Kuutazama Ulimwengu
Hazina Zinazotoweka
Katika miaka 12 iliyopita, Urusi imepoteza kiasi kipatacho kuwa asilimia 90 ya hazina yayo ya sanaa, kama vile michoro na sanamu, kulingana na ripoti ya utafiti katika Moscow News. Katika 1990, maofisa wa forodha walitwaa mali ya pesa nyingi ya sanaa ya kale, sarufi za dhahabu, na vitu vya kidini. Hata hivyo, hiyo ilikuwa sehemu tu—labda kuanzia asilimia 2 hadi 5—ya mali zote zilizoingizwa kiharamu. Moscow News ladai kwamba magenge 40 hivi yenye kuingiza bidhaa kiharamu, ambayo yako sanasana katika Ujerumani na Italia, kwa sasa yanafanya kazi humo nchini. Hayo husafisha na kutengeneza tena vitu vyenye thamani zaidi na kisha kuvipeleka vikauzwe katika nchi tajiri.
Asamehewa Hatimaye
Papa John Paul 2 amempa Galileo “msamaha uliofikiriwa kwa uzito.” Hadi sasa, Kanisa Katoliki lilimwona mfizikia huyo mwenye kusifiwa kuwa mtu “aliyeshutumiwa na Baraza Takatifu la Kuwahukumu Wazushi wa Kidini” katika 1633 kwa kusisitiza kwamba dunia huzunguka jua. Sasa, miaka 360 baadaye, papa alitaka amalize suala hilo kikamili kwa hotuba yenye kufikiriwa kwa uzito mbele ya Chuo cha Sayansi cha Kipapa. Lakini kulingana na gazeti la Italia Corriere della Sera, hata kwenye pindi hii papa hakujizuia kusisitiza kwamba Galileo alikosea katika angalau jambo moja. Inaonekana mfizikia huyo alikataa “dokezo” kwamba atoe mikataa yake kuwa nadhariatete hadi kuwe na “ithibati isiyopingika.”
Maisha ya Kiwango cha Chini Zaidi
Mushar wa India “sikuzote wamekuwa katika kiwango cha chini zaidi” cha jamii, likasema India Today hivi karibuni. Jumuiya hiyo ya wasioguswa, kama vile jamii yao inavyoitwa, ni kama milioni tatu, wengi wao wakiishi katika jimbo la Bihar. Wengi wao, kulingana na Mushar mwenye umri wa miaka 60, “hawajui kinachomaanishwa na mlo kamili.” Gazeti India Today laeleza waziwazi juu ya kikundi cha watoto Wamushar ambao, wanapotafuta chakula kondeni, hutoa panya wengi kwenye mashimo yao kwa kutumia moshi, wanawapiga kwa fimbo, wanawachoma, na kuwala. Katika lugha ya wenyeji, gazeti hilo laeleza, “Mushar” lamaanisha “mwinda panya.”
Ushetani wa Matineja
Ushetani unaenea katika mashule jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Kulingana na gazeti The Star, msaikolojia mmoja asema kwamba ametibu idadi fulani ya wanafunzi walioathiriwa na Ushetani. Wagonjwa walisema juu ya mikutano ya washirikina viungani mwa jiji waliotumia dawa za kulevya na kufanya ngono na karamu za ukatili. Kinyume cha dhana za kawaida, yeye asema, “watoto hao huonekana wenye kustahika kabisa.” Ofisa wa polisi aliliambia The Star kwamba polisi wanajua juu ya vikundi vya kishetani kotekote nchini. Ushetani haujaharamishwa, lakini polisi hufuatilia uhalifu unaohusu sherehe za kishetani. Hivi karibuni walimshika msichana tineja na mvulana rafiki yake kuhusiana na kuuawa kimakusudi kwa mwanamke wa miaka 38. Wote walihusika na Ushetani, na waliwaambia polisi kwamba waliua kimakusudi chini ya uvutano wa kishetani.
Vimbunga Vinavyoletwa na Ongezeko la Halijoto
Wanasayansi wengi wana wasiwasi kwamba ongezeko la ghafula la vimbunga vikali hivi karibuni vyaweza kuhusishwa na ongezeko la halijoto, kupanda joto kwa anga kwa sababu ya uchafuzi wa kibinadamu. Kulingana na gazeti Newsweek, halijoto ya wastani ambayo ina digrii chache tu juu zaidi yaweza kuchochea vimbunga hivyo na kupanua eneo la bahari linalovifanyiza. Gazeti hilo linasema kwamba Kimbunga Andrew cha 1992, kilichokuwa na kipimo cha 5 kwenye kipimio cha pointi 5 cha ukubwa wa kimbunga, wakati mmoja kingeliitwa dhoruba ya kila baada ya miaka mia moja kwa sababu misiba kama hiyo haitukii mara nyingi. Lakini Kimbunga Hugo katika 1989 kilikuwa na kiwango cha 4, na Gilbert cha 1988 pia kilikuwa na kiwango cha 5. Hivyo, Newsweek linafanya muhtasari wa hangaiko la wanasayansi wengi: “Tazama Andrew; hivyo ndivyo ulimwengu wenye ongezeko la halijoto ungekuwa.”
Msaada kwa Ajili ya Nani?
Pesa zote za misaada zinazokusanywa kila mwaka huenda wapi? Nyingi zazo huenda kwa watu wanaoandaa misaada hiyo. Kulingana na uchunguzi mmoja, zaidi ya theluthi moja ya mashirika 100 makubwa zaidi ya kutoa misaada katika United States, kila mmoja wa waelekezi wakuu alipata donge nono la dola 200,000 (za U.S.) katika mishahara na bakshishi mwaka jana. Ndivyo International Herald Tribune linavyoripoti. Watatu kati ya waelekezi hao walipokea zaidi ya dola 500,000 kila mmoja. Uchunguzi huo ulianzishwa baada ya kuondolewa kwa msimamizi wa shirika moja, aliyeshtakiwa kwa kusimamia pesa vibaya na kutumia pesa ovyo. Alikuwa anapata dola 390,000 kwa mwaka. Mwandamizi wake hupata “tu” dola 195,000.
Talaka Tu Ndiyo Itatutenganisha
Katika 1991 ndoa zaidi ya 130,000 ziliishia kwenye mahakama za talaka katika Ujerumani, ndivyo linavyoripoti gazeti Allgemeine Zeitung. Kuvunjika kwa ndoa kumekuwa kwa kawaida sana hivi kwamba kadi za kutoa pole baada ya talaka zimeongezeka, zikiwa na shime kama “Pongezi kwa talaka yako” au “Karibu kwenye siku ya kwanza ya siku nzuri zaidi za maisha yako.” Asilimia 10 ya waume na wake katika Ujerumani sasa hufanya matayarisho ya talaka kimbele kabla ya ndoa. Wao huandika maafikiano yanayosema kihususa kila mwenzi atapata nini—nyumba, fanicha—iwapo talaka itatokea. Mbona kuna talaka nyingi hivyo? Gazeti Allgemeine Zeitung lasema: “Miaka michache tu baada ya ndoa, asilimia 80 ya wanawake hulalamika kwamba waume zao hawapendezwi nao. . . . Uchunguzi uliofanywa kwa waume na wake 5,000 ulithibitisha kwamba mara nyingi walizungumza pamoja kwa dakika tisa tu kwa siku baada ya miaka sita ya ndoa.”
Wazazi Watozwa kwa Ukosefu wa Nidhamu
Mahakama katika Tokyo, Japan, hivi karibuni ilikata kesi kwamba wazazi wa washiriki watatu matineja wa genge la pikipiki lazima wasaidie kugharimia uhalifu wa watoto wao. Wavulana hao walikuwa wamemchapa na kumpiga mateke mtu mmoja tumboni baada ya yeye kulalamika juu ya kelele ya pikipiki zao. Mtu huyo alikufa mwezi mmoja baadaye. “Uhalifu huo ulionyesha aina ya maisha ambayo vijana hao wanne walikuwa nayo, wakikosa-kosa kwenda shule, wakilewa, wakivuta sigara na kuendesha pikipiki,” ndivyo Mainichi Daily News ilivyomnukuu hakimu kuwa akisema. “Hali wakijua vema aina ya mtindo wa maisha ambayo wana wao walikuwa wakiishi, wazazi wa washiriki wa genge hilo hawakuwatia nidhamu,” yeye akasema na kuagiza wazazi hao walipe jumla ya Yen 83,000,000 (karibu dola 700,000 za U.S.) katika kufidia familia ya yule mtu aliyekufa.
Uchafuzi na Kiasi cha Vifo vya Watoto
Uchunguzi wa hivi karibuni katika Brazili unafungamanisha uchafuzi na vifo vya watoto wenye miaka mitano na chini ya hiyo mijini. Kulingana na gazeti O Estado de S. Paulo, Paulo H. N. Saldiva, mtafiti wa Idara ya Utibabu wa São Paulo, ameona kwamba wakati wowote ambao hewa ina oksidi ya nitrojeni (gesi inayotoka kwa kuchoma mafuta ya diseli, petroli, na alkoholi), kuna ongezeko katika idadi ya vifo kwa sababu ya matatizo ya kupumua. Ongezeko katika sehemu ya kumi tu ya gesi hiyo katika kila sehemu milioni ya hewa humaanisha kifo kwa watoto wanane zaidi kila juma katika São Paulo. Kwa kuwa watoto maskini na wasiolishwa vizuri ndio huathiriwa sana, Saldiva asema: “Wale wanaoteseka kwa sababu ya uchafuzi wa magari ni wale hasa wasiofurahia ustarehe wa gari.”
Kueneza Evanjeli Katika Anga la Nje?
Kanisa Katoliki bado linafikiria juu ya tatizo la kueneza evanjeli kwa ulimwengu mpya. Waastronomia wa Makao ya Papa waliohusika katika kutafuta uhai wenye akili katika anga la nje tayari wamechanganua matokeo ya kitheolojia ya kupata uhai huo. “Kubatiza viumbe vya nje ya anga? Kwa nini tusifanye hivyo?” auliza Myesuiti George Coyne, mkurugenzi wa jengo la Vatikani la kutazama anga katika Italia. “Ikiwa siku moja tunafanikiwa kukutana nao, tungekuwa na jukumu la kufikiria tatizo hilo.” Coyne aona jambo hilo hivi: “Kwanza, tungewajibika kuuliza kiumbe hicho maswali kadhaa, kama vile: ‘Je! umepata kuwa na ono lilelile kama la Adamu na Hawa, yaani, dhambi ya awali?’ Na kisha baada ya jibu: ‘Je! unajua pia juu ya Yesu fulani aliyekufidia?’” Ikiwa jibu ni la, basi “suala la yeye kutolewa evanjeli lingezuka bila shaka.”
Ndoa Zenye Kudumu, Zenye Furaha
“Ni msemo uleule: fanya yote kwa kufuata Sheria Kumi na uishi kwa furaha daima,” akalalamika msaikolojia Gary Schoener katika toleo la hivi karibuni la gazeti la Newsweek. Kusudi la dhihaka yake lilikuwa nini? Habari yenye kutangazwa sana ya uchunguzi wa karibu watu 6,000 inayoonyesha kwamba waume na wake wenye umri mkubwa wana furaha zaidi ya waseja wachanga ambao hufanya ngono ovyo-ovyo. Ugunduzi huo, ambao Schoener anaupuuza kuwa unatetea ndoa na adili, unaonyesha kwamba ingawa mahusiano ya kingono hupungua kadiri fulani kwa sababu ya umri, watu wenye furaha zaidi waliofanyiwa uchunguzi walikuwa waume na wake wenye umri mkubwa ambao bado wanaona wenzi wao “wakivutia sana kimwili” na bado hufurahia mapenzi kwa ukawaida. Uchunguzi mwingineo umeonyesha kwamba wale wanaodhibiti uzani wao na kufanya mazoezi kwa ukawaida wanaelekea zaidi kudumu wakiwa watendaji kingono katika miaka yao ya baadaye.
Siku ya Mwisho ya Kuchukuliwa Mbinguni Yapita—Tena
Misheni ya Siku Zijazo katika Korea ilitabiri kwa uhakika kwamba mnamo Oktoba 28, 1992, “kuchukuliwa mbinguni” kungetukia, washiriki waaminifu wa kanisa wakichukuliwa hadi mbinguni. Gazeti Korea Times liliripoti kwamba maelfu ya watu waliokubali unabii huo waliacha kazi zao na familia na kuuza mali zao. Inaripotiwa kwamba, mwamini mmoja alitoa mimba akihofu kwamba kijusu kingemfanya awe mzito wakati wa kupaa kwake mbinguni. Siku hiyo ikaja na kupita bila tukio lolote, isipokuwa kwamba waenda kanisa kadhaa waliokasirika waliwapiga wahubiri wao, wakitaka kujua kwa nini kuchukuliwa huko hakukutukia. Hata hivyo, mwanzilishi wa kanisa hilo alikuwa tayari gerezani. Alikuwa amekamatwa kwa kutumia vibaya fedha za kanisa. Korea Times lasema: “Baadhi ya mali zake zilitia ndani hati za malipo ambazo zingelipwa Mei ujao, miezi mingi baada ya siku ya mwisho aliyokuwa ametabiri.”