Tiba ya Akili na Mwili
UTAFITI waonyesha kwamba kicheko kirefu huburudisha na hufaa kwa afya ya akili na mwili. “Kinaweza kuondoa si mkazo wa akili tu, bali pia kuongeza uwezekano wa kuokoka ugonjwa hatari,” lasema gazeti Your Better Health. Ni kama “kukimbia kindani kwa ajili ya mazoezi.” Mipimo yaonyesha kwamba kicheko kirefu kinaweza kupunguza maumivu na vilevile kuwa zoezi zuri kwa moyo. Mzunguko wa damu mwilini huwa bora zaidi, kiwambo hufanyizishwa mazoezi, na kiwango cha oksijeni katika damu huongezeka. Misuli ya kifua, shingo, uso, na ngozi ya kichwa pia hupata mazoezi, pamoja na misuli ya macho inayodondoza machozi.
Jarida Journal of the American Medical Association liliripoti juu ya uchunguzi “uliodokeza kwamba programu ya kitulizo cha ucheshi inaweza kufanya maisha ya wagonjwa wenye matatizo ya kudumu kuwa bora na kwamba kicheko kina matokeo ya kuondoa dalili za ugonjwa kwa wagonjwa hawa.” Matokeo ya mfikio huo wa kisaikolojia wenye kusudi la kurudisha afya yalifanya Shirika la Kansa la British Columbia liongeze “chumba cha ucheshi” kwenye maktaba yao.
Hata hivyo, kucheka nyakati zote maishani hakutahakikisha afya njema. Badala ya hivyo, usawaziko unahitajiwa. Biblia husema kwamba kuna wakati wa kucheka na wakati wa kunyamaza. Kicheko kisichofikiriwa chaweza kukwaruza masikio ya wengine na kinalinganishwa na milio ya miiba inayochomeka chini ya sufuria kwa sababu hakina maana na hakijengi mtu.—Mhubiri 3:4, 7; 7:6.