Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kansa ya Matiti Asanteni sana kwa kuchapisha ule mfululizo “Kansa ya Matiti—Hofu ya Kila Mwanamke.” (Aprili 8, 1994) Nimejichunguza mara kwa mara na nimewaza kabisa kwamba tezi zangu ni ngumu. Nikiwa ninahisi wasiwasi mwingi, sikuchukua hatua yoyote. Hata hivyo, baada ya kuisoma makala, nilienda hospitalini nikajua nina kansa. Mipango ilifanywa nipasuliwe. Nawashukuru nyinyi kwa moyo mweupe kabisa.
T. Y., Japani
Tangu nipasuliwe, sijaweza kusoma lolote juu ya kansa. Kwa hiyo gazeti hilo lilipotokea, sikulisisimukia. Lakini kwa kawaida nilisoma matoleo yote ya Amkeni! jalada hadi jalada, na usiku huo niliamua kusoma kidogo kisha niache nikiingiwa na woga. Lakini sikuweza kuacha kulisoma. Lilitayarishwa vizuri sana, likiwa lenye kuarifu sana, na lenye kujali sana.
G. K., Marekani
Makala hiyo ilinisaidia kuona jinsi Yehova aelewavyo hofu zetu za kukabili ugonjwa wa kutisha uhai. Sikuzote mimi nilikuwa nimefikiri watu ni dhaifu au wamekosa imani ikiwa walihisi hivi. Kwa kweli ilinisaidia kuiona huruma nyingi sana aliyo nayo Yehova.
K. G., Marekani
Ikiwa kuna wakati gazeti limepata kusema na mtu fulani hususa, basi toleo hilo hakika lilisema na mimi. Mume wangu na mimi tulikalia kiti cha starehe huku gharama za tiba ya upasuaji wangu wa kansa ya matiti zikiwa zimesambazwa pote kutuzunguka. Tulipokuwa tukiandika mfululizo wa hundi, mpeleka-barua alituletea toleo hili la Amkeni! Niliisoma makala siku hiyohiyo, kwa upendezi usio wa kawaida. Asanteni kwa niaba ya wanawake wote watakaojipa moyo mkuu kutokana na makala hizo.
E. J., Marekani
Majiji Nina miaka 16 na nilisisimuka kuzisoma makala juu ya majiji. Katika darasa la jiografia tuliombwa tutoe hotuba fupi juu ya habari ya kujichagulia. Nilitoa yangu kwa msingi wa ile makala “Jiji Lililokuwa Limejaa Watu.” (Januari 22, 1994) Nilipokwisha kusoma hotuba yangu kwa sauti kubwa darasani, kila mtu alipiga makofi. Asanteni kwa kunisaidia kuboresha uelewevu wangu wa jiografia.
T. R., Ujerumani
Katika ile makala “Na Tujijengee Jiji,” mlisema: “Katika 1900, London lilikuwa jiji pekee ulimwenguni pote lenye idadi ya watu milioni moja.” (Januari 8, 1994) Lakini katika toleo lililofuata, mlisema: “Kufikia katikati ya miaka ya 1800 jiji hilo [Edo, ambalo sasa laitwa Tokyo] lilikuwa na watu zaidi ya milioni.” Ni jipi sahihi?
S. T., Japani
Ile taarifa kuhusu London yaonekana ilikuwa kosa. Ilikuwa na msingi wa chapa ya 1985 ya “Illustrated Atlas of the World” (Rand McNally and Company). Hata hivyo, “The World Almanac and Book of Facts 1993” chaonekana kuwa sahihi kisemapo kwamba majiji kadhaa yalikuwa na idadi za watu wazidio milioni moja kufikia 1900. Poleni kwa mvurugo huo.—Mhariri.
Kufuatia Fedha Nikiwa msomaji mchanga wa Amkeni!, niliguswa kikweli na ule mfululizo “Kufuatia Fedha—Kutaishia Wapi?” (Machi 22, 1994) Mimi naona ni kama marika wangu wana mradi mmoja tu: kujitafutia madonge ya fedha. Hata hivyo, inaheshimika zaidi kufuata afundishayo Yehova kuliko kuabudu vitu vyenye kutoweka.
K. R., Ufaransa
Michezo Asanteni kwa kile kihabari “Je! Mungu Huunga Mkono Upande Wowote Michezoni?” (Februari 8, 1994) Mimi nimelifanya kosa la kusali nipate ushindi katika uwanja wa mbio; pia nimesali ili washindani wangu washindwe. Sasa najua kwamba mapenzi ya Yehova hayahusiani na michezo. Ninaweka wakfu maisha yangu kwa Yehova, nami nahisi nimestareheka zaidi kujua kwamba yeye anasikiliza sala zangu kikweli.
J. T., Marekani