Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ulemavu Makala ya “Vijana Wanauliza . . . Kwa Nini Niteseke kwa Ulemavu?” (Mei 22, 1993) ilishughulikia tatizo hilo kwa uhalisi. Nimelemaa katika miguu yote miwili na nina hisia nyepesi watu wanaponitazama kwa kunihurumia. Kile kinachoumiza zaidi ni wakati mtu anaponipa upaji—kana kwamba mimi ni mwombaji! Kile kinachonifariji ni kujua kwamba Yehova huwa hatazami hali ya kimwili bali “huutazama moyo.”—1 Samweli 16:7.
A. A. A. S., Brazili
Ni lazima nipinge jambo mlilosema kwamba kupooza kwa ubongo ni ugonjwa. Kupooza kwa ubongo ni hali inayosababishwa na dhara kwa ubongo, kunakotukia hasa kabla, wakati, au muda mfupi baada ya kuzaliwa. Huwa hauzidi kuwa mbaya zaidi wala hauambukizwi. Si ugonjwa na haipasi kurejezewa hivyo.
L. Z., United States
Twasikitika ikiwa uteuzi wetu wa maneno ulikuudhi. Tulitumia neno “ugonjwa” katika maana ya kawaida kabisa inayotolewa katika “Kamusi ya Kiswahili Sanifu,” yaani, “kitu kinachosababisha mtu . . . kuwa katika afya mbaya.”—MHARIRI.
Uchinjaji wa Wanawake Asanteni kwa kufunua jinsi mazoea ya kuchinja viungo vya uzazi vya wanawake kulivyo jambo la kishetani, linalochukiza! (“Mamilioni Wanateseka—Je! Wanaweza Kusaidiwa?” Aprili 8, 1993) Ikiwa mtoto mmoja tu aweza kulindwa asipatwe na uhalifu huo wa ukimya, na usiri, basi kutangaza makala hiyo kutakuwa kumethibitika kuwa kumestahili.
J. C., United States
Macho yangu yalijawa na machozi kwa kuwaza kwamba wazazi huletea watoto wasio na kinga mateso hayo. Habari kama hizo hazichapwi katika magazeti yetu ya habari, kwa hiyo ninawashukuru kwa kutupatia habari za karibuni.
C. C. G. M., Brazili
Kazi ya Shule ya Kufanyia Nyumbani Asanteni sana kwa makala yenu “Vijana Wanauliza . . . Nifanye Nini Kuhusu Kazi Nyingi ya Shule ya Kufanyia Nyumbani?” (Aprili 8, 1993) Nilisoma makala hiyo wakati nilipokuwa chini ya mkazo mwingi sana wa kazi ya shule ya kufanyia nyumbani. Sikuwa na wakati wa kustarehe au kutayarisha mikutano ya Kikristo. Sasa ninatumia madokezo yenu.
M. H., United States
Kuhamia Kwingine Nina furaha kutoa shukrani zangu kwa makala “Vijana Wanauliza . . . Je! Nihamie Nchi Yenye Utajiri Zaidi?” (Aprili 22, 1993) Nina miaka 16 na nimefikiria kuhamia nchi ambako ninaweza kufanikiwa maishani. Lakini baada ya kusoma makala hiyo, ninahisi kwamba haidhuru tunaishi wapi. Tukitanguliza Ufalme wa Yehova maishani, kwa kweli tutafanikiwa [kiroho] kwa kuwa Yehova atatusaidia.
V. L. A., Brazili
Kunajisiwa Nilikuwa na hisia zilizochanganyika wakati nilipopokea toleo la Machi 8, 1993, juu ya “Kunajisiwa—Hofu Kuu ya Wanawake.” Waona, mama yangu, ambaye ni mweneza evanjeli wa wakati wote kwa miaka mingi, alishambuliwa vibaya na kukawa majaribu ya kumnajisi nyumbani mwake mwenyewe. Kusoma makala hizo kumesaidia kuendelea kupona.
P. G., United States
Mimi ni mkurugenzi mdogo wa shirika la “Huduma za Jeuri ya Familia na Mashambulizi ya Kingono” la hapa kwetu. Mmoja wa watumishi wenu wachanga alitufanya tuanze kusoma Amkeni! alipoleta toleo juu ya kutenda watoto vibaya kingono. (Oktoba 8, 1991, Kiingereza) Sasa tumeandikisha. Nataka kuwajulisha jinsi nilivyovutiwa na matoleo yenu juu ya jeuri ya nyumbani na kunajisiwa. Yaliandikwa vema na kufanyiwa utafiti mwingi sana.
D. G., United States