Moyo wa Kumweka Mungu Kwanza
KULIKUWA na sauti yenye kuogofya kwenye mlio wa simu yetu saa tisa za usiku. Alikuwa ni mshiriki wa kibiashara wa Baba ambaye alikuwa ametoka tu kuhudhuria mkutano wa wanajeshi wa zamani wa U.S. Alikuwa mwenye wasiwasi mwingi. “Wally,” akamwambia babangu kwa sauti kubwa, “usipopiga simu kwa ofisi ya Philadelphia Inquirer mara moja kwa ajili ya toleo la asubuhi na kusema utaisalimu bendera, watu watalivamia duka lako na familia yako leo, na sitahusika kwa yatakayotokea!” Baba na Mama walikuwa wameshapatwa na jeuri ya wafanya ghasia hapo awali. Wakiwa wameamka sasa, walianza kusali.
Walituamsha sisi sote watoto sita kukipambazuka. Baba alimwambia ndugu yangu mdogo Bill awapeleke watoto wetu nyumbani kwa babu na nyanya yetu. Kisha Bill na mimi tukasaidia katika kazi ya nyumbani na duka kama kawaida. Baba alienda kwa mkuu wa polisi wa Minersville na kumwambia juu ya tisho hilo. Upesi gari la Polisi wa Jimbo la Pennsylvania likaja na kuegesha mbele ya duka letu na kushinda hapo mchana kutwa. Tuliendelea na shughuli zetu dukani na kutumikia wateja, lakini tuliendelea kutazama-tazama sehemu ya nje ya duka letu. Mioyo yetu ingegutuka tulipoona kikundi cha watu kimetua. Lakini umati huo wenye ghasia haukuja kamwe. Labda walipunguza hasira siku ilipoendelea kupita—na kwa kuona gari la polisi!
Tunapata Kweli
Lakini ni nini kilichoongoza kwenye hali hiyo mbaya? Ilikuwa kwa sababu ya dini yetu. Yaani, katika 1931, nilipokuwa na umri wa miaka saba, Nyanya na Babu yangu walikuja kukaa nasi kwa muda. Walikuwa Wanafunzi wa Biblia, kama vile Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo.
Babu hakumhubiria Baba, lakini wakati Nyanya na Babu walipokuwa nje, Baba angeenda kwenye chumba chao na kutazama ni nini kilichokuwa kwenye fasihi hiyo yao. Aliisoma kwa hamu nyingi! Bado naweza kusikia sauti yake yenye shangwe: “Ona vile Biblia inasema!” Kweli ilikuwa shangwe halisi kwake. Mama aliisoma fasihi hiyo pia, na kufikia 1932 alijiuzulu kutoka Kanisa la Methodisti, na tukawa na funzo la Biblia la nyumbani. Nilifurahi pia kama wao kusikia juu ya dunia Paradiso ya ajabu itakayokuja. Nikaifanya kweli iwe yangu kuanzia hapo.
Mwishoni mwa 1932, Mama aliniuliza kama nilikuwa tayari kwenda katika kazi ya kuhubiri mlango kwa mlango. Siku hizo, tuwe wachanga au wazee, tulienda peke yetu milangoni. Na tulitumia kadi ya kutoa ushuhuda. Ningesema tu hivi: “Habari ya asubuhi, nina ujumbe wa maana. Tafadhali ungeweza kusoma hii?” Ikiwa mwenye nyumba alikuwa haonekani kuwa mwenye kukubali mara moja, ningesema tu, “Haya, kwaheri,” alipomaliza kusoma.
Kabla ya muda mrefu, upinzani ukaja. Katika masika ya 1935, tulitoa ushahidi katika mji wa New Philadelphia. Nakumbuka nikisimama katika kizingiti cha mlango mmoja na kuzungumza na mtu wakati polisi walipokuja na kunichukua pamoja na wengine waliokuwa wakitoa ushahidi. Mwenye nyumba alitazama kwa mpagao kwamba wangeshika msichana huyu mwenye umri wa miaka 11. Walitupeleka kwa nyumba ya moto ya orofa mbili. Huko nje kulikuwa na umati mkubwa wa watu karibu elfu moja wenye makelele. Kwa wazi walikuwa wameacha ibada za makanisa mapema Jumapili hiyo ili kutia moyo kila mmoja wao ashiriki. Tulipokuwa tukipitishwa katikati ya umati, msichana mmoja aliupiga mkono wangu ngumi. Lakini tulifika salama ndani, na walinzi waliokuwa na silaha waliuzuia umati usivunje mlango.
Tulikuwa watu 44 tuliokuwa tumeijaza nyumba ya moto, na tulilazimika kuketi kwenye ngazi. Hatukuwa na huzuni; tulikuwa wenye furaha kukutana na baadhi ya Mashahidi kutoka Kundi la Shenandoah ambao walikuwa wakitusaidia kuhubiri mjini. Nilikutana na Eleanor Walaitis huko, na tukawa marafiki washikamanifu sana. Baada ya muda wa saa chache, polisi walituachilia.
Suala la Kusalimu Bendera Latokea
Katika mkusanyiko mkuu wa Mashahidi wa Yehova katika Washington D.C., wa 1935, mtu mmoja alimwuliza Ndugu Rutherford, msimamizi wa Watch Tower Society, juu ya kama watoto wa shule wanapaswa kusalimu bendera. Alijibu kwamba lilikuwa jambo la kukosa uaminifu kwa Mungu kuonyesha kwamba wokovu unatoka kwa mfano wa kidunia kwa kuisalimu; alisema kuwa yeye hangefanya hivyo. Jambo hilo lilimpendeza Bill nami. Tulilizungumzia pamoja na wazazi wetu na kutazama Kutoka 20:4-6, 1 Yohana 5:21, na Mathayo 22:21. Mama na Baba hawakutusonga wala kutufanya tujihisi wenye hatia. Shule zilipofunguliwa katika Septemba, tulijua sana jambo tulilopaswa kufanya. Lakini kila wakati walimu wetu walitazama upande wetu, tuliinua mikono yetu kiupuzi-upuzi na kufanya midomo yetu kana kwamba tunaimba. Tatizo langu moja lilikuwa ni woga wa kupoteza marafiki wa kilimwengu ikiwa ningechukua msimamo.
Lakini mapainia fulani walipotutembelea, niliwaambia tuliyokuwa tukifanya. Sitasahau kamwe alilosema dada mmoja: “Lillian, Yehova humchukia mnafiki.” Halafu, katika Oktoba 6, Ndugu Rutherford alitoa hotuba ya redio katika sehemu zote za U.S. yenye kichwa “Kusalimu Bendera.” Alieleza kwamba tunaiheshimu bendera lakini kufanya zile desturi mbele ya sanamu au mfano kulikuwa kuabudu sanamu kwa kweli. Uhusiano wetu na Yehova ulikataza jambo hilo kabisa.
Katika Oktoba 22, Bill, akiwa na miaka kumi tu, alikuja nyumbani kutoka shuleni akiwa na furaha tele. “Niliacha kuisalimu bendera!” akasema kwa shangwe. “Mwalimu alijaribu kuweka mkono wangu ili niisalimu, lakini nikaiweka mikono mifukoni mwangu.”
Asubuhi iliyofuata, moyo ukidunda, nilienda kwa mwalimu wangu ili nisiwe mdhaifu. “Bi Shofstal,” nikagugumiza, “Siwezi kusalimu bendera tena. Biblia katika Kutoka sura ya 20 husema kwamba hatuwezi kuwa na miungu mingine mbele ya Yehova Mungu.” Kwa mshangao wangu alinikumbatia na kusema nilikuwa kisichana kipenzi kama nini. Basi, wakati wa kuisalimu bendera ulipowadia, sikushiriki kuisalimu.a Upesi kila mtu akanikodolea macho. Lakini nilifurahi sana. Yehova ndiye aliyenipa moyo mkuu wa kutoisalimu.
Wasichana niliowapenda shuleni walipigwa na butaa. Mmoja au wawili walikuja na kuniuliza kwa nini, na mazungumzo mazuri yakafuata. Lakini watoto walio wengi walianza kunipuuza. Nilipofika shuleni kila asubuhi, wavulana wachache wangesema kwa nguvu, “Ndiye huyu Yehova anakuja!” na kunirushia changarawe. Wote shuleni walitazama kwa majuma mawili. Kisha wakaamua kuchukua hatua. Katika Novemba 6, halmashauri ya shule ikakutana na Baba na Mama na wazazi wa mvulana mwingine Shahidi. Msimamizi, Profesa Charles Roudabush, alisisitiza kuwa msimamo wetu ulikuwa kutotii; wengine nao wakakubaliana naye. Wakatufukuza shuleni.
Shule ya Nyumbani Yaanza
Walituruhusu tubaki na vitabu vyetu vya shule, na upesi tukaanzisha shule ya nyumbani katika orofa yetu ya juu kabisa, tukisimamiwa na msichana mchanga ambaye alikuwa akisaidia Mama nyumbani. Lakini barua ikafuata upesi ikisema kwamba ikiwa hatukuwa na mwalimu aliyehitimu, tungepelekwa kwenye shule ya kuadibisha.
Paul na Verna Jones, waliokuwa na shamba kilometa 50, walitupigia simu baada ya siku chache. “Tulisoma kwamba watoto wako walifukuzwa,” Paul akamwambia Baba. Walikuwa wameondoa ukuta kati ya sebule yao na chumba chao cha kulia ili kukifanya kiwe darasa la shule. Walitukaribisha tuingie. Mwalimu mchanga kutoka Allentown ambaye alipendezwa na kweli alikubali kazi hiyo kwa moyo, ingawa ingemaanisha kupata fedha chache kuliko alizopewa kutoka shule za umma. Shule kama hizo za Mashahidi zilianza kotekote katika U.S.
Kina Jones walikuwa na watoto wanne wao wenyewe; lakini walichukua wengine kumi. Tulilala watoto watatu-watatu kwa kitanda kimoja na sote tukakubaliana kubadilisha jinsi ya kulala wakati uleule! Familia nyingine ya Mashahidi iliyokuwa karibu ilichukua wengi kadiri hiyo pia na upesi hudhurio la shule likawa zaidi ya 40. Kulikuwa na mambo mengi ya kufurahisha na kuchekacheka, lakini kulikuwa na mambo ya kufanya. Tuliamka saa 12:00 asubuhi. Wavulana walisaidia kufanya kazi nje, na wasichana walisaidia kazi ya jikoni. Wazazi wetu walikuja Ijumaa baada ya shule kutupeleka nyumbani kwa ajili ya mwisho-juma. Siku moja watoto wa kina Walaitis walifika, pamoja na rafiki yangu Eleanor.
Matatizo ya shule yaliendelea kuja. Ndugu mpendwa Paul Jones akafa, kwa hiyo Baba akageuza kigari chetu cha kubebea mizigo kuwa basi ya shule ya kutupeleka kilometa 50 shuleni. Kisha baadhi yetu tukafika umri wa kwenda shule ya upili na tukahitaji mwalimu ambaye alihitimu kwa ajili ya kikundi cha umri huo. Kwa kila kizuizi, ilionekana Yehova aliandaa utatuzi.
Kwenda Mahakamani
Kwa wakati huo Sosaiti ilitaka kuleta mashtaka yanayohusika na kusalimu bendera mahakamani. Mamia kati yetu ambao walichukua msimamo waliongezeka kuwa maelfu. Familia moja baada ya nyingine zilichaguliwa, lakini mahakama za jimbo zilikataa kusikiliza kesi zao. Familia yetu ilifikiwa, na wakili wa Sosaiti pamoja na wakili wa Chama cha Kutetea Haki za Binadamu walipeleka mashtaka katika Mahakama ya Wilaya ya Philadelphia katika Mei 1937. Tarehe ya kusikilizwa kwa kesi iliwekwa iwe Februari 1938.
Bill na mimi tulipaswa kutoa ushuhuda mahakamani. Bado nakumbuka ile baridi na hisia za woga nilizopata nikitazamia jambo hilo! Wakili wa Sosaiti alitueleza mara kwa mara maswali ambayo huenda tungeulizwa. Kule mahakamani Bill alikuwa wa kwanza kusema. Walimwuliza ni kwa nini hangesalimu bendera, na alijibu akitumia Kutoka 20:4-6. Kisha zamu yangu ikaja. Swali lilo hilo. Nilipojibu, “1 Yohana 5:21,” wakili mpinzani akasema: “Napinga!” Alihisi lile andiko moja lilikuwa li-metosha! Kisha Profesa Roudabush akachukua zamu, akidai kuwa tulikuwa tumefundishwa vibaya na tulieneza “kutokuheshimu . . . bendera na nchi.” Lakini Hakimu Albert Maris akatoa uamuzi wenye kutupendelea.
‘Msijaribu kurudi shuleni tena!’ ulikuwa ujumbe kutoka kwa baraza la shule. ‘Tutakata rufani.’ Kwa hiyo tulirudi tena Philadelphia, wakati huu kwenye Mahakama ya Rufani ya U.S. Katika Novemba 1939, Mahakama ya mahakimu-watatu iliamua kwa kutupendelea. Baraza la shule lilighadhabika. Kesi ilikatwa rufani hadi kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya U.S.!
Mahakama Kuu Zaidi
Tulifurahi sana kusikia kwamba Ndugu Rutherford mwenyewe angetetea kesi yetu! Kikundi chetu kilikutana naye katika Stesheni ya gari-moshi ya Union katika Washington D.C., usiku wa kabla ya kesi. Ulikuwa wakati mzuri kama nini! Ilikuwa Aprili 1940 na bado kulikuwa na baridi. Siku iliyofuata mahakama ilikuwa imejawa kabisa na Mashahidi wa Yehova. Hatimaye ikawa zamu yetu, na Ndugu Rutherford akainuka azungumze. Sitasahau kamwe alivyotufananisha sisi watoto wa Mashahidi na nabii Danieli, Washiriki watatu Waebrania wa Danieli, na watu wengine wa Biblia. Mazungumzo yake yalikuwa yenye kuvutia sana, na wasikilizaji walisikiliza kwa makini sana.
Hatukuwazia kwamba uamuzi wa mahakama ungekuwa mbaya. Ilitazamiwa, kwa sababu tulikuwa tumeshinda kesi zile nyingine mbili. Lakini katika asubuhi ya Juni 3, 1940, Mama nami tulikuwa tukifanya kazi jikoni na radio ikisikika kwa sauti ya mbali. Kwa ghafula habari ikaja. Waamuzi waliamua dhidi yetu—na si kwa kiwango kidogo tu bali kwa kadiri 8 kwa 1! Mama nami tulisimama zizima, bila kuamini. Kisha tukakimbia chini kuwaambia Baba na Bill.
Uamuzi huo ulifungua wimbi la mnyanyaso lenye kutisha. Kote nchini, kulikuwa kipindi cha kunyanyasa Mashahidi wa Yehova bila kujizuia. Watu walifikiri walikuwa wakitumikia nchi kwa kutushambulia. Baada ya siku chache Jumba la Ufalme katika Kennebunk, Maine, lilichomwa. Katika Illinois, umati wenye ghasia ulishambulia Mashahidi 60 walipokuwa wanahubiri, wakapindua magari yao na kuharibu fasihi. Katika Shenandoah, eneo la Pennsylvania, migodi ya makaa-mawe, viwanda vya nguo, na shule zote zilifanya kwa mfululizo sherehe za kuisalimu bendera. Kwa hiyo, watoto wa Mashahidi wakafukuzwa shuleni, na wazazi wao wakapoteza kazi zao yote hayo kwa siku moja tu.
Kukabiliana na Mnyanyaso
Ilikuwa wakati huu ambapo familia yetu ilipopata tisho lililoelezwa mwanzoni. Baada ya hilo kushindwa, kanisa la Minersville likatangaza kususia duka letu. Biashara ilipungua kabisa. Ilikuwa ndiyo riziki yetu, na sasa kulikuwako na watoto sita katika familia. Ilimbidi Baba akopeshe pesa ili aandae mahitaji ya maisha. Lakini baada ya muda, ususiaji ulififia; watu wakaanza kurudi tena ili kununua vitu. Wengine hata walisema kwamba “ilikuwa kupita kiasi” kwa kasisi wao kuwaambia mahali pa kununua bidhaa zao. Hata hivyo, familia nyingi za Mashahidi zilipoteza biashara zao na nyumba zao wakati wa miaka hiyo.
Usiku mmoja nilikuwa nikiendesha familia yetu katika gari tukirudi nyumbani kutoka kwa mafunzo ya Biblia. Mara tu Mama na Baba walipoingia kwenye gari, genge la matineja lilikuja kutoka kule lilikuwa limejificha na kulizingira gari. Walianza kutoboa magurudumu. Kwa ghafula nikaona nafasi ya kuponyokea. Nilikanyaga mafuta na upesi tukaenda! “Lillian, usifanye hivyo tena,” Baba akanishauri. “Ungeumiza mtu.” Hata hivyo, tulifika nyumbani salama.
Wakati wa jeuri hiyo yote ya kupita kiasi, magazeti yalitupendelea sana. Angalau magazeti mashuhuri 171 yalilaumu uamuzi wa 1940 wa kuisalimu bendera. Ni magazeti machache tu yaliyokubali. Katika safu yake “Siku Yangu,” Eleanor Roosevelt, mke wa rais aliandika akitutetea. Bado, hakukuonekana kama ujeuri huo ungeisha.
Badiliko Hatimaye
Hata hivyo, kufikia 1942, baadhi ya mahakimu wa Mahakama Kuu Zaidi walihisi kwamba waliamua vibaya katika kesi yetu. Kwa hiyo Sosaiti ikaleta kesi ya Barnett, Stull, na McClure, kikundi cha watoto Mashahidi ambao walikuwa wamefukuzwa kutoka shuleni katika West Virginia. Mahakama ya U.S. ya Wilaya ya West Virginia iliamua kwa kupendelea Mashahidi wa Yehova! Sasa, Halmashauri ya Elimu ya Jimbo ilikata rufani na kupeleka kesi kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya U.S. Familia yetu ilikuwa huko Washington, D.C., wakati wakili wa Sosaiti, Hayden C. Covington, alipotoa hoja kwa bidii mbele ya Mahakama Kuu Zaidi. Uamuzi ulitolewa siku ya bendera, Juni 14, 1943. Mashahidi wa Yehova walishinda kesi hiyo kwa kura sita kwa tatu na mahakimu wa Mahakama Kuu Zaidi!
Kotekote nchini, mambo yakaanza kutulia baada ya hilo. Bila shaka, kulikuwa na wale wenye kukataa mabadiliko ambao bado walitafuta njia za kufanya maisha yawe magumu kwa dada zetu wachanga wa kimwili waliporudi shuleni, lakini Bill nami tulikuwa tumepita umri wa shule. Miaka minane ilikuwa imepita tangu tuchukue msimamo wetu.
Kazi-Maisha ya Kumtumikia Yehova
Lakini huo ulikuwa mwanzo tu wa kazi-maisha ya kumtumikia Yehova. Bill akawa painia akiwa na umri wa miaka 16. Eleanor Walaitis (sasa Miller) nami tukawa mapainia wenzi na kutumikia katika Bronx, Jiji la New York. Baada ya mwaka mmoja, nilifurahia kutumikia katika Betheli ya Brooklyn, makao makuu ya ulimwengu ya Watch Tower Society. Huko nako nimefanyiza urafiki ambao umedumu maishani.
Katika kiangazi cha 1951, nilikuwa katika makusanyiko ya Ulaya wakati nilipokutana na Erwin Klose. Katika kitumbuizo kimoja huko Ujerumani, yeye na ndugu wengine Wajerumani waliimba vizuri wakitutumbuiza. Nilimwambia kwa uchangamfu jinsi alivyokuwa na sauti nzuri. Alitikisa kichwa kwa fadhili, na niliendelea kuongea. Hakuelewa nilichokuwa nikisema kwa maana hakuelewa Kiingereza! Baada ya miezi kadhaa nilimwona Erwin katika Brooklyn, New York, katika Betheli, kwa kuwa alikuwa ameandikishwa kwenye Watchtower Bible School of Gilead ili kuzoezwa kwa kazi ya mishonari. Niliongea naye kirefu tena, nikimkaribisha Brooklyn, na alitabasamu kwa fadhili tena. Bado aliona vigumu kunielewa! Ingawa hivyo, tulikuja kuelewana hatimaye. Haikuwa muda mrefu kabla ya kuchumbiana.
Nikawa mishonari na kujiunga na Erwin katika kazi yake Austria. Lakini afya ya Erwin ikadhoofika kwa sababu ya jinsi walivyotendwa kikatili mikononi mwa Wanazi kwa sababu ya kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Nilipokuwa nimefukuzwa shuleni, alikuwa katika magereza na kambi za mateso.b Tulirudi United States mwishoni mwa 1954.
Tumekuwa na shangwe ya kumtumikia Yehova palipo na uhitaji mwingi zaidi na kulea watoto wawili wazuri katika njia za Yehova. Watoto walipokwenda shuleni, niliona kwamba mambo hayajabadilika kabisa. Judith na Stephen walishambuliwa kwa sababu ya usadikisho wao, na Erwin nami tulihisi mioyo yetu imejawa na shangwe na fahari walipoonyesha moyo wa kuchukua msimamo wao kwa mambo yaliyo sawa. Na sikuzote niliona kwamba mwishoni mwa mwaka wa shule, walimu wao walikuja kujua kuwa Mashahidi si kikundi cha watu washupavu, na sisi wazazi na walimu tukafanya uhusiano mchangamfu sana.
Ninapoangalia nyuma miaka iliyopita, naweza kuona kwa hakika kwamba Yehova amebariki familia yetu. Sisi sote sasa ni familia ya watu 52 ambao wanamtumikia Yehova. Kuna wanane ambao wamepokea zawadi yao ya kimbingu au wanangojea ufufuo wa kidunia, kutia ndani na wazazi wangu wapendwa, ambao walituachia urithi mzuri ajabu wa kumweka Yehova kwanza maishani. Katika miaka ya karibuni tumefikiria sana mfano huo. Baada ya kuishi maisha ya aina hiyo ya utendaji na matokeo, Erwin ameng’ang’ana na ugonjwa wa neva wa misuli ambao umemfanya asitimize mengi.
Kujapokuwa majaribu hayo yote, tunatazamia mbele kwa wakati ujao tukiwa na shangwe na uhakika wa kweli. Hatujasikitika tena kamwe kwa ajili ya uamuzi wetu wa kumwabudu Yehova Mungu pekee.—Kama ilivyosimuliwa na Lillian Gobitas Klose.
[Sanduku katika ukurasa wa 17]
Kwa Nini Mashahidi wa Yehova Hawaisalimu Bendera?
KUNA kanuni ya ibada ambayo Mashahidi wa Yehova hukazia zaidi ya vikundi vinginevyo vya kidini: upekee. Yesu alitaja kanuni hiyo kwenye Luka 4:8: “Msujudie Bwana [Yehova, New World Translation] Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Mashahidi basi wanachagua kuepuka kuelekeza ibada yao kwa yeyote au kitu kingine chochote katika ulimwengu ila kwa Yehova. Kushiriki kusalimu bendera ya nchi yoyote ile, ni kama tendo la ibada kwao ambalo lingeweza kuingilia na kuharibu ibada yao ya pekee kwa Yehova.
Waisraeli na pia Wakristo wa kwanza walionywa mara nyingi dhidi ya ibada ya vitu vilivyotengenezwa na wanadamu. Kufanya hivyo kulionwa kuwa ibada ya sanamu. (Kutoka 20:4-6; Mathayo 22:21; 1 Yohana 5:21) Je! kweli bendera inaweza kuonwa kuwa sanamu? Ni watu wachache wanaoweza kutoa hoja kuwa ni kitambaa tu. Inaonwa kuwa ishara takatifu, na heshima yayo inashinda ile inayopewa vitu vitakatifu. Mwanahistoria wa Katoliki Carlton Hayes alisema hivi: “Ishara kuu ya imani ya utaifa na kitu kikuu cha ibada ni bendera.”
Hilo halimaanishi kwamba Mashahidi wa Yehova wanakosa kuheshimu bendera au wale wanaoisalimu bendera. Kwa ujumla watasimama kwa heshima wakati wa sherehe hizo mradi hawahitajiwi kuzishiriki. Wanaamini kwamba mtu anaonyesha heshima ya kweli kwa bendera kwa kutii sheria za nchi inayowakilisha.
Watu wengi watakubali kwamba kuisalimu bendera hakuhakikishi kuiheshimu. Ukweli wa jambo hilo ulionekana katika kisa kimoja katika Kanada. Mwalimu mmoja na mkuu wa shule walimwamuru msichana mdogo ambaye husalimu bendera aitemee mate; alifanya hivyo. Kisha walimwamuru msichana mchanga Shahidi katika darasa hilo afanye vivyo hivyo, lakini yeye alikataa katakata. Kwa Mashahidi wa Yehova, ni kanuni kubwa kuiheshimu bendera. Hata hivyo, ibada yao, huenda kwa Yehova peke yake.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa ujumla, Mashahidi wa Yehova wako tayari kuheshimu viapo na nyimbo katika njia ambazo hazionyeshi kushiriki katika matendo ya ibada ya kidini.
b Ona Amkeni! ya Novemba 22, 1992, Kiingereza, “Wanazi Hawangetukomesha!”
[Picha katika ukurasa wa 16]
Erwin na Lillian katika Vienna, Austria, 1954
[Picha katika ukurasa wa 17]
Lillian leo
[Hisani]
Dennis Marsico