Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Hatari ya Kuendesha Gari Kusoma kile kihabari “Ni Uchovu wa Kuendesha Gari?” (“Kuutazama Ulimwengu,” Februari 22, 1994) kulirudisha kumbukumbu za wakati nilipokuwa dereva wa lori miaka 20 na kitu iliyopita. Nilikuwa nikiendesha gari kwenda nyumbani baada ya kushika usukani mchana kutwa nilipopatwa na usingizi. Kwa ghafula, kishindo kikubwa kiliniamsha, nami nilishtuka kwa hofu kuona kwamba nilikuwa nikiendesha gari upande usiofaa wa barabara. Nilikuwa nimegonga kikuta cha barabara, lakini hakukuwa na magari wala watembea-miguu. Niliponyoka nikiwa huru huria, lakini lilikuwa somo ambalo sitalisahau kamwe. Ningaliweza kuua mtu kwa sababu sikujipatia pumziko nilipolihitaji. Ushauri wangu? Someni kihabari hicho katika Amkeni!, na mtii!
M. Y., Uingereza
Uzito Mwingi Mno Nataka kutoa shukrani maalumu kwa ile makala “Vijana Huuliza . . .” ya Aprili 22, 1994, “Mbona Mimi Ni Mnene Sana?” Mimi nina miaka 13 na sikuzote nilijifikiria kuwa mnene, ingawa chati za uzani zilinionyesha nilikuwa na uzani wa wastani. Kwa sababu ya mtazamo wangu, niliacha kabisa kujitumaini nikapatwa na mshuko wa moyo. Wakati mmoja hata niliona laiti ningekuwa nimekufa. Huo wasikika kuwa ujinga mwingi, lakini hivyo ndivyo nilivyohisi. Kwa msaada wa Yehova na makala hiyo, naweza kushughulika na mshuko wangu wa moyo vizuri zaidi.
C. S., Ujerumani
Mgonjwa Mchanga wa Kansa Nikiwa nimetoka sasa tu kusoma ile makala “Maisha Yawapo Magumu,” iliyosimuliwa na Kathy Roberson, ni lazima niseme kwamba nimeguswa kwelikweli. (Agosti 22, 1994) Nililazimika kuandika na kuonyesha uthamini wangu wa kina kirefu kwa ajili ya makala nzuri kama hiyo. Mimi nina miaka 14 na nimepatwa na mnyanyaso shuleni kwa sababu ya kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Hali yangu si yenye kujaribu kama ya Kathy Roberson, lakini kuona jinsi Yehova alivyomtegemeza muda wote wa jaribu lake kulinitia nguvu.
C. G., Marekani
Lo, ni makala nzuri iliyoje! Mimi pia nilipata kuwa mgonjwa sana nikiwa na miaka tisa na hatimaye nikatumia miezi mingi hospitalini. Hata hivyo, niliweza kurudia afya njema kufikia wakati nilipoingia shule ya sekondari. Ni lazima iwe ilikuwa vigumu sana kwa Kathy Roberson kukabiliana na kurudi-rudi kwa ugonjwa wake. Mtazamo na nguvu zake zimenisaidia niwe na mwelekeo chanya zaidi wa akili.
D. V., Marekani
Kunyonyesha Maziwa ya Mama Mnamo miezi mitatu ijayo natazamia kuzaa mtoto wetu wa pili. Kwa hiyo nilipopokea toleo langu la Agosti 22, 1994, la Amkeni! na kufungua kwenye ile makala “Mambo ya Msingi ya Kunyonyesha Maziwa ya Mama,” nilijawa na shangwe. Iliburudisha kwelikweli kusoma makala iliyompa Mwanzilishi wa uhai ustahili na sifa impasayo. Mimi sielewi ni jinsi gani mtu yeyote angeweza kukana kwamba kuna Muumba mwenye hekima na upendo wakati afikiriapo jinsi mama alivyotayarishwa kwa vifaa vizuri sana vya kulisha mtoto wake.
L. K., Marekani
Nina hakika mtapokea barua nyingi za shukrani kwa makala hii. Ninapotazama nyuma, naona imekuwa baraka kubwa na chaguo lenye kutumika kuwanyonyesha watoto wetu wote watatu maziwa ya mama. Najua makala hii itawatia moyo akina mama na watarajiao kuwa akina mama.
C. S., Marekani
Uchoraji Sanifu Moyo wangu ulidunda nilipoona ile picha ya ufufuo katika toleo la Juni 8, 1994. Uthamini wangu kwa lile tumaini zuri ajabu la ufufuo uliongezewa kina hata zaidi. Hakika hakuna maneno yatakayoweza kuonyesha shangwe yangu nimwonapo dada yangu mdogo katika Paradiso ya wakati ujao.
M. U., Japani
Kupenda Fedha Asanteni kwa ajili ya ile makala “Kupenda Fedha—Shina la Uovu Mwingi.” (Machi 22, 1994) Katika nchi yangu mna upelelezi wa kuiba, uvunjaji nyumba na usumbufu wa umma—yote yakifanywa kwa ajili ya fedha. Hivyo gazeti hili lilitokea wakati upasao na lilifaa, nami nilipata furaha nyingi katika kuangushia wengine toleo hili. Kwa kweli, wauza-mikate fulani waliyapigania nilipokuwa sina nakala za kutosha!
A. F. S., Afrika Magharibi