Wauaji-Wasiozuilika
MARGARET alitafuta dawa kwa bidii wakati mwana wake Tito alipopata malaria. Dawa aina tatu, kutia ndani “chloroquine” yenye kusifiwa sana zilitumiwa. Hata hivyo, Tito alikufa—akiwa na umri wa miezi tisa pekee.
Katika Kenya, nchi anakoishi Margaret, msiba kama huo hutokea sana. Gazeti “Newsweek” laripoti hivi: “‘Anopheles gambiae,’ yule malkia wa mbu wasababishao malaria, husitawi sana katika sehemu hii ya ulimwengu. Lakini watoto hawasitawi. Asilimia tano kati yao hufa kwa malaria kabla ya kufikia umri wa kwenda shule.”[1]
Katika 1991 maradhi ya kifua-kikuu yaliua wafungwa 12 na mlinzi mmoja katika Jimbo la New York, U.S.A. “Tutayadhibiti katika magereza,” asema Dakt. George DiFerdinando, Jr., “lakini tatizo kubwa ni yatadhibitiwaje kwa vile sasa yamesitawi katika jumuiya?”[2]
Shirika la Afya Ulimwenguni laripoti kwamba watu bilioni 1.7—karibu theluthi moja ya idadi ya watu ulimwenguni—wana bakteria ya kifua-kikuu.[3] Watu milioni nane kati yao husitawisha maradhi hayo kila mwaka, na milioni tatu hufa.[4]
Katika hospitali moja ya New York, kisichana kimoja kilizaliwa majuma 11 kabla ya wakati wacho, lakini hilo lilikuwa sehemu tu ya tatizo lacho. Ngozi yenye kubambuka ya mikono yacho, vidonda vya miguu yacho, ini na wengu vilivyopanuka, vyote vilitoa uthibitisho wa wazi kwamba kisichana hicho kilikuwa kimepata kaswende kilipokuwa tumboni mwa mama yacho.
“Watoto fulani huharibiwa sana na maradhi hayo wakiwa tumboni mwa mama zao kiasi cha kwamba wao huzaliwa wakiwa wamekufa,” laripoti “The New York Times.” “Wengine wachache hufa punde tu baada ya kuzaliwa, wengine wakiwa na majeraha mabaya ya ngozi yanayopasuka wakati wa kuzaliwa.”[5]
Malaria, kifua-kikuu, na kaswende—maradhi hayo yote matatu yalifikiriwa kuwa yamedhibitiwa na kukaribia kuondolewa kabisa katika miongo michache iliyopita. Kwa nini maradhi hayo yamerudi tena kwa njia yenye uharibifu mkubwa?