Kuutazama Ulimwengu
Wauaji wa Watoto
Maradhi matatu husababisha karibu theluthi mbili za vifo milioni 13 miongoni mwa watoto katika nchi zinazositawi kila mwaka, likasema gazeti la Afrika Lesotho Today. Maradhi hayo ni kichomi, kuhara, na surua. Ripoti hiyo yaongezea kwamba maradhi kama hayo yaweza kuponywa au kuzuiwa kwa dawa zinazopatikana na zenye gharama ya chini. Kwa kielelezo, kichomi, muuaji mkubwa zaidi ya wote wa watoto, husababisha vifo vya watoto milioni 3.5 kila mwaka. Katika visa vingi tatizo huwa la kibakteria na hilo laweza kudhibitiwa kwa kutumia mfululizo wa dawa za kuua vijidudu wenye kuchukua muda wa siku tano na kugharimu senti 25 za (U.S.). Kuhara huua watoto milioni tatu kila mwaka. Karibu nusu ya vifo hivyo vyaweza kuzuiwa wazazi wakitumia unyweshwaji maji yenye chumvi na sukari wenye gharama ndogo. Surua husababisha vifo vya watoto 800,000 kila mwaka. Ripoti hiyo yaonyesha kwamba hilo laweza kuzuiwa kupitia chanjo. Dawa ya chanjo ya surua hugharimu chini ya senti 50 kwa kila mtoto.
Kifo kwa Bunduki
Kwa kila vifo 4 miongoni mwa vijana Waamerika, kifo 1 huhusisha bunduki. Kulingana na Kitovu cha Taifa cha Takwimu za Afya, kama ilivyoripotiwa katika International Herald Tribune, bunduki huua vijana wengi zaidi wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 kuliko visababishi vingine vyote vya vifo vikijumlishwa. Ni aksidenti za magari pekee zinazoua watu wengi zaidi wenye miaka hiyo. Katika kipindi cha 1990, mwaka wa karibuni zaidi ambao takwimu zao zimekamilika, idadi ya matineja waliokufa kwa risasi katika visa vya mauaji, kujiua, au aksidenti ilikuwa karibu 4,200. Katika 1985 idadi ilikuwa karibu 2,500.
Je! Dunia Yaweza Kuokolewa?
Hakuna jambo lolote ila tu mabadiliko makubwa katika sera za serikali na mielekeo ya watu liwezalo kuokoa mazingira ya dunia isiharibiwe, kulingana na ripoti moja kutoka Taasisi ya Worldwatch. Ripoti hiyo yaonya kwamba matatizo kama ukuzi wa idadi ya watu, kuongezeka kwa karboni, na kupungua kwa tabaka ya ozoni, kupotea kwa misitu, na mmomonyoko wa udongo yakidumu, kutakuwa na watu wengi duniani bila viasili vingi vya kuwategemeza. Pia inataja kwamba programu za kutengeneza vitu upya na za uhifadhi hupunguza tatizo hilo lakini kwamba hatua hizo zilizochukuliwa hazitoshi. Ili kuwe na suluhisho kubwa, mabadiliko makubwa ya serikali, viwanda, na umma yahitajiwa.
Kupigana na Kipindupindu
Siki ya divai nyekundu yaweza kuzuia mweneo wa kipindupindu, kulingana na gazeti la Brazili Manchete. Jaribu lililofanywa na Taasisi ya Chakula ya Katibu ya Kilimo na Ugawanyaji ya São Paulo lilifunua kwamba siki ya divai nyekundu ina matokeo kuliko chokaa ya kuua wadudu kwa mara mia moja katika kuua wadudu kwenye mboga zilizoambukizwa. Gazeti hilo laripoti kwamba siki ilipunguza bakteria ya kipindupindu katika mboga ya letasi kwa kiwango cha mara 10,000 huku maji ya klorini yakifanya hivyo kwa kiwango cha mara 100 pekee. Kiasi kinachopendekezwa ni mchanganyiko wa vijiko vikubwa vitano vya siki kwa lita moja ya maji.
Mama Wenye Mkazo wa Akili Mwingi Mno
Ni kikundi kipi cha wakazi wa Ujerumani ambacho hupatwa zaidi na mkazo wa akili kuliko vikundi vingine vyote? Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Idara ya Kitiba ya Kisoshiolojia ya Chuo Kikuu cha Dawa kilichoko Hanover, “kwa ujumla akina mama hupatwa na mkazo na msononeko zaidi wa kiakili na wa kimwili kuliko kikundi kingingecho chote cha wakazi.” Gazeti Nassauische Neue Presse, lililoripoti juu ya uchunguzi huo, lilitaja kwamba “akina mama huenda kwa daktari wakiwa na hisia za mkazo, maumivu ya tumbo, hangaiko, na kupoteza usingizi zaidi ya mara mbili kuliko washiriki wengine wa vikundi vingine vya wakazi.” Wakishapata mashauri ya daktari, mama wengi hupokea dawa za kupoesha uchungu, dawa za usingizi, na dawa nyinginezo. Katika visa fulani hilo hutokeza uzoelevu wa dawa.
Ujeuri wa Vijana—Kwa Nini?
“Mashtaka ya polisi wa Kanada dhidi ya vijana (wenye miaka 12-17) kwa uhalifu wa jeuri yameongezeka kwa zaidi ya mara mbili kwa kipindi cha miaka mitano ambayo imepita,” ladai gazeti The Toronto Star. Vitendo hivyo vya jeuri hufanywa pasipo sababu yoyote ya wazi. Kutazama tu macho kwaweza kutokeza tendo la jeuri dhidi ya msimama-kando asiye na hatia. Yaonekana kuwa jambo la “ujeuri bila sababu yoyote,” laongeza gazeti Star. Kisababishi ni nini? Watu fulani waamini kwamba kuna uhusiano kati ya visa vya ujeuri wa vijana na zile mandhari zenye jeuri zinazoonyeshwa katika sinema na kwenye televisheni. “Fungu la televisheni ni kufisha hisia na kufanya vijana wetu wafikiri kwa njia tofauti, na katika kutukuza ujeuri kuwa njia bora zaidi ya kusuluhisha matatizo,” lasema ga-zeti Star. Labda sasa wazazi wengi zaidi watataka kudhibiti mambo yale watoto wao huona katika televisheni.
“Jiji Kuu la Mauaji ya Kimakusudi Ulimwenguni”
“Johannesburg kwa kweli limepata sifa mbaya ya kuwa jiji kuu la mauaji ya kimakusudi ulimwenguni,” lasema The Star, gazeti la Afrika Kusini. “Kulingana na takwimu za polisi, Johannesburg na Soweto yakiwa pamoja yalikuwa na mauaji ya kimakusudi 3 402 katika 1992—mauaji ya kimakusudi 9,3 kila siku, au uuaji mmoja wa kimakusudi kila muda wa saa 2 1/2.” Hilo lilirudisha Rio de Janeiro, lililokuwa hapo awali “jiji kuu la mauaji ya kimakusudi” kwenye nafasi ya pili. Rio lilikuwa na wastani wa mauaji ya kimakusudi 8,722 kila mwaka kwa mwongo wa miaka uliopita. Hata hivyo, idadi ya wakazi wa Rio ni zaidi ya milioni 10, na jumla ya idadi ya wakazi wa Johannesburg na Soweto inasemwa kuwa milioni 2.2. Paris, lenye idadi ya watu inayokaribia Johannesburg, lilikuwa na wastani wa mauaji ya kimakusudi 153 kila mwaka. Uwezekano wa kuuawa kimakusudi ulitolewa kama ifuatavyo: 1 kwa 647 katika Johannesburg; 1 kwa 1,158 katika Rio de Janeiro; 1 kwa 3,196 katika Los Angeles; 1 kwa 4,303 katika New York; 1 kwa 6,272 katika Miami; 1 kwa 10,120 katika Moskow; na 1 kwa 14,065 katika Paris.
Tatizo Katika Makanisa
“Tatizo la kutenda vibaya kingono katika kanisa halitaisha,” laripoti The Toronto Star. Kashfa za kingono miongoni mwa viongozi wa kidini zimeenea sana. Hazifanywi na waeneza evanjeli wa televisheni na Kanisa Katoliki pekee. Matendo mabaya “yanafanywa [pia] katika Jeshi la Wokovu, katika United Church, katika Presbyterian Church,” akasema ofisa mmoja wa Jeshi la Wokovu. Askofu Mkuu wa Anglikana alisema kwamba matendo hayo mabaya ni tatizo lenye “kina sana na lililo baya” katika kanisa. Kulingana na Star, Askofu Mkuu Peers alikiri kwamba kwa muda ambao umepita itikio la kanisa hilo kwa mashtaka ya kutenda vibaya kingono “limekuwa ni kukanusha na udhibiti.” Yaripotiwa kwamba Timothy Bently kutoka Kituo cha Toronto cha Familia alitaja kwamba kama “makanisa hayawezi kukabili tatizo hili ambalo hasa ni la kiroho kwa njia ya wazi na kwa haki mamlaka yao ya kuhubiri juu ya maadili ya kingono yatakwisha.”
Ibada ya Panya?
Kila siku, waabudu wapatao 1,000 na watalii wapatao 70 huzuru hekalu la Karni Mata katika Deshnoke, India. Kwa nini? Katika hekalu hilo panya wapatao 300 huzurura-zurura bila matatizo huku waumini wakitoa upaji wao kwa sanamu. Panya hao “waheshimiwa sana na kila uhitaji wao huandaliwa na waabudu wenye kuwastahi sana,” lasema gazeti Evening Post la New Zealand. Makuhani wa hekalu pamoja na panya hao hula kutoka kwenye bakuli zilezile na kunywa maji yaleyale. Mmoja wa makuhani adai kwamba “hao si panya, hao ni wajumbe wa Mungu, zawadi ya kijimungu-kike kwetu.” Kulingana na Post, kuhani huyo alisema kwamba makuhani wa hekalu wanapokufa, wao hupata wokovu na kuzaliwa tena wakiwa panya. Panya hao wanapokufa, aliongeza kusema, wao huzaliwa tena wakiwa makuhani.
Ukosefu wa Starehe Hewani
Kusafiri kwa ndege “kumekuwa chanzo chenye kuendelea cha maumivu, ukosefu wa starehe na hata magonjwa miongoni mwa abiria na wafanyakazi wa ndege katika miaka ya karibuni,” ladai The New York Times. Baada ya safari ya muda wa saa kadhaa katika viti vilivyofinyana, wasafiri wameripoti mgandamano wa damu katika mapafu, maumivu ya mgongo, mafua, maumivu ya kichwa, kutaka kutapika, na kichomi. Kupoteza maji ni tatizo jingine. “Kiwango cha unyevu kwa kawaida kikiwa karibu asilimia 10, hali ya hewa katika ndege huwa imekauka kuliko Sahara,” lasema gazeti Times. Dalili za kupoteza maji zatia ndani kushikamana kwa damu, uchovu usio na sababu, na kuumwa macho. Pia, kukauka kwa vijia vya juu vya kupumua huvifanya viwe rahisi zaidi kupatwa na ambukizo. Gazeti hilo lapendekeza kunywa maji glasi moja kwa kila muda wa saa moja ya safari ya ndege ili kuzuia kupoteza maji.
Ghadhabu Juu ya Ugoni wa Maharimu Katika Ailandi
Kituo cha Tatizo la Unajisi cha Dublin chasema kwamba hesabu ya visa vilivyoripotiwa vya kutenda watoto vibaya kingono katika Ailandi imeongezeka kutoka 408 katika 1984 hadi 2,000 katika 1992. Kisa kimoja chenye ukatili sana cha ugoni wa maharimu kilichotokea huko kimetokeza ghadhabu nchini kote. Baba mmoja mwenye uzoevu wa pombe kali iitwayo poteen, alimnajisi na kumshambulia binti yake mara kwa mara kwa kipindi kinachozidi miaka 16 na kupata mtoto naye. Alimpofusha jicho moja kwa kumpiga kwa fimbo. Na kama ilivyo kawaida kwa visa kama hivyo, mama ya msichana huyo alijua juu ya ugoni huo wa maharimu lakini alidanganya polisi ili alinde mume wake; majirani vilevile walijua juu ya hali ya msichana huyo lakini hawakufanya jambo lolote kumsaidia. Ingawa mtu huyo alikiri mashtaka ya unajisi, ugoni wa maharimu, na mashambulizi, hakimu aliliona jambo hilo kuwa tu ugoni wa maharimu. Baba huyo alifungwa jela miaka saba, adhabu kali zaidi kwa mashtaka ya ugoni wa maharimu, na anaweza kufunguliwa baada ya miaka minne. Wakighadhabika juu ya kesi hiyo, Wakatoliki wengi Waailandi wanataka kanisa liseme kihususa dhidi ya ugoni wa maharimu.