Kuutazama Ulimwengu
Tairi Zinazokufuru?
Kampuni kubwa ya mpira katika Yokohama, Japan, iliacha kutokeza mfululizo wa tairi za magari kwa sababu Waislamu waliudhiwa nazo. Waislamu walilalamika kwamba alama zilizo chini ya tairi zilifanana na neno la Kiarabu linalomaanisha “Allah.” Gazeti Asahi Evening News lilisema kwamba kampuni hiyo ilikuwa imeomba msamaha kwa kutojua Kiislamu na ikaeleza kwamba kompyuta ilibuni alama hizo kwa ajili ya usalama bora zaidi wa kuendesha gari. Haikukusudia kuudhi au kumkufuru Allah. Kampuni hiyo inachukua tena au kubadilisha tairi katika nchi za Waislamu.
Kueneza Evanjeli “Kupya” na Wakatoliki
Kanisa la Katoliki ya Roma linaweka mkazo mpya juu ya kueneza evanjeli, yaripoti New York Newsday. Maofisa wa Kanisa wana wasiwasi juu ya kupoteza idadi kubwa ya Wakatoliki wenye kuhama kwa vikundi vinginevyo vya kidini. Hivyo, Papa John Paul 2 ametoa wito wa “kueneza evanjeli kupya” na amefanyiza shirika, Evangelization 2000, kwa kusudi hilo hususa. “Jitihada hizo zinatia ndani hata kueneza evanjeli mlango kwa mlango, njia ambayo kwa kawaida hushirikishwa na Mashahidi wa Yehova na vikundi vingine vya Kikristo,” yaripoti Newsday.
Uhalifu wa Australia Wenye Gharama Kubwa
Jumla ya gharama ya kila mwaka ya uhalifu katika Australia imekadiriwa kuwa dola 1,600 za Australia, kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto nchini, kulingana na Taasisi ya Uhalifu ya Australia. Jumla ya gharama ya kila mwaka ni dola bilioni 27 za Australia, inayowakilisha asilimia 2.7 ya jumla ya mazao ya taifa. Kiasi hicho chenye kugutusha huhesabiwaje? Gazeti The Australian lanukuu tarakimu kutoka kwa ripoti ya taasisi hiyo. Madai bandia ya bima ya magari yanaongezeka, na jumla ya gharama ya aina zote za hila sasa inafikia dola bilioni 13 za Australia kila mwaka; gharama za mashambulizi ni karibu dola milioni 300 za Australia kila mwaka. Gharama ya kila mwaka ya wawekaji sheria imefikia dola bilioni 2.5 za Australia, na gharama ya kuweka mfungwa mmoja tu gerezani kwa mwaka mmoja sasa imepanda kuwa dola 50,000 za Australia.
“Jiji Lisilo na Nzi”
Wenyeji wa Beijing, Uchina, wametangaza vita kamili dhidi ya nzi, laripoti International Herald Tribune. “Lengo letu ni kufanyiza jiji lisilo na nzi,” akasema ofisa mkuu wa afya. “Lakini hatutawaua tu nzi. Tunataka tufanyize majiji safi.” Katika kampeni ya “kutendesha kazi umati,” raia waliweka vibandiko na kugawanya makaratasi milioni mbili wakitangaza kampeni hiyo. Wakati wa “juma la mashambulizi” la pekee lililofuata, jiji hilo liligawanya karibu tani 15 za viua-wadudu na vipiga-nzi 200,000. Katika juma jingine la mashambulizi mwezi uliofuata, vikundi 1,000 vya wazee kwa watoto walipigana na nzi kwa kilo 8,000 za sumu. Katika Juni sehemu fulani za Beijing zilijaa nzi wafikao 33 kwa kila chumba. Lengo ni kupunguza wingi wa nzi hadi wawe wawili kwa kila vyumba 100.
Jumuiya ya Ulaya ya Walio Maskini?
Huku asilimia 18 ya mapato yote ya ulimwengu yakigawanywa kati ya watu wa Ulaya walio asilimia 6 ya watu wote duniani, Jumuiya ya Ulaya ingeonekana kuwa yenye amani na ufanisi. Na bado, Le Monde Diplomatique, gazeti la Paris, laripoti kwamba miongoni mwa mataifa 12 ya Jumuiya ya Ulaya, sasa kuna watu milioni 53 hivi wanaoishi chini ya kiwango cha umaskini. Katika Ugiriki, Ailandi, Ureno, na Uhispania, maskini hufanyiza kati ya asilimia 20 hadi 25 ya idadi ya watu, na idadi yao inaongezeka upesi katika Uingereza, Italia, na Uholanzi. Ukosefu wa kazi ya kuajiriwa unaoongezeka umekuwa kisababishi kikuu cha idadi inayokua ya maskini. Miongoni mwa watu milioni 13 wasio na kazi katika Jumuiya, zaidi ya nusu yao hawajaajiriwa kwa muda mrefu.
Upande Usiopendeza wa United Church
“Wengi wetu tuna dhana isiyo ya kiakili kidogo kwamba mambo kama vile kutendwa vibaya kingono hayawezi kutukia kanisani na hayawezi kamwe kufanywa na makasisi,” akasema mhudumu wa United Church Sylvia Hamilton. Hata hivyo, Hamilton adokeza kwamba “hilo ni tatizo kubwa.” Kulingana na Toronto Star la Kanada, kutendwa vibaya kingono “kuanzia mzaha hadi ngono ya kulazimishwa—kumo sana kanisani kama vile kulivyo katika jumuiya kwa ujumla, ikiwa si zaidi yayo.” Peter Lougheed, mshiriki mtendaji wa United Church alikiri kwamba “kanisa ni mahali pasipo na usalama kwa mwenda kanisani na kwa wanawake kuliko katika mahali pa kazi.” Ripoti ya Star yaongeza: “Baada ya miaka ya kukana na kuficha makosa, tatizo hilo sasa linabubujika tu juu kama mapovu katika kidimbwi.”
Risasi (Madini) Yenye Thamani Kubwa Sana
Shehena ya vipande vya risasi vilivyopatikana katika magofu ya meli ya Roma iliyozama katika pwani ya Sardinia miaka elfu mbili iliyopita “ina thamani kubwa sana,” lasema gazeti la Italia Il Messaggero. Katika Roma ya kale, inayofikiriwa kuwa mahali risasi hiyo ilikusudiwa kupe-lekwa mwanzoni, madini hiyo ingelikuwa yenye thamani katika “kutengeneza mirija, mifereji iliyolehemiwa, na mawe ya kupimia.” Lakini wanasayansi wanaona uvumbuzi huo kuwa wenye thamani zaidi. Kwa kuwa vipande hivyo vilikuwa katika sakafu ya bahari, vikilindwa na matokeo ya mialianga na “tandiko kubwa la mchanga,” muda umeondoa mnururisho wote. Risasi hiyo iliyo ngumu kupatikana mahali penginepo, ni yenye thamani kubwa kwa wafizikia watafiti kwa ajili ya kinga zenye kulinda ambazo hazitaathiri vipimo vyenye uangalifu wanavyofanya katika maabara yao.
Umoja wa Kikristo?
Mnamo Agosti 1992, WCC (Baraza la Makanisa Ulimwenguni) liliteua Dakt. Konrad Raiser kuwa katibu mkuu mpya walo. Dakt. Raiser alichukua mahali pa Emilio Castro, aliyekuwa mkuu wa shirika hilo tangu 1984. WCC, lililofanyizwa na makanisa zaidi ya 300 ya Kiprotestanti, Kianglikana, na ya Mashariki, lilifanyizwa katika 1948 katika jitihada ya kuleta umoja zaidi kati ya makanisa. Likieleza juu ya kushindwa kwalo kuleta umoja huo, gazeti la Paris Le Monde lilisema: “Mazungumzo ya mafundisho yamekoma, na kuhusika katika siasa kumegawanya WCC. Kuhusika kwalo katika Afrika Kusini dhidi ya serikali ya ubaguzi wa rangi, kuuzwa kwa silaha, na [msimamo walo wa kupendelea] nadharia ya uhuru hakujaleta upatano . . . na kumeharibu sifa yalo. Likijitia zaidi na zaidi katika upigaji ubwana, WCC huamsha udadisi kidogo tu, au, halitambuliwi.”
Kuajiriwa kwa Watoto
“Miaka ya 80 haikuwafaa watoto na wabalehe Wabrazili, kulingana na mkataa wa Shirika la Brazili la Taasisi ya Jiografia na Tarakimu,” laripoti Jornal da Tarde. Uchunguzi ulifunua kwamba, kati ya watoto milioni 59.7, milioni 32 walikuwa wa familia ambazo mapato yao ya kila mwaka yalikuwa chini ya nusu ya kiwango cha chini cha mshahara cha karibu dola 40. Badala ya kwenda shule, asilimia 17.2 ya watoto Wabrazili wa kati ya miaka 10 na 14—karibu milioni kumi—hufanya kazi ya kuajiriwa ili kusaidia familia zao zinazoteseka. Tokeo? Msosholojia Rosa Ribeiro alisema: “Ni umaskini unaoenea na unaodumu. Bila masomo yafaayo, mtoto hana fursa ya kubadili hali yake ya kijamii.”
Dawa za Kulevya Katika Misri ya Kale
“Wanasayansi katika Vyuo Vikuu vya Munich na Ulm [nchini Ujerumani] wamevumbua dalili za hashishi, kokeni, na nikotini katika maiti za Wamisri,” yaripoti Frankfurter Allgemeine Zeitung. Watafiti walichunguza sampuli za mifupa, nywele, na tishu zilizotolewa katika maiti kadha za kati ya 1070 K.W.K. na 395 W.K. Mavumbuzi hayo ya kisayansi yatuambia nini kuhusu maisha katika Misri ya kale? “Kwa wazi Wamisri walitumia dawa za kulevya ili hata kutuliza watoto wanaolia,” gazeti hilo lasema. Wanasayansi hao wajuaje? Funjo moja laeleza juu ya mchanganyiko wa kinyesi cha nzi na mbegu za mpopi kuwa kitulizo chenye nguvu.
Fito za Vinyozi Zenye Hatia ya Damu
Fito zenye alama nyekundu na nyeupe hutambulisha vibanda vya vinyozi. Kwa nini? Kwa sababu wakati wa Enzi za Kati, vinyozi hawakukata nywele na ndevu tu, bali pia walingoa meno na kuvujisha damu ya watu kikiwa kiponyi cha magonjwa yote. “Wakati wa kuvujwa damu,” laripoti The Toronto Star, “Ilikuwa desturi kwa mgonjwa kusindilia ufito mmoja kwa nguvu juu ya mkono mmoja ili mishipa ivimbe na damu nyingi itoke.” Ili kupunguza kuonekana kwa alama za damu kwenye ufito, ulipakwa rangi nyekundu. “Ulipokuwa hutumiwi, uliangikwa nje ya kibanda ukiwa tangazo, ukiwa umefungwa kwa bandeji nyeupe iliyotumiwa kufunga mikono iliyovujwa damu.” lasema Star. Vinyozi walirithi alama ya biashara ya ufito huo wakati kazi hiyo ilipogawanywa kati ya wapasuaji na vinyozi wakati wa utawala wa Henry wa 8, mfalme wa Uingereza katika karne ya 16.
Anga Moja la Ulaya?
“Katika muda wa miaka minane ijayo, usafiri wa ndege katika Ulaya utafikia hali ya kutotenda kazi kabisa,” lasema La Repubblica. Katika Miaka miwili iliyopita, ndege zinazosafiri zimeongezeka kwa asilimia 8. Na bado, kuchelewa kunakoletwa na matatizo ya kudhibiti safari za ndege “kumeongezeka kwa asilimia 62,” na karibu robo ya ndege zote huwasili zikiwa zimechelewa dakika 24. Msimamizi wa Shirika la Ndege za Ulaya, Giovanni Bisignani asema kwamba kukosekana kwa mfumo mkuu wa usimamizi wa anga la Ulaya ndiko kumesababisha msongamano huo. Kwa sasa, kuna vituo 54 vya usimamizi wa ndege, vinavyotumia mifumo 31 tofauti. Utatuzi usipopatikana, kuwasili kwa wakati barabara kutakuwa ni “ndoto” tu.
Matokeo ya Sinema Zenye Jeuri
Katika mahoji na gazeti la Brazili Veja, mkurugenzi wa filamu Steven Spielberg aliulizwa kuhusu tokeo la jeuri katika vitumbuizo juu ya watazamaji. Spielberg alisema: “Kutazama jeuri katika sinema au katika programu za TV huchochea zaidi watazamaji waige yale wanayoona kuliko vile yangeonwa kihalisi au katika habari za TV. Katika sinema, jeuri huonyeshwa kwa mwangaza ufaao, mandhari zenye kutokeza, na katika mwendo wa polepole, ikifanywa iwe ya mahaba zaidi. Hata hivyo, katika habari, umma unaweza kuona vizuri zaidi jinsi jeuri inavyoweza kuhofisha sana, na inatumiwa kwa makusudi yasiyopatikana katika sinema.” Spielberg aongeza kwamba kufikia sasa hajaruhusu mwanawe mchanga atazame baadhi ya sinema zake mashuhuri (Jaws, mfululizo wa Indiana Jones) kwa sababu ya umwagaji damu na jeuri inayoonyeshwa.