Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 12/8 kur. 4-7
  • Kwa Nini Maradhi “Yanayoponyeka” Yamerudi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kwa Nini Maradhi “Yanayoponyeka” Yamerudi?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Malaria—Yatisha Karibu Nusu ya Watu wa Ulimwengu
  • Kifua-Kikuu—Muuaji wa Kale Mwenye Mbinu Mpya
  • Kaswende—Kurudi Kwayo Kwenye Hatari
  • Je! Mwisho Wayo U Karibu?
  • Kifua Kikuu Charudi kwa Pigo!
    Amkeni!—1996
  • Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu
    Amkeni!—1999
  • Shangwe ya Ushindi na Huzuni
    Amkeni!—1997
  • Wauaji-Wasiozuilika
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 12/8 kur. 4-7

Kwa Nini Maradhi “Yanayoponyeka” Yamerudi?

NYUMBA imetoka tu kusafishwa kabisa. Hata hivyo, siku, majuma, na miezi ipitapo, mavumbi na uchafu hurudi hatua kwa hatua. Kwa hiyo, usafishaji mmoja mkubwa hautoshi. Usafishaji wa kuendelea ni muhimu sana.

Kwa wakati fulani ilionekana kama dawa za kisasa zilikuwa zimeondoa kabisa malaria, kifuakikuu, na kaswende. Lakini mara nyingi kuyaondoa kwa usafishaji wa kuendelea kupitia utafiti na tiba kulipuuzwa. Sasa “mavumbi na uchafu” umetokea tena. “Hali ya malaria ni mbaya na inazidi kuwa mbaya zaidi duniani pote,” asema Dakt. Hiroshi Nakajima wa WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni). “Ni lazima watu watambue kwamba maradhi ya kifua-kikuu yamerudi—na yamerudi kwa ghadhabu nyingi,” aonya mtaalamu wa kifua-kikuu Dakt. Lee Reichman.[2] Na gazeti The New York Times lilitangaza hivi mapema katika mwongo huu: “Visa vipya vya kaswende vimefikia kiwango cha juu zaidi tangu 1949.”[3]

Malaria—Yatisha Karibu Nusu ya Watu wa Ulimwengu

Sasa, karibu miaka 40 tangu itangazwe kuwa karibu imetoweshwa,[4] malaria yatisha sana katika Afghanistan, Brazili, India, Indonesia, Kambodia, Sri Lanka, Thailand, Uchina, Vietnam, na sehemu kadhaa za Afrika.[5] “Watoto wawili hufa kutokana na ambukizo hilo kila dakika,” laripoti gazeti la Ufaransa Le Figaro.[6] Jumla ya vifo kila mwaka ni milioni mbili—wengi zaidi ya wale wanaouawa kwa UKIMWI.[7]

Watu wakaribiao milioni 270[8] wameambukizwa kimelea cha malaria, lakini watu bilioni 2.2 huonwa kuwa katika hatari ya kuambukizwa malaria.[9] “Inakuwaje kwamba malaria, ambayo wakati mmoja ilikuwa imeangamizwa au kudhibitiwa sana kwa asilimia 90 ya idadi ya watu ulimwenguni, sasa yatisha zaidi ya asilimia 40 yetu?” auliza Phyllida Brown katika gazeti New Scientist.[10] Kuna sababu nyingi.

Kufyekwa kwa misitu na kutwaliwa kwa maeneo mapya. Kuishi kwa watu katika misitu ya mvua yenye kujaa mbu kumetokeza ongezeko kubwa la malaria katika Brazili. “Tulikuwa tumevamia mazingira ya mbu,” asema mstadi wa kinga ya mwili Claudio Ribeiro. Yeye asema kwamba walowezi “hawakujua malaria wala hawakuwa na kinga ya maradhi hayo.”[11]

Uhamiaji. Wakimbizi kutoka Myanmar wanaotafuta kazi huja kwa wingi katika migodi ya vito vyenye thamani ya Borai, ambao ni mji mdogo katika Thailand.[12] “Kuhama kwao kwa daima hufanya kudhibiti malaria kusiwezekane,” laripoti Newsweek.[13] Visa vya malaria vipatavyo 10,000 hurekodiwa kila mwezi—miongoni mwa wachimba migodi pekee![14]

Utalii. Watu wengi ambao huzuru sehemu zenye malaria hurudi nyumbani wakiwa wameambukizwa. Hivyo, katika 1991 visa vipatavyo 1,000 viligunduliwa katika United States na visa 10,000 katika Ulaya.[15] Kila mwaka mamia ya watalii na wafanyakazi wa nchi za ng’ambo hurudi Kanada wakiwa wameambukizwa. Katika kisa kimoja chenye msiba, watoto wawili walishikwa na homa-kali punde tu baada ya familia yao kurudi kutoka Afrika. Daktari hakudhani ni malaria. “Kufikia wakati wazazi wao walipowapeleka hospitali, kulikuwa kumechelewa mno,” laripoti Globe and Mail la Toronto. “Walikufa mmoja baada ya mwingine kwa muda wa saa chache.”[16]

Aina za malaria zenye kukinza dawa. Shirika WHO laripoti kwamba aina fulani za malaria zenye kukinza dawa zimeenea katika sehemu zote za tropiki ya Afrika.[17] Katika Asia ya Kusini-Mashariki, lasema Newsweek, “ukinzaji wa dawa unaenea haraka sana hivi kwamba karibuni aina fulani za [malaria] hazitaweza kutibika.”[18]

Ukosefu wa Vifaa. Katika sehemu nyingi hospitali hukosa vifaa vya kufanya upimaji sahili uitwao mpako-damu.[19] Katika sehemu nyinginezo sehemu kubwa ya matumizi ya fedha kwa ajili ya afya huhitajiwa kwa mambo mengine ya dharura, hilo likitokeza upungufu wa dawa za kuua wadudu na dawa za tiba.[20] Nyakati nyingine linakuwa suala juu ya kupata faida. “Hakuna faida katika kutibu maradhi ya kitropiki,” lakiri New Scientist, “kwa sababu kwa ujumla, wale wanaoathiriwa hawawezi kugharimia madawa.”[21]

Kifua-Kikuu—Muuaji wa Kale Mwenye Mbinu Mpya

Streptomycin, dawa iliyoahidi kuwa ingedhibiti kifua-kikuu, ilianza kutumiwa katika 1947.[22] Wakati huo, ilifikiriwa kwamba maradhi ya kifua-kikuu yangemalizwa kabisa. Lakini nchi fulani zimeshtuliwa na hali ya hatari: kwani viwango vya kifua-kikuu vimeongezeka sana katika miaka ya karibuni. “Katika maeneo ambayo umaskini umeenea katika Amerika,” laripoti The Washington Post, “viwango vya kifua-kikuu ni vya juu zaidi ya viwango vilivyoko nchi za Afrika zenye umaskini zaidi zilizoko kusini mwa Sahara.”[23] Nchini Côte d’Ivoire kuna tukio ambalo jarida moja laliita “kurudi kwa kifua-kikuu kwa njia ya kikatili.”[24]

Dakt. Michael Iseman aomboleza hivi: “Tulijua jinsi ya kuyaponya. Tulikuwa tumeyadhibiti. Lakini tulishindwa kuyaangamiza kabisa.”[26] Ni nini kilichozuia pigano dhidi ya kifua-kikuu?

UKIMWI. Kwa sababu maradhi hayo hufanya mtu apoteze kinga dhidi ya ambukizo, UKIMWI huonwa kuwa kisababishi kikuu cha kurudi kwa kifua-kikuu.[27] “Wasipokufa kutokana na kisababishi kingine kwanza,” asema Dakt. Iseman, “karibu asilimia 100 ya wagonjwa wa UKIMWI wenye bakteria ya kifua-kikuu watakuwa na ugonjwa huo.”[28]

Mazingira. Magereza, makao ya kutunzia wagonjwa, makao ya wasio na makao, hospitali, na mashirika mengine yaweza kuwa sehemu zenye kusitawisha kifua-kikuu.[29] Dakt. Marvin Pomerantz asimulia kwamba matumizi ya aina moja ya tiba ihususuyo pumzi katika hospitali moja yaliongeza kukohoa kwa wagonjwa wenye kichomi na hivyo yakatokeza mweneo mkubwa wa kifua-kikuu miongoni mwa wafanyakazi wa hospitali hiyo.[30]

Ukosefu wa fedha. Mara ilipoonekana kwamba maradhi ya kifua-kikuu yalikuwa yamedhibitiwa, msaada wa kifedha ulikoma, na uangalifu wa umma ulielekezwa mahali pengine.[31] “Badala ya kuondoa kifua-kikuu,” asema Dakt. Lee Reichman, “tuliondoa programu za kifua-kikuu.”[32] Mbiolojia-kemia Patrick Brennan asema hivi: “Mapema katika miaka ya 1960 nilifanya kazi kwa bidii juu ya dawa ya kukinza kifua-kikuu lakini niliamua kuacha kwa sababu nilifikiria maradhi ya kifua-kikuu yalikuwa yameponyeshwa.”[33] Hivyo, madaktari wengi hawakutazamia kurudi kwa kifua-kikuu. “Katika juma moja [katika vuli ya 1989],” tabibu mmoja akasema, “niliona visa vipya vinne vya ugonjwa huo ambao mwalimu wangu wa shule ya tiba alisema sitapata kuuona tena.”[34]

Kaswende—Kurudi Kwayo Kwenye Hatari

Yajapokuwa mafanikio ya penisilini, maradhi ya kaswende bado yameenea katika Afrika.[35] Katika United States, yanarudi kwa nguvu zaidi kuliko miaka 40 iliyopita. Kulingana na The New York Times, kaswende sasa “yanapumbaza kizazi cha madaktari ambao ama wameyaona mara chache sana ama hawajapata kuyaona.”[36] Ni kwa nini yamerudi?

“Crack” (aina ya kokeini kali). Uzoelevu wa Crack umeanzisha jambo ambalo daktari mmoja aliita “matumizi makubwa sana ya kokeini na ngono.”[37] Ingawa mara nyingi wanaume huiba ili kutegemeza uzoelevu wao, wanawake wanaelekea zaidi kufanya umalaya ili kupata dawa za kulevya.[38] “Katika majumba ya kuuza crack,” asema Dakt. Willard Cates, Jr., wa Vituo vya Kudhibiti Maradhi vya U.S., “kuna kufanya ngono pamoja na wenzi wengi. Ambukizo lolote lenye kuenea sana katika mazingira hayo litakuwa ndilo lenye kupitishwa.”[39]

Ukosefu wa Kinga. “Ijapokuwa ile kampeni ya ‘ngono salama,’” laripoti gazeti Discover, “matineja bado ni wazembe katika kutumia kondomu za kujikinga na maradhi.”[40] Uchunguzi mmoja katika United States ulifunua kwamba ni asilimia 12.6 pekee kati ya wale wafanyao ngono na wenzi wanaoweza kuwa na maradhi hutumia kondomu daima.[41]

Ukosefu wa fedha. The New York Times lataarifu hivi: “Kupunguzwa kwa matumizi ya fedha kumepunguza uwezo wa kliniki za umma ambako kaswende nyingi na maradhi mengine yapitishwayo kingono hugunduliwa.”[42] Kwa kuongezea, njia za upimaji si sahihi nyakati zote. Katika hospitali moja mama kadhaa walizaa watoto walioambukizwa, ilihali damu za mama hao zilizopimwa hapo awali hazikuonyesha kuwapo kwa kaswende.[43]

Je! Mwisho Wayo U Karibu?

Vita ya mwanadamu dhidi ya maradhi imekuwa ndefu na yenye kufadhaisha. Mara nyingi sana mafanikio katika kupigana na magonjwa fulani hubatilishwa na kule kushindwa katika vita dhidi ya magonjwa mengine. Je! mwanadamu ataendelea daima kupigana vita asiyoweza kushinda kamwe? Je! kweli kutapata kuwa na ulimwengu bila maradhi?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Madhara ya Kaswende

KASWENDE husababishwa na Treponema pallidum, spiroketi (kijidudu) yenye umbo la parafujo, na mara nyingi hupatwa kupitia viungo vya uzazi. Kisha spiroketi hiyo huingia katika mkondo wa damu na kuenea mwilini mwote.

Majuma kadhaa baada ya ambukizo, kidonda kiitwacho pangusa hutokea. Kwa kawaida kidonda hicho hutokea kwenye viungo vya uzazi lakini chaweza kutokea kwenye midomo, matezi ya kooni, au kwenye vidole. Hatimaye pangusa hupona yenyewe ikiacha kovu. Lakini vijidudu huendelelea kuenea kotekote mwilini mpaka dalili za pili zitokee: vipele vya ngozi, maumivu ya koo, maumivu ya mafundo, kupoteza nywele, vidonda, na kufura kwa macho.

Yasipotibiwa, maradhi ya kaswende huingia katika hali-zimwe ambayo yaweza kubaki maishani mwote. Mwanamke akiwa mja-mzito katika kipindi hicho, mtoto wake aweza kuzaliwa kipofu, mlemavu, au akiwa amekufa.

Miongo ya miaka baadaye, watu wengine wataingia katika kipindi cha baadaye cha kaswende, kipindi ambacho spiroketi hiyo huweza kukaa moyoni, ubongoni, katika uti wa mgongo, au sehemu nyinginezo za mwili. Spiroketi hiyo ikikaa ubongoni, yaweza kusababisha degedege, kupooza kwa ujumla, na hata kurukwa akili. Hatimaye, maradhi hayo yaweza kuua.

[Hisani]

Biophoto Associates/Science Source/Photo Researchers

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

“Mwigaji Mkubwa”

SPL/Photo Researchers

HIVYO ndivyo Dakt. Lee Reichman ayaitavyo maradhi ya kifua-kikuu. “Yaweza kufanana na mafua, mkamba, homa,” yeye asema. “Kwa hiyo isipokuwa daktari awe anafikiria kifua-kikuu, huenda akakosa kuyagundua.”[1a] Eksirei ya kifua huhitajika ili kuthibitisha ambukizo.[1b]

Kifua-kikuu hupitishwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kupitia hewa. Kohozi laweza kutokeza visehemu vidogo sana viwezavyo kuingia mapafuni.[1c] Hata hivyo, kwa kawaida kinga ya mwili huwa na nguvu kiasi cha kuweza kuzuia ambukizo lisienee. Dakt. Reichman aeleza hivi: “Ni [wale] tu walio na bacillus (vijidudu) nyingi za kutosha katika matundu ya vifuani mwao—vijidudu milioni 100 tofauti na vijidudu vinavyopungua 10,000 kwa webebaji wasioambukiza—[wanaoweza] kueneza maradhi hayo.”

[Hisani]

SPL/Photo Researchers

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Joto Lenye Kuongezeka Duniani na Malaria

MARADHI ya malaria hayawezi kuanza bila yule mbu Anopheles gambiae aambukizaye. “Badili idadi ya [mdudu] huyo ayabebaye na utabadili kutokea kwa maradhi hayo,” laonelea The Economist.[1a]

Majaribio katika maabara yameonyesha kwamba maongezeko madogo-madogo katika halijoto yaweza kubadili sana idadi ya wadudu. Hivyo, wastadi fulani hukata kauli kwamba joto lenye kuongezeka duniani laweza kuongeza sana visa vya malaria.[1b] “Halijoto ya Dunia yote ikiongezeka hata kwa digrii Sentigredi moja au mbili,” asema Dakt. Wallace Peters, “yaweza kuongeza maeneo ambayo mbu hutagia mayai hivi kwamba malaria yaenee zaidi kuliko sasa.”

[Hisani]

Dakt. Tony Brain/SPL/Photo Researchers

[Picha katika ukurasa wa 6]

Makao ya wasio na makao yaweza kuwa mahali pa kusitawisha kifua-kikuu

[Hisani]

Melchior DiGiacomo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki