Vyombo vya Ushetani Dawa za Kulevya na Muziki wa Vyuma Vizito
CARL A. RASCHKE, mkurugenzi wa Taasisi ya Mambo ya Ubinadamu katika Chuo Kikuu cha Denver, aliandika: “Haikutukia kwa aksidenti kwamba dawa za kulevya, [muziki] wa vyuma vizito, unyama, na jeuri ya ovyoovyo yote yamekuwa ishara za kuchukiza sana za kuangamia kwa mwanadamu tuelekeapo kwenye mwongo wa tatu wa Muhula wa Shetani.” Alisema hivi pia: “Ungeweza kusema kwamba muziki wa roki ya vyuma vizito ni Ushetani uliojitungia mtindo wao wenyewe hali moja na vile muziki wa gospeli ulivyo kwa Ukristo. Ni watu wachache sana ambao hugeuka kufuata Ukristo kwa kusikiliza tu muziki wa gospeli redioni. Lakini vyuma vizito ni kikazio chenye nguvu sana. Huhalalisha yale mambo ovyo ambayo watoto wamekwisha kuingilia.”
Hili ni hukumio kali dhidi ya yale ambayo wengi sana wa vijana wa leo huyaona kuwa starehe nzuri tu za kujituliza na mahangaiko ya maisha—muziki wa vyuma vizito na dawa za kulevya. Je, mashtaka haya ni ya kweli? Je, yaweza kuwa kwamba dawa za kulevya na muziki wa vyuma vizito waweza kuwa dalili za Ushetani? Fikiria maelezo ya wale ambao wamekabiliana uso kwa uso na jeuri ya waabudu wa kishetani na ambao wamezipeleleza.
“Ule ujumbe wa uchochezi wa muziki wa vyuma vizito ni ‘wa kidini,’ kwa jinsi ambayo huenda isishangaze—katika maana ya kwamba huo hupiga mbiu ya mamlaka ya juu zaidi iliyo mwangalizi wa ulimwengu wote mzima. Hata hivyo, mamlaka hiyo si Mungu,” akaandika Raschke, katika kitabu chake Painted Black. “Huo . . . huchochewa na yule Zimwi mkuu mwenyewe.” Kwa kuongezea, alisema: “Ile mamlaka na jeuri ya kishetani ni kitu ambacho vijana walioachwa bila tumaini, na wakiwa na dhamiri iliyodumaa, waweza kukiingilia kwa urahisi. . . . Vijana wenye masumbuko na wenye kutendwa vibaya huamini, kwa kuongozwa na mambo yaliyoathiri maisha yao ya mapema bila kutambulikana waziwazi, kwamba ile Mamlaka ya Juu Zaidi lazima iwe ni ya uovu. Vyuma vizito huiongezea nguvu ‘theolojia’ hii na kuipa hadhi ya juu katika muziki huo.”
Kulingana na Dakt. Paul King wa Chuo Kikuu cha Tennessee, aliyeshuhudia mbele ya Bunge la Marekani juu ya muziki wa vyuma vizito, muziki ambao wengi wa vijana wenye masumbufu hupendelea ni ule wa “habari zisizo za kidesturi za jeuri, chuki, uasi, ngono za kishenzi, kutenda wanawake mabaya, na kumtukuza Shetani. Mtindo-maisha wa mbalehe uhusishapo dawa za kulevya, huelekea zaidi kupendelea mambo hayo.” Muziki wa vyuma vizito hutukuza na kusifu sana nguvu ya uovu, akasema King. Katika muziki wa vyuma vizito, “matendo maovu hutukuzwa yakapata hadhi bora katika maonyesho,” akasema.
Fikiria matokeo ya ujumbe ulio chinichini ya muziki wa vyuma vizito katika habari zifuatazo.
Mwaka jana katika New Jersey, Marekani, wavulana wawili wa miaka 15 waliua kinyama mbwa wa aina ya Labrador aitwaye Binti-Malkia aliye kipenzi cha familia moja. “Ilikuwa dhabihu kwa Shetani,” wakadai. Walimshika mbwa huyo wa kike kwenye mnyororo wake, wakampiga mateke akafa, wakang’oa ulimi wake wakautumia katika desturi ya ibada ya kishetani. Waliangika maiti iliyokatwa maungo ya mbwa huyo juu ya kulabu kubwa ya chuma na kuining’iniza katika ua wa jirani. Michoro ya Kishetani ilipatikana juu ya kichwa cha mbwa huyo, na pentagramu (nyota ya ncha tano katika duara—mfano wa Kishetani) ulichorwa ardhini chini ya maiti ya mbwa huyo. Usiku wa mauaji, walikuwa wakisikiliza “Deicide” (maana yake kuuawa kwa Mungu), kikosi kimoja cha roki ya vyuma-kifo, ambacho mwimbaji wacho mkuu hujisifia kutesatesa na kuua wanyama.
Katika California, wapenzi matineja wawili, ambao, kulingana na marafiki, walipagawa na ibada ya Shetani, waliua mama ya msichana yule kinyama kwa kumdunga kwa kisu na kwa kumpiga kwa spana. Katika eneo hilohilo, kijana mwingine alimtolea Shetani sala kisha akafyatua baba yake na kumwua. Polisi wenye kupeleleza uhalifu huo walisadiki kwamba muziki wa vyuma vizito ulipasa kulaumiwa. “Kwa msingi, muziki huo hufundisha kwamba si lazima uwasikilize wazazi wako, na kwamba wapaswa kuishi maisha utakayo,” akasema mjuzi mmoja polisi.
Katika Uingereza wenye kunajisiwa mfululizo na wanagenge waliripoti kwa polisi kwamba mmoja wa wanajisi alikuwa na mikatokato ya mwili ya ishara ya beni moja ya muziki wa vyuma vizito wenye maneno ya ujumbe wa unajisi na jeuri.
Katika Arkansas, Marekani, tineja wa mashambani alijaribu kuua wazazi wake kwa kuwapiga kwa rungu kisha kuwakatakata kwa kisu cha mkata-nyama. Polisi walipata katika mashine yake ya audiokaseti iliyofunguliwa iimbe wimbo wa beni moja ya vyuma vizito, “Altare ya Dhabihu,” ambamo maneno hupiga mayowe hivi: “Kuhani mkuu anangojea, simi mkononi, akimwaga damu ya bikira safi kabisa. Uchinjaji wa Shetani, kifo cha kisherehe, hujibu kila amri atoayo. Ingia milki ya Shetani . . . Jifunze maneno matakatifu ya sifa, ‘Mshangilie Shetani.’”
Kwa habari ya maneno ya nyimbo nyingine ziimbwazo na washiriki wenye kupiga mayowe wa beni za vyuma vizito—ambazo huwa zimerekodiwa mapema na kuigizwa kwa mdomo na mashabiki wao katika maonyesho ya kujisukasuka kwa fujo nyingi, au kusikilizwa katika kanda za audiokaseti kwa mfululizo wa saa nyingi—jumbe hizo zina athari gani juu ya vijana wenye kuvutwa kwa urahisi? Fikiria, kwa kielelezo, maneno haya: “Shetani bwana-mkubwa wetu hutuongoza kwa kila hatua ya kwanza katika kuharibuharibu kwa nia mbovu,” na “Mwaga damu yako, acha inichuruzikie mimi. Nishike mkono na uache uhai wako ukutoke . . . Umeimwaga damu. Mimi nina nafsi yako.”
“Ikiwa tayari twayakubali maoneleo ya kwamba pornografia ingeweza kuchochea mshikashika uchi wa watoto,” akaandika Carl Raschke, “mbona tusilipokee wazo la kwamba maneno ya nyimbo zipigazo mayowe zikisema ua, kata maungo, lemaza, tesatesa, futilia mbali zingeweza kwa kweli kuhamasisha mtu mwenye ubongo ulioruka atende kihususa matendo hayo?”
Ni maoni ya watafiti kila mahali kwamba utumizi mbaya wa dawa za kulevya na Ushetani huambatana pamoja. David Toma aliyekuwa naibu mpelelezi aomboleza kwamba “hajapata kamwe kukuta mwabudu wa Shetani asiyetumia dawa za kulevya.” Gazeti ’Teen liliripoti kwamba utumizi wa dawa za kulevya hutatanisha mambo kwa matineja “wageukiao kuabudu ibilisi, ikifanya iwe vigumu zaidi na zaidi kupambanua kati ya mambo halisi kikweli na yale yaonekanayo tu kuwa halisi yaonwapo kwa msisimko bandia wa dawa za kulevya na alkoholi.”
“Vyuma vizito huambatana pamoja na utumizi mzito wa dawa za kulevya hali moja na jinsi michezo ya nasibu iambatanavyo pamoja na wacheza-kamari wa kupindukia,” akasema Raschke. “Mbalehe ambaye kemikali za mwili wake zimeingiwa na uraibu huchagua mtindo-maisha wa unyeti, unyama, wizi na uzidifu wa ngono—yote hayo yakiongezewa nguvu na ile migumo na mivumo ya vikundi vya wanamuziki wa vyuma vizito.”
Bila shaka, kijana huwa windo rahisi kwa uvutano wa Shetani wakati utimamu wa ubongo umwondokapo na badala yake akaingiwa na mawazo ya upotovu na jeuri.
[Blabu katika ukurasa wa 8]
Mtu huwa windo rahisi kwa uvutano wa Shetani wakati utimamu wa ubongo umwondokapo na badala yake akaingiwa na miminiko la upotovu na jeuri
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wewe unajaza akili yako nini?