Kuutazama Ulimwengu
Ole za Kiuchumi
“Kwa mara ya kwanza tangu ule mshuko wa thamani ya fedha katika miaka ya 1930, nchi zenye viwanda, na pia nchi zinazositawi, zakabili ukosefu wa daima wa kazi za kuajiriwa,” asema Michel Hansenne, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO). Kulingana na Jornal da Tarde: “Asilimia 30 ya wafanyakazi wa ulimwengu—karibu watu milioni 820—ni wasioajiriwa kazi au walioajiriwa kazi ya hali ya chini.” Kuhusu ripoti ya ILO juu ya Amerika ya Latini, Jornal do Brasil laeleza hivi: “Kumekuwako ongezeko la kugutusha katika idadi ya wale waitwao wafanyakazi ‘wa wasiwasi’—wafanyakazi wa muda, wasiolipwa vizuri—katika kuvuna na kutayarisha kahawa, kukata miwa, kuvuna pamba, matunda na mboga za kupeleka nchi za nje.”
Utumizi wa Mabavu Shuleni
Mvulana aliyefukuzwa katika Koleji Ndogo ya Kobe ya Ufundi wa Manispaa katika Japani anatoa ombi rasmi apewe haki yake ya kuelimishwa. Kwa sababu ya dhamiri yake ya kidini akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, yeye hakushiriki mazoezi ya kendo (mchezo wa Kijapani wa kushindana kwa panga zisizo kali) zilizofunzwa kuwa sehemu ya elimu ya kuzoeza mwili. Shule ilimfukuza ingawa alikuwa mwanafunzi wa kiwango cha juu ijapokuwa alikadiriwa kuwa wa hali ya chini kuhusu elimu ya kuzoeza mwili. “Ni kinyume kabisa cha ‘kufikiri kuzuri’ shuleni,” akasema Profesa Tetsuo Shimomura wa Chuo Kikuu cha Tsukuba katika Yomiuri Shimbun, “kufukuza mwanafunzi ili kumtia nidhamu kwa sababu ya kutofanikiwa sana masomoni na hali yeye hana tatizo jingine, kwa sababu tu amepungukiwa kupita somo fulani hususa kwa alama chache za mtihani.” Aliomba kuwe na kupindikana kisha akasema: “Jambo la kuhangaisha sana katika kisa hiki ni kwamba shule ingali na maelekeo yaliyokolea sana ya kutumia mabavu.”
“Makosa Makubwa ya Kiadili Katika Historia”
“Rekodi ya Vatikani kuhusiana na lile Teketezo la Umati ni mojapo makosa makubwa ya kiadili katika historia—kosa ambalo Kanisa Katoliki halijapona bado kutokana nalo,” aandika mwandika-safu James Carroll katika The Boston Globe. Kutegemeza wazo lake, anaorodhesha habari za kihistoria zinazofuata: “1929—Yale Mapatano ya Laterani kati ya Mussolini na Pius 11 yaipa Vatikani uhuru na fedha, tena yampa Mussolini fahari ihitajiwayo. [1933]—Vatikani yatia sahihi Mkataba pamoja na Hitler, mafanikio yake ya kwanza ya kimataifa. . . . 1935—Mussolini avamia Abyssinia. Maaskofu Wakatoliki wabariki vikosi vya Kiitalia . . . 1939—Mussolini aamrisha haki za Wayahudi zikomeshwe katika Italia. Papa hasemi lolote. . . . 1942—Papa apokea ripoti kutoka makasisi wa jeshi Waitalia juu ya kufutiliwa mbali kwa Wayahudi. Katika ujumbe wake wa Krismasi, aonyesha masikitiko juu ya msiba uliowapata ‘watu wasiojaliwa’ waliouawa kwa sababu ya jamii yao, lakini hataji Hitler, Ujerumani wala zile kambi za kifo. Mara nyingine tena, neno ‘Myahudi’ halitumiwi. . . . 1943—Wajerumani waanza kuwazingira Wayahudi katika Italia, hata katika Roma karibu na Vatikani. Papa angali kimya.”
Je, Kanisa Katoliki Litubu?
Katika barua moja waliyopelekewa makardinali Wakatoliki, Papa John Paul 2 amehimiza kanisa likubali makosa yaliyofanywa “na watu wao, kwa kutumia jina lalo” kisha litubu kuyahusu. Papa akiri kwamba “njia za kutumia nguvu, zisizopendelea haki za kibinadamu” zilizotumiwa na kanisa “zilitumiwa wakati huo na mawazo ya kutumia mabavu ya karne ya 20,” lasema La Repubblica la Roma. Lakini Kanisa Katoliki lahitaji kutubu juu ya nini? “Juu ya mambo mengi,” akiri Marco Politi mwelezaji wa Vatikani. “Kuhusu kuwasaka wenye maoni tofauti, kuhusu kupeleka wazushi wakachomwe moto kwenye mti, kuhusu wanasayansi na walio huru kueleza fikira zao ambao walitishwa kwa kuteswateswa, kuhusu kuunga mkono sera za tawala za Kifashisti, kuhusu machinjo yaliyotekelezwa katika ule Ulimwengu Mpya chini ya ishara ya Msalaba,” licha ya “kuhusu kujifikiria kuwa ni jamii kamilifu, na limekabidhiwa mamlaka kamili ya kusimamia dhamiri za watu,” na “kuhusu kuamini, wakati fulani katika historia, kwamba kwa kweli papa alikuwa ndiye vikari wa Kristo—kufuru la kitheolojia.”
Kutoka na Kwenda Dini ya Badala
Kanisa la Uingereza linapatwa na kutoka kwa makasisi kwa wingi. Kwa nini? “Kichochezi kionekanacho kusababisha hilo kimekuwa uamuzi wenye kubishaniwa wa Kanisa la Uingereza kuweka rasmi mapadri wa kike,” laripoti The Toronto Star. “Zaidi ya mapadri Waanglikana 130 wamekimbia tayari. Na sasa yaonekana kwamba karibuni kutakuwa na kishindo cha kuondoka kwa wengine,” ladai Star. Maaskofu saba Waanglikana na mapadri zaidi ya 700 wanatafuta uwezekano wa kujiunga na Kanisa Katoliki. Tangu Vita ya Ulimwengu 1, wenye kuunga mkono Kanisa la Uingereza wamepungua pole kwa pole. Katika Uingereza, kati ya wale watu milioni 20 wadaio kuwa Waanglikana waliobatizwa, ni milioni moja tu waliohudhuria ibada za Jumapili. Nyakati ngumu ziko mbele. Kule kutoka kwa kuliacha kanisa yaelekea kutaendelea.
Gharama Kubwa Mno ya Uhalifu
Ripoti ya hivi majuzi iliyotolewa na Taasisi ya Australia ya Uchunguzi wa Uhalifu ilifunua kwamba gharama ya uhalifu katika Australia yajumlika kuwa dola bilioni 26 kila mwaka. Hii ni kama dola 130 kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto katika Australia. Msemaji aliyenukuliwa katika gazeti Sunday Telegraph la Sydney alisema kwamba namna ya uhalifu ulio wa gharama kubwa zaidi ni upunjaji—unaosababisha utumizi uwezao kuwa wa karibu dola bilioni 14 kwa mwaka. Makadirio mengine ya gharama: uuaji, dola milioni 275 kwa mwaka; makosa ya kutumia dawa za kulevya, dola milioni 1,200; kuvunja nyumba na kuingia ndani, dola milioni 893; na, kwa kushangaza, kuiba madukani, kufikia dola bilioni 1.5. Ripoti hiyo ilimalizia kwa maelezo ya kwamba gharama ya uhalifu inazidi tu kuongezeka.
Ulimwengu Uliocharazwa
Mwaka 1994 ulipokuwa ukianza, ulimwengu ulikuwa ukicharazwa na vita 43, kulingana na ripoti moja kutoka Taasisi ya Kisiasa kwenye Chuo Kikuu cha Hamburg, Ujerumani. Ikieleza juu ya ripoti hiyo, Huduma ya Habari za Muungano wa Kidini yaandika kwamba vita 22 vilipiganwa katika Asia, 13 katika Afrika, 5 katika Amerika ya Latini, na 3 katika Ulaya. Taasisi hiyo ilipata pia kwamba wakati wa miaka ya 1950, wastani wa kila mwaka wa hesabu ya vita ilikuwa 12. Katika miaka ya 1960 iliongezeka kuwa 22, na leo hesabu hiyo imekuwa karibu maradufu.
Kutazama Kwingi Zaidi —Kusoma Kuchache Zaidi
Kwa nini watoto watazamao sana televisheni hupoteza upendezi wa kusoma? Baada ya kuchunguza tabia ya watoto Waholanzi 1,000 wa shule ya msingi kwa muda wa miaka mitatu iliyopita, mtafiti C. M. Koolstra alipata sababu mbili. Kwa kutazama sana televisheni, watoto hupoteza raha yao ya kusoma na hupunguza uwezo wao wa kukaza fikira. Kwa wale watazamao televisheni mara nyingi—zaripoti habari zilizotolewa na Chuo Kikuu cha Leiden katika Uholanzi—pole kwa pole huwa ni vigumu zaidi na zaidi kushika wanayosoma na kuweka akili yao ikiwa imekazwa katika ukurasa ulio mbele yao. Muda si muda, wao husukuma kando kitabu chao na kunyoosha mkono wachukue kibofyo cha kudhibiti televisheni. Pia mtafiti huyo alipata kwamba aina ya programu zinazotazamwa haileti tofauti. Iwe watoto hao walikuwa wakitazama vipindi vingi vya ucheshi, programu za watoto, drama, au programu za kuarifu, tokeo lilikuwa lilelile: “mzoroto katika kusoma.”
Kuendeleza Majangwa na Afya Mbaya
Ingawa asilimia 85 ya maskini wa mashambani wa Tanzania wahitaji sana kuni za kupikia, kujipasha joto, na kumulika, kila mwaka hektari 17,000 za msitu haba hukatwa ili kusaidia kurekebisha mazao ya tumbako nchini, yaripoti Synergy, barua-habari ya kutoka Sosaiti ya Kikanada kwa Afya ya Kimataifa. “Ni kinyume cha kushangaza kwamba tunaangusha miti yenye thamani na kufanyiza majangwa ili tupate fedha za kigeni kwa kupeleka tumbako nchi za nje,” aeleza Profesa W. L. Kilama, mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Tanzania ya Utafiti wa Kitiba. “Ni kinyume cha kushangaza pia,” yeye aongeza, “kwamba nchi zinazositawi zinafanyiza tumbako inayoendeleza afya mbaya.”
Uhalifu wa Kingono Waongezeka
Uhalifu wa kingono—kulala watu kinguvu, kufanya ngono na watu wa ukoo, na kutumia watoto vibaya—ulioonwa wakati mmoja kuwa tatizo la ulimwengu wa Magharibi, yaonekana waongezeka katika mabara fulani ya Kiafrika. Katika miezi ya hivi majuzi, vyombo vya habari vimeeleza mara nyingi juu ya uhalifu wa kingono. Times of Zambia liliripoti kwamba mwanamume wa miaka 37 alipewa kifungo cha miaka mitano jela na kuagizwa apigwe viboko sita kwa kufanya ngono na binti yake wa miaka 13. Alipatikana kuwa alikuwa amemtumia vibaya msichana huyo kingono wakati mke wake alipomwacha baada ya ugomvi. Msichana huyo aripotiwa kuwa alisema wakati wa kesi hiyo kwamba hatakuwa tena wa baba yake.
Idadi Inayoongezeka ya China
Idadi ya watu katika China itafika bilioni 1.2 mwaka huu, likaripoti Xinhua ambalo ni shirika rasmi la habari la Kichina. Ijapokuwa China ina sera ya kufuatilia sana kupanga familia itiayo moyo kusiwe na zaidi ya mtoto mmoja kwa familia, ongezeko la watu kufikia bilioni 1.2 lilikuja miaka sita mapema kuliko vile wapanga-idadi walivyokuwa wametarajia. Shirika hilo la habari lilidokeza sababu mbili kwa ongezeko hilo: Kwanza, wanawake wengi wa mashambani wako tayari kulipa faini iliyowekwa kwa kuwa na zaidi ya mtoto mmoja. Pili, wafanyakazi wahamaji wahamiao majijini kutoka maeneo ya mashambani waweza kuepuka vidhibiti vya kupanga familia visimamiavyo visa vya uzazi katika maeneo yenye kukaliwa na watu.