Wamishonari Mawakili wa Nuru au wa Giza?—Sehemu 4
Nuru ya Kiroho kwa “Kontinenti Yenye Giza”?
“CHINI ya miaka 100 iliyopita, Afrika iliitwa ile Kontinenti Yenye Giza kwa sababu sehemu yayo kubwa haikujulikana na Wanaulaya.” Kile ambacho The World Book Encyclopedia yakirejezea hapa hakikuwa giza la Kiafrika, bali giza la Kiulaya—kukosa ujuzi kwa Ulaya juu ya kontinenti ambayo kwa kadiri kubwa haikuvinjariwa. Kwa hiyo si kupinganisha mambo kusema kwamba yawezekana kuwa Afrika imepata jina layo kutokana na neno la Kilatini aprica, limaanishalo “-enye jua.”
Na bado, katika jambo moja, Afrika ilikuwa katika giza—katika giza kwa habari ya kweli ya Biblia. Donald Coggan, aliyekuwa Askofu-Mkuu wa Canterbury hapo zamani, aziita Afrika na Asia “zile kontinenti kubwa mbili ambamo Makanisa ya Magharibi yamemwaga rasilimali zao za nguvu-binadamu na fedha muda ulio mwingi wa miaka mia mbili iliyopita.”
Wengi wa wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo bila shaka walikuwa na moyo mweupe. Kwa kushughulikia kazi yao, wengine hata walidhabihu uhai wao. Walileta mabadiliko makubwa juu ya maisha ya Kiafrika. Lakini je, wao ‘walitoa nuru kupitia habari njema’ kama Kristo alivyokuwa amefanya, hivyo wakiiondolea giza layo la kiroho ile iitwayo Kontinenti Yenye Giza?—2 Timotheo 1:10, NW.
Wamishonari Wenyeji Watoa Vimulimuli vya Kwanza vya Nuru
Mkristo wa kwanza kuingia katika rekodi ya kuhubiri katika Afrika alikuwa Mwafrika yeye mwenyewe, yule towashi Mwethiopia atajwaye katika Biblia kwenye Matendo sura 8. Akiwa ni mwongofu Myahudi, alikuwa njiani kwenda nyumbani akitoka kuabudu hekaluni katika Yerusalemu wakati Filipo alipomwongoa kwenye Ukristo. Pasipo shaka, kwa kupatana na bidii ya Wakristo wa mapema, baadaye Mwethiopia huyu akiwa mtendaji alihubiri ile habari njema aliyokuwa amesikia, akipata kuwa mishonari katika bara lake mwenyewe.
Hata hivyo, wanahistoria hushindwa kukubaliana juu ya kama hivyo ndivyo au sivyo Ukristo ulivyokuja kuanzishwa katika Ethiopia. Kanisa Orthodoksi la Ethiopia laonekana kuwa ni la tangu nyuma kwenye karne ya nne, wakati mwanafunzi wa falsafa Msiria jina lake Frumentius alipowekwa rasmi na Athanasius, askofu wa Kanisa Kopti la Alexandria, ili awe askofu kwa “Wakristo” Waethiopia.
Kanisa Kopti—Copt limetokana na neno la Kigiriki la kusema “-a Kimisri”—ladai kwamba mwanzilishi walo na askofu wa kwanza alikuwa Marko yule Mweneza-Evanjeli. Kulingana na pokeo, yeye alihubiri katika Misri muda mfupi tu kabla ya katikati ya karne ya kwanza. Kwa vyovyote, “Ukristo” ulisambaa kufika Afrika Kaskazini tarehe ya mapema, huku wanaume kama Origen na Augustino wakikwea kwenye umashuhuri. Shule ya kikatekisti katika Alexandria, Misri, ilikuja kuwa kitovu maarufu cha uanachuo “wa Kikristo” huku Pantaenus akiwa msimamizi wayo wa kwanza. Lakini kufikia wakati wa halifa wa Pantaenus, Clement wa Alexandria, yaonekana wazi uasi-imani ulikuwa umeleta madhara. The Encyclopedia of Religion yafunua kwamba Clement “alitetea kupatanishwa kwa fundisho la Kikristo na Biblia pamoja na falsafa ya Kigiriki.”
Kanisa Kopti lilikuwa limeendesha kampeni kali ya kimishonari, hususa mashariki mwa Libya. Machimbuo ya kiakiolojia katika Unubi na Sudan ya chini yafunua pia athari za Kikopti.
Wamishonari Wanaulaya Wawasili
Wanaulaya walifanya kazi kidogo ya kimishonari katika Afrika kabla ya karne ya 16 na ya 18, wakati Wakatoliki walipopata mafanikio ya kadiri fulani. Dini za Kiprotestanti hazikuwasili mpaka mapema katika karne ya 19, wakati Sierra Leone ilipopata kuwa nchi ya kwanza ya Afrika Magharibi kufikiwa na wamishonari wao. Ingawa Waprotestanti walijaribu sana kuwafikia, leo kila nchi ya Kiafrika ijivuniayo kuwa na idadi kubwa ya watu “Wakristo” ina Wakatoliki wengi kuliko Waprotestanti, isipokuwa chache.
Kwa kielelezo, idadi ya watu wa Gabon ni asilimia 96 ya Wakristo wa jina. Muda mfupi kabla ya Vita ya Ulimwengu 1, Albert Schweitzer, Mlutheri, alianzisha hospitali ya kimisheni huko na baadaye akaongezea koloni la wenye ukoma. Japo kile kishindo kikubwa ambacho utendaji wake wa umishonari wa Kiprotestanti wa miaka 40-na-zaidi umekuwa nacho juu ya nchi hiyo, bado Wakatoliki ni wengi kuliko Waprotestanti kwa uwiano wa zaidi ya 3 kwa 1.
Hata hivyo, ushiriki wa Kiprotestanti ulipoongezeka, utendaji wa umishonari wa Kiafrika uliongeza mwendo. Adrian Hastings wa Chuo Kikuu cha Leeds aeleza kwamba “urithi wa maana wa kipindi hiki [nusu ya pili ya karne ya 19] ulikuwa mwanzo mkubwa wa tafsiri ya Biblia katika lugha nyingi za Kiafrika.”
Tafsiri za Biblia katika lugha za kienyeji ziliandaa msingi wa kueneza “Ukristo,” uliokuwa umekosekana hapo awali. Waafrika wengi waliamini ndoto na maono, wakaona magonjwa kuwa ni kurogwa, na walizoea ndoa ya wenzi wengi. Kuwa na Biblia katika lugha za kienyeji kuliwapa wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo fursa ya kutoa nuru ya Kimaandiko juu ya habari hizi. Hata hivyo, kulingana na Hastings, “mara nyingi Waafrika walibaki bila kusadiki mambo haya.” Tokeo? “Kuanzia mwisho wa karne ya kumi na tisa wingi wa makanisa yenye kujitegemea ulianza kutokea, kwanza katika Afrika Kusini na Nigeria, halafu katika sehemu nyingine nyingi za kontinenti hiyo ambako tayari kulikuwa na wamishonari wengi.”
Kwa kweli, leo harakati mpya za kidini zipatazo 7,000, zenye wafuasi zaidi ya 32,000,000, zimo katika Afrika ya chini ya Sahara. Kulingana na The Encyclopedia of Religion, “harakati hizi zimetokea sana-sana katika maeneo ambako jitihada za umishonari wa Kikristo zimekuwa nyingi.” Kwa wazi wamishonari walishindwa kuungamanisha wageuzwa wao katika “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja” aliousema mishonari Paulo.—Waefeso 4:5.
Kwa nini? Chanzo kilichotajwa hapo juu chaeleza ilikuwa kwa sababu ya “kutamauka kwa wageuzwa wenyeji kwa kutopata madhanio na matokeo kwa Ukristo . . . , migawanyiko iliyohisiwa katika Ukristo wenye madhehebu na kushindwa kwao kutimiza mahitaji ya kienyeji [na] kushindwa kwa Ukristo wa misheni kuvunja vipingamizi vya kijamii na kitamaduni na kuchochea watu wajihisi kuwa na ujumuiya.”
Kiasi cha “nuru” ya kiroho ambayo wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo walitoa juu ya ile “Kontinenti Yenye Giza” kilikuwa kidogo mno. Kwa hiyo kilikuwa hafifu mno kuondosha lile giza la kukosa elimu ya Biblia.
Je, Ni Mawakili wa Ukoloni?
Ijapokuwa wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo walitimiza mema, The Encyclopedia of Religion yalazimika kukubali hivi: “Wamishonari walihimiza, na pia wakatoa vifaa, ili ukoloni uchukue mamlaka, hivi kwamba Ukristo na ushindi wa kikoloni zingeweza kuonekana nyakati fulani kuwa kama sehemu mbili za sarafu moja. Upinga-ukoloni-mamboleo mara nyingi umebandika Ukristo katika Afrika kuwa mshiriki wa ukoloni, na umekuwa na haki fulani ya kufanya hivyo.”
The Collins Atlas of World History hutoa ufahamu wenye kina ielezapo kwamba mataifa ya Magharibi yalihamasishwa na usadikisho wa kwamba “ukolonisho ungeleta nuru ya usababu mzuri, kanuni za kidemokrasi na manufaa za sayansi na tiba kwa yale makabila ya ndani-ndani yaliyofikiriwa kuwa ya kishamba.” Na The New Encyclopædia Britannica yataarifu hivi: “Imekuwa vigumu kwa misheni za Katoliki ya Kiroma kujitaliki kutoka kwenye ukoloni, na wamishonari wengi hawakutaka talaka hiyo.”
Basi, yaonekana wazi kiakili kwamba kwa kadiri wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo walivyotetea demokrasi na kusifu manufaa za maendeleo ya Magharibi ya kisayansi na kitiba, ndivyo walivyokuja kuonwa kuwa mawakili wa ukoloni. Watu walipoacha kuvutiwa na miundo ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii ya mamlaka za kikoloni, walipoteza imani katika dini za Kiulaya pia.
Kuhubiri—Ndio Umaana wa Kwanza?
Wakati wowote wamishonari wa Kiprotestanti katika Afrika watajwapo, jina David Livingstone kwa jumla hutokea. Yeye alizaliwa Scotland katika 1813, akawa mishonari wa kitiba na alisafiri sana kotekote Afrika. Upendo wake mwingi kwa ile “Kontinenti Yenye Giza” na msisimko wa ugunduzi zilimwandalia hamasa zaidi. The New Encyclopædia Britannica yataja “Ukristo, ubiashara, na ustaarabu” kuwa “ndio utatu ambao yeye aliamini kuwa ulikusudiwa kuifungua wazi Afrika.”
Matimizo ya Livingstone yalikuwa mengi. Hata hivyo, umaana wake wa kwanza kwa wazi haukuwa kuihubiri gospeli. Britannica yatoa muhtasari hivi juu ya miaka yake 30 ya kazi ya mishonari “katika Afrika ya kusini, ya kati, na ya mashariki—mara nyingi ikiwa katika mahali ambapo hakuna Mwanaulaya aliyekuwa amepata kuvinjari”: “Huenda ikawa Livingstone aliathiri mitazamo ya Magharibi kuelekea Afrika zaidi ya mtu mwingine yeyote mmoja wa kabla au baada yake. Magunduo yake—ya kijiografia, kiufundi, kitiba, na kijamii—yaliandaa fungu la ujuzi tata ambao ungali unavinjariwa. . . . Livingstone aliamini kwa moyo wote kwamba Mwafrika ana uwezo wa kusonga mbele katika ulimwengu wa kisasa. Kwa njia hii, yeye alikuwa mtangulizi si wa ubeberu tu wa Ulaya katika Afrika bali pia wa utaifa wa Kiafrika.” Livingstone alionyesha huruma nyingi kwa Waafrika.
Ingawa wamishonari fulani waliunga mkono au angalau waliachilia biashara ya watumwa, ingekuwa si haki kuwashtaki kuwa walifanya hivyo wakiwa kikundi. Lakini, kwa kufikiria matukio yaliyopita, ni vigumu kuamua kama ile huruma waliyoonyesha wengi wao ilihamasishwa na tamaa ya kutegemeza viwango vya Mungu vya kutopendelea na kuchukua watu wote kwa usawa au ilihamasishwa na hisia za kawaida za hangaiko la kibinafsi juu ya hali njema ya watu mmoja-mmoja.
Hata hivyo, jambo hilo la mwisho lingepatana na matakwa yaliyotangulizwa na walio wengi kati ya wamishonari hao. Kitabu Christianity in Africa as Seen by Africans chakiri kwamba hakuna yeyote ‘awezaye kulingana na kiwango chao cha kazi ya kufadhili wanadamu.’ Lakini kujenga hospitali na shule kulimaanisha kuweka mahitaji ya kimwili ya wanadamu mbele ya kuhubiri Neno la Mungu kwa kufuatia masilahi ya kimungu. Wamishonari fulani hata walianzisha vituo vya biashara kuwezesha Waafrika wafurahie bidhaa zaidi za kimwili za Ulaya, hivyo wakiboresha kiwango chao cha maisha.Yaeleweka ni kwa nini Waafrika wengi leo hushukuru kwa manufaa za kimwili ambazo wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo walifanya ziwezekane. Kama vile Adrian Hastings ataarifuvyo: “Hata wakati wanasiasa Waafrika wachambuapo sana wamishonari na makanisa, ni mara haba wao hukosa kuonyesha shukrani kwa mchango wao kuelekea elimu ya upili.”
‘Ikiwa Nuru Iliyo Ndani Yako Ni Giza . . .’
Kulingana na Hastings, mpaka karne za majuzi Afrika ilikuwa “kontinenti ambamo Ukristo ulishindwa kupenya kwa mafanikio ya kudumu.” Kwa kweli, kufikia katikati ya karne ya 18, misheni za Kikatoliki zilikuwa karibu zimefilia mbali, hiyo ikiongoza mtungaji J. Herbert Kane atie shaka jinsi “kushindwa kwa kadiri kubwa hivyo” kulivyowezekana. Kwanza, kiasi cha kufa miongoni mwa wamishonari kilikuwa juu. Kisababishi kingine kilikuwa mhusiko wa Ureno katika biashara ya watumwa. Kwa kuwa wamishonari wote Wakatoliki walikuwa Wareno, hii “ilifanya dini ya Kikristo ifikiriwe kwa maoni mabaya sana.” Lakini “zilizotumika kwa kufaa zaidi, na labda zenye kufanikiwa zaidi,” aongeza Kane, “zilikuwa zile njia za umishonari wa kijuujuu, zilizotokeza ‘wageuzwa’ wa haraka-haraka na mabatizo ya halaiki ya watu.”Wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo walishindwa kuhamasisha Waafrika wabadili dini zao wafuate mafundisho ya wamishonari. Kugeuzwa kulimaanisha kubadili majina ya juujuu tu ya kidini, lakini si lazima iwe ni imani na mwenendo. Eleanor M. Preston-Whyte wa Chuo Kikuu cha Natal asema: “Mawazo ya Kizulu juu ya maumbile yameingizwa katika wazo la Kizulu juu ya Ukristo kwa njia nyingi zisizoonekana wazi.” Na Bennetta Jules-Rosette wa Chuo Kikuu cha California kule San Diego asema dini za kisasa za Kiafrika “huchanganya mambo ya dini ya kimapokeo ya Kiafrika na yale ya dini zilizoanzishwa baadaye, Ukristo na Uislamu.”
Kulingana na Zaburi 119:130, “kufafanusha maneno yako [Mungu] kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga.” Kwa kuwa wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo kwa sehemu kubwa walishindwa kutanguliza kufafanua Neno la Mungu, ni nuru gani wangeweza kutoa? Wajinga walibaki bila ufahamu.
“Nuru” iliyotolewa na wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo katika karne zilizopita, “kazi njema” zao, ilitokana na ulimwengu ulio gizani. Japo madai yao, hawakuwa wakitoa nuru ya kweli. Yesu alisema: “Ikiwa kwa kweli nuru iliyo ndani yako ni giza, jinsi lilivyo kubwa giza hilo!”—Mathayo 6:23, NW.
Kwa wakati huo, wamishonari walikuwa wakiendeleaje katika zile Amerika, katika ule Ulimwengu Mpya? Sehemu ya tano ya mfululizo wetu itajibu.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kwa kufuatia kazi yao, wamishonari wengine hata walidhabihu uhai wao
[Hisani]
Kutoka kitabu Die Heiligkeit der Gesellschaft Jesu
[Picha katika ukurasa wa 26]
Wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo, kama vile Livingstone, hawakutanguliza kuhubiri kuwe ndilo jambo la kwanza kabisa sikuzote
[Hisani]
Kutoka kitabu Geschichte des Christentums