Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kashfa ya Utiaji Damu Mishipani
  • Watawa wa Kiume Watakikana
  • Nzige Warudi
  • Kuzuia Kujiua
  • Je! Yawezekana Kushika Mimba Baada ya Hedhi Kukoma?
  • Papa John 23 Alimsifu Mussolini
  • Misitu ya Mvua Iwezayo Kushika Moto
  • Viyoga Vyaelekea Kutoweka
  • Msingi wa Kuamini wa Kisayansi
  • Nguzo za Misri Zimo Hatarini
  • Je! Hii Ni Haki?
  • Kutumiwa Vibaya kwa Misitu ya Mvua
    Amkeni!—1998
  • Huzuni kwa Msitu Huo wa Mvua
    Amkeni!—1997
  • Kukabiliana na Komahedhi
    Amkeni!—1995
  • Kufunua Siri Zake
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kashfa ya Utiaji Damu Mishipani

Ujerumani, ambayo hutumia visehemu vingi zaidi vya damu kwa kila mtu kuliko nchi nyingine yoyote, imepata pigo kubwa la kashfa ambayo “imefanya mojayapo sehemu za ulimwengu za kutegemeka zaidi kitiba ishambuliwe sana,” gazeti Süddeutsche Zeitung laripoti hivyo.[1] Kashfa hiyo yahusu kampuni moja inayoshughulika na damu, ambayo kwa miaka kadhaa, imekuwa ikiuzia hospitali mbalimbali visehemu vingi sana vya damu ambavyo havikuwa vimechunguzwa ifaavyo.[2] Kwa hiyo, maelfu ya wagonjwa ambao wametumia visehemu hivyo vya damu wamo katika hatari ya kuambukizwa virusi HIV.[3] Waziri wa Afya wa nchi hiyo Horst Seehofer ametoa mashauri kwamba “mtu yeyote anayetaka kuhakikisha kwamba hajapata virusi HIV kupitia damu iliyoambukizwa au visehemu vya plazima wakati wa upasuaji” aende akachunguzwe.[4] Gazeti Die Zeit laripoti kwamba “asilimia 71 ya idadi yote ya watu sasa wanahofu kwamba wanaweza kupata UKIMWI kwa kutiwa damu mishipani.”[5]

Watawa wa Kiume Watakikana

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya kidini ya Japani, watawa wa kiume watasajaliwa kutoka kwa watu wa kawaida. “Mtu yeyote ambaye anamcha Mungu na asiye na mwelekeo wa kilimwengu aweza kuwa kuhani mkuu,” akasema mtawa mmoja wa kiume wa cheo cha juu wa dhehebu la Tendai la dini ya Buddha. Dhehebu hilo lapanga kuwa na “mtihani wa mchujo” kuanzia 1995 kwa wale wanaotaka kazi hiyo. Kulingana na ofisa mmoja wa dhehebu hilo, ujuzi kidogo wa dini wahitajiwa ili kupita mtihani huo. Kidesturi, wana wa makuhani walikuwa wakichukua wadhifa wa baba zao wakiwa makuhani wa hekalu. “Hata hivyo, hivi karibuni, wana wa makuhani katika madhehebu yote hawapendi kuwa watawa,” laripoti gazeti Mainichi Daily News. Akitoa maelezo juu ya hali hiyo, Hiroo Takagi, ambaye ni mstadi wa dini, alisema hivi: “Kwa vile sasa mfumo wa urithi unaharibika, madhehebu ya dini ya Buddha yana wasiwasi juu ya ukosefu wa vijana wanaotaka kuwa makuhani.”

Nzige Warudi

Pigo la nane la Misri, nzige, “wako tayari tena kushambulia Afrika,” laripoti gazeti The Weekly Mail & Guardian. Tayari hektari 80,000 zimeharibiwa katika Yemeni, na makundi tayari yamefika Chad, Niger, na Mali. Msemaji mmoja wa idara fulani ya utafiti wa kilimo alisema kwamba uharibifu huo waweza kuwa mkubwa zaidi ya lile pigo baya sana la 1986-87 lililoharibu mazao katika nchi 28 za kaskazini mwa Afrika. Yeye aliongezea hivi: “Hali za mazingira zikiwafaa nzige, makundi hayo yaweza kuongezeka mara kumi kwa kizazi kimoja tu (siku 45).” Nzige waweza kushambulia mazao yote ya chakula katika eneo la Sahel mwaka wa 1994.

Kuzuia Kujiua

“Kujiua kwa vijana kwaongezeka,” laripoti gazeti la Brazili O Estado de S. Paulo. Uchunguzi uliofanywa na Wizara ya Sheria ya Brazili waonyesha kwamba “sababu kuu ya kujiua ni ugonjwa, ukifuatwa na mapenzi yaliyovunjika, ulevi, na matatizo ya kifedha.” Kwa kuwa msaada wa washiriki wa familia na wa marafiki ni muhimu sana katika kuzuia kujiua, mtaalamu wa akili Christian Gauderer apendekeza hivi: “Usipuuze uwezekano” wa kujiua. Na kwa sababu uwasiliano waweza kuondoa mkazo wa akili, “uliza sababu zinazoleta mshuko wa moyo, mbona mtu huyo anafikiria kujiua, na jinsi anavyokusudia kufanya hivyo.”

Je! Yawezekana Kushika Mimba Baada ya Hedhi Kukoma?

Je! yawezekana kushika mimba baada ya hedhi kukoma? Jibu laonekana kuwa ndiyo, kulingana na ripoti ya kitiba katika gazeti la kila siku la Paris Le Figaro. Ripoti hiyo yasema kwamba “kwa wazi kuna idadi inayoongezeka ya wanawake wanaojikuta kuwa na mimba baada ya kuthibitishiwa kuwa wameacha kutokwa hedhi.” Uchunguzi huo wa Ufaransa, uliotia ndani madaktari wa wanawake na wakunga 6,000, ulifunua kwamba mwanamke ana uwezekano wa juu zaidi wa kushika mimba baada ya kukoma kwa hedhi ikiwa alikuwa akitumia tiba aina ya HRT (tiba ya kuongeza hormoni). Ikichunguzwa kwa njia ya tarakimu, wanawake hao kwa wastani walikuwa wameacha kutokwa hedhi kwa muda wa miaka miwili, wengi zaidi waliacha kutokwa hedhi mapema maishani, na asilimia 71 walikuwa wakipata tiba ya HRT. Kwa kupendeza, Dakt. Christian Jamin, aliyesimamia uchunguzi huo, alisema kwamba kila mwanamke ana uwezo wa kupata mtoto hata baada ya hedhi kukoma.

Papa John 23 Alimsifu Mussolini

Kwa muda fulani sasa, inaonekana kumekuwa na shindano katika Kanisa Katoliki kati ya wale wanaopendelea kutawazwa kwa Papa John 23 kuwa mtakatifu na wale wanaopinga hatua hiyo. Hivi karibuni umma ulikuja kujua kwamba kabla John 23 awe papa, yeye alimsifu Benito Mussolini, yule mtawala Mfashisti wa Italia wa miaka ya 1930 na 1940, katika barua kadhaa za tangu miaka ya 1930. Mtu huyo ambaye baadaye alikuja kuwa papa alisema kwamba Mussolini alionekana anaongozwa na “Mungu.” Barua hizo zilikuwa zimechapishwa miaka mingi iliyopita, lakini mhariri wazo, aliyekuwa katibu wa kibinafsi wa John 23, alikuwa ameondoa sehemu iliyomsifu mtawala mkatili Mfashisti ili “kuepuka”—sasa yeye asema—“zisitumiwe vibaya kisiasa.” Watu fulani wanafikiria kwamba sehemu zilizoondolewa zimejulishwa kwa umma wakati huu tu ili kukomesha ule mwendo wa kujaribu kumfanya papa wa sasa atangaze John 23 kuwa “mbarikiwa.” Kwa vyovyote vile, lasema gazeti la Milan Corriere della Sera, mambo yaliyofunuliwa na maandishi hayo “hayaongezi mambo mengi kwa yale ambayo tayari yamejulikana kuhusu mtazamo wa wenye mamlaka wa kanisa kuelekea Ufashisti.”

Misitu ya Mvua Iwezayo Kushika Moto

Mioto katika Kalimantan Mashariki, Indonesia, iliharibu hektari milioni 3.5 za misitu katika miaka ya ukame ya 1983 na 1991. Lakini moto katika misitu ya mvua ya Amazon yenye unyevu yahatarisha hata zaidi. Kwa nini? Kwa kawaida kifuniko cha juu cha misitu ya mvua hunasa hewa yenye unyevu chini yacho, jambo linalofanya miti iwe yenye unyevu sana hivi kwamba haiwezi kushika moto. Katika miaka mitano iliyopita, laripoti Manchester Guardian Weekly, sehemu ya mashariki mwa msitu wa Amazon umekatwa-katwa na barabara nyingi zinazotumiwa na wakataji miti ambao wametafuta na kukata miti mikangazi yenye thamani kubwa sana, na hivyo kuondoa hewa yenye unyevu. Matawi na vichwa vya miti visivyohitajiwa vinavyobaki katika sakafu la msitu huchomwa moto, jambo linalohatarisha msitu. Kulingana na uchunguzi mmoja, kukata asilimia 2 tu ya miti huharibu kifuniko cha msitu kipatacho asilimia 56. Wakulima wa Brazili wameripoti kuona moto wenye kuenea kilometa tano unaopitia miti iliyosimama.

Viyoga Vyaelekea Kutoweka

“Kati ya aina zipatazo 4,400 za uyoga zinazopatikana katika Ujerumani, theluthi moja vimo katika orodha ya viyoga vinavyoelekea kutoweka,” lasema Frankfurter Allgemeine Zeitung. Hata wanasayansi wanaonya kwamba kuna hatari kwamba mbali na viyoga, kuna aina nyinginezo za ukungu zitakazotoweka katika Ulaya. Kwa nini? Yaonekana kwamba uchafuzi na kutumiwa vibaya kupita kiasi kwa mimea hiyo kunaiharibu sana. Namna nyinginezo za uhai, kama vile mti oki na misunobari na aina kadhaa za wadudu waitwao mende-milia, wanategemea viyoga kwa uhai wao. Kwa hiyo, kutoweka sana kwa ukungu kwaweza kutokeza msiba wa kimazingira.

Msingi wa Kuamini wa Kisayansi

“Kuna uwezekano wa mtu kuwa mwanasayansi na aamini kwamba kuna Mungu,” lasema gazeti la Afrika Kusini The Star.[1] Makala hiyo iliripoti juu ya hotuba ya dakika 90 iliyotolewa na Profesa David Block, mwastronomia katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha Johannesburg.[2] Block alieleza kwamba sayansi yathibitisha jinsi ulimwengu wote mzima “ulivyowekwa vizuri na kwa usawaziko.”[3] Kwa maoni ya Block na wanasayansi wengine, jambo hilo laonyesha ubuni uliokusudiwa, ambao nao, waonyesha kwa nguvu sana kwamba kuna Mbuni.[4] Kulingana na The Star, Block amalizia kwamba kuna ushuhuda mwingi sana wa kuwako kwa Mungu “hivi kwamba mtu asiyeamini kwamba kuna Muumbaji angehitaji kuwa na imani nyingi kuliko yule anayeamini [kwamba kuna Muumbaji].”[5]

Nguzo za Misri Zimo Hatarini

Nguzo za kale zilizoko kotekote Misri zinahatarishwa na kuinuka kwa maji ya chini ya ardhi. Nguzo 400 za kihistoria jijini Cairo, na vilevile nguzo nyinginezo zilizoko kusini zaidi, kama vile Hekalu la Luxor zimo hatarini. Ile sanamu ya nusu-mnyama nusu-binadamu iitwayo Sphinx tayari imepoteza fumba moja, laripoti The UNESCO Courier. Sababu moja itokezayo tatizo ni kule kujengwa kwa Bwawa Kuu la Aswân, linalofanya maji ya Naili yaendelee kutiririka na kiwango cha maji kuwa juu. Kabla ya kujengwa kwa bwawa hilo, mto huo haukupokea maji kwa miezi tisa katika mwaka na ulipungukiwa sana maji. Sababu nyingine tena itokezayo tatizo ni mfumo wa kutupa takataka wa Cairo uliotengenezwa miaka mia moja iliyopita, na ambao huvuja na kufurikwa mara nyingi. Maji yapenyapo misingi ya majengo, maji huvutwa futi kadhaa juu katika jengo, kunamotokea utendaji wa kikemikali unaofanyiza chumvi ambazo nazo hushambulia kuta.

Je! Hii Ni Haki?

“Michael Charles Hayes aliua watu wanne katika North Carolina kwa kuwafyatulia risasi—na sasa, familia za wale watu aliowaua zinalalamika, yeye anaishi vizuri kushinda jinsi ambavyo amepata kuishi maishani mwake, kwa gharama ya walipaji kodi,” yasema taarifa ya shirika la habari la Associated Press. Akihukumiwa kuwa amerukwa akili na kupelekwa kwa makao ya watu waliorukwa akili, Hayes aliweza kupata manufaa za Malipo ya Ulemavu na kupokea dola 536 kila mwezi. Hizo zimemwezesha kununua pikipiki, mavazi mengi sana, na awe na chumba kilichojaa vifaa vya muziki na vidio za bei ghali sana kwa sababu tayari yeye ameandaliwa makao, na chakula ambazo malipo hayo ya ulemavu yapaswa kugharamia. Serikali hutoa karibu dola milioni 48 kila mwaka kwa wahalifu wenye kurukwa akili. Kiongozi wa mashtaka Vincent Rabil ataja tukio hilo kuwa “haki iliyopotoshwa” naye aongezea: “Walipaji kodi wanamlipa muuaji. Hilo ni jambo lisilo la akili.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki