Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 6/8 kur. 4-7
  • Raha Isiyodhuru au Sumu ya Akili?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Raha Isiyodhuru au Sumu ya Akili?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Muziki Wenye Mdundo Mzito na wa Rapu
  • Je! Kuna Athari?
  • Vipi Wewe?
  • Jilinde na Muziki Usiofaa!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Muziki Wangu Una Ubaya Gani?
    Amkeni!—1993
  • Muziki Waweza Kweli Kuniumiza?
    Amkeni!—1993
  • Je, Nihudhurie Maonyesho ya Roki?
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 6/8 kur. 4-7

Raha Isiyodhuru au Sumu ya Akili?

Katika wonyesho mmoja wa jukwaani wa muziki wa roki, mmoja wa wanamuziki hao alimweka mwanamke katika sanduku na akapasua sanduku hilo kwa shoka. Damu bandia ikafoka kutoka kinywani mwa mwanamuziki huyo, naye akaitema kwa wahudhuriaji.

Katika 1984, mvulana mwenye miaka 19 alijipiga risasi. Wazazi wake wanadai kwamba kujiua kwake kulichochewa na maneno ya wimbo mmoja wa roki unaoitwa “Suicide Solution” (Suluhisho la Kujiua).

Gazeti moja la vijana lilichapisha habari za ngono iliyopotoka inayofanywa na washiriki wa beni ya muziki katika chumba chao cha kubadilishia mavazi na vilevile katika studio wakati wa kurekodi muziki. Kifuniko kimoja cha muziki kilikuwa na picha yenye kuchukiza sana ya uume na uke.

UJEURI, kujiua, na ngono ya kikatili—hayo ni baadhi tu ya mambo yasiyofaa yanayoonyeshwa katika muziki wa roki, katika vidio, na katika maonyesho ya muziki jukwaani. Masuala yanapozushwa juu ya programu hizo zenye kupotoka na hata yanapowasilishwa mahakamani, wanamuziki na makampuni ya kurekodi hujaribu kutoa sababu kwa kutetea sehemu hizo zisizopendeza. Kwa mfano, mchoro wenye kuchukiza kiadili sasa husemwa kuwa tegemezo la habari inayozungumzia “ufisadi wa kiakili katika Jamii ya Waamerika na jinsi ufisadi huo unavyotuangamiza hatimaye.” Vivyo hivyo, katika baadhi ya muziki, maneno ambayo kwa wazi ni mifano ya uume (kama vile bunduki au visu) sasa yanadaiwa kuwa yenye maana halisi.

Wanamuziki na makampuni ya kurekodi huenda wasihukumiwe, lakini je, kweli watu wanadanganywa? Je! wewe wadanganywa? Je! huwezi kukubali kwamba ujeuri, ngono, na uchawi ndiyo mambo ya maana sana katika muziki wa roki unaouzwa leo?

Muziki Wenye Mdundo Mzito na wa Rapu

Kwa miaka ambayo imepita, aina nyingi za muziki wa roki zimetokea. Mitindo miwili, ule wenye mdundo mzito na wa rapu, imeshutumiwa hivi karibuni kwa sababu ya ukosefu mkubwa wa adabu.

Kwa kawaida, muziki wenye mdundo mzito ni muziki wa kielektroni wenye nguvu, uliokuzwa sauti sana na ambao una mdundo unaopi-gapiga. Kulingana na gazeti Time, “wanamuziki wa mdundo mzito hupatanisha muziki wao na mawazio yasiyo ya kawaida ya wanaume weupe wachanga hasa kwa kujionyesha kwamba wao ni watu walioona ukweli ambao wameacha ulimwengu wenye ufisadi.” Muziki mwingi wenye mdundo mzito hukusudiwa ushtushe. Baadhi ya maneno yao hayawezi kutajwa. Jarida moja la kitiba katika Texas lilionelea kwamba mengi ya maneno yaliyo katika muziki wenye mdundo mzito yanatukuza “mielekeo isiyo ya kawaida inayohusu ngono, ujeuri, chuki, na uchawi.”

Ujeuri unaohusianishwa na muziki wenye mdundo mzito ni hangaiko jingine. Kwa mfano, wakati wonyesho mmoja ulipokatizwa kwa sababu ya mwimbaji mmoja kuwa mgonjwa, wahudhuriaji walizusha ghasia na hata wakachoma moto jumba hilo. Katika wonyesho mwingine wa muziki, vijana watatu walisongwa pumzi wakafa wakati maelfu ya mashabiki walipojisukuma kuelekea jukwaa, huku wakiangusha watu waliokuwa mbele na kuwakanyaga.

Katika muziki wa rapu, unaoitwa pia hipi-hopu, mwimbaji (au waimbaji) hurudia-rudia mashairi kwa kufuatana na mdundo wa kichini-chini wa muziki, mara nyingi mdundo huo ukifanyizwa kwa kurekodi sauti ya kurudia-rudia. Muziki mwingi wa rapu hufanyizwa na wanamuziki weusi lakini huuziwa wasikilizaji weusi na weupe pia. Ujumbe mchache wa rapu hufaa, ukipinga tabia kama kutendea watoto vibaya na matumizi mabaya ya dawa za kulevya. Hata hivyo, muziki mwingi wa rapu hukazia uasi dhidi ya mamlaka, ujeuri, kuchukia wanawake, na ubaguzi wa rangi. Muziki mwingi una maneno machafu na ufafanuzi mchafu wa ngono.

Ujeuri umekuwa tatizo katika maonyesho mengine ya muziki wa rapu. Katika wonyesho mmoja, genge lenye watu 300 walishambulia wahudhuriaji, ambao nao walilipiza kwa kutumia viti vya chuma mpaka polisi walipokuja na kukomesha wonyesho huo. Watu 45 walijeruhiwa.

Mwaka uliopita, Shirika la Wakuu wa Polisi wa Jimbo la New York waliomba watu wasusie makampuni yote ya Time Warner, Inc., mpaka kampuni hiyo ikome kuuza wimbo wa rapu unaoitwa “Cop Killer” (Mwuaji wa Polisi). Kiongozi wa shirika hilo la wakuu wa polisi, Peter Kehoe, alisema hivi: “Wimbo huo unatangaza chuki na kuendeleza na kutukuza kuua polisi. Tokeo la moja kwa moja la wimbo huo litakuwa ni kuuawa kwa polisi.” Hatimaye ulikoma kuuzwa.

Je! Kuna Athari?

Wanamuziki wanapoimba juu ya uovu au hata kuuigiza jukwaani, kitendo hicho kinawaathirije wasikilizaji na watazamaji? Ebu fikiria maelezo na maono yanayofuata.

Dkt. Karl Taylor, profesa mdogo wa sheria ya uhalifu katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan, akazia kwamba wanamuziki mashuhuri wa roki “wanaendeleza mtindo fulani wa maisha. . . . Washiriki wa beni kwa kweli hushawishi watoto, sana sana.”

Mvulana mmoja aliyeokoka jaribio la kujiua alisema kwamba muziki ulipotosha yeye na rafiki yake (aliyefaulu kujiua) wafikirie kwamba “suluhisho kwa matatizo ya maisha ni kifo.”

Katika 1988, vijana watatu waliua rafiki yao kwa kujifurahisha tu. Mmoja wao alisema kwamba uvutio wake kwa kifo ulianza na muziki wenye mdundo mzito.

Baada ya wonyesho mmoja wa muziki wa rapu, vijana walivunja-vunja vioo katika sehemu za umma. Mkuu wa usalama wa umma wa Pittsburgh, Pennsylvania, alisema hivi: “Sina shaka lolote kwamba muziki wa rapu huchochea ujeuri.”

Uchunguzi mmoja wa vijana na madhehebu ya kishetani ulifunua kwamba wengi wa wale wanaojihusisha na ibada ya Ibilisi hutumia sana dawa za kulevya na husikiliza muziki wenye mdundo mzito, unaotukuza matumizi ya dawa za kulevya na kutia moyo ukosefu wa adili katika ngono. Matokeo ni kwamba, vijana wasiokuwa na kinga wanavutiwa na madhehebu ya kishetani.

Bila shaka, vijana wanapojiingiza katika dawa za kulevya, uhalifu, au kujiua, kuna uwezekano wa visababishi vingine zaidi vya tabia hizo mbali na muziki. Kuvunjika kwa maisha ya familia na kwa jamii ya kibinadamu kwa ujumla bila shaka huchangia kwa sehemu kubwa kutokea kwa tabia kama hizo. Lakini muziki waweza kutumika ukiwa kichocheo cha kuwatia moyo vijana wasio na kinga wafanye mambo ambayo huenda hata wasiwazie kufanya. Je! watu ambao tayari wameshuka moyo kwa sababu ya matatizo ya maisha wanahitaji muziki unaowatia moyo wakubali mielekeo yenye kuharibu?

Ukweli ni kwamba muziki mbaya waweza kuwa sumu ya akili kwa wasikilizaji wao. Kumbuka, ujumbe mbalimbali katika muziki kama huo ni wenye nguvu hata zaidi kwa sababu unatoka kwa watu mashuhuri, mashujaa, ambao karibu wanaabudiwa na mashabiki wao.

Vipi Wewe?

Wewe husikiliza muziki wa aina gani? Labda tayari wewe ni mwangalifu kwa muziki unaochagua, na unastahili pongezi kwa jambo hilo. Kwa upande mwingine, ikiwa wewe ni mmoja wa wale wanaosikiliza muziki ambao umepotoka au ambao ni wenye kutilika shaka, je, umeathiriwa vibaya sana? Hata kama tabia yako haijabadilika, je, waweza kusema kwa unyoofu kwamba mwelekeo wako haujaathiriwa kuwa mbaya zaidi? Kwa vyovyote, kusikiliza kwa kurudia-rudia mambo yasiyofaa kwaweza kufisha dhamiri yako, kukikufanya uhisi kwamba mambo hayo si mabaya sana.

Ebu fikiria mfano wa kijana mmoja aliyejaribu kupatanisha maisha yake akiwa Mkristo na tabia ya kusikiliza muziki wenye mdundo mzito na rapu. Yeye hakufikia hatua ya kuua, kujiua, au ya ibada ya Ibilisi. Lakini ona jinsi mwelekeo wake ulivyoathiriwa. Yeye alisema hivi: “Muziki huu ni wa kinyama kabisa. Ulinifanya kuwa mtulivu na mwenye utaratibu huku nikiruhusu mielekeo mibaya na yenye jeuri zaidi. . . . Niliishi katika ulimwengu wa mawazio wenye chuki. Hakuna siku hata moja iliyopita bila mimi kufikiri kwa uzito juu ya kujiua.” Aliamua kufanya mabadiliko makubwa kwa yale aliyokuwa akisikiliza. Alipofanya mabadiliko hayo, alikuwa na maendeleo makubwa sana katika mtazamo wake.

Wenye kutetea muziki ambao umepotoka watabisha kuwa muziki wa roki ni sawa. Lakini umeamua nini? Je! waweza kuacha kutazama na kusikiliza mambo yao yenye kupotoka sana? Je! waweza kuhudhuria maonyesho ya muziki kama yale yaliyosimuliwa mapema bila kuhofia usalama wako? Na vipi juu ya uhusiano uliopo kati ya muziki kama huo na matendo ya aibu ya wanamuziki na wasikilizaji wao?

Ikiwa unajali afya yako, yaelekea kwamba unaepuka vyakula vinavyoweza kukudhuru hata kama ni vitamu. Muziki usiofaa, uwe ni roki au wa aina nyingineyo, ni tisho kwa afya ya akili yako. Je! ungependa kujihatarisha kwa vitumbuizo vyenye sumu ya akili? Bila shaka sivyo. Kwa hiyo, waweza kufanya nini ili uwe na maoni timamu, na yaliyo na usawaziko juu ya jambo hilo? Tafadhali fikiria mambo yanayotokezwa katika makala inayofuata.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Ibada ya Ibilisi ni Nini

Ibada ya Ibilisi, inayoendelezwa na baadhi ya maneno ya muziki wenye mdundo mzito, si raha isiyodhuru. Jarida Texas Medical/The Journal lilieleza kwamba ibada kama hiyo hutia ndani tabia zinazoanzia ”desturi zisizodhuru hadi kunywa damu inayotoka kwenye sehemu ambazo mmoja anajikatakata na kwenye dhabihu za wanyama.” Madhehebu ya kishetani hutangaza ”utii kwa Ibilisi. Desturi nyinginezo hususa hutumiwa ili kupata nguvu kutoka kwa Shetani hadi kwa wafuasi....Wazo la uhuru wa kuchagua na wa hiari wamaanisha kufanya chochote unachotaka bila kumfikiria Mungu, bila hisi ya hatia, na bila dhamiri.” Kama tokeo, wengine hushiriki katika uhalifu kuona haya.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Usingeingiza takataka tumboni mwako. Kwa nini uiweke akilini mwako?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Je! wapaswa kujihisi starehe kuhudhuria tukio kama hili?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki