lake kwa wakati ujao vilivutia watu na kutoa ushahidi mzuri kwa ajili ya jina la Yehova.

Laurel alilala kidogo sana. Ilikuwa vigumu kuchoka kama sisi wengine, kwa kuwa yeye hangeweza kujongea. Kelele na mvuto wa daima wa mivukuto chini ya mashine yake ya kupumulia ilimweka katika hali ya kukaa ameamka. Alifanya nini na saa hizo? Aliongea na Baba yake wa kimbingu, akiwasiliana naye kwa ukamili katika sala yenye kuhisiwa moyoni. Mimi nina hakika alisali apate nguvu na uvumilivu, lakini mara nyingi zaidi alikuwa akisali kwa ajili ya ndugu na dada zake Wakristo. Alikuwa na huruma nyingi kwa ajili ya wengine naye alimshukuru Yehova kila siku kwa ajili ya baraka zake.

Mwakilishi asafiriye wa Mashahidi wa Yehova alipokuja kwenye eneo lake, alikuwa sikuzote akimtembelea Laurel. Wengi wa wanaume hao walikuwa wakisema kwamba baada ya kuwa na Laurel, wao ndio waliokuwa wamejengwa! Hiyo ilikuwa njia yake. Sikuzote yeye alikuwa mwenye mwelekeo wenye uhakika na wenye shangwe naye alitafuta kila fursa ya kutoa ushahidi kwa ajili ya kweli

Laurel alipatwa na mambo mengi yenye kugutusha, mengi mno kuweza kusimulia. Wakati mmoja ilikuwa lazima apate upasuaji wa dharura ili kuondolewa kibole, nalo gari kutoka hospitali ya wilaya likaja kumchukua. Kwa sababu kibole chake kilikuwa kimepasuka, aliviringishwa kwa haraka kuingizwa katika gari na kukimbizwa hospitalini, ambamo daktari alilazimika kufanya upasuaji huo bila dawa ya nusukaputi. Waona, katika miaka ya 1950, hawakujua jinsi ya kumpa mgonjwa wa pafu la chuma dawa ya nusukaputi ya ujumla.

Upasuaji Mwingi Lakini Bila Damu

Laurel alivumilia kansa, upasuaji mwingi mkubwa, na magonjwa ya ngozi yenye kusedeka. Lilikuwa jambo lenye kumuudhi sana wakati alipotaka kujikuna naye asiweze na ikawa lazima mhudumu wake amfanyie hivyo. Hata ingawa misuli yake ilikuwa imepooza, alikuwa na hisi mwili wake wote. Hilo lilimfaa sana, kwa kuwa lilimzuia kupata vidonda visababishwavyo na kuwa kitandani daima. Alikuwa mwenye kudhamiria sana juu ya utunzaji wa ngozi yake. Ilihitaji watu wanne kati yetu kumgeuza na kumuogesha kikamili mara moja kwa juma. Hilo lilikuwa gumu kwa Laurel kuvumilia, lakini aliliweza kama vile alivyoweza kila jambo jinginelo maishani mwake.

Nyakati hizo za kuwa pamoja naye zilikuwa furaha na zenye kupendeza ijapokuwa kazi ngumu. Tulipokuwa tukigeuza ukosi juu kuzunguka shingo yake ili kudumu juma jingine, kufanya kidude hicho kikazike kadiri iwezekanavyo ili kisiingize hewa, Laurel alikuwa akikereza meno na kusema: “Ubuni wa Ibilisi mwenyewe!” Ndiyo, Laurel alijua mahali pa kuweka lawama kwa hali mbaya hivyo. Ilianza na Shetani, aliyeshawishi wanadamu wa kwanza wampe Yehova kisogo, na hivyo kuleta dhambi, ugonjwa, na kifo kwa ainabinadamu.

Laurel aweza kuwa alikuwa amepooza kimwili lakini kwa wazi si kiroho. Alitumia kila fursa kufundisha watu juu ya tumaini lake la Paradiso. Hata karibu na mwisho wa uhai wake, alipokuwa akikabili upasuaji wa dharura, aliweza kuchukua msimamo kwa ajili ya uadilifu. Ilikuwa katika 1985, naye Laurel alikuwa na umri wa miaka 72. Upasuaji wake ulipokaribia, daktari wake aliingia na kumwambia kwamba hawangeweza kufanya upasuaji bila damu. Binti yake Kay alieleza matakwa ya mama yake ya kujiepusha na damu kwa sababu wakati huo Laurel alikuwa dhaifu sana asiweze kuongea. Alikuwa na mirija ndani ya koo yake naye angeweza kunong’oneza tu. Mwili wake wote ulikuwa umetiwa sumu na kinyezi kilichozuiwa matumboni mwake, naye alionekana karibu kama amekufa.

Lakini daktari alisema kwamba alitaka kusikia msimamo huo juu ya damu kutoka kwa Laurel. Tulimnong’onezea sikioni mwake: “Laurel, wahitaji kumwambia daktari wewe mwenyewe juu ya damu.” Ghafula, kwa mshangao wangu, macho yake yalifumbuka wazi, sauti yake ikawa kubwa, naye akanena na daktari juu ya msimamo wake juu ya damu. Alitaja maandiko, akieleza kwamba Mashahidi wa Yehova huhisi kwamba kukubali kutiwa damu mishipani kungekuwa dhambi dhidi ya Mungu. Sitasahau kamwe alilofuata kusema: “Daktari, ukiokoa maisha yangu nami niamke na kuona kwamba umeuhalifu mwili wangu, nitatamani ni afadhali kama ningekuwa mfu, nawe utakuwa umefanya kazi bure.” Kusikia hilo, daktari hakusadikishwa tu juu ya msimamo wake bali alishangazwa na nguvu zake, naye akakubali kufuata matakwa yake.

Laurel alifanyiwa upasuaji wa saa nne ndefu uliofanikiwa kwa kadiri fulani. Baada ya upasuaji, madaktari walimwondoa ndani ya pafu kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 37 na kumweka kitandani hospitalini. Walimshikisha kwenye mashine ya ki-siku-hizi ya kupumlia akitumia koo yake iliyopasuliwa. Hiyo ndiyo iliyokuwa hofu yake kuu kupita zote. Sasa, kwa sababu mashine hiyo ya kupumlia ya ki-siku-hizi ilishikishwa kwenye mrija kupitia koo lake lililopasuliwa, hakuweza kunena. Alishikwa na hofu kuu alipohisi kwamba hakuwa akipata hewa ya kutosha. Alikufa siku tatu baadaye, Agosti 17, 1985, kutokana na matatanisho yaliyohusiana na ule upasuaji.

Nakumbuka maneno yake ya mwisho kwangu, labda ndiyo maneno ya mwisho aliyonena, kabla tu ya kuwekwa chini ya nusukaputi. Alisema hivi: “Chris, usiniache kamwe.” Sasa ninapotazamia mwisho wa huu mfumo wa mambo wa kale na ufufuo ujao, nawazia siku ambapo naweza kumkumbatia rafiki yangu Laurel Nisbet na kusema: “Mimi hapa. Sikukuacha kamwe.”—Kama ilivyosimuliwa na Christine Tabery.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki