Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ukosefu wa Haki kwa Wahalifu Nataka kuwaambia jinsi nilivyotumia toleo la zamani la Amkeni! Binti yangu alishikiwa bunduki na wezi wa magari alipokuwa ndani ya gari. Mwizi alipatikana kuwa na hatia, lakini shtaka la kumtisha kwa bastola, lilikataliwa. Nikiwa nimevunjika moyo, niliruhusiwa kuongea kwa niaba ya binti yangu kwa shtaka la mhalifu. Mapema, nilikuwa nimepata kuona ile makala “Je! Uhalifu Unafaa?” (Agosti 8, 1985, Kiingereza) Nikitumia habari iliyo kwenye sanduku yenye kichwa “Mfumo Usio na Haki wa Uhalifu,” niliiambia mahakama kwamba “mhalifu ana uchaguzi—wa kutenda uhalifu au kutotenda. Mtendwa uhalifu hana uchaguzi.” Mwizi huyo alifungwa jela, akapokea kifungo kirefu.
D. M., United States
Wazazi Wenye Kupuuza Asanteni sana kwa makala “Vijana Wanauliza . . . Kwa Nini Wazazi Wangu Hawaonyeshi Kupendezwa Nami?” (Novemba 8, 1992, Kiingereza) Nililia nilipoisoma. Miezi michache iliyopita, nilihisi nimepuuzwa, kwa hiyo nikaasi. Nafikiri nilikuwa na hasira sana na kuumizwa ndani. Makala hiyo ilinisaidia nifikiri lililotendeka. Asanteni kwa kutujali sisi vijana sana kwa kutupa habari hiyo yenye maana.
N. C., United States
Makala hiyo ilifikia moyo wa binti yangu wa miaka kumi. Nikiwa mzazi aliye peke yake, ninajitahidi sana, lakini sikuzote sina nishati na subira ya kushughulika na mkazo wa akili ninaokabili kila siku. Baada ya kuzungumza habari hiyo pamoja naye, alielewa jinsi ninavyohisi wakati mwingine. Sote tulilia, na alitambua kuwa ninampenda.
C. L., United States
Juu ya Ulaya Nataka kuwashukuru kwa makala “Juu ya Ulaya kwa Reli.” (Desemba 8, 1992, Kiingereza) Ilinitia moyo kuzuru Jungfraujoch, karibu na Interlaken, Uswisi. Nikiwa katika mwinuko wa meta 3,454 juu ya usawa wa bahari, niliweza kuthamini uzuri wa kazi stadi za Mungu na ukubwa wa milima iliyofunikwa na theluji.
P. L., Italia
Muziki Nina umri wa miaka 12. Ile makala “Vijana Wanauliza . . . Muziki Wangu Una Ubaya Gani?” ilikuwa yenye msaada kwelikweli. (Februari 8, 1993) Mimi pia nimekuwa nikishindwa kuzima muziki wangu, hata kuusikiliza ninaposoma. Pia nina rekodi ambazo si nzuri sana, na nimekosana na wazazi wangu mara nyingi kwa sababu yazo. Niliposoma jinsi kusikiliza muziki kunavyoniathiri, nilihisi kana kwamba moyo wangu ulikuwa unachomwa kwa kisu. Sasa ninafikiria juu ya kuzitupa rekodi zozote zinazoeleza mambo mabaya. Asanteni sana.
M. H., Japani
Niliona makala hiyo kuwa yenye maana. Inasikitisha jinsi makundi ya vijana yanavyojiingiza katika muziki wenye kuasi na mitindo ya nguo. Makala hizo zafaa sana kwetu sisi vijana Wakristo.
M. M., Italia
Makala hiyo ilionyesha muziki wa rapu katika njia isiyopendeleka kabisa. Mara nyingi mimi huwa na vijana wengine, na sisi hucheza rapu. Ni kweli kuna nyimbo zilizo na maneno machafu. Lakini kujumlisha muziki wote wa rapu kuwa mbaya si sawa.
B. R., Ujerumani
Makala hiyo haikushutumu muziki wote wa rapu. Badala ya hivyo, ilionya dhidi ya kujiingiza na aina yoyote ya muziki ambao ujumbe wayo kwa ujumla na roho yayo haupatani na viwango vya Biblia. Ushuhuda unaonyesha wazi kwamba muziki wa rapu unapungukiwa sana katika jambo hilo.—MHARIRI.