Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 5/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Chanzo cha Mateso Makubwa kwa Kanisa”
  • Mbona Uraibu wa Kutumia Dawa za Kulevya?
  • “Taifa Lenye Jeuri Zaidi”
  • Muhali wa Kanisa
  • Mshuko wa Moyo Waongezeka
  • Kuendeleza Watoto Wakiwa Wenye Afya
  • Utumwa Leo
  • Namna ya Kuwa Mnene Mno
  • Kisiwa cha Sikukuu
  • Kutembea Ukiwa Mlevi
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1994
  • Ziara ya Papa kwa UM—Ilitimiza Nini?
    Amkeni!—1996
  • Jitihada za Kuwaokoa Watoto
    Amkeni!—1994
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 5/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

“Chanzo cha Mateso Makubwa kwa Kanisa”

Katika mazungumzo yake pamoja na maaskofu wa Kanada ya mashariki, John Paul 2 alielekeza fikira zake kwenye matumizi mabaya ya ngono yafanywayo na mapadri. Kama ilivyoripotiwa katika L’Osservatore Romano, papa aliambia hao makasisi Wakanada kwamba “kashfa iliyoletwa na washirika hao wa jamii ya mapadri na Wanadini hao ambao wamekosa katika jambo hilo imekuwa chanzo cha mateso makubwa kwa Kanisa katika Kanada.” Aliongezea kwamba yeye alikuwa amesali “kwa ajili ya wale ambao wametendwa mwenendo mbaya wa ngono, na pia wale ambao wamekuwa na hatia ya kuutenda.” Baadhi wanaamini kwamba kuondolea mbali useja wa lazima kwa mapadri kungeweza kuchangia kupunguza kashfa zinazohusiana na utumizi mbaya wa ngono unaofanywa na mapadri na pia kutatua “kupungua au kutosambaa vizuri kwa mapadri” kulikotajwa na papa. Lakini kulingana na John Paul 2, “magumu yahusikayo leo katika kutunza useja si sababu inayotosha kupindua usadikisho wa Kanisa kuhusu thamani na kufaa kwa useja huo.”

Mbona Uraibu wa Kutumia Dawa za Kulevya?

“Watu wengi huamini kwamba utalaamu wa ki-siku-hizi wa dawa una kibonge kidogo kiwezacho kutatua lolote la matatizo yetu. Ikiwa mtu hawezi kulala, ameze kibonge kidogo. Akitaka kuboresha mafanikio yake kazini, ameze kingine,” ndivyo aelezavyo Alberto Corazza, mkuu wa polisi wa São Paulo, kama alivyonukuliwa katika gazeti Veja la Brazili. “Iko wazi ni kwa nini utamaduni wa jinsi hiyo huathiri vijana.” Yeye aongezea hivi: “Asilimia themanini ya waraibu wa dawa za kulevya wana matatizo mazito ya kifamilia. Wao hutoka katika familia yenye kukandamiza sana au yenye kuendekeza sana au katika nyumba isiyo na baba.” Lakini wazazi waweza kulindaje vijana wao na dawa za kulevya? Asema hivi Corazza: “Huenda likaonekana kuwa jambo lisiloelekea kuwezekana, lakini katika nyumba yenye usawaziko mzuri ambamo mna upendo kwa watoto na mazungumzo, itakuwa vigumu dawa za kulevya zipate nafasi yoyote.”

“Taifa Lenye Jeuri Zaidi”

“Amerika ndilo taifa lenye jeuri zaidi ulimwenguni,” aandika mwanasafu wa magazeti Ann Landers. “Katika 1990, bunduki za mkononi ziliua watu 10 katika Australia, 22 katika Uingereza, 68 katika Kanada na 10,567 Marekani.” Hilo pia ndilo taifa lenye silaha nyingi zaidi. Watu walo wana silaha za kufyatua moto zaidi ya milioni 200—karibu mmoja kwa kila wakaaji milioni 255. Shule hazikosi kuhusika na jeuri hiyo. Karibu asilimia 20 ya wanafunzi wote wa shule ya sekondari hubeba silaha ya namna fulani. Karibu vitendo vya uhalifu milioni tatu kwa mwaka hutukia katika au karibu na nyanja za shule. Kila siku walimu 40 hushambuliwa kimwili, na karibu 900 hutishwa kutendwa madhara ya kimwili. Kulingana na Shirika la Elimu ya Kitaifa, wanafunzi 100,000 hubeba bunduki kuzipeleka shuleni kila siku, na siku ya kawaida itaona watoto 40 wakiuawa au kujeruhiwa na silaha za kufyatua moto. “Uvumilio wetu kuhusu jeuri ni mwingi ajabu, na shule ni dalili ndogo tu ya kuonyesha hivyo,” asema John E. Richters wa Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Akili. Mwalimu mmoja wa Kiingereza, aliyekuwa amefanikiwa asilimia 10 tu kufanya wanafunzi wake wa darasa la 12 waandike insha, alipata mafanikio ya asilimia 100 alipowagawia kuandika juu ya kichwa “Silaha Yangu Niipendayo Zaidi.”

Muhali wa Kanisa

Maaskofu wa kutoka Kanada ya magharibi wameiomba Vatikani ilegeze sheria ya kanisa kuhusu useja na kuruhusu mapadri waliooa watumikie wenyeji katika Maeneo ya Kaskazini-magharibi. Maaskofu hao wahisi kwamba kufikiria hali za kitamaduni, pamoja na upungufu wa mapadri katika mikoa ya kaskazini, kwastahilisha ombi lao. “Askofu Denis Croteau,” laripoti The Toronto Star, “asema jamii za watu wa Inuit na Dene huithamini kanuni ya kifamilia katika utamaduni wao ambamo, kama mwanamume hajaoa, akalea familia na kuwa mzee, ‘wewe si kiongozi na watu hawatakusikiliza.’” Ingawa Papa John Paul 2 na maofisa wengine wa Vatikani walisikiliza ombi la maaskofu hao, hakuna badiliko litakalofanywa. Kardinali Jozef Tomko, kichwa cha Ushirika wa Vatikani wa Kueneza Evanjeli kwa Jamii za Watu, alionyesha hofu kwamba “kuruhusu jambo hilo katika Kanada kungefanya vyombo vya habari vielekeze fikira zote huko na kufungulia miminiko la maombi katika Afrika, Amerika Kusini na kwingineko,” lasema Star.

Mshuko wa Moyo Waongezeka

“Machunguzi kumi na mawili yaliyofanywa mbali mbali kuhusu mahojiano na jumla ya watu 43,000 katika nchi tisa yamethibitisha utafiti uliofanywa mapema kidogo Amerika kwa kuonyesha kwamba kadiri ya mshuko mkubwa wa moyo imezidi kuongezeka katika sehemu nyingi za ulimwengu wakati wa karne ya 20,” yataarifu The Harvard Mental Health Letter. Baada ya kuwapanga wahusika “katika vikundi-vikundi vilivyoamuliwa na mwongo wa [miaka ya] kuzaliwa kwao, kuanzia 1905 na kumalizika baada ya 1955,” karibu kila uchunguzi ulionyesha kwamba “watu waliozaliwa baadaye walielekea zaidi kuwa walishuka moyo kwa kadiri nzito wakati fulani wa maisha zao.” Machunguzi yaliyo mengi yalionyesha pia ongezeko thabiti la mshuko mkubwa wa moyo muda wote wa karne hii.

Kuendeleza Watoto Wakiwa Wenye Afya

“Zaidi ya watoto milioni 230 wasiofika umri wa kwenda shuleni katika ulimwengu unaositawi, au asilimia 43, wamedumaa ukuzi wao kwa sababu ya utapiamlo kutokana na ukosefu wa chakula na ugonjwa,” yasema habari moja iliyochapishwa na UM. Katika 1993 watoto wanaokadiriwa kuwa milioni nne walikufa kwa sababu ya utapiamlo, ama moja kwa moja ama kwa sababu hiyo iliongezea uzito wa magonjwa ya kuambukiza. Jawabu ni nini? Shirika la Afya Ulimwenguni lapendekeza kwamba “vitoto vichanga vyote vilishwe maziwa ya matitini tu tangu kuzaliwa hadi umri wa miezi 4-6. Baada ya hapo, watoto wapaswa kuendelea kunyonyeshwa, huku wakipokea chakula cha ziada kifaacho na kutosha kufikia umri wa miaka 2 na kupita hapo.” Akina mama na waandalizi wa utunzaji wa afya huhimizwa wasiamue vibaya kwamba hatua za ukuzi wa vitoto vichanga vinavyonyonyeshwa zinakwamisha ukuzi na kuanzisha vyakula vingine mapema mno. Hiyo yaweza kuwa hatari kwa vitoto vichanga na kuchangia utapiamlo na ugonjwa, hasa mahali ambapo vyakula vyenye kuanzishwa vina viini vibaya na havijengi kwa kadiri ya kutosha.

Utumwa Leo

Ingawa Azimio la Ulimwengu Wote la Haki za Kibinadamu hutaarifu kwamba “hakuna mtu atakayeshikiliwa katika utumwa au utumikisho,” mamia ya mamilioni ya watu hata hivyo wanateseka wakiwa watumwa. Idadi ya watu walio chini ya mazoea ya kiutumwa leo, laonyesha gazeti UN Chronicle, kwa kweli ni kubwa hata kuliko idadi ya watumwa wakati wa karne ya 16 hadi ya 18, “ule muhula wa kilele cha biashara ya watumwa.” Jambo moja la kugutusha juu ya utumwa wa leo ni kwamba wengi wenye kutendwa hivyo ni watoto. Watoto wa miaka saba hadi kumi hutoa jasho kwa muda wa saa 12 hadi 14 kwa siku viwandani. Wengine hufanya utumwa wakiwa watumishi wa nyumbani, malaya, au askari-jeshi. “Kibarua cha watoto chatakiwa sana,” charipoti Kituo cha Haki za Kibinadamu cha UM, “kwa sababu ni cha bei rahisi” na kwa sababu watoto “huogopa mno kulalamika.” Utumwa, wasema UM, ungali ni “uhalisi wa ki-siku-hizi” wenye kusikitisha.

Namna ya Kuwa Mnene Mno

Hesabu ya saa ambazo watoto wasiofika umri wa kwenda shule hutumia kwa siku wakitazama televisheni yahusiana moja kwa moja na ongezeko la mafuta ambalo hutokea mwilini baadaye utotoni, adai Dakt. Munro Proctor wa Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Boston. Dakt. Proctor alifanya uchunguzi wa miaka minne wa watoto 97 wasiofika umri wa kwenda shule ambao, hapo kwanza, walikuwa na umri kati ya miaka mitatu na mitano. Wazazi walisimamia saa za watoto wao kutazama televisheni kila siku, huku vipimo vya mikunjo ya ngozi katika mwili wote vikichukuliwa kila mwaka. Kama ilivyoripotiwa katika The Medical Post la Kanada, “kila mtoto aliketi mbele ya ule mrija wa picha kwa wastani wa saa mbili kila siku. Kwa kila saa ya ziada ya kutazama televisheni kwa siku, kulikuwa na ongezeko la milimeta 0.8 katika badiliko la mkunjo wa ngozi ya juu na ongezeko la milimeta 4.1 katika badiliko la jumla ya mikunjo ya ngozi.” Dakt. Proctor alikata shauri kwamba kutazama televisheni huongoza kwenye upungufu wa utendaji wa mwili na umeng’enyaji wa chakula na kuachia watoto hatari ya wazi ya kusikiliza matangazo ya kula vyakula vyenye kalori nyingi ambavyo huliwa wakati wa kutokuwa na utendaji.

Kisiwa cha Sikukuu

“Benki [ya Ulimwengu] na [Hazina ya Fedha ya Kimataifa] zinaomba serikali ipunguze hesabu ya siku za kutofanya kazi katika Sri Lanka, kwa sasa zikiwa ni 174 kati ya zile 365, ambazo yawezekana zikawa ndiyo rekodi ya ulimwengu,” lasema The Economist. “Nchi yawezaje kufanya maendeleo wakati watu wayo wako kwenye sikukuu karibu nusu-mwaka?” Ile hesabu kubwa ya siku za mapumziko yaonyesha jinsi Sri Lanka ilivyo na mchanganyiko wa jamii na dini mbalimbali. Kuongezea zile sikukuu 5 za kiserikali, kuna sikukuu 20 za kidini kwa ajili ya imani za Kibuddha, Kihindu, Kiislamu, na Kikristo. Watumishi wa serikali hupata siku 45 za mapumziko ya ziada kila mwaka—ambazo zalingana na za biashara nyingi za watu binafsi. Hata hivyo, uchumi wa Sri Lanka wazidi kukua. “Ukulima ndicho kiini cha uchumi na hutegemea zile pepo mbili za monsuni ambazo hupita katika kisiwa hicho katika majira ya kuvuna mazao,” lataarifu The Economist. “Pepo za monsuni haziendi mapumziko.”

Kutembea Ukiwa Mlevi

“Kunywa na kuendesha gari havichangamani,” ndivyo yasemavyo matangazo, na adhabu kali hufikilizwa juu ya wale waendeshao magari hali wameingiwa na kileo. Ingawa fikira nyingi zaidi zimeelekezwa juu ya madereva walevi, ni chache ambazo zimeelekezwa juu ya kunywa na kutembea. Kulingana na Usimamizi wa Usalama wa Kusafiri Katika Njia Kuu za Kitaifa, watembea-miguu 5,546 waliuawa na magari Marekani katika 1992, na zaidi ya theluthi moja ya watembea-miguu hao walikuwa wamelewa. Idadi hiyo ilikuwa asilimia 14 ya vifo vyenye kuhusiana na magari. Kati ya wale waliozidi umri wa miaka 14, asilimia ipatayo 36 walikuwa na kadiri kubwa ya kileo katika damu yao kiasi cha kutosha kuwataja kuwa madereva walevi kama wangalikuwa wakiendesha gari. Ni machache yajulikanayo kwa sasa juu ya ni jinsi gani ya kuzuia vifo hivyo na ni nani walio katika hatari kubwa zaidi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki