‘Alimkumbuka Muumba Wake Katika Siku za Ujana Wake’
ADRIAN sikuzote alihangaikiwa sana na wazazi,” baba yake akasema. “Akiwa na umri wa miaka minne aliendesha gari la familia akaligongesha kwenye mti, akafanya kila mtu achelewe mkutano wa kutaniko. Akiwa na miaka mitano alikusanya vyura wengi sana na kuwaleta ndani ya nyumba. Ilichukua siku kadhaa kuondolea mbali vitu hivyo. Tulihisi tukiwa kama familia ya Wamisri wakati wa lile pigo la Kibiblia la vyura.
“Alipokuwa na miaka 11, alipata rakuni wachanga watatu kando ya njia kuu akawapeleka shuleni katika mfuko wake wa vitabu. Mwalimu alipoingia, darasa lilikuwa limejaa kelele—watoto walisongamana kuuzunguka mfuko wa vitabu wa Adrian, wakipayuka kwa msisimko. Mwalimu alichungulia ndani, akawaona rakuni, akambeba yeye na wanyama hao vipenzi vyake ndani ya gari hadi mahali pa kuwapokea wanyama mayatima. Adrian alitoa machozi kwa kuwaza kuwapoteza watoto wake, lakini baada ya kutalii mahali hapo na kuona mbweha wachanga na mayatima wengine wakitunzwa vema, aliwaacha rakuni wake huko.”[1]
Baba yake aliendelea kusema: “Adrian hakuwa mvulana mbaya. Alikuwa mwenye shughuli sana tu. Alikuwa na akili chapuchapu iliyoendeleza uchangamshi maishani.”[2]
Mama ya Adrian alionyesha hali nyingine kumhusu—mpenda-familia, mpenda-nyumbani, mvulana mwenye upendo sana. Mama huyo asimulia hivi: “Watoto shuleni walieleza kuwa yeye ni mtu ambaye hangeumiza yeyote. Msichana mmoja katika darasa lao alikuwa na uhaba wa akili ingawa si punguani. Alikuwa akisafiri ndani ya basi ya shule pamoja na Adrian. Watoto wengine walimcheka, lakini mama yake alituambia kwamba sikuzote Adrian alimtendea kwa staha na fadhili ya pekee. Adrian alikuwa na hali ya kujichukua kwa uzito pia—mvulana mwenye ufikirio sana akiwa na huruma ya kina kirefu bila kuionyesha wazi mara nyingi. Lakini alipoionyesha, alitushangaza kwa maelezo yaliyolenga kabisa kiini cha mambo.”
Mama huyo alimalizia hivi kadirio lake juu ya mwanaye: “Ugonjwa wake ulimfanya akomae haraka na kutokeza ndani yake hali ya kiroho yenye kina kirefu zaidi.”[3a]
Alikataa Katakata—Damu Hapana!
Eti ugonjwa wake? Ndiyo. Ulianza Machi 1993, Adrian alipokuwa na miaka 14.[4] Uvimbe wenye kukua kasi ulipatikana katika tumbo lake. Madaktari walitaka uchunguzi wa kuondoa tishu fulani za mwili lakini wakahofu damu nyingi mno ingetoka na kusema kwamba huenda ikawa lazima kutia damu mishipani. Adrian alisema hapana. Alikataa katakata. Alisema hivi, huku machozi yakimlenga machoni: “Kama ningetiwa damu ningeshindwa kabisa kuendelea kujiheshimu.”[5] Yeye na familia yake walikuwa Mashahidi wa Yehova, ambao hukataa kutiwa damu mishipani kwa sababu za Kibiblia zilizoandikwa kwenye Mambo ya Walawi 17:10-12 na Matendo 15:28, 29.
Akiwa katika Kituo cha Afya kwa Watoto cha Dakt. Charles A. Janeway katika jiji la St. John’s, Newfoundland, akingoja uchunguzi wa kuondoa tishu za mwili—wa kufanywa bila damu—Adrian aliombwa na mtaalamu wa vivimbe Dakt. Lawrence Jardine ajisemee mwenyewe juu ya suala la damu.[6]
“Yaani,” Adrian akasema, “haingekuwa kitu hata kama wazazi wangu wangekuwa au hawangekuwa Mashahidi wa Yehova. Bado mimi singekubali damu.”
Dakt. Jardine akauliza, “Je! wang’amua kwamba ungeweza kufa usipokubali kutiwa damu mishipani?”
“Ndiyo.”
“Nawe uko tayari kufanya hivyo?”
“Ndiyo ikiwa sina namna.”
Mama yake, ambaye pia alikuwapo, akauliza, “Kwa nini unachukua msimamo huo?”
Adrian akajibu: “Mama, hakuna kitu bora cha kubadilishana. Kutomtii Mungu na kurefusha maisha yangu kwa miaka michache sasa kisha nikose ufufuo na uhai wa milele katika dunia yake ya paradiso kwa sababu ya kutotii kwangu—hiyo si akili kamwe!”—Zaburi 37:10, 11; Mithali 2:21, 22.[7]
Uchunguzi wa kuondoa tishu za mwili ulifanywa Machi 18. Ulionyesha kwamba Adrian alikuwa na uvimbe mkubwa katika tezi ya eneo la kutengeneza chembe nyeupe za damu. Uchunguzi fulani uliofuata kufanywa wa uboho wa mifupa uliithibitisha hofu ya kwamba alikuwa amesitawisha leukemia. Dakt. Jardine sasa akaeleza kwamba njia ya pekee ambayo Adrian labda angeweza kuishi ni kwa kutibiwa sana kwa kemikali na mitio ya damu mishipani. Hata hivyo, Adrian bado alikataa kutiwa damu mishipani. Matibabu ya kikemikali yalianzwa, bila ile mitio ya damu mishipani.
Hata hivyo, wakati hatua muhimu hii ya matibabu ilipokuwa ikiendelea, kulikuwa na hofu kwamba Idara ya Masilahi ya Watoto ingeweza kuingilia na kutafuta agizo la mahakama ili wapewe haki ya utunzaji na mamlaka ya kumpa mitio ya damu mishipani. Sheria iliruhusu mtu yeyote mwenye umri wa miaka 16 au zaidi ajiamulie juu ya matibabu. Njia pekee kwa mtu yeyote aliye chini ya miaka 16 kupata haki hiyo ilikuwa kupangwa katika kikundi cha watoto waliokomaa.
Katika Mahakama Kuu ya Newfoundland
Kwa hiyo asubuhi ya Jumapili, Julai 18, mkurugenzi mtendaji wa Masilahi ya Watoto alianzisha hatua za mahakama ili kupata haki ya utunzaji.[8] Upesi, mwanasheria wa kutokeza mwenye kustahiwa sana, David C. Day, wa Tuzo la Malkia, jijini St. John’s, Newfoundland, aliajiriwa amwakilishe Adrian. Alasiri iyohiyo, saa 9:30, Mahakama Kuu ya Newfoundland ilikutana, msimamizi akiwa Hakimu Robert Wells.[9]
Wakati wa kipindi cha alasiri, Dakt. Jardine alimweleza wazi sana hakimu kwamba yeye alimwona Adrian kuwa mtoto aliyekomaa mwenye usadikisho wa kina kirefu dhidi ya kutumia damu na kwamba yeye, Dakt. Jardine, alikuwa amemwahidi Adrian kwamba hangehusisha mtio wa damu mishipani katika utibabu wowote. Hakimu Wells alimwuliza daktari kwamba uamuzi ukiwa ni kumtia damu mishipani kwa agizo la mahakama, je, yeye angeitia? Dakt. Jardine akajibu: “Hapana, mimi binafsi singefanya hivyo.” Alitaja kwamba Adrian alihisi kwamba tumaini lake la Kibiblia la kupata uhai wa milele lingetishwa. Ushuhuda wa moyo mweupe wa daktari huyu wa kutokeza ulikuwa wa kustaajabisha na wa kuchangamsha moyo pia na uliwafanya wazazi wa Adrian watoe machozi ya shangwe.[10]
“Tafadhali Mnistahi Mimi na Matakwa Yangu”
Mahakama ilipokutana Jumatatu, Julai 19, David Day alitoa nakala za hati ambayo Adrian—akiwa mgonjwa mno asiweze kufika mahakamani—alikuwa ametayarisha na kutia sahihi akitaarifu matakwa yake mwenyewe kuhusu utibabu wa kansa yake bila damu au vifanyizo vyenye damu.[11] Humo Adrian alisema hivi:
“Mtu hufikiria mengi akiwa mgonjwa, na akiwa mgonjwa wa kansa, yeye hujua angeweza kufa na hufikiria hilo.[12] . . . Mimi sitakubali damu wala kuacha itumiwe; hiyo hakuna. Najua ningeweza kufa damu isipotumiwa. Lakini huo ndio uamuzi wangu. Hakuna aliyeniambia nikatae. Mimi namtumaini sana Dakt. Jardine. Naamini yeye ni mtu wa kutimiza ahadi yake. Yeye asema atanipa matibabu barabara bila kutumia damu kamwe. Alinieleza hatari zilizopo. Naelewa hilo. Najua msiba waweza kutokea.[13] . . . Maoni yangu ni kwamba nikitiwa damu yoyote, hiyo itakuwa kama kuninajisi, kushikashika mwili wangu kwa makusudi mabaya. Mimi siutaki mwili wangu ikiwa hilo litatendeka. Siwezi kuishi nivumilie hilo. Sitaki utibabu wowote ikiwa damu itatumiwa, hata uwezekano wa kuitumia. Mimi nitakinza utumizi wa damu.”[14] Hati ya Adrian ilifikia mwisho kwa sihi hii: “Tafadhali mnistahi mimi na matakwa yangu.”[15]
Muda wote wa usikizi wa kesi Adrian alibaki kwenye chumba chake cha hospitali, na Mwamuzi Wells alifanya fadhili sana kuja kumwona hapo, David Day akiwapo. Akitoa usimulizi wa mahoji hayo, Bw. Day alisema juu ya maelezo yenye kuvuta fikira na kuchochea sana ambayo Adrian alimtolea hakimu juu ya kichwa kimoja hiki, maana kuu ikiwa hii: “Najua mimi ni mgonjwa sana, nami najua ningeweza kufa. Wanatiba fulani wasema damu itasaidia. Mimi sifikiri hivyo, maana nimesoma juu ya hatari nyingi kuihusu. Isaidie isisaidie, imani yangu yapinga damu. Stahi imani yangu na utanistahi mimi. Usipostahi imani yangu, mimi nahisi nimenajisiwa. Ukistahi imani yangu, naweza kukabiliana na ugonjwa wangu kwa fahari. Yaonekana kitu pekee ambacho nimebaki nacho ni imani, na sasa hicho ndicho kitu cha maana zaidi ambacho nakihitaji kunisaidia nipigane na ugonjwa huo.”[16]
Bw. Day alikuwa na maelezo yake mwenyewe juu ya Adrian: “Yeye alikuwa mteja mwenye uwezo wa kushughulikia ugonjwa wake hatari kwa saburi, kwa ujasiri, na kwa uhodari. Azimio lilionekana machoni mwake; uhakika usiosikika wazi sana ulikuwa katika sauti yake; ukakamavu katika tabia yake. Juu ya yote, dalili za maneno yake na mwili wake zilinijulisha kwamba yeye ni mwenye imani ya kudumu. Chapa yake ilikuwa imani. Ugonjwa usiokubali kumwacha ulimfanya ahitajike kukabiliana na magumu ya utu mzima yasiyowaziwa ujanani. Imani ilimsaidia kufanya hivyo.[17] . . . Yeye alikuwa msema-wazi asiyesita na, kwa maoni yangu, msema-kweli. . . . Mimi nilikuwa macho kufikiria kama wazazi wake [walikuwa wamemlazimisha] afuate upinzani wao kwa utumizi wa damu katika kumtibu. . . . Niliridhika [kwamba] alitumia akili yake mwenyewe katika kueleza takwa lake kwamba atibiwe pasipo damu.”[18]
Katika pindi nyingine Bw. Day alieleza juu ya imani za Adrian ambazo “zilikuwa za thamani kubwa kwake kuliko uhai wenyewe” kisha akaongezea hivi: “Kijana huyo thabiti, ajapokabili matatizo ya jinsi hiyo, anifanya nihisi kwamba ole zote za maisha yangu si kitu. Yeye atabaki amekazika kikiki katika kumbukumbu langu milele. Yeye ni mtoto aliyekomaa mwenye moyo mkuu ajabu, ufahamu wa kina kirefu, na uelewevu.”[19]
Uamuzi—Adrian Ni Mtoto Aliyekomaa
Jumatatu, Julai 19, usikizi wa kesi ulimalizika, na Hakimu Wells akatoa uamuzi wake, uliochapishwa baadaye katika Human Rights Law Journal, Septemba 30, 1993. Visehemu vyao ni hivi vifuatavyo:
“Kwa sababu zifuatazo, maombi ya Mkurugenzi wa Masilahi ya Watoto yamefutwa; mtoto huyo hahitaji ulinzi; utumizi wa damu au vifanyizo vyenye damu kwa makusudi ya kutia au kudunga sindano ya damu mishipani haukuonyeshwa kuwa muhimu, na katika hali hususa za kisa hiki, ungeweza kuwa na madhara.[20]
“Badiliko la hali lisipoleta umuhimu wa agizo la ziada, utumizi wa damu au vifanyizo vyenye damu katika utibabu wake umekatazwa: na mvulana huyo atangazwa rasmi kuwa mtoto aliyekomaa ambaye ni lazima takwa lake la kupokea utibabu bila damu au vifanyizo vyenye damu listahiwe. . . .[21]
“Hakuna swali kwamba ‘kijana’ huyu ana moyo mkuu sana. Nafikiri yeye ana tegemezo la familia yenye upendo na yenye kujali, nami nafikiri yeye anakabili mateso yake kwa moyo mkuu sana. Sehemu ya imani yake ya kidini ni kwamba ni kosa kwake kutumia vifanyizo vyenye damu kwa kuacha viingizwe katika mwili wake, kwa makusudi yoyote yale . . .[22] Mimi nimepata fursa nzuri zaidi ya kusoma hati iliyotayarishwa na A. jana, tena nimepata fursa nzuri zaidi ya kumsikia mama yake, aliyetoa uthibitisho, na nikapata fursa nzuri zaidi ya kuongea na A. mwenyewe.[23]
“Mimi naridhika kwamba yeye aamini kwa moyo wake wote kwamba kukubali damu kungekuwa kosa na kwamba kulazimishwa kukubali damu katika hali ambazo tunasema juu yazo kungekuwa kuvamia mwili wake, kuvamia faragha yake, na kuvamia utu wake wote, kwa kadiri ya kwamba kungelemea vibaya sana nguvu na uwezo wake wa kukabiliana na utesi mbaya sana ambao lazima umpate, vyovyote iwavyo.[24]
“Mimi nakubali kwamba yule daktari alisema jambo la akili kabisa aliposema kwamba ni lazima mgonjwa awe katika hali ya akili yenye ushirikiano na maoni yafaayo juu ya utibabu wa kikemikali na matibabu mengine ya kansa ili kuwe na tumaini lolote, tumaini lolote la kweli, la mafanikio, na kwamba mgonjwa mwenye kulazimishwa kupokea kitu fulani kinyume cha imani zake za kina kirefu angekuwa ni mgonjwa ambaye matibabu hayo hayangemfaa sana. . . .[25]
“Mimi nafikiri kwamba yale ambayo yametendeka kwa A. yamefanya akomae kwa kadiri ambayo haingewazika kwa [mvulana] wa miaka 15 asiyekabiliana na kuishi pamoja na kile ambacho yeye anaishi nacho na atakacholazimika na anacholazimika kukabiliana nacho. Mimi nafikiri kwamba jambo linalompata ni jambo baya kwa kadiri niwezayo kuwazia, nami nahisi kwamba imani yao ni mojapo mambo yanayotegemeza yeye na familia yao. Mimi nafikiri kwamba jambo ambalo limetendeka limemfanya A. akomae kupita tarajio lolote la kawaida au akomae kupita [mvulana] wa miaka 15. Mimi nafikiri mvulana niliyesema naye asubuhi hii ni tofauti sana na [mvulana] wa kawaida wa miaka 15, kwa sababu ya jambo hili lenye msiba.[26]
“Mimi nafikiri yeye amekomaa vya kutosha kueleza maoni ya kusadikisha, naye amenieleza hayo . . . ili mimi niyafikirie matakwa yake, nami nafanya hivyo.[27] Matakwa yake ni kwamba vifanyizo vyenye damu visitiwe mwilini, nami naridhika pia kwamba matakwa haya yakipingwa kwa njia fulani na yule Mkurugenzi kwa agizo la Mamlaka hii, masilahi yake bora yangeathiriwa dhahiri na katika maana halisi sana . . . Zaidi ya hilo, ikiwa—na hili lawezekana sana—kweli angewezwa na ugonjwa huu, ingekuwa hivyo akiwa katika hali ya akilini ambayo, kwa kufikiria imani zake za kidini, ingekuwa ya kuhuzunisha sana, ya kusikitisha sana, na isiyotamaniwa hata kidogo. Mimi ninafikiria yote haya. . . .[28]
“Katika hali zote hizo, mimi nahisi kwamba yafaa nikatae lile ombi la kwamba vifanyizo vyenye damu vitumiwe katika utibabu wa A.”[29]
Ujumbe wa Adrian kwa Hakimu Wells
Ujumbe ambao kivulana huyu, aliyejua alikuwa akifa, alimpelekea Mwamuzi Robert Wells ulikuwa wenye ufikirio wa ajabu, nao uliwasilishwa na Bw. David Day, kama ifuatavyo: “Nafikiri ningekuwa sijali ikiwa, kwa niaba ya mteja wangu niliyesema naye kwa muda mfupi tu baada ya wewe kuondoka hospitalini leo, singekutolea shukrani yake ya moyo mkunjufu kabisa, moyo ambao ni wa fadhili sana, kuhusu jinsi wewe ulivyoshughulikia jambo hili kwa haraka na kujali na kwa haki nyingi. Yeye ana shukrani nyingi kwako, Mheshimiwa, nami nataka kumbukumbu liwe na maandishi ya kuonyesha hivyo. Asante.”[30]
Mama ya Adrian ayakumbuka matukio yenye kuimalizia hadithi.
“Baada ya ile kesi Adrian alimwuliza Dakt. Jardine, ‘Nina muda gani zaidi wa kuishi?’ Daktari kajibu: ‘Juma moja au mawili.’ Nikamwona mwanangu akitoa chozi moja, alilominya kutoka kwenye kope zilizoshikamana sana. Mimi nilienda kumzungushia mikono, naye akasema: ‘Acha, Mama. Ninasali.’[31] Baada ya dakika chache, nikauliza, ‘Wakabilianaje na jambo hili, Adrian?’ ‘Mama, hata iweje nitaishi tu, hata nikifa. Na ikiwa nina majuma mawili tu ya kuishi, nataka kuyafurahia. Kwa hiyo changamka.’[32]
“Alitaka kuzuru tawi la Watch Tower katika Georgetown, Kanada. Alifanya hivyo. Aliogelea katika kidimbwi huko pamoja na mmoja wa rafiki zake. Alihudhuria mchezo wa kikoa cha besiboli cha Blue Jays na kupigwa picha pamoja na baadhi ya wachezaji.[33] Jambo la maana zaidi ni kwamba, katika moyo wake alikuwa amejiweka wakfu kumtumikia Yehova Mungu, na sasa alitaka kuonyesha wakfu huo kwa kuzamishwa katika maji. Kufikia sasa hali yake ilikuwa imeharibika zaidi, naye alikuwa amerudi hospitalini na hangeweza tena kuondoka huko. Kwa hiyo wauguzi walimpangia kwa fadhili atumie moja la matangi ya chuma-cha-pua katika chumba cha matibabu ya kukandwa mwili. Alibatizwa humo Septemba 12; alikufa siku iliyofuata, Septemba 13.[34]
“Maziko yake yalikuwa makubwa zaidi ya yote yaliyopata kuwa katika yale makao ya maziko—wauguzi, madaktari, wazazi wa wagonjwa, wanadarasa wenzake, majirani, na wengi wa ndugu na dada zake wa kiroho kutoka kutaniko lake mwenyewe na makutaniko mengine.[35] Sisi wazazi, hatukuzing’amua kamwe sifa zote zilizo nzuri ajabu zilizoonekana wazi katika mwana wetu alipokuwa akivumilia majaribu yake mengi wala fadhili na ufikirio uliokuwa sehemu ya utu wake wa Kikristo wenye kusitawi. Mtunga-zaburi aliyepuliziwa alisema hivi: ‘Wana ni urithi kutoka kwa Yehova.’ Hakika huyu alikuwa hivyo, nasi twatazama mbele kumwona katika ulimwengu mpya wa Yehova wa uadilifu, ambao sasa uko karibu kuanzishwa katika dunia iliyo paradiso.”[36]—Zaburi 127:3; Yakobo 1:2, 3.
Kuhusiana na Adrian na tutazamie utimizo wa ahadi ya Yesu kwenye Yohana 5:28, 29: “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.”
Kwa kukataa mitio ya damu mishipani ambayo yadhaniwa ingaliweza kurefusha maisha yake ya wakati uliopo, Adrian Yeatts alijionyesha kuwa mmoja wa vijana wengi ambao humtanguliza Mungu.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
‘Uhai U Katika Hiyo Damu’
Damu ni kitu tata ajabu, nayo hufikia kila chembe katika mwili. Katika tone moja tu, chembe nyekundu 250,000,000 za damu hubeba oksijeni na kuondoa kaboni dayoksaidi; chembe nyeupe 400,000 hutafuta na kuharibu wavamizi wasiotakwa; visahani 15,000,000 hukusanyika mara ileile mahali penye mkato na kuanza ugandishaji-damu wa kuziba ule mpasuko. Yote hayo hutegemea plazima nyangavu, yenye rangi ya pembe-ndovu, ambayo yenyewe imefanyika kutokana na mamia ya vichanganyiko vitimizavyo sehemu za muhimu katika kazi nyingi za damu. Wanasayansi hawaelewi kazi zote ambazo damu hufanya.[1]
Si ajabu kwamba Yehova Mungu, Muumba wa umajimaji huu wa kimuujiza, atangaza kwamba ‘uhai u katika hiyo damu.’—Mambo ya Walawi 17:11, 14.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Pandikizo la Moyo Bila Damu
Oktoba uliopita, Chandra Sharp mwenye umri wa miaka mitatu alilazwa hospitalini katika Cleveland, Ohio, Marekani, akiwa na moyo ambao licha ya kuwa mkubwa zaidi ulikuwa ukishindwa kazi pia. Msichana huyo hakuwa akila chakula cha kutosha, ukuzi wake ulidumaa, uzani wake ulikuwa kilo tisa tu, naye alihitaji pandikizo la moyo. Alipewa majuma machache tu ya kuishi. Wazazi wake walikubali lile pandikizo la moyo lakini wakakataa damu isitiwe mishipani. Wao ni Mashahidi wa Yehova.[1]
Hilo halikuwa tatizo kwa mpasuaji, Dakt. Charles Fraser. The Flint Journal la Michigan liliripoti hivi Desemba 1, 1993: “Fraser alisema Kliniki ya Cleveland na vituo vingine vya kitiba vinakuwa na ustadi wa kufanya mapasuo mengi—kutia na mapandikizo—bila kutia ndani ya mgonjwa damu ya watu wengine. ‘Tumejifunza mengi zaidi juu ya jinsi ya kuzuia kuvuja kwa damu, na jinsi ya kujaza umajimaji wa namna nyinginezo ambazo si damu katika mashine ya kutumiwa kuhusiana na moyo na mapafu,’ akasema Fraser.” Kisha akaongezea: “Hospitali fulani maalumu zimekuwa zikifanya mapasuo makubwa ya moyo kwa miongo kadhaa bila kutia damu mishipani. . . . Sikuzote sisi hujaribu kufanya upasuaji bila damu (ya kutia mishipani).”[2]
Oktoba 29, yeye alimfanyia Chandra pandikizo la moyo bila damu.[3] Mwezi mmoja baadaye Chandra aliripotiwa kuwa akiendelea vema.[4]